SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

[emoji848][emoji848][emoji848][emoji848][emoji848][emoji848]
 
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II ---- 10*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Kichwani mwake alijawa na mawazo. Kama mawazo hayo yangekuwa na uzito wa kilo, farasi yule asingeweza kumbeba hata kidogo.

Baada ya muda mchache akawa amefika makaoni. Akapita getini akipewa heshima zote, moja kwa moja akaenda kuonana na mfalme. Akamkuta kiongozi huyo akiwa ameketi na yule mwanajeshi ambaye watoto wake wametoka kumtafuta usiku mzima wakamkosa.

Moyo wake ukapiga fundo kubwa.

ENDELEA

“Alah!” mfalme akahamaki. “Karibu sana mzee, mbona ujio wa ghafla hivi?”

“Niwie radhi mfalme wangu, hakika n’takuwa nimekukwaza!” akasema mzee akiinamisha uso wake. Mfalme akamkarimu na hata akamtaka mwanjeshi wake awape faragha wapate kuteta.

“Niambie ni lipi hilo shida?” mfalme akauliza. Walikuwa tayari wameshaketi mezani wakiwa tayari wamehudumiwa kila aina ya chakula.

“mfalme wangu, hamna shida ya kushtusha bali nimekuja kwa ajili ya kesi yangu ya kale. Umefikia wapi kumpata yule mwanamwali? Naona kimya,” mzee akasema akimtazama mfalme kwa shauku. Basi mfalme akacheka na chakulache mdomoni. Akasema:

“Mzee! Wajua mfalme hawezi kuingiza mguu mahali pasipo salama. Nafanya tafiti kwanza kama anastahili kuletwa ndani ya kasri!”

“Hakika!” mzee akaunga mkono. “Na hilo ndilo ambalo limenikimbiza kuja hapa upesi. Je, mfalme wangu, nani umemuweka huko kumfuatilia mwanamwali huyu?”

Mfalme akasema ni yule mwanajeshi aliyemkuta naye, na pia akasema yale ambayo kibaraka wake huyo ameyagundua kwa Tattiana. Mzee akatahamaki, akasema:

“Mfalme, kwanini unamwachia kijana huyo badala ya kummaliza? Anawezaje kutaka kula meza moja na mfalme na ilhali mikono yak ni michafu?”

Mfalme akatikisa kichwa na kutabasamu kwa mbali. Hakuona haja ya kufanya hivyo kwani alikuwa anaamini upendo hauilazimshwi. Si kwakuwa yeye ni mfalme na basi kila amtakaye atamtaka pia.

“Ninamfuatilia kujua kama ananipenda na yuko radhi kuwa nami, na si vinginevyo. Kama moyo wake haupo upande wangu, basi akatafute furaha uko kwingine. Si kwasababu mimi ni mfalme basi nina vibali vya mioyo ya watu.”

Jambo hili halikuwa jema sana kwa mzee wa baraza. Kwake ilikuwa ni lazima Tattiana afunge ndoa na mfalme kwasababu ya biashara yake. Kwake hilo halikuwa chaguo bali lazima. Hivyo akaapa kufanya jambo juu ya hilo lakini asisahau lililomleta, akaulizia na ratiba ya mwanajeshi yule kule kwa Tattiana. Mfalme akamweleza maelezo ambayo kwake aliyaona yana tija. Basi akaaga na kwenda zake.

Akasindikizwa na mawazo kichwani. Akafika nyumbani na kuteta na wanaye. Akawaambia juu ya mwanajeshi yule na ratiba zake na kisha akawatonya juu ya Tattiana na mahusiano na mwanaume mwingine.

“Inabidi mwanaume huyo ashghulikiwe upesi. Endapo akimfanya mfalme akamwacha Tattiana, basi tutakuwa kwenye hali mbaya sana.”

Basi akawapa wanaye kazi mbili, mosi kummaliza yule kibaraka wa mfalme, na pili wamshughulikie Roboth, yaani wamuue. Yote hayo yafanyike kwa siri pasipo kutengeneza venge la mashaka.

“Inafaa wakauawa kwa sumu ya siku mbili,” mzee akapendekeza.

“Tutaitolea wapi sumu hiyo?” akauliza Ottoman. Mzee akawapa kazi ya kwenda kumtafuta mbapa huko maporini na ni yeye ndiye atafanya utaalamu wa kutengeneza sumu hiyo kwa ustadi.

“Baba…” akaita Oragon, “Unamaanisha Mbapa nyoka?” akastaajabu.

“Ndiye mwenyewe,” mzee akaajibu. “Unadhani utaipata sumu kwa nyani?”

Hakutaka mjadala kwenye hilo, akawataka waende upesi kutekeleza agizo. Wakiwahi watamkuta jikoni akiandaa vihitajika.


***


“Tupumzike kwa ajili ya kupata chakula sasa,” akasema Malkia akishuka toka kwenye mgongo wa farasi. Wakasimamisha farasi zao na kuketi chini ya mti mkubwa wenye kivuli cha kutosha. Wakatoa vyakula kwenye vihifadhio vyao na kuanza kutafuna. Vilikuwa ni vyakula vikavu walivyovishushia na vinywaji.

“Hivi vyakula havitaweza kumaliza hata robo ya safari yetu,” alisema Seth. “Kuna haja ya kutafuta vyakula kama tunahitaji kuishi.”

“Tutavipatia wapi vyakula hivyo?” akauliza Zura. Malkia na Fluffy walikuwa watazamaji wakiendelea kutafuna.

“Humuhumu ndani ya msitu,” akasema Seth. “Kuna matunda na wanyama. Tukamate kadiri tuwezavyo kwani hatupo mbali na jangwa. Tusipokuwa na akiba ya kutosha, hatutaweza kutoka hai kwenye jangwa hilo.”

Kila mtu akakubaliana na wazo la Seth, wale kisha watazame ndani ya msitu nini watapata vya kutia mifukoni.

Seth alipomaliza kula, akanyanyuka na kusonga kando kwa ajili ya haja ndogo. Akarejea upesi na kufunga kila kitu kwenye mifuko na kuweka juu ya farasi. Lakini uso wake ulikuwa na mashaka, na mikono yake ilikuwa inatetemeka.

Malkia akamtazama na kumuuliza:

“Seth, kuna shida?”

Seth hakusema kitu. Akahema kwanza na kutazama chini. Alikuwa amepaliwa woga, ukimwona ukamjua.

“Tuondokeni upesi!” akaropoka akipanda juu ya farasi.

“Seth, kuna nini?” Fluffy akaropoka. Wakawa sasa wanatazama huku na huko kana kwamba wana miadi na vibwengo.

“Tumepita njia ya Azeth!” Seth akasema. Uso wake ulikuwa na mafinyazi ya woga. “Pandeni farasi tuondoke upesi kabla hatujakutwa hapa!”

“Si ulisema lakini …” Fluffy akataka tia neno, Seth akamkatiza, “Hatuna tena muda huo. Nilikosea! Panda farasi twende!”

Wakapanda farasi na safari ikaendelea kwa kasi mno! Seth akawaambia alipoenda kule kukojoa, kwa bahati akaona nyayo ya Azeth.

“Ni kubwa kutengeneza bwawa la kuogelea. Na nyayo hizo si za muda mrefu!”

Kama dakika tano kupita wakiwa wameshaondoka, jitu kubwa likafika kwenye mti waliokuwa wameketi wakila. Alikuwa amevalia ngozi ngumu yenye manyoya manyoya akiziba sehemu zake za siri. Masikio yake yalikuwa marefu, pua ndefu na macho makubwa yaliyozama ndani. Ndevu zake zilikuwa nyingi zikitiririka mpaka kitovuni mwake. Mkono wake wa kushoto alikuwa ameshikilia gongo kubwa.

Alikuwa ni mkubwa haswa. Tembea yake ilikuwa inatikisa ardhi na hata matunda yale yaliyokuwa yamekwiva mtini yakadondoka yenyewe.

Jitu hilo lililokuwa pweke, likatazama pale chini ya mti na kuokota mabaki ya chakula yaliyoachwa hapo. Akanusanusa mabaki hayo, akatupa macho yake huku na huko. Akatazama nyayo, akagundua kulikuwapo na binadamu na farasi wakiwa wamekatiza hapo.

Akatazama njia kwa urefu wake wote lakini hakuona kitu. Basi akapaza sauti yake kubwa akisema:

“Hababth hababth! Tefu na shik! Tefu na shik! Worota nabigh!”

Sauti yake ilikuwa kubwa mno zaidi ya ile ya kipaza sauti. Ilisafiri kwenda kila pande ya maeneo hayo ya karibu na wenzake wote wakaisikia. Habari habari! Kuna wavamizi! Kuna wavamizi! Funga malango!

Akarudia mara mbili kusema na kisha akaanza kukimbia. Sauti yake haikubagua, ikawafikia hata Malkia na wenzake.

“Wamegundua uwepo wetu!” Seth akaropoka. “Ongeza kasi!”

Wakakimbia haraka sana waking’ang’ania barabara. Lakini baada ya punde, mbele yao wakaona magogo makubwa yakirushiwa barabarani. Magogo hayo yalikuwa makubwa kiasi kwamba hawakuona hata mbele walipokuwa wanaelekea.

“Tunafanyaje sasa?” Zura akayuya kwa tepe za hofu. Kule mbele wakatokea majitu matatu waliotupia yale magogo njiani, wakaanza kusogea kuwafuata Malkia na wenzake.

“Geuza, tukimbie!” Malkia akaagiza. Basi upesi wakageuka na kuanza kurudi nyuma walipotokea. Napo hawakukimbia kwa muda mrefu, wakaona majitu mengine mawili yakijongea. Sasa hawakuwa na pa kukimbilia, isipokuwa pembeni, ndani ya misitu!

Haraka wakazama humo na farasi zao. Lakini farasi hawakuweza kukimbia sababu ya idadi kubwa ya miti, na hata matope, basi Malkia na wenzake, hawakuwa na budi, wakalazimika kushuka wakimbie kwa miguu.

Kabla hawajakimbia, Malkia akambusu farasi wake na kumnong’oneza. Farasi akakimbia upesi kuelekea kushoto kwake wakati mwenzake akiwa haelewi cha kufanya. Malkia akiwa nyuma, wakakimbia kadiri ya uwezo wa miguu yao, wakizama msituni, kujiokoa na majitu yaliyokuwa yanakuja kwa kasi ya kishindo kikuu!

Majitu hayo yakamkamata farasi aliyekuwa amebakia akisimama, wakamtafuna kama karanga! Kasi yao wakipasua na kusukuma miti ilikuwa kubwa, na punde wakawa wamewafikia walengwa wao kiasi cha kunyoosha mikono kuwadaka. Lakini ghafla wakasimama na kuwatazama Malkia na wenzake wakiendelea kukimbia kwa juhudi zote.

Hatua tatu mbele, mara Malkia na wenzake wakajikuta wameingia mtegoni. Ardhi ilifunguka wakazama ndani ya shimo kubwa lenye giza, huo ukawa mwisho wa mbio zao za sakafuni.

Baada ya muda mfupi, Malkia na wenzake wakawa wamefungiwa kwenye magogo makubwa, wamewekwa begani mwa majitu wakipelekwa wasikokufahamu.

Kwa mwendo wa kama dakika kumi, wakafika kwenye kijiji cha wana Azeth, kwenye kijiji hicho hakukuwa na nyumba hata moja bali mashimo makubwa. Majitu hayo yalikuwa yakiishi ndani ya mashimo hayo kama panya buku.

Magogo yakatupwa chini mbele ya jitu moja lililokuwa limevalia bangili na mikufu ya mafuvu ya vichwa vya watu. Kisha wale waliowaleta wakina Malkia wakainamisha vichwa vyao na kusema:

“Khari eta bumva … khari atta kevha.”

Lile jitu lililovalia mkufu wa mafuvu likabinua mdomo wake na kisha likasimama. Likanyoosha mikono yake juu ya kupaza sauti kuwaambia majitu yaliyokuwa yamesimama na kumtazama kwa ukakamavu.

“Veta zhi voyaaaaaa!”

Majitu yale yakaanza kushangilia yakicheza mithili ya watoto. Malkia akamuuliza Seth:

“Nini wanaongea?”

Seth akamwambia kwa sauti ya chini, na sura yake ikiwa imelowa huzuni:

“Wanatupeleka motoni!”

Kabla Malkia hata hajafikiria cha kufanya, magogo yakanyanyuliwa na yale majitu yakaanza kuimba yakielekea upande wao wa kaskazini. Wakafika kwenye tanuri kubwa, wakawasha moto.

Zura akamtazama Malkia, macho yake yalikuwa mekundu, akamuuliza:

“Malkia, ndiyo tunakufa?”

Malkia akamtazama pasipo kusema jambo. Akajikuta chozi linamtoka.

.
.
.
.
***
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom