SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II --- 14*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

"Seth, una uhakika na kile ulichokisema?" Malkia akauliza.

"Ndio, kwa asilimia zote. Usijali," Seth akasema kwa kujiamini akitikisa kichwa. Safari ikaanza.

Hakukuwa na maongezi sana huko njiani. Kabla hawajakiacha mbali kijiji cha Azeth, farasi wa Malkia akajiri tokea misituni. Malkia akamkumbatia na kumpanda mnyamawe anayempenda.

Lakini walivyotembea kwa umbali mfupi tu, farasi huyo akaanza kulegea na kukosa nguvu. Ghafla akadondoka chini na kupoteza fahamu. Malkia pamoja na wenziwe wakastaajabu nini kilitokea.

Jitu moja, kati ya wale majitu mawili ya Azeth, likampekua farasi huyo kwa kumnusa na kumkagua mwili, kisha likasema:

"Venerdi kashaka!"

"Anamaanisha nini?" Malkia akawahi kuumuliza Seth.

"Amepewa sumu!" Seth akajibu upesi.

"Waulize kama kuna namna ya kunsaidia, tafadhali!"

Seth akafanya hivyo. Malkia akaona majitu yale yakitikisa kichwa.

"Tafadhali, waombe wamsaidie. Tafadhali!" Malkia akasisitiza.

Seth akawaambia. Wale majitu wakamjibu kuwa farasi huyo atakuwa amekula majani ya sumu, au amepewa sumu.

"Na wakina nani?" Malkia akawahi kuuliza.

ENDELEA

Wale majitu ya Azeth wakatazamana na kuteta kidogo, alafu mmoja akamtazama Seth na kumpatia majibu.

"Wanaasema hapa karibuni kuna binadamu huwa wanakuja kuwinda, huwaua wanyama kwa kutumia sumu na hata huwa wanawadhuru wao kwa kutumia sumu hiyo. Wanadhani hao ndio watakuwa wanahusika."

"Na dawa je?" Akauliza Malkia. Seth akamjibu na dawa pia inapatikana kwa hao watu, lakini ni hatari sana kwenda huko kwani si watu marafiki.

"Malkia, ni bora tukaendelea na safari," Seth akashauri. Malkia akakaa kimya kwanza, wote wakimtazama, mara akanyanyuka na kusema:

"Siwezi nikaondoka, na siwezi kuendelea na safari hii mpaka pale nitakapomtibia farasi wangu."

"Lakini Malkia, ni hatari!" Akasisitizia Fluffy. Malkia akamtazama na kumwambia:

"Huyu farasi si tu mnyama kwangu, bali familia. Tangu nikiwa mtoto amekuwa nami mpaka sasa. Siwezi nikamwacha sasa, afe nami namtazama."

"Sasa utafanyaje? Wataka kwenda hivi?" Akauliza Seth.

"Nitaenda. Hata kama ikinibidi niende mwenyewe," Malkia akajibu kwa kujiamini.

Seth na wenzake wakabaki wakitazamana. Hawakujua cha kufanya. Hawawezi kumwacha Malkia aende peke yake, ila si kutafuta visa huku? Kwenda tena kufanya vita na watu wengine na huku wametokea pona chupu?

"Ni wapi walipo watu hao?" Akauliza Malkia kwa kupaza sauti. Seth akamtazama akitamani kumzuia.

"Fanya upesi, maana muda haupo upande wangu!" Malkia akasihi akimtazama kwa macho yasiyo na utani. Upepo ukavuma kuinamisha miti na kukimbiza ndege.


***


Giza lilikuwa linaingia sasa, taa za makazi ya zamani ya Rhoda bado hazikuwa zimewashwa na chumbani kulikuwa kuna mzozo ukisikika. Mzozo huu haukuwa wa mwingine, bali wa wale bibi walozi toka Tanashe.

Walikuwa wamesimama wima, mwili wa Rhoda ukiwa kitandani, ila hawakuwa watatu, bali wawili, nyuso zao zikiswahibu mambo hayakuwa shwari hata.

Wakinyoosheana vidole vyao virefu, na wakitoleana macho ambayo kila mmoja wao alikuwa analo moja moja! Wakapayuka na kupaza sauti.

"Mpaka lini?" Mmoja akauliza.

"Sasa unadhani tutafanyaje na ndivyo imekuwa vivyo?" Mwingine akajibu kwa kuuliza.

"Tutafanyaje!" Mwenzake akatahamaki. "Tukiendelea hivi, tutafikia wapi? Tumekuja huku kunywa damu za watu ama kushika dola?"

"Natambua hilo. Na si kosa la yeyote yule kati yetu!"

"Vipi kama akikamatwa huko? Vipi ikagundulikana? Itakuwa bahati yetu kama tukarejeshwa Tanashe tukiwa hai. Si tu kwamba tutapoteza uhai, bali lengo lililotuleta huku!"

"Sasa wapaza koromo na mtu angali hayupo? Yasaidiani?"

"Napaza kwakuwa wewe ndiye ulikuwa naye mara ya mwisho kabla hajatokomea tena. Ulishindwa mzuia? Ama amekupa nawe ahadi ya kukuletea pande la nyama ya binadamu?"

"Hakuniaga! Na sikuwa naye tukisongamana kama vifungo. Sijui na wala sihusiki na tukio lake la kwenda huko!"

Kukawa kimya kidogo wakivuta kwanza pumzi na kupunguza msongamano wa pumzi za jazba vifuani mwao. Wakaketi kila mtu akigeukia upande wake. Mwili wa Rhoda ulikuwa katikati yao.

"Tulipanga kwenda kuonana na mfalme, hayajatimia kisa yeye, siku imeisha. Tuliweka mwili wa binadamu yule mlevi ukauke kwa ajili ya kutengenezea dawa, kaumaliza kwa kuutafuna." Akasema kikongwe mmoja akishika tama.

"Hatuwezi kumbadili, tumesema na sasa imeshageuka kuwa matumbuizo masikioni mwake. Amekuwa samaki mkavu, sufuriani hatoshi," akasema mwingine. Wote wakiwa wameshika tama.

"Hakuna namna, inabidi tufanye maamuzi magumu," akasema mwingine.

"Yapi hayo?"

"Kummaliza!"

"Unasema?"

"Ndio, kama ulivyonisikia."

"Huoni kama tutakuwa tumeenda mbali sana?"

"Itabidi twende huko mbali kama njia ya karibu hamna. Unafikiri ni nini tutafanya? Hatuwezi tukamfungia, atatoka. Hatuwezi kumrudisha Tanashe."

Mara wakasikia sauti ya mlango ukisukumwa huko sebuleni. Haraka wakatazama kioo chao cha kilozi na kugundua ni mwenzao.

"Anarejea!"

Mlango ukarejeshewa na mlozi huyu aliyeingia, akapaza sauti akiulizia wenzake kama wapo. Akawasha taa zao za maginga ya moto na kisha akapandisha ngazi kuelekea juu kuwakuta wenziwe.

Akafungua mlango asione kitu. Kitanda kilikuwa kitupu, hawakuwepo wale vikongwe wala mwili wa Rhoda! Akapaza sauti kuita wenzake akijiuliza wapi walipo.

Napo mule chumbani akawasha ginga la moto lililokuwa linaning'inia ukutani. Akaangaza kushoto na kulia, hakuona kitu. Akaguna na kuketi kitandani. Nguo yake ilikuwa ina mabaki ya damu kwa shingoni na kifuani.

Akanyanyuka na kwenda kabatini, akafungua na kuangaza. Ila ghafla akahisi kuna watu nyuma yake, basi akageuka upesi. La haula! Akaona panga likiwa hewani, hajahema, likamkita kichwani na kudondoka chini!

Haikupita muda mrefu, vikongwe wawili wakatoka ndani ya jengo wakiwa wamebebelea kifurushi cheusi. Wakiwa wamejawa na tahadhari wakaelekea nyuma ya nyumba na kuchimba shimo kisha wakazamisha kifurushi kile ndani yake.

