*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II --- 11*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Nini wanaongea?”
Seth akamwambia kwa sauti ya chini, na sura yake ikiwa imelowa huzuni:
“Wanatupeleka motoni!”
Kabla Malkia hata hajafikiria cha kufanya, magogo yakanyanyuliwa na yale majitu yakaanza kuimba yakielekea upande wao wa kaskazini. Wakafika kwenye tanuri kubwa, wakawasha moto.
Zura akamtazama Malkia, macho yake yalikuwa mekundu, akamuuliza:
“Malkia, ndiyo tunakufa?”
Malkia akamtazama pasipo kusema jambo. Akajikuta chozi linamtoka.
ENDELEA
Hakushindwa kujinasua toka kwenye huo mtego lakini hakutaka kutoka peke yake. Hawezi kuokoa nafsi yake akawaacha wenzake wateketee. Akajikuta anajuta sana kwanini usiku kuamkia siku hiyo hakuwa amelala kwani angelipata kuyaona haya yote kwa kupitia njozi, na basi wakajiokoa.
“Teraneth abissa yaka yaka twee! Kashek vatta, munir vuninga!” akasema lile jitu lenye mkufu wa mafuvu ya binadamu. Mdomo wake ulikuwa mpana, sura ya kutisha, sauti kubwa ya kutetemesha anga. Akiwa hapa kwenye mwanga, akaonekana vema, kumbe jicho lake la kushoto lilikuwa limepooza, halikuwa linaona na rangi yake ilikuwa nyeupe kahawia.
Akaendelea kuongea na kuongea. Na majitu yote yalikuwa kimya yakimtazama na kumsikiza, lakini pia yakijawa na uchu kutamani nyama ya Malkia na wenzake. Hata sijui wangeweza kuwaganaje baada ya nyama hiyo kuchomwa.
Lakini katikati ya maneno hayo, mawingu yakaanza kujikusanya angani. Jua likamezwa, mwanga ukawa hafifu. Haikupita punde ndefu, matone ya mvua yakaanza kushuka taratibu taratibu, mara yakachanganyia kwa kasi. Moto wa tanuru ukazima!
Yule jitu lenye mkufu wa mafuvu ya binadamu likaagiza Malkia na wenzake wafunguliwe na wakatupiwe ndani ya jela kwa ajili ya kuchomwa siku au muda mwingine. Wakaenda kutupiwa ndani ya shimo na geti kubwa, zito la miti likaziba njia.
Ndani ya shimo kulikuwa kuna mwanga hafifu, na joto pia. Na maji ya mvua yalikuwa yanaingia sema pasipo kuwafikia. Shimo lilikuwa limechimbwa na kukukunjwa kona mbili. Maji yaliyoingia yalipitiliza kuzamia chini.
“Malkia, ile ilikuwa jitihada yako?” akauliza Zura. Malkia akatikisa kichwa.
“Hapana, sikufanya chochote kile. Pengine muda wetu wa kufa bado haujawadia.”
“Inabidi sasa tufanye jambo. Hatuwezi tukakaa kungojea mpaka tuje kuchomwa,” akashauri Fluffy. Seth akasafisha koo lake na kusema:
“Wanaamini Mungu wao hayupo tayari kuipokea sadaka yao na ndiyo maana mvua ikanyesha. Kwahiyo kwa sasa wapo kwenye maombi kumwomba Mungu wao akubali sadaka yao. Endpao Mungu wao akiikubali, basi watarudia zoezi lao muda kama huu kesho yake.”
Zilipopita kama dakika kumi, wakasikia sauti ya kufunguliwa lango, na mara kishindo kikubwa kilichowatikisa.
“Wanakuja!” Zura akapayuka. Wakasogelea ukutani kwa woga. Likatokea jitu moja lililowatazama kwa mahesabu, na kisha likamyaka Malkia.
“Shabi naba atruu!” akanguruma jitu hilo. Seth na wenzake wakajaribu kumkomboa Malkia pasipo mafanikio. Jitu lile liliwasukuma kwa kuwapiga kumbo kwa mkono wake tu, wote wakaachwa hoi hawajiwezi. Likaondoka na Malkia!
“Wanampeleka wapi?” akauliza Zura. Alikuwa ana hofu. Macho yake yalikuwa mekundu akihema kwa pupa.
“Sijui wanampeleka wapi,” akasema Seth. “Wamesema yeye ndiye ameteuliwa.”
“Ameteuliwa na nani?” Zura akauliza tena.
“Sijui!” akajibu Seth akipandisha mabega.
Malkia akapelekwa mpaka mbele ya yule jitu kiongozi, lilikuwa limeketi kwenye kigoda kikubwa chini ya mti mkubwa mithili ya mbuyu, nyuma yake lilikuwa limesimama jitu kubwa mkononi limebebelea rungu. Akaamrishwa apige magoti. Mvua bado ilikuwa inanyesha lakini chini ya mti huo haikuwa inapenya.
Yule Jitu likamwongelesha Malkia kwa lugha isiyoeleweka, Malkia akashindwa kujua dhamira yake nini. Kwa ishara akamwambia hamwelewi.
Kule shimoni, bado Seth na Zura walikuwa wanaendelea kuulizana maswali ambayo hayakuwa na majibu. Zura alikuwa anataka kujua Malkia atakuwa anafanywa nini huko alipopelekwa. Alikuwa anataka kujua kama kuna namna ya kumkomboa Malkia na wao wenyewe, maswali ambayo Seth hakuwa na majibu yake.
Ndani ya muda mfupi, wakasikia lango linafunguliwa na mara kishindo kikubwa. Wakamwona yule jitu ambalo lilikuja mara ya kwanza kumchukua Malkia. Likawatazama kwa mahesabu, na mara likaegesha macho yake kwa Seth na kusema;
“Bharu zuk pazam?” wewe ndiye unayejua lugha? Seth akatikisa kichwa chake akasema:
“Yu!” ndio.
Yule jitu likamnyakua Seth na kwenda naye. Likaenda kumtupia mbele ya kiongozi wao. Basi akaanza kuulizwa maswali na yeye akiyakalimani kumwelezea Malkia, na majibu ya Malkia akiyapeleka kwa jitu.
Jitu lile kiongozi lilikuwa linataka kujua wao ni wakina nani na wametokea wapi. Kwanini sadaka yao imekataliwa na mungu wao, haijawahi kutokea. Malkia akajieleza kinaga ubaga. Jitu lile likataka kujua kuhusu huko wanapoeanda, yani Misri. Malkia akamdanganya kwa kumwambia kuna kitu wanaenda kuchukua.
“Nabir sik batchu!” akasema yule jitu kiongozi. Yaani na yeye anataka kwenda huko. Malkia akakataa kwa jitihada zote, lakini lile jitu halikutaka kuelewa abadani. Akasema kama hawataki kwenda naye, basi atawatoa sadaka hata kwa lazima.
“Marheb na kebu. Tulisha mujhu na beedi!” akawapatia muda wa kufikiria na kutoa majibu mpaka pale kesho asubuhi. Jitu lile lililowaleta likawakusanya na kuwarejesha kwenye shimo na kuwafungia humo.
***
“Umemaliza kufanya kazi yako?” Sauti ya mama ikauliza. Roboth alikuwa chumbani na mama alikuwa amesimama mlangoni akiegesha sikio lake mlangoni.
“Nimemaliza kila kitu mama, tayari!” Roboth akajibu tokea ndani.
“Una uhakika? Unajua sitaki kugombana na mtu, Robo!”
“Nimemaliza kweli mama!” Roboth akapaza sauti. Mara huko nje ikasikika sauti ya farasi, mama akashtuka, na upesi akatoka kwenda kutazama. Akakuta farasi watatu wakiwa wamewabebelea wanaume watatu, wawili miongoni mwao walikuwa ni wanajeshi waliobebelea mikuki, na mmoja aliyekuwa ametangulia mbele, ni bwana Melkizedek.
Pasipo kusalimu, Melkizedek akashuka toka kwenye mgongo wa farasi na kumuuliza mama yupo wapi mwanaye, Roboth?
“Kuna nini bwana?” mama akauliza. “Karibuni ndani, si vema wageni kukomea nje.”
“Hauna sebule ya kunikaribisha mimi kuingia ndani. Mwambie huyo mwanao namhitaji hapa nje sasa hivi!”
“Amefanya nini lakini?”
“Muite hapa, na utajua.”
Mama akamuita Roboth. Melkizedek akamwambia akae mbali na mwanaye kama anataka usalama wa maisha yake na ya familia yake kwa ujumla. Akae mbali na mwanae, na akikaidi hayo yatamtokea puani. Alipomaliza kusema, akamgeukia na mama akamwambia amkanye mwanae, asilete damu yake ya kimaskini kwenye familia yao.
“Kwaheri,” Melkizedek akaaga na kwendaze. Mama akabaki ameduwaa. Akatazama Melkizedek mpaka anapotelea. Akamgeukia mwanae na kumuomba ajiweke mbali na watoto wa watu kwani yeye hataki matatizo na mtu.
“Unajua baba yako amefariki. Sisi ni familia isiyo na uwezo wala jina lolote ndani ya Goshen. Tafadhali jiepushe na watu wenye meno. Tafadhali Roboth!”
Roboth hakusema kitu. Akainamisha uso wake na kuingia ndani, chumbani. Akajilaza na kulia kwa kumwaga machozi. Akajikuta anauchukia sana umasikini kuliko shetani. Moyo wake ukamuuma sana kwanini hali yake ni dhalili.
Hakubanduka hapo kitandani mpaka jua lazama, usiku unaingia.
Kwenye majira ya saa sita ya usiku kwa mishale ya saa ya sasa, Roboth akakurupuka kitandani akiwa anakohoa. Hali ya hewa ilikuwa nzito, na kadiri alivyokuwa anahema, ndivyo alivyokuwa anakohoa. Akasikia vishindo vya watu dirishani. Haraka akafungua pazia kutazama. Kwa mbali akaona watu wakiyoyoma.
Hakuweza kuzingatia kwa maana alikuwa anakohoa sana. Mama yake akaamka upesi na kuja kugonga mlango. Akamkuta mwanaye anakohoa na huku akivuja jasho jingi. Akamuuliza nini shida, Roboth akashindwa kuongea kwani alikuwa anakohoa kupita kiasi. Alipokuja kutulia, akamwambia mamaye ameona watu wakiwa wanayoyoma.
Zikapita dakika kadhaa, Roboth akatulia na kumweleza vema mama yake. Hakupata usingizi tena, akajilaza akawa anatazama huku na huko.
*****