*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN (MSIMU WA II) 02*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Mama akamuuliza mfalme ni wa baridi kivipi? Tattiana akaeleza vema. Alishindwa hata kumkumbatia wala kukaa naye karibu. Kwani alikuwa ana baridi kana kwamba barafu la kule kaskazini ya Kinabey!
Mama akastaajabu. Linawezekaaje hilo? Ila kama haitoshi, Tattiana akasema ya kwamba mfalme alimwambia hiyo iwe siri yake na asimwambie mtu mwingine yeyote!
ENDELEA
“Unayosema ni kweli?” mama akauliza. Tattiana akamthibitishia hilo kwa kumwonyeshea vidole vyake vilivyosinyaa. Hata alipomgusa mamaye bado alikuwa ana kaubaridi kwa mbali.
Mama akamuuliza kwahiyo haukufanya naye mapenzi. Tattiana akatikisa kichwa na kumwambia mamaye kwamba wamefanya ila kwa wakati huo mfalme hakuwa katika hali hiyo ya ubaridi.
“Alikuwa kama mimi na wewe, ila ajabu baadae akabadilika!”
Wakawa wamemezwa na maswali wasijue majibu. Lakini mama akamwambia Tattiana itampasa avumilie kwani hata iweje ni lazima ampate mfalme. Asahau hayo yote na yatakuja kupatiwa ufumbuzi huko mbeleni.
“Tuangalie hili la hapa mbele kwanza. Hayo tutaja tatua tukiwa ndani ya nyumba.”
Mama hakukaa sana, akaaga anaenda mashariki kupeleka mzigo kwa mfanyabiashara mmoja wa huko. Akamtaka Tattiana apumzike na wataongea kadiri na muda utakavyokuwa unaenda. Wala asiwe na hofu.
Alipotoka, Fanty akaungana na dadaye. Akampeleleza juu ya huko kasrini mwa mfalme lakini Tattiana hakusema hata jambo. ila kabla binti huyo hajanyanyuka na kwenda, Fanty akamwambia habari za Roboth!
Jana yake mwanaume huyo alikuja nyumbani muda mfupi tu baada ya yeye kutoka kwenda kwa mfalme. Tattiana akamezwa na hiyo mada na akataka kujua zaidi.
“Mama amesema hataki kumwona Roboth tena hapa!” Fanty akamalizia habari kwa amri. Mara Tattiana akanyanyuka akibebelea gauni lake na mkono, mbio akatimka kuelekea nje!
Kichwani Roboth alikuwa ametawala. Aliona ana haja ya kuonana na mwanaume huyo na kumweleza yale yaliyojiri kwani hajawahi kumkosea kwa namna yoyote ile, hivyo hakuwa na sababu ya kumhukumu.
Japokuwa Fanty alimuita na kumkata kufanya hilo, Tattiana hakujali wala kusimama. Akaendeleza mbio ambayo ilikomea mbele ya jengo la wakina Roboth. Jengo kuukuu na lisilovutia.
Akaita Roboth mara mbili na mara akatoka mama mmoja mnene mwenye mashavu makubwa na kamdomo kadogo. Alikuwamama Roboth. Akamwambia Roboth ametoka kwenda ng’ambo ya mto.
Pasipo kungoja, Tattiana akafyatua tena miguu yake kwenda huko alipoambiwa. Hakungoja maelezo yoyote yale kwani alishajua mahali ambapo atamkuta Roboth huko. Ni mahali kulekule ambapo walikuwa wanapenda kupeana miadi ya kukutania.
Akasimama na kuvuta pumzi, kisha akaendelea na mbio. Akasimama tena na kuendelea na mbio, mpaka anafika alikuwa hoi bin taaban! Akamkuta Roboth akiwa ameketi juu ya jiwe kubwa lililokuwa limesimama kwenye maji ya mto.
Alikuwa na macho mekundu na sura nyong’onyevu. Mdomo wake ulikuwa umekauka. Alikuwa amekumbatia miguu yake akitazama maji yanavyotiririka.
Tattiana akaita, na mara Roboth akamfuata na kumkumbatia. Akashtaki yale aliyoambiwa na Fanty, kisha akauliza:
“Ni kweli hayo?”
Kwa namna ambavyo alikuwa anamtazama Tattiana, akamfanya binti huyo adondoshe chozi. Na kabla hajajibu chochote, akamkumbatia tena Roboth na kumweka kitako. Akamwambia yale aliyoasikia ni kweli, na ameshalala na mfalme.
Moyo wa Roboth ukajikunja kwa uchungu. Akahisi kana kwamba mtoto aliyetengwa na wazazi wake. Ama yule aliyeadhibiwa vikali asijue kosa lake ni nini. Tattiana akamwambia ni kwasababu ya familia yake, anafanya hivyo.
Roboth aliyejawa na uchungu hakuelewa sababu hiyo, akajikuta analia! Akanyanyuka na kwenda mbali. Akamwambia Tattiana hataki kumwona tena na moyo wake kamwe hautamsamehe.
Tattiana akabaki akilia. Alipojiona ni mwepesi sasa na angalau machozi yake yamepunguza uchungu alonao, akanyanyuka na kurudi nyumbani njia nzima akimfikiria Roboth.
Alijiona yupo njia panda na hajui cha kufanya. Aende kwa mfalme wa ‘baridi’ ama abaki na Roboth, kipenzi cha roho? Je Familia itamwelewa?
Alipofika nyumbani akamkuta mama yake na Fanty wakiwa wamekaa sebuleni. Kwa namna mama yake alivyomtazama, akafahamu tayari Fanty atakuwa amemfikishia taarifa juu ya huko atokako.
Mama akamuita na kumuuliza wapi alipotoka. Pasipo woga akasema ametoka kwa Roboth, alafu akakimbilia chumbani na kujifungia!
***
Ngo! Ngo! Ngo!
Hodi ilibishwa mara moja. Punde mlango ukafunguliwa na Bozi aliyetazama kushoto na kulia kisha akamruhusu mgeni wake aingie ndani.
Alikuwa ni mwanaume aliyevalia sare za jeshi. Akaketi mezani na kumwambia Bozi taarifa za Benadi. Ya kwamba mwanaume huyo alikuwa ameuawa huko karibia na kwake baada ya kuonekana kusaliti kile walichokubaliana.
Bozi akatahamaki kwa taarifa hizo. Hakutegemea kama Benadi angejitosa nje ya chombo chao. Sasa mpango wake wa kufanya tukio la mapinduzi lilikuwa hatihati kutekelezeka kwa njia ya amani.
“Tulimgundua akifanya mawasiliano ya siri na Malkia. Alimwandikia barua kumuonya juu ya mpango wetu.”
Mwanajeshi akatoa barua waliyoikamata toka kwa Benadi na kumkabidhi Bozi ambaye aliifungua haraka na kuipitia kwa macho yake ya kizee.
‘_Malkia wangu mtukufu, maisha yamebadilika … sasa wale uliowakomboa toka kwenye mikono ya wanyang’anyi na waonevu, wamekugeuka. Wanataka damu yako. Wanataka kula nyama yako na kunywa damu yako. Wale uliowahangaikia, leo wanahangaika kukutoa kitini na kukufanya mkimbizi_
_Malkia wangu, sijahusika na sitahusika na mpango huo. Ila tayari watu uliowapa imani yako wamekugeuka. Vita hii ni kubwa kuliko ile uliyopambana hapo awali kwa kuwafahamu maadui. Leo hii adui ni yule ambaye unakula naye meza moja_’
Barua ikaendelea kueleza na pia kutaja wale wote ambao anawajua wakihusika na mpango huo. Mpaka Bozi anamaliza kuisoma, alikuwa amepandwa na hasira za kutosha. Alijawa na jazba. Na akaona Benadi alikuwa anastahili kunyongwa kabisa kwa waya wa chuma.
“Mwili wake upo wapi?” akauliza. Mwanajeshi akamwambia wameuhifadhi ndani na walikuwa wanasubiria amri yake ili waufukie. Basi kutaka kuamini Bozi akaongozana na mwanajeshi huyo kwenda kuuona mwili.
Akakuta mfuko mkubwa uliohifadhi mwili wa Benadi. Akaufungua mfuko huo na kuangaza. Mwili ulikuwa wa baridi tayari. Tumboni ulikuwa na majeraha matatu ya kisu!
Benadi alishindiliwa visu vitatu kabla uhai wake haujachoropoka! Alikuwa ameenda na mapenzi yake, uaminifu na msimamo wake. Bozi akatabasamu na kisha akaufunga mwili huo baada ya kutupia humo barua ya Benadi iliyoishia njiani.
Akatoa amri mwili huo ukafukiwe, na kisha aitiwe wajumbe wake kwa ajili ya majadiliano. Akaenda zake.
Punde wajumbe wakawa wamefika nyumbani, Dummy na wale wenzake watano: watatu walikuwa ni wanajeshi, wawili wafanya biashara. Bozi akawaambia mpango wa kutumia njia ya amani hauwezi ukafanikiwa.
Benadi ameshakwenda, Fluffy na Seth wamewashikilia. Pasipo shaka hili jambo litatengeneza mashaka. Upesi inabidi wachukue hatua kabla mambo hayajawageukia. Wakakubaliana.
Usiku huo wakavamia makazi ya Malkia, wamtie nguvuni yeye na watu wake. Jeshi lipo tayari na linangoja amri muda wowote. Bozi akateta na wale wanajeshi na akawataka wanajeshi wanne atakaongozana nao kwenda kwa Malkia.
Ndani ya muda wa dakika kumi tu, kila kitu kikawa tayari. Bozi alipewa kikosi kizima cha wanajeshi kuongozana nacho. Akachukua hatua kwenda kwenye kasri ya Malkia akiwa anajiamini, analindwa.
Akazama kasrini, wanajeshi wake wakipambana na walinzi na kuwamaliza. Akafika mpaka ndani mwa Malkia lakini hakukuta mtu. Wakasaka kasri nzima pasipo kumwona yeyote. Si Malkia wala Zura!
Bozi akashusha bendera ya Sawaridi na kupandisha ya kwake. Bendera nyekundu yenye upanga wa njano. Akatangaza mapinduzi, Malkia amekimbia himaya na kuacha mikononi mwake! Akatangaza ni muda wa himaya kurudi mikononi mwa wenyeji, mikononi mwa wanaume!
Wanajeshi wakatapakaa huku na huko kumtafuta Malkia, lakini hakuna hata aliyempata wala kuona kiashiria. Hawakujua wapi alipo, wapi amejifichia! Watu ndani ya himaya wakashikwa na taharuki juu ya nini kinachoendelea.
“Mkuu, hata Fluffy na Seth hawapo ndani!” alisema mwanajeshi mmoja mkakamavu. Bozi akashupaza shingo yake, akauliza imewezekanaje kwa watu waliofungiwa na mlango mgumu? Mwanajeshi akajibu wamekuta shimo kubwa chumbani.
Mateka hao watakuwa wametorokea kwa kupitia shimo hilo ambalo lilienda umbali wa nusu kilomita toka kwenye chumba hicho!
“Sasa wapo wapi?!” akafoka Bozi.
“Nao hatujawaona, mkuu!” akajibu mwanajeshi. Bozi akawafukuza wakawatafute na wawalete haraka iwezekenavyo. Wakatazame huko njiani mpaka mpakani. Wahakikishe hakuna sehemu ya himaya itakayoachwa pasipo kutazamwa!
Basi wanajeshi wakaenda nje haraka kutimiza agizo. Wakachukua kama lisaa, lakini bado hawakufanikiwa. Wakarudi kasrini kumtaarifu Bozi. Ajabu wakamkuta amefariki!
Kichwa chake kilikuwa kimewekwa kifuani mwake wakati kiwiliwili kikiachwa solemba. Kiwiliwili hicho kilikuwa kimetuama kwenye dimbwi zito la damu!
Wanajeshi wakahamaki na kushikwa na hofu. Haraka wakatoka na kwenda kwa Dummy wakampashe habari. Lahaula! Hawakumkuta Dummy, bali mwili wa Dummy! Dummy alikuwa amekufa!
Alikuwa ananing’inia na kamba shingoni. Kamba iliyojishikiza kwenye kingo ya dirisha. Wanajeshi wakatokwa na macho.
***