"Kazi imekwisha," mmoja akasema akikung'uta mikono yake. Basi wakatoka huko nje na kurudi zao ndani.

"Tutamkumbuka sana."

"Hakika! Hatujawahi kuwa pungufu namna hii, ila sasa tunaweza tukatimiza mipango yetu."

Wakapandisha juu kuelekea chumbani. Ila muda si mrefu, mlango ukagongwa mara tatu. Wakatazamana na kuulizana kabla hawajateka kioo chao na kutazama. Wakamwona askari akiwa amesimama na mwanaume mmoja ambaye hawakumtambua.

"Unahisi nini?" Akauliza mmojawao. Punde wakashuka chini wakiwa tayari wamevalia mwili wa Rhoda.

"Vipi muda huu?" Wakauliza.

"Tafadhali, tumekuja kufanya ukaguzi," akajibu Askari. Na kumbe yule mwanaume aliyekuwa kando yake alikuwa ni yule mlevi ambaye mwenziwe alikufa baada ya kuingia ndani ya jengo la walozi hawa.

"Ukaguzi?" Akatahamaki Rhoda. "Kuna nini?"

"Madam, hamna maelezo ya ziada kwenye hilo. Tunaomba tuongozane wote kwenda ndani," Askari akasema kwa mkazo. Basi wakazama ndani kupekua kama Rhoda yu mwenyewe. Walipomaliza pasipo matunda, wakamtaka waelekee uani.

Rhoda akasita. Akamtazama yule mlevi kwa jicho hasidi, ila mwishowe wakaamua kuelekea huko.

"Fukua!" Akaamuru askari akimkabidhi Rhoda chepeo. Mpaka hapo wale vikongwe wakatambua kuwa watakuwa wameonekana walipokuwa wamemzika mwenzao.

Wafanye nini? Wakaanza kujadiliana ndani ya kifua cha Rhoda.


***
 
MKUFU WA MALKIA II --- 15*
*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

"Tafadhali, tumekuja kufanya ukaguzi," akajibu Askari. Na kumbe yule mwanaume aliyekuwa kando yake alikuwa ni yule mlevi ambaye mwenziwe alikufa baada ya kuingia ndani ya jengo la walozi hawa.

"Ukaguzi?" Akatahamaki Rhoda. "Kuna nini?"

"Madam, hamna maelezo ya ziada kwenye hilo. Tunaomba tuongozane wote kwenda ndani," Askari akasema kwa mkazo. Basi wakazama ndani kupekua kama Rhoda yu mwenyewe. Walipomaliza pasipo matunda, wakamtaka waelekee uani.

Rhoda akasita. Akamtazama yule mlevi kwa jicho hasidi, ila mwishowe wakaamua kuelekea huko.

"Fukua!" Akaamuru askari akimkabidhi Rhoda chepeo. Mpaka hapo wale vikongwe wakatambua kuwa watakuwa wameonekana walipokuwa wamemzika mwenzao.

Wafanye nini? Wakaanza kujadiliana ndani ya kifua cha Rhoda.

ENDELEA

Haikupita muda mrefu, mara Rhoda akageuka na kumzaba Askari kwanguvu kwa chepeo, Askari akadondoka chini na kuzirai! Kisha akamtazama yule mlevi ambaye tayari alikwishakaa mbali kwa woga.

Akamwambia akimnyooshea kidole:

"Kifo kinakuita. Na hicho ndicho utapata kama malipo ya kufuatilia ya Ngoswe!"

Ajabu ni kwamba mara hii sauti ya Rhoda ilikuwa ni yale vikongwe kabisa na si ile ya kuigiza. Basi yule mlevi akaogopa na moyoni akahisi ni jini lipo mbele yake. Akasisimika ngozi na kusimamisha vinyweleo.

Rhoda akapandisha chepe lake juu kwanguvu, kufumba na kufumbua, akautupa mkonowe alambe kichwa cha mlevi yule 'mchonganishi', vuuuup! chepe likapita kando! Mlevi alilikwepa na kudondoka chini! Haraka akanyanyuka na kukimbia kama mwehu.

