JANA mwenyekiti wa Jumuiya ya madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka aliibuka na kusema anajiandaa kumwaga mboga juu ya wale waliomteka. Aliwaambia maneno haya baadhi ya waandishi wa habari aliokutana nao:
"Bado niko imara. Sijanunuliwa. Walionichagua (madaktari wenzake) wanafahamu hivyo. Hata walioniteka wanajua kuwa hawawezi kuninyamazisha na kwamba katika kutetea maslahi ya taifa, mimi sina bei. Bali kimya changu kimetokana na kufuatilia kwa karibu masharti ya matibabu yake na katu si kwa kuwaogopa watesi wangu."
Dk. Ulimboka alitekwa, kuteswa kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno; na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande, usiku wa 26 Juni 2012.
Amesema, "Watanzania na wapenda haki duniani kote, wanahaki ya kujua kwa kina yale yaliyonisibu pamoja na watu waliohusika katika kutekwa kwangu. Hivyo ninao wajibu mkubwa wa kueleza ukweli huo na bila kuuma maneno."
Amesema mapambano hayo ni muhimu kuendelezwa kwa kuwa ndiyo njia pekee itakayoifanya serikali kuboresha huduma za afya nchini, ambapo amesema ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa mamia ya wananchi wanakufa kwa kutokana na kukosa huduma bora za afya.
Kauli yake hiyo, inaiweka serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika wakati mgumu hasa kutokana na ukweli kuwa iliamua kulifungia gazeti la kila wiki la Mwanahalisi ili lisiweze kuchapisha taarifa juu ya kutekwa kwa kiongozi huyo. Sasa Ulimboka anasema atasema kila neno na kutaja kila mmoja.
Ikiwa hili litafanyika, basi bila shaka kuwa Ulimboka atakuwa amemaliza kiu ya Watanzania. Atakuwa amesaidia sana taifa katika kufahamu ukweli wa kilichotokea. Lakini kikubwa zaidi atakuwa amewafanya seriakli waliofungia Mwanahalisi ili kumlinda mtekaji, Ramadhani Ighondu Abeid ionekane serikali ya wapuuzi.
Hatua hiyo, itamfanya pia Zoka Jack afiche sura yake kwa aibu.