*MKUFU WA MALKIA (MSIMU WA II) – 03*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Kichwa chake kilikuwa kimewekwa kifuani mwake wakati kiwiliwili kikiachwa solemba. Kiwiliwili hicho kilikuwa kimetuama kwenye dimbwi zito la damu!
Wanajeshi wakahamaki na kushikwa na hofu. Haraka wakatoka na kwenda kwa Dummy wakampashe habari. Lahaula! Hawakumkuta Dummy, bali mwili wa Dummy! Dummy alikuwa amekufa!
Alikuwa ananing’inia na kamba shingoni. Kamba iliyojishikiza kwenye kingo ya dirisha. Wanajeshi wakatokwa na macho.
ENDELEA
Kila kitu kilich0kuwa kinatokea mbele ya macho yao hawakuwa wanaamini. Ni kama vile mchezo wa kuigiza! Hawakuelewa nini kinaendelea na nani anasababisha. Zikapita dakika kadhaa na mara wanajeshi hao wakaseikia kelele huko nje.
Kutoka kutazama, wakamwona Malkia akiwa beneti na Fluffy, Seth na Zura. Watu hawa walikuwa wamesimama juu ya jukwaa, na watu wakiwa wamekusanyika kuwatazama.
Mara wakakamatwa na wenzao na kuwekwa chini ya ulinzi. Wakaona na wenzao wengine nao wakiwa chini ya walinzi. Wakafahamu sasa mapinduzi yao yamekwama. Kule mbele wakaona na wale wanaume wafanyabiashara waliokuwa wanahusika na mapinduzi.
Walikuwa wamepiga magoti wakiinamisha vichwa vyao chini. Nyuma ya migongo yao walikuwa wamesimama wanajeshi waliokuwa wamebebelea silaha. Mapinduzi yalikuwa yamekomea mbele ya midomo ya bunduki!
Malkia akapaza sauti yake, na watu wote wakanyamaza. Akaeleza kila njama iliyokuwa imepangwa juu yake, kila hatua na kila mwenendo. Namna alivyokuwa amejifanya mjinga kwa kutokujua chochote, na namna ambavyo aliacha watesi wake wajigambe na kujivuna.
“Hakuna mtu anayejua nguvu na uwezo wangu, hata mimi pia. Kadiri ninavyopitia matatizo na changamoto, ndivyo ninavyovumbua na kujua uwezo wangu zaidi na zaidi! Lisilokuua linakutia nguvu.”
Lakini zaidi Malkia akaeleza namna gani alivyoumizwa na njama hizo, kwani ni kiashiria cha kutokuwa na imani naye. Zimemfadhaisha na kumfanya ajihisi mtupu kwani kwake alikuwa ameachukulia kama sehemu za familia. Kutaka kummaliza kumemfanya ajihisi yatima.
Wakati akieleza hayo machozi yakambubujika. Akashindwa kuongea, Zura akambembeleza na kumfuta machozi. Kisha akaendelea na kusema. Akashukuru kwa yote na sasa umefikia wakati wa yeye kuondoka.
Pale hapakuwa nyumbani, na hata jitihada zake za kupageuza kuwa hivyo, hazikufanikiwa! Sasa anataka aende awaache kama alivyowakuta, na ulimwengu wao wa kibabe, kumwagana damu!
“Inatosha. Nitatafuta nyumba yangu pale ilipo. Nitarejea kwetu.”
Baada ya kusema hayo akashuka zake na kuongoza njia mpaka kwenye farasi wake. Akamkwea, nyuma akiongozana na Zura, Fluffy pamoja pia na Seth.
Ingawa watu walimwomba Malkia asiondoke, kwa machozi na manung’uniko, vilio na simanzi, Malkia hakukata shauri na kubaki. Alifunga masikio na macho, akaenda zake.
Japokuwa ilikuwa ni nyakati za usiku, safari yake haikukoma. Wakatembea kwa umbali wa nusu saa kabla hawajaamua kusimama na kupumzika. Baridi lilikuwa kali. Upepo ulikuwa unapuliza sana.
Wakatandika shuka chini na kumruhusu Malkia ajilaze kwanza. Alafu wakatandika na mashuka yao baada ya kuwasha moto wa kuwapasha joto. Moto ulikuwa mkubwa mno kiasi cha kuonekana hata kwa umbali mrefu.
Hapo ndiyo Fluffy akamweleza Malkia juu ya karatasi yake, ile ambayo mama yake alimkabidhi. Karatasi iliyokuwa inaeleza juu ya siri za huko Misri. Malkia akawahi kumuuliza karatasi hiyo ipo wapi kwani amekuwa akivutiwa sana na habari za himaya ya huko.
Fluffy akamwambia ilikwapuliwa, hanayo tena.
“Haukumbuki hata kidogo?” Makia akamuuliza. Fluffy akatikisa kichwa, na kabla hajasema jambo Seth akadakia. Yeye anaikumbuka karatasi hiyo kwa kichwa. Fluffy na Malkia wakamtazama kwa macho ya mshangao.
“Kweli?” Fluffy akauliza. Kuthibitisha ambacho alichosema ni kweli, akatoa taarifa chache za huko. Alah! Alikuwa anakumbuka kana kwamba anasoma mahali.
“Twaweza kwenda huko?” Malkia akauliza. Lakini kabla hajajibiwa na yeyote, mwenyewe akajikosoa. Huko palikuwa mbali sana. wanahitaji rasilimali ambazo hawana kwa muda huo.
Fluffy akapendekeza jambo, wakiwa nyumbani kwao kwa ajili ya mapumziko, watafute jambo la kufanya na kuanza kujipanga kwa ajili ya safari hiyo ambayo inaweza kubadili kabisa maisha yao.
Lakini Zura akawakatisha, na akamkumbusha Malkia jambo. Ya kwamba anaweza kufanikisha hilo kwa kutumia mkufu wake. La hasha! Malkia akasema. Hawezi kwenda mahali ambapo hapafahamu.
“Mkufu haukumbuki sehemu mpya, lah! Unakumbuka mahali ambapo ulishawahi kuwapo.”
Wote wakakubaliana kutafuta njia. Ilibidi safari hiyo ya kuelekea Misri ifanikiwe wakiamini kila kitu kina mara ya kwanza.
Huko Misri wanaenda kutafuta kofia ya dhahabu ya Farao, kofia ambayo ilikuwa na madaraka ndani yake. Nguvu ndani yake. Mamlaka ndani yake! Kofia ambayo imefichwa kwa miaka mingi sasa.
Na aliyeificha akifariki akiwa amemwambia siri hiyo mtu mmoja tu. Mtu ambaye ameshakuwa mzee na sasa hana haja nayo. Mzee huyo anayeishi kando kando ya bahari ya Mediterania.
Lakini kwenda mbele na nyuma, kupata kofia hiyo haikuwa kitu chepesi wala cha mzaha. Kulikuwa kuna majaribu kadha wa kadha ndani ya Piramidi ya Giza! Majaribu ya nguvu za giza.
Majaribu ya vinyamkera na vitu visivyoeleweka. Kubwa zaidi ikiwa ni kupambana na jeshi la wafu waliokufa na kufukiwa kwa miaka alfu mbili sasa!
Juu ya yote haya, bado Malkia na wenzake walikuwa na imani. Isipokuwa Zura. Moyo wake haukumtuma na aliona safari hiyo ni kujipeleka kwenye domo la simba mwenye njaa!
Lakini hakukatisha watu tamaa. Akakaa na jambo lake kifuani akiamini pengine hali inaweza ikabadilika muda wa mbeleni, ama siku za usoni.
Asubuhi wakaendelea na safari yao.
***
“Nimeshakamilisha kila kitu,” akasema bibi mmoja kuwaeleza wenzake. Yalikuwa ni majira ya asubuhi iliyo tulivu na yenye giza. Walikuwa wamesimama ndani ya sebule yao wakijiandaa kwa ajili ya tambiko.
Tambiko na zindiko zito la kunuwia madaraka na mamlaka juu ya mwili wa Rhoda. Mwili waliokuwa wameuteua kwa ajili ya zoezi lao la kutoka ndani ya himaya ya Tanashe.
Uchaguzi wao ulizingatia jinsia lakini pia na mamlaka aliyokuwa nayo mhusika ndani ya himaya ya Gosheni.
Kama kawaida kulikuwa ni giza ndani. Mishumaa ilikuwa imewashwa na kitabu chao kikubwa cha kilozi kilikuwa kimefunguliwa na kutengwa mahali palipokuwa panahitajika kusomwa.
Kurasa mia tano hamsini na mbili!
Mwili wa Rhoda ulikuwa umelazwa juu ya kiti, ukiwa hauna fahamu. Miili ya Bonasi na Tretho ilikuwa pembeni kwa ajili ya kutoa damu ya kafara. Nayo si kwamba haikuwa na fahamu, bali haikuwa na uhai.
Basi bibi yule mmoja, ilikuwa ngumu kuwatofautisha kutokana na ufanano wa mavazi na sura, akasoma kilichokuwa kitabuni kwa sauti kubwa. Alipomaliza aya moja tu, radi zikaanza kutia na kunguruma huko nje!
Pepo kali ikapuliza lakini haikuzima mishumaa!
Bibi akasoma ukurasa mmoja mzima, akafungua ukurasa mwingine wa pili. Mara mwili wa Rhoda ukasimama na kukakamaa kana kwamba sanamu. Bibi akaendelea kusoma.
Akiwa amebakiza aya tatu amalize ukurasa, mwenzake mmoja akausogelea mwili wa Rhoda na kusimama mbele yake. Aya moja iliposomwa na kuisha, mara bibi huyo akazama ndani ya mwili wa Rhoda!
Ikafuatia aya ya pili, na hapo bibi mwingine, wa pili, akasimama mbele ya Rhoda. Aya hiyo ilipomalizika, naye akazama ndani ya mwili wa Rhoda. Sasa akabakia bibi mmoja tu.
Akabeba kitabu akiendelea kusoma aya iliyobakia. Alipoimaliza, naye akapotelea ndani ya mwili wa Rhoda. Kitabu kikadondokea chini! Rhoda akafungua macho. Macho yake yalikuwa na rangi nyekundu wakati kiini chake kikiwa cha kijani!
Hapo Rhoda akawa ni wakati uliopita. Mwili ulikuwa wa Rhoda lakini nafsi na roho zilikuwa za wale bibi!
Zikapita dakika kumi. Mara ikatokea rundo moja kubwa la popo lisijulikane limetokea wapi! Popo hawa wakazingira nyumba ya wale bibi na kuifunika kabisa kana kwamba ni giza, hamna kitu! Popo hao wakajikusanya na mara akatokea binadamu.
Binadamu huyo hakuwa mwingine bali kaka yake Venin! Macho yake mekundu yalikuwa yamebebelea ghadhabu. Nywele zake nyeupe kama sufi zilikuwa zinapepea pamoja na nguo yake.
Akatazama na kusaka huku na huko. Akaona kitabu chini na miili ya Tretho na Bonas. Mwanaume huyo akapiga kelele kali. Akalia.
Alishajua nini kilichofanyika na tayari alikuwa katika kundi la mkosaji. Akalalama, akageuka kundi kubwa la popo na kupotea eneo hilo kufumba na kufumbua!
Akaenda kuranda randa huku na huko kutafuta wale wabibi na kumtafuta Rhoda lakini hakuona kitu ndani ya himaya.
Mwili wa Rhoda ulikuwa tayari umeshatoka ndani ya himaya! Mlozi huyu akawa hana cha kufanya zaidi ya kuutazama ukitokomea. Roho ikimuua na kumsuguza.
***
"Tattiana!" Sauti ya mama ikaita baada ya kugonga mlango mara tatu. Kimya.
Mama akaendelea kugonga na kuita. Bado kimya. Mtoto hakutoka ndani tokea jana yake mpaka muda huo sasa ukielekea kuwa mchana.
Hakula chakula cha usiku na wala chai hajatia tumboni.
Mama akaita mara tano kabla hajaamua kuacha na kwenda sebuleni kumuita Fanty ambaye naye alimwambia amejaribu sana pasipo mafanikio. Tattiana hakuufungua mlango.
"Atakuwa ana shida gani?" Mama akauliza akiwa na uso wa mkanganyiko. Wakafika mlangoni na Fanty akaambiwa auvunje mlango wakapate kumjulia hali.
Fanty pasipo hiyana akauvunja mlango. Ndani wakamkuta Tattiana akiwa amelala kitandani. Hata hakushtuka! Wakamsogelea na kumwamsha, Tattiana hakuamka!
Tattiana hakutikisika!
Tattiana alikuwa amekunywa sumu.
****