"Hawezi kutoroka!" Rhoda akafoka na sauti yake ya kizee. "Hawezi kuwa hai!"

Akaanza kumkimbiza mlevi yule kwanguvu zote akitaka kummaliza kuzika ushahidi. Haki mwendo wake ulikuwa mkali na punde ndogo tu akawa amemfikia mlengwa wake, lakini kabla hajamdaka, mlevi akapiga kelele kali za woga. Kuna watu walikuwa wanapita kwa mbali, wakasimama na kutazama, Rhoda akajificha upesi na kumwacha mlevi atokomee!

"Ni jinii! Ni jiniiii!" Mlevi alikuwa anapayuka visigino vya miguu yake vikigusa kisogo. Lakini nani atamzingatia mlevi? Wakamtazama wakimkebehi:

"Ama kweli pombe si supu!" Kisha wakajiende zao. Huku Rhoda akiachwa na manung'uniko na majuto!

"Nini sasa tumefanya?"

"Usijali sana, yu mlevi. Umeona, kinywa chake hakitaaminika."

"Nani kasema? Mbona kimetuletea askari?"

"Sasa tungefanyaje? Kumkimbiza mwehu aliyekwapua nguo kipindi tunaoga? Lisingetufanya tukaonekana wazima!"

"Hapana! Hapana! Ni lazima tumpate na kumuua. Tena mwili wake tuukaushe na kuutokoa dawa. Yeye ndiye mtu pekee hatari kwetu aliyebakia. Si salama moyo wake kuendelea kudunda," wakajadili wakiufuata mwili wa Askari waliounyanyua na kuuingiza ndani.

Wakauficha na kukubaliana kuutokomeza kwa namna ya kilozi. Lakini pia usiku ule usikome mpaka pale watakapomtia mikononi yule mlevi, na kumtenda vile wanataka.

Kujua siri za ndani, ni kazi ya mwandani na si hayawani. Akiijua hayawani, siri haipo sirini bali kinywani. Yeye ni nani? Lazima afukiwe chini! Chini! Chini! Wakaimba vikongwe. Na kisha wakacheka kuujaza usiku.


***


"Hapa ndipo penyewe?" Akauliza Malkia akikodoa.

"Ndio, kama kweli watakuwa wametuelekeza vema," akajibu Seth. Walikuwa wamejibana nyuma ya mti mkubwa wakitazama vibanda fulani vilivyokuwa vimerundikana. Vibanda hivi vilikuwa vina mwanga hafifu, na watu kadhaa walionekana huku na kule wakiwa ni wafupi kimaumbo.

Walikuwa wamevalia ngozi za wanyama kuziba sehemu zao za siri. Usoni walikuwa wamejichora michoro ya ajabu kwa kutumia wino mweupe. Kichwani walikuwa wamevalia mataji ya majani makavu.

"Sasa?" Akanong'oneza Seth akimtazama Malkia.

"Tumkamate yeyote yule," Malkia akajibu. "Si walisema yeyote anajua kuhusu dawa?"

Wakapanga cha kufanya. Muda si mrefu wakafanikiwa kumvuta mmoja kwa kuigiza sauti ya mnyama na kuchezesha majani. Wakamziba mdomo na kumlaza chini, Seth akamuuliza kuhusu dawa.

"Totos tatip!" Akajibu kiumbe kile akitoa macho makali.

"Anamaanisha nini?" Malkia akamuuliza Seth.

"Anasema hatuelewi!" Seth akajibu na kisha akabadili lugha kumuuliza yule kiumbe kwa lugha anayoijua. Bado wakaambulia patupu. Mateka hakuwa tayari kusema kitu.

"Mwambie hatuna muda, na akiendeleza ukaidi tutamuua!" Malkia akasisitiza, Seth akafikisha ujumbe. Lakini kwa kebehi, kiumbe kile kikajibu:

"Haogopi na yuko tayari kufa!"

Malkia akaweka upanga wake shingoni kwa mateka huyo na kuubinyia hapo. Akatishia mtu huyo aseme, lakini bado hakufua dafu.

"Nadhani ni bora tukaenda naye. Hapa si salama, ataenda kusema huko huko mbele ya safari!" Seth akapendekeza. Malkia akaona ni sawa, wakamfunga yule mateka na kumlazimisha atembee.

Lakini mateka akaendeleza ukaidi. Na mara hii, akafanya ujanja wa kutaarifu wenzake kwa kutumia sauti ya mluzi. Kabla Seth hajawahi kumfumba mdomo, tayari ujumbe wa kutosha ulikuwa umeshawafikia wenzake.

Hawakuchukua muda mrefu, wakazingirwa na wanaume watano wakiwa wamebebelea silaha walizoziweka mdomoni. Zilikuwa ni mabomba madogo yaliyobebelea sindano zenye sumu!

"Seth, usiniambie tunatekwa tena!" Malkia akafadhaika. "Hapana, inabidi tufanye namna."

Lakini kabla hawajaifanya hiyo namna, wakastaajabu wamechomwa mwilini na sindano za sumu. Hawakuchukua hata sekunde tatu, wakadondoka chini wakiwa wamepoteza fahamu!
.
.
"Pengine itatuchukua muda kuliko tunavyodhani..."

"Na unavyodhani, hakuna namna nyingine ya kufika huko upesi?"

"Una maanisha njia za mkato?"

"Ndio!"

"Labda zipo. Ila hakuna ninayoijua, mimi sijawahi kufunga safari kwenda Misri!"

"Hata mimi pia, nilidhani labda unaweza ukawa umesikia."

"Hapana. Ila naamini Seth atakuwa anafahamu."

"Seth? Naogopa sasa kila atakaloniambia."

"Kwanini?"

"Hukuona alipotupeleka?"

"Huwezi jua. Ni mara yake ya kwanza tu, bado namuamini."

Malkia alisikia sauti hizo zikilumbana kwa mbali masikioni mwake. Akafungua macho na kuangaza. Kulikuwa kuna mwanga, lakini hakuwa anaona vema, aliona maruweruwe na mwanga mkali wa jua ulikimbizia uso wake pembeni.

Alikuwa juu ya kitu kinachotembea akiwa amelazwa. Kando yake pia kulikuwa kuna mtu amelazwa kama yeye.

Ilimchukua kama dakika moja mpaka alipoanza kuona angalau, japo si vema. Ni kama vile ukungu ulikuwa umejaa machoni mwake. Aliwaona watu kwa mbali, akawatambua kama Fluffy, Zura na wale majitu mawili wakiwa wanatembea.

Akakohoa.

"Zura, Malkia ameamka!" Fluffy akaropoka kwa furaha. Haraka wakamsogelea Malkia na kumuuliza hali yake. Hapo Mallkia akatambua yeye na Seth wamewekwa juu ya kibebeo kidogo cha mbao juu ya farasi.

Macho yake bado hayakuwa yanaona vema. Na kando yake, Seth bado hakuwa ameamka
"Tumefikaje hapa?" Akauliza Malkia kwa mbali. Akajaribu kuamka lakini akashindwa, hakuwa na nguvu.

"Tulikuja kuwaokoa," akajibu Fluffy. "Ila pasipo msaada wa hawa Azeth tusingeweza abadani!"

Zura akamkatiza.

"Nadhani ni sahihi ukapumzika, Malkia," akasema akiwa amemuwekea kiganja kwenye paji lake la uso. "Mlidungwa sumu kali na wale watu. Miili yeni imechoshwa sana kwani mlikuwa mkitota sana. Pumzika sasa, tutaongea hapo baadae."

Malkia akataka kunyanyuka. Zura akamrudisha chini.

"Tafadhali. Kama unataka kuishi, fanya ninachokuambia, Malkia. Bado tunakuhitaji."

Malkia akataka kusema jambo, ila kichwa na macho vikamzidi uzito, akapitiwa pasipo ruhusa!

"Unadhani atakuwa sawa?" Akauliza Fluffy.

"Natumai atakuwa sawa. Yeye ni Malkia, hakuna hii safari pasipo yeye."




***
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom