SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN – 01 (Msimu wa Pili)*
*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

“Nimewapa muda ili mnipe sababu za kuwaachia uhai wenu.”

Hawakujua anayenena ni nani. Wakauliza ila hawakujibiwa. Walitawaliwa na hofu kubwa. Ukapita kama dakika tatu, na mara popo wakavamia eneo hilo. Wakatanda kiti na mara akatokea mtu hapo!

Popo wale wote walipotelea ndani ya mwili wa huyo mtu. Yaani yeye ndiye aliyekuwa popo hao wote.

ENDELEA

Mtu huyu alikuwa ni yule kaka yake Venin! Uso wake ulikuwa unatisha na mwili wake ukiwa mwembamba na mweupe pe! Macho yake yalikuwa mekundu na nywele zake zikiwa ndefu na nyeupe kama sufi.

Akatabasamu na kumtazama Rhoda, akamtazama na Tretho na kisha Bonas. Wote walikuwa na hofu kwenye viini vya macho yao. Basi akafurahi zaidi na kuwataka watu hao wampatie sababu za yeye kuwaacha hai.

Akawaambia damu zao ni muhimu mno kwake. Alikuwa anawatazama tokea muda kwani alikuwa anatarajia ujio wao tangu pale ambapo mdogo wake alimwambia kuwahusu.

“Yule mjinga alinitaarifu juu ya ujio wako. Na hata akadiriki kuwaombea niwabakize hai. Lakini sasa akasahau namna gani ninavyotaka kutoka katika ardhi hii ya kijinga. Nataka kuwa huru. Nataka kuurejea utawala wangu!”

Akaangua kicheko. Lakini kabla hajaendelea, Rhoda akamtaka awabakize hai kwani ana sababu ya kumpa. Mlozi yule akauliza kwa hamu sababu gani hiyo. Rhoda akamwambia atamsaidia kuuteka upya utawala wake.

Mlozi akastaajabu na akataka kujua kivipi Rhoda atafanya vivyo. Rhoda akamwambia mlozi huyo kwamba anahitaji muda zaidi wa kutengua hicho kitendawili. Mlozi asiamini kauli ya Rhoda akaagiza watu hao watiwe ndani mpaka pale mwezi utakapozuka kwa ajili ya kufanya ibada yake.

Kwa makadirio aliyoyafanya, ilikuwa bado siku tatu ama mbili na mwezi utaonekana angani. Siku hiyo ndiyo itakuwa mahususi kwake kuchinja binadamu hao na kufanya hitimisho ya kafara yake ambayo ilishatanguliwa na wale wengine.

Basi pasipo kujulikana nini kimetokea, popo wakazuka na kuwatwaa wakina Rhoda kwa mtindo wa kimbunga. Wakawafungasha na kwenda kuwamwagia ndani ya chumba kimoja dhoofu, na kikuukuu, lango likafungwa!

Chumba hicho kilikuwa kimejawa na kila aina ya wadudu, kuanzia wanaotambaa mpaka wanaoruka. Harufu yake haikuwa ya kuvutia kabisa, ukitazama dirisha lilikuwa lipo mbali na ni dogo.

Rhoda akamuuliza Tretho kama kuna la kufanya wajiokoe toka mule. Tretho akasema wasubiria aone kama kuna namna. Akatazama huku na kule, japokuwa kulikuwa ni giza, akaona panya mmoja ukutani.

Basi akamdaka na kumnyonga kwa mikono yake upesi na kumnyofoa kichwa. Panya akamwagika damu. Tretho akapakaa damu hiyo mikononi mwake na kwenye paji lake la uso, kidogo. Alafu akamtupia panya kando!

“N’taomba muwe kimya kidogo,” akasema akiketi kitako. Akaweka mikono yake mbele mithili ya ombamba, akasema maneno kadhaa yasiyotambulika ni ya lugha gani. Baada ya kama dakika tatu, akafumbua macho yake na kumwambia Rhoda ajiandae na afanye kazi yake.

Rhoda akawa ameshajua nini kinafuata. Ilikuwa ni kazi ya kukariri maneno atakayoyatema na kisha amwambia atakaporejea fahamuni.

Haikupita muda Tretho akaanza kuyatema maneno hayo. Hakuchukua muda mrefu akarejea fahamuni na kumuuliza Rhoda nini alichoambulia. Rhoda akamwambia.

Mzee huyo akatikisa kichwa na kusema:

“Haiwezekani.”

“Kwasababu gani?” Rhoda akawahi kuuliza akitoa macho.

Tretho akasema jengo lile ambalo wamo ndani, siyo hata jengo halisi bali ni ulozi wa kufikirika tu. Ni jengo kwa mujibu wa macho yao na wala halipo kiuhalisia! Ni ngumu sana kutoka maana mfumo wake ni wa kilozi wa ngazi za juu.

“Kwahiyo tutafia humu?” Rhoda akakabwa na hofu. Tretho hakuwa na jibu la kumpatia zaidi tu ya kumtazama kwa macho ya njia panda.

Kukawa kimya kwa muda.

Lakini katika usiku huo huo, usiishe, kuna mambo mengine bado yalikuwa yanakuja. Unakumbuka wakina Rhoda walikumbwa na kadhia ya kimbunga cha popo wakiwa eneo gani?

Eneo la wale wabibi!

Basi na humo Tanashe kila mtu na himaya yake. Kila mtu na kaya yake, na hakuna mwingine wa nje anayetakiwa kuingia katika hema ya mwenzake katika namna yoyote ile!

Wakitambua kwamba wanadamu hao walikuwa wametia miguu kwenye ardhi yao, wale bibi watatu wakawa wamapanga kufanya jambo. Na jambo hili halikuwa lingine bali kwenda kutwaa kile kilicho chao!

Walikuwa wamevalia magauni meusi na kofia ndefu zilizochongoka. Kila mtu alikuwa ana jicho moja moja na kipande cha mti mkononi. Mti mwembamba wenye kafundo ka rungu kule mbele.

Kabla hawajatoka kwenye jengo lao, wakahakikisha kila kitu kipo sawa na salama. Kufumba na kufumbua, wakapotea mazingirani! Hawakuonekana hewani, wala ardhini. Ila baada ya punde, kule upande wa yule mlozi wa jengo la kufikirika, Tretho akahisi jambo.

Wenzake walikuwa wamelala akawaamsha na kuwaambia: “Kuna watu wanakuja!”

Wakatazama huku na kule wasione jambo. Tretho naye hakuwa na viambata vyake vyovyote vya kazi, vyote vilipotelea huko.

Basi baada ya muda wakajikuta wanapoteza fahamu na wakadondoka chini kama vifurushi. Tayari walishabebwa!


***


“Naomba uniwie radhi, mimi.”

“Nshakwambia sitaki kusikia wala kuambiwa chochote!”

“Kaka, usilipe baya kwa baya. Mabaya mawili hayatengenezi zuri moja!”

“Kwani yeye hakulijua hilo hapo kabla?”

Yalikuwa maongezi moto kati ya Sultana na Karim. Sultana alikuwa ameketi sebuleni wakati Karim akiwa amesimama mwili wake ukifunikwa na kanzu ya rangi ya zabibu. Sultana alikuwa amejivika gauni refu lenye rangi ya maji ya bahari. Zaidi alikuwa amejivika hofu na mashaka kwani laka yake hakutaka kuelewa na alikuwa amedhamiria haswa kulipiza kisasi kwa Sultan.

Sultana akauliza, hii vita itatupeleka wapi na je haoni kama itamaliza himaya yao nzima? Karim akacheka kwanza alafu akadaka kiuno chake kwa mikono miwili. Akasema kwani Sultan hakuyajua hayo?

Vipi kama majeshi yake yangefanikiwa kummaliza? Leo angekuwepo hapo?

Basi zogo hilo lisipate suluhisho, Karim akaenda zake ndani na kumwacha dada yake akilalama. Hakutaka kujali na wala hakutaka kusikia tena juu ya mada hiyo. Akasema kama kweli Sultan anaomba msamaha basi alete mwenyewe miguu yake pale na si kumtuma mkewe.

“Kwani wewe ndiye mkosaji?” alimuuliza dadaye. “Kama anataka amani aje apa na ameze majivuno yake kukiri makosa. Amenidhalilisha sana, na anataka kunimaliza pia.”

Sultana akabakiwa na mawazo sana. Ni nini afanye na hakuwa radhi kurudi nyumbani akiwa na jibu hasi? Aliona mkono wake ndiyo ulianzisha vita hiyo na hivyo hana budi kuimaliza!

Akala na kufikiri sana. Akatoka nje kwenda kurandaranda na baadae hata akarudi ndani pasipo kupata majibu. Nafsi yake ikamwambia ajaribu tena kuongea kwa mara nyingine pindi watakapokuwa mezani kupata chakua cha mchana na kakaye.

Labda anaweza kutengua mawazo yake.

Akafanya hivyo. Lakini Karim hakutia neno hata moja pasipo kujali namna gani dada yake ameongea. Alikuwa kimya akishurutisha mdomo wake kula.

Sultana akaghafirika. Akasusa na kula. Akanyanyuka na kwenda zake jikoni aondoke hata pale kwenye uwepo wa kaka yake ‘mkaidi’. Moyo wake ukapuliza kwa haraka na kuuma.

Akafikiri na sasa shetani akatia nanga kwenye akili yake. Akawaza kumuua Karim, nduguye! Hilo likawa suluhisho lake la mwisho kumaliza mjadala. Hakukuwa na njia nyingine sasa kukwepesha vita hii.

Akatazama pembeni na kukwapua kisu kimoja kirefu. Akakificha nyuma ya mgongowe na kwenda hatua za pole. Moyo wake ulikuwa unakita na kukimbia sana kwa hofu lakini haukufanikiwa kusimamisha miguu yake.

Akamsogelea Karim aliyekuwa amempa mgongo, akamkita kisu cha ubavu! Karim akapiga kelele moja kali kabla hajamshika dada yake mkono na kumtazama kwa macho mekundu yanatoa chozi, na mdomo uliochama.

Akamuuliza dadaye kwa sauti ya kutiatia maji:

“Mkono wako ndugu yangu ndiyo unaonimaliza?”

Sultana akajikuta anabubujika machozi mengi akimshuhudia kakaye akipokwa uhai. Akajuta sana na labda akadhani ni macho yake, kaka ataamka. Haikuwa hivyo. Kaka akasema kauli yake ya mwisho:

“Na hamtabaki salama!” kisha akaenda.

Sultana akamburuza kaka yake mpaka chumbani. Akafuta damu zote zilizokuwa pale na akarejesha mazingira kama yalivyo. Hakuona tena salama kukaa hapo, na basi akamwita mwanajeshi aliyekuja naye na kumtaka waondoke upesi.

Wakapanda farasi na kupotea wakimwacha Karim huko chumbani amefungiwa na kisu chake bado kipo ubavuni.

Njia nzima Sultana akawa anabubujika machozi! Moyo wake ulikuwa mzito ukibeba manung’uniko na lawama. Sura ya kaka yake haikuacha akili yake salama.


***


“Mama, mfalme ni wa baridi!” Ilikuwa kauli ya Tattiana punde tu mama yake alipomuuliza juu ya huko alipotokea.

Yalikuwa ni majira ya mchana na ndiyo muda ambao Tattiana alikuwa amerejea toka kwa mfalme baada ya kuruhusiwa. Sasa alikuwa ameketi na mama yake sebuleni mama akiwa na hamu kubwa ya kujua yaliyojiri.

Mama akamuuliza mfalme ni wa baridi kivipi? Tattiana akaeleza vema. Alishindwa hata kumkumbatia wala kukaa naye karibu. Kwani alikuwa ana baridi kana kwamba barafu la kule kaskazini ya Kinabey!

Mama akastaajabu. Linawezekaaje hilo? Ila kama haitoshi, Tattiana akasema ya kwamba mfalme alimwambia hiyo iwe siri yake na asimwambie mtu mwingine yeyote!


LAKO JICHO***
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom