SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II ---06*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

“Wazazi wako wamefika. Wanataka kukuona pia,” daktari alisema akitabasamu. Tattiana naye akatabasamu ila moyoni akijazwa na hofu. Vipi kama Roboth akionekana?

Wakati daktari akitoka ndani kwenda nje kuwakaribisha wazazi, akagundua kuna alama za nyayo za viatu. Akasita na kumuuliza Tattiana: kuna yeyote aliyekuja kumwona kabla yake?

Upesi Tattiana akatikisa kichwa na kusema: Hapana, nilikuwapo mwenyewe usiku mzima na hata asubuhi hii.

ENDELEA

“Una uhakika?” Daktari akauliza. Tattiana akatisa kichwa akisema uhakika anao. Akarudia ya kwamba alikuwa mwenyewe muda wote ule tangu alipoachwa. Daktari akaondoka zake kwenda kuwaita wazazi ambao hawakuchukua muda mrefu kabla hawajafika ndani.

Wakamjulia hali binti yao wakifurahishwa na namna ambavyo mwili wake unarejea haraka katika hali yake. Wakampongeza daktari kwa juhudi na kazi yake inayoonekana.

Mama akamwambia Tattiana: asije akarudia tena kufanya hivyo kwani ataua wazazi wake kwa presha. Walikuwa wanawaza sana kumhusu na walikosa raha kabisa ndani ya nyumba. Tattiana akaomba msamaha. Lakini wakati huo akili yake ilikuwa inamuwaza tu Roboth, na si kingine.

Alikuwa na hofu, na ilizidi pale alipomwona daktari akienda kabatini kutazama madawa. Akahisi mwili wake unatetemeka. Japokuwa hakuwa anaona vema, alijitahidi kuangaza ajue kitakachoendelea huko.

Baba akamuuliza kama kuna tatizo lolote, akakana lakini uso wake ukimsaliti.

“Mwanangu,” mama akaita. “Nakuomba sana mama, kaa mbali na yule mwanaume. Nakupenda sana na sitaki kuona ndoto yako inayoyoma. Kumbuka hii ni nafasi kubwa sana kwetu na kama tukija kuipoteza tutajutia. Msimu wa ndoa karibu unakaribia, na huenda mfalme akakuchukua. Naomba ujitunze na uwe makini sana. skauti wa mfalme wanaweza wakawa wanaranda.”

Tattiana hakusema kitu, akatazama chini. Aliogopa kunena lolote kwa kuhofia kumuumiza Roboth ambaye alikuwa na uhakika anayasikia yote hayo. Basi akaishia kutikisa kichwa.

Baba yake akamwambia mfalme aweza kuja kumjulia hali. Asije akathubutu kumwambia kilimchofanya akanywa sumu, kwani atakuwa ameharibu kila kitu. Amwambie alikula chakula njiani alichopewa na mwanamsafiri asiyemfahamu.

“Sawa?” baba akauliza.

Tattiana akatikisa tena kichwa pasipo kutia neno.

“Weka maanani, familia yetu ipo mikononi mwako,” baba akasema kabla hawajatoka kwenda nje. Roboth akatoka naye nyuma ya kabati akamuaga Tattiana. Alimwambia atakuja siku nyingine kumjulia hali. Akachoropoka kwa kupitia dirishani.

Pasipo kujua mlinzi wa mfalme alikuwa anamtazama, Roboth akaangaza huku na huko kutazama usalama wake alafu akakatiza kueleka nyumbani. Ni punde ndogo tu alipishana na familia ya Melkizedeck wakijikokota toka hospitalini.

Akatembea kwa kasi. Lakini mbele yake akakutana na mwanajeshi yule wa mfalme. Akaogopa sana. alitaka kukimbia, lakini mwanajeshi akamtahadharisha:

“Usithubutu.”

Basi akasimama na kutazama kwa woga. Moyo wake ulikuwa unakimbia kwa kasi, akihofia kwenda kuswekwa korokoroni.

Mwanajeshi akamuuliza ametokea wapi? Akadanganya. Mwanajeshi akamtahadharisha tena:

“Usithubutu.”

Kwa hofu, Roboth akaeleza ukweli kuwa alitoka kumwona Tattiana. Mwanajeshi akamuuliza kwa utaratibu kama anataka uhai wake ama lah! Roboth akasema bado anataka kuishi, basi mwanajeshi akamwambia aachane na Tattiana.

“Wewe ni nani ukashea na mfalme mwili mmoja? … Una umri mdogo kufa, ardhi bado haikutamani. Fuata ushauri wa mdomo wangu kabla hujafuata ushauri wa upanga wangu.” Mwanajeshi akajiendea. Roboth akakanyaga mguu kwenda nyumbani.

Saa hii hakuwa anakimbia, bali anatembea, tena akiwa ameweka mikono yake nyuma. Kichwa chake kilichoelemewa na mawazo kilikuwa kinatazama chini.


***


“Baba, kila kitu kipo sawa,” alisema kijana mwenye makamo ya miaka thelathini na tatu, nne ama tano. Kwa jina anaitwa Oragon. Alikuwa amevalia joho rangi nyeusi mikononi akilikunja. Nywele zake zilikuwa vurugu na ndevu zake zilizojaza uso zilikuwa zimetapakaa vijani vidogo vidogo rangi ya zambarau.

Maneno haya alikuwa anamwambia mzee yule wa baraza – kuwadi aliyefanikisha kumkutanisha Tttiana na mfalme. Mzee huyu alikuwa ameketi kwenye kiti akijipatia kahawa nyeusi ndani ya kikombe kidogo cheupe. Kwa pembeni, kulikuwa kuna birika kubwa la chuma.

“Sawa, nakuja,” akasema mzee huyu alafu akanywa mafundo mawili ya kiuoga akikimbiza lips zake toka kwenye moto wa kinywaji. Oragon akaenda zake akifuata korido nyembamba na kupotelea.

Nyumba hii haikuwa kubwa sana wala ndogo lakini ilikuwa chakavu. Hapa sebuleni ungeona viti kadhaa vya mbao imara. Kioo cha wastani juu ya ukuta na vibandiko kadhaa vya urembo, ila vikiwa vimechoka.

Ungeweza kubashiri kwa upesi nyumba hii haikuwa na jinsia ya kike ndani.

Mzee akanyanyuka akiwa amebebelea kikombe chake, akafuata korido iliyomchukua Oragon na muda si mrefu akajikuta kwenye chumba kikubwa kilichokuwa kimeshamiri matunda mekundu yenye vishiko vidogo vya majani rnagi ya zambarau.

Matunda hayo yalikuwa yamejaa pomoni na yakitengwa kimakundi makundi kutokana na hatua ambayo yamo. Ukitazama makundi makundi hayo vema, utaona kila kundi lina mwonekano sawa wa matunda, toka kwenye yale yaliyokoza mpaka yale yaliyoanza kubadilika rangi kuwa kahawia.

Mbali na matunda walikuwepo wanaume wawili vijana, mmoja ndiye yule Oragon na mwingine alikuwa ameketi kitako, akiwa naye amevalia joho jeusi na nywele zake kichwani zilikuwa nyingi mno na nyeusi ti, jinale Ottoman.

“Safi sana, mmefanya kazi vema,” alipongeza mzee akiangaza macho yake na huku akitabasamu. Akamuuliza Oragon kama tayari wameshapakia mzigo na kuuhifadhi ndani ya magunia na makapu. Oragon akamwambia tayari kila kitu.

Mzee akafurahi na kupongeza. Sasa akamwambia Ottoman akaandae farasi watatu kwa ajili ya safari. Oragon akamuuliza: huoni itakuwa hatari kusafirisha mzigo huo wakati jua lawaka? Kwanini wasingoje watu wakiwa vitandani usiku wa manane?

“La hasha!” mzee akapaza sauti. “Mchana ndiyo muda mzuri kwani hamna mtu anayetilia shaka, watadhani ni wakulima. Lakini nyakati za usiku wanajeshi wanaranda huku na huko, ni rahisi kutiliwa shaka na kukaguliwa! Utasema unapeleka wapi mzigo wakati huo?”

Ottoman akarejea na kuwaambia farasi wapo tayari kwa ajili ya safari. Mzee akamuuliza kama ameweka tayari majani ya mzeituni kwa ajili ya kukata harufu ya matunda hayo huko nje? Oragon akasema ni jambo la dakika tu, atafanya hivyo wakiwa wanashindilia matunda mengine kwa juu kuficha magendo yao.

Basi kila kilipokuwa vema machoni mwao, Oragon pamoja na Ottoman wakajipaki kwenye farasi wao wawili waliofungiwa mkokoteni.

“Kuwe makini,” mzee akawaambia, na safari ikaanza.

Ingawa walipokuwa wanaelekea hapakuwa panazidi maili tatu, nyumbani kwa Melkizedeck, ila ilikuwa ni kama vile maili mia kutoka na kile walichokuwa wamekibeba. Hii ilikuwa ni safari yao kwanza wakibeba matunda hayo ambayo ni marufuku kabisa kuuzwa ndani ya himaya wala nje ya himaya – kwa jina Cedar.

Matunda haya yalikatazwa kuuzwa kwakua ni maarufu sana kwa sumu yake kali ambayo wadhalimu huwa wanayatumia kutengenezea silaha mbalimbali zenye madhara makubwa.

Lakini pia yanatumika kwenye ulozi, wachawi wakiyatumia kwenye mauaji ama utengeneza maagano. Ndiyo maana matunda yakapewa jina la ‘matunda ya shetani’ watu hawa wakiamini yana mahusiano na lile lililomfukuza Adam na Hawa bustanini. Wengine wakiyaita ‘matunda ya nyoka’.

Kukamatwa ukiwa unayapanda, ingemgharimu mkulima mikono na macho yake. Na ukiwa unayauza, inagharimu maisha ya mfanyabiashara akinyongwa mbele ya umati wa watu.

Lakini mbali na hayo, matunda haya yalikuwa na gharama kubwa mno endapo mfanyabiashara angelipata mteja! Faida yake ilikuwa ni kabambe na inaweza kukuamsha tajiri ilhali ulilala maskini.

Wateja wake ni walozi, wakabaji wa jangwani na wakwapuzi wa ndani za himaya. Wachache sana wakiwa watu wakubwa ambao wangetaka kuyanunua kwa ulinzi binafsi.

Si ajabu mtu kukupatia kipande cha dhahabu kubadilishana na matunda haya. Ila biashara yake ilikuwa ni ya siri mno! Watu wangeliweza kuuziana mbele yako na wewe usijue kinachoendelea.

Oragon na Ottoman wakakata maili moja wakitembea na farasi wao. Waliendelea na safari wakitazama usalama kwa hali na mali. Macho yao yalikuwa huko nje yakipekua na kupekua. Na kama vile mbwa wanaonusa, wakawa wanazikwepa zile barabara zenye wanajeshi!

Wakafika mbele ya nyumba ya Melkizedek. Hapo wakakutana na walinzi waliowasimamisha na kuwataka wajitambulishe. Oragon akawambia wao ni wageni wenye miadi, haraka waruhusiwe kuingia ndani.

Walinzi hao wakawa wagumu kutii, Oragon akawafokea akitaka kuingia ndani kwa lazima. Melkizedeck alisikia makelele akatoka nje na kuwataka wakina Oragon waruhusiwe. Wakazama ndani wakielekeza farasi wao nyuma ya nyumba.

Wakapakua mzigo na kuingiza ndani upesi!

Lakini kule getini, kwa mbali kabisa, yule mlinzi wa mfalme aliona sakata lile la wakina Oragon wakiwa wanazoza na walinzi. Hakujua nini kile ambacho wakina Oragon wamebeba na kwanini wanapeleka kwa Melkizedeck.

Basi akangoja kwa nje. Na baada ya dakika kama kumi na kitu, Oragon pamoja na mwenzake wakatoka na farasi wao wakiwa watupu. Mwanajeshi huyu akaanza kuwajongea.

Punde akawafikia na kuwasimamisha. Akawauliza wametokea wapi na walikuwa wamebebelea nini.


****
 
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II --- 07*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Wakapakua mzigo na kuingiza ndani upesi!

Lakini kule getini, kwa mbali kabisa, yule mlinzi wa mfalme aliona sakata lile la wakina Oragon wakiwa wanazoza na walinzi. Hakujua nini kile ambacho wakina Oragon wamebeba na kwanini wanapeleka kwa Melkizedeck.

Basi akangoja kwa nje. Na baada ya dakika kama kumi na kitu, Oragon pamoja na mwenzake wakatoka na farasi wao wakiwa watupu. Mwanajeshi huyu akaanza kuwajongea.

Punde akawafikia na kuwasimamisha. Akawauliza wametokea wapi na walikuwa wamebebelea nini.

ENDELEA

Kigugumizi kikamkaba Oragon. Kwa muda kidogo hakuwa na cha kujibu ispokuwa kupigwa na butwaa. Mwanajeshi akautumia mwanya huo kurusha macho yake mule ndani ya toroli kupekua huku na huko.

“Kuna vitu tulivipeleka kwa bwana Melkizedek,” akasema Oragon lakini hakuwa anajiamini hata kidogo. Macho yake yalimsaliti. Hata mikono yake aliyokuwa ameilaza juu ya mapaja ilikuwa inatetemeka kwa hofu.

Mwanajeshi yule wa mfalme katika upekuzi wake, akaona kijani kidogo rangi ya zambarau, akakiokota na kukitazama, asichukue muda mrefu akawaruhusu Oragon na Ottoman waondoke zao. Akasimama na kuwatazama wakiishia, alafu akatoa lile jani na kuendelea kulitazama.

Akalinusa na kulipekuapekua. Lilikuwa geni machoni mwake, lakini siyo geni! Akili yake ilisema amewahi kuliona mahali lakini macho yake yakikataa na kusema akionacho ni kipya kinyemi.

Akaliweka lile jani mfukoni mwake, na kisha akajipaki juu ya mgongo wa farasi wake akajiondokea.

“Tatizo wewe muoga sana!” Ottoman alimsonta Oragon. “Ulivyokuwa unatetemeka maana yake nini? Ulikuwa unahofia kitu gani wakati unajua mzigo tumeshautua?”

“Otto, usijifanye zuzu, usijifanye zuzu nakwambia! Unadhani tungekamatwa pale ingekuaje? Upo tayari kwenda kunyongwa?”

Ottoman akaangua kicheko kikali.

“Sasa ukamatwe kwa ushahidi gani, Oragon? Kwa farasi na toroli?” Akauliza na tena akaangua kicheko wakati Oragon akimtazama kwa macho makavu.

“Unajua haya siyo matani,” Oragon akanena. “Unadhani yule ni mtoto mdogo kuvumbua nyendo? Ulimwona namna alivyokuwa anatazama lile jani?”

“Jani lipi?” Ottoman akauliza. Alionyesha kushtushwa. Macho akayakaza na mdomo akaachama.

“Jani lipi? – kwani hukumwona?”

“Sikumwona!” Ottoman akapaza. “Sikumwona akiwa ameshika chochote.”

Basi Oragon akamwambia mwenzake ya kwamba mwanajeshi yule aliona baki la jani la Cedar kwenye kitoroli cha farasi, na janii hilo amebaki nalo. Ottoman akawa mgumu kuamini. Na hata upesi akatazama kwenye kitoroli. La haula akaona kijani kingine. Haraka akakikwapua na kukikagua. Kilikuwa ni cha Cedar!

Akamuuliza Oragon nini watafanya? Jani la tunda lile lilikuwa tofauti na majani ya mimea mingine yoyote, kuanzia rangi mpaka na umbo. Mwanajeshi yule akijua walibebelea matunda hayo haitakuwa nongwa kwa Melkizedek?

“Shida sio hiyo tu. mwanajeshi yule atakuwa ametutilia shaka, nap engine kutuacha kwetu huru ni kwasababu anataka kufanya upelelezi, ajue wapi tulipotoa matunda hayo, na tunayafanyia kazi gani. Hiyo si tu kwamba tupo hatarini, bali Melkizedek vilevile.”

Kwa muda wakakosa cha kusema. Furaha ya kuufikisha mzigo salama ilibadilika na kuwa huzuni ghafla. Mpaka wanafika karibia na maeneo ya nyumbani ndipo wakafungua vinywa kujiuliza kama kuna haja ya kumwambia baba yao kuhusu habari za huko watokako.

“Puuzia! Huoni tutakuwa tumejichongea?” akasema Ottoman. “Mwache baba aendelee kuwa gizani na kwenye amani.”

“La hasha!” Oragon akapinga. “Unadhani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumesuluhisha tatizo ama kulitengeneza jipya? Baba ana wadhfa mkubwa serikalini, tumuweke wazi atajua namna ya kuenenda.”

Mpaka wanafika hawakuwa wamekubaliana. Yalikuwa ni majira ya jioni. Walimkuta baba yao akiwa ameketi nje ya nyumba akiwasikiliza watu wawili; mwanamke na mwanaume walioonekana kujawa na mgogoro. Wakasalimu na kwenda zao ndani bado wakiendeleza mjadala.

Baba yao alimaliza kuongea na wageni, akaingia ndani. Akauliza:

“Kunani? Mbona mzozo ndani ya nyumba yangu?”

Oragon na Ottoman wakatazamana pasipo kusema kitu.

“Si nawauliza nyie? – nini shida nasuluhisha ya wengine na huku kwangu kwafukuta?” mzee akauliza akiketi kwenye kiti chake kilichopakana na meza yenye birika la kahawa.

Oragon akajitoa kimasomaso kumweleza baba yake. Akamwambia wamefika salama huko walipoelekea, lakini kuna mwanajeshi kawaona. Baba akapigwa bumbuwazi. Macho yalimtoka na kuwa mekundu ghafla. Mkono wake wa kizee ukakamaa akamwaga kahawa yake kikombeni.

Akauliza tena kana kwamba hakusikia na mara hii alikuwa amesimama. Oragon akaogopa kurudia kunena. Lakini baba hakungoja Oragon aseme tena kauli yake, akarusha birika la kahawa! Oragon na mwenzake wakalikwepa, likagonga ukutani.

Baba akawashutumu kwa uzembe. Akawakumbushia ni kwa namna gani aliwaambia wawe makini kwani swala hilo ni la maisha na kifo.

“Tulikuwa makini, ba …” Ottoman alijaribu kufungua kinywa, baba akafoka kumkatiza:

“Nyamaza! … mnajua ni namna gani mlivyo mzigo hapa. Mnajua kabisa nafanya haya kwasababu tu ya kuwakomboa nyie na familia zenu alafu bado mnaleta uzembe! Mnataka nikaishie kitanzini na huu uzee wangu?”

Baba akakunja ngumi na kuketi chini. Akasaga meno akitafakari kwa kina. Zikapita dakika kama tano, akili yake ikawa imetulia, akawauliza wanaye kama wanamjua huyo mwanajeshi kwa sura na wapi walikutana naye?

Kwa maelezo waliyotoa, mzee akagundua mwanajeshi huyo atakuwa ametumwa na mfamle kumfuatilia Tattiana na familia yake. Akatulia na kupembua pumba na mchele. Akaagiza tena kahawa, haraka akaletewa mezani. Akanywa mafundo mawili na kusema:

“Sasa mnanisikia, hakuna namna nyingine hapa ya kujiokoa zaidi ya kuhakikisha jambo letu linakuwa siri. Kadiri jambo hili litavyokuwa siri na ndivyo na sisi tutakavyokuwa hai na kufanikiwa … Hatuwezi kumhonga mwanajeshi huyo maana bado haitaondoa siri hiyo kichwani mwake. Kwahiyo ni njia gani iliyobakia?”

Akawatazama wanaye machoni, Ottoman akajibu:

“Kumuua.”

Baba akatabasamu na kutikisa kichwa. Akasema:

“Inabidi auawe. Tena haraka iwezekanavyo!”

Oragon akaanza kutetemeka tena.


***


Usiku ulikuwa umekua sasa, watu wakawasha maginga ya moto kupata nuru. Majumbani na hata kwenye vilabu vya kunywea pombe, na huko njiani, watu walikuwa wanapewa mwanga na moto uliokuwa unametameta kwenye vichwa vya miti.

Lakini kinyume kabisa na hivyo, makazi ya Rhoda yalikuwa gizani. Hakukuwa na kona hata moja ya nyumba iliyokuwa nuruni, kote kulikuwa giza kana kwamba shimo ndani ya msitu mkubwa!

Mazingira yalikuwa tulivu mno, usingeweza kusikia kitu chochote kama ungelikuwa maeneo hayo ya karibu na pengine ungejihisi umekuwa kiziwi.

Kwa kadiri muda ulivyosonga mbele, hakukuwa na dalili ya kubadilika kwa mazingira hayo na basi hali hiyo ikawavutia wakwapuzi, wale ambao tamaa za kumiliki vitu na mali za haraka zilikuwa zimewajaa.

Kwa mbali walevi wawili wakipita, wakasimama na kutazama makazi hayo ya Rhoda. Wanaume hawa walikuwa wamebebelea chupa za vileo mikononi, wakiyumba na kuropoka kilevi. Mavazi yao yalikuwa madabwada na yanayonuka mikojo.

Mmoja akampiga mwenzake begani akamwambia: huoni kama kule kuna fursa? Vipi kama tukipata chochote kitu tukaenda kuongeza kinywaji kingine klabuni? Lakini mwenzake akajawa na tahadhari, akamuuliza vipi kama kuna watu?

“Watu gani wa kuishi gizani?” akasema yule mlevi anayemmshawishi mwenziwe. Kwa kuwa midomo ya walevi haijawahi tosheka na kileo, miguu yao ikasogelea eneo la tukio. Wakatazama kule na huku, hawakuona mtu wala dalili!

Basi yule mlevi aliyemwonyesha mwenzake fursa, akasema:

“Kaa hapa na mimi nitaingia ndani. Utakapoona kuna hatari yoyote utanitaarifu nitoke upesi!”

Akazama ndani mwenzake akiwa anayumbishwa na upepo kutazama huku na huko kuhakikisha na kudumisha usalama. Akili yake ilikuwa inawaza ni kwa namna gani atakavyokuwa anafaidi vileo vingi vya kumwaga muda si mrefu.

Hawakujiuliza wenyeji wapo wapi, na wala hawakutaka kujisumbua.

Ikapita dakika mbili … tatu … nne, mlevi aliyekuwepo ndani akaropoka:

“Alah! Kuna vitu vingi vya thamani!”

Sijui alikuwa anaonaje ndani ya kiza. Mwenzake akamhasa avikombe vyote waende zao haraka. Baada ya maongezi hayo kukawa kimya kidogo mbali na sauti ya sahani iliyoanguka.

Baada ya muda kidogo, sauti kali ya mlevi ikatoka ndani! Akalalama anauawa! Mara akalalama ananyonywa damu! Mlevi aliyetenga kama mlinzi asifanye jambo, mara akaona mkono wa mwenzake chini ya mlango. Kufumba na kufumbua, mkono huo ukavutiwa ndani!

Basi akawehuka kwa hofu. Akakimbia kadiri ya uwezo wake akipiga yowe! Kuna wauaji! Kuna wanyonya damu kwa Rhoda!

***
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom