SoC01 Serikali ifanyie kazi kilio cha wakulima nchini

Stories of Change - 2021 Competition

alwatanpeks

New Member
Aug 16, 2021
3
0
Tanzania bado ina safari ndefu ya kumwinua mkulima ili ajikwamue kutoka kwenye kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha kibiashara ambacho kitamwezesha kuwekeza kwenye sekta hiyo kikamilifu.

Zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima lakini wengi wao wanafanya kilimo cha kujikimu wakati asilimia chache ndiyo wanafanya kilimo cha kibiashara, wanaongezea thamani ya mazao yao na kuuza nje.

Serikali imekuwa ikifanya jitihada kadhaa za kuwainua wakulima lakini bado hazijazaa matunda na kukifanya kilimo kichangie zaidi katika pato la taifa kwa sababu watu wengi wamejikita huko, hivyo, mapato yake yanatarajiwa kuwa makubwa kushinda sekta nyingine.

Kwa bahati mbaya, serikali imeweka udhibiti mkubwa ambao unaingilia soko huria hasa katika mazao ya wakulima kwa sababu ya kuanzishwa kwa mfumo wa kuwa na vyama vya ushirika (Amcos).

Kwa sasa, wakulima hawawezi kuuza mazao yao kama vile kahawa, korosho, pamba au chai kwa mtu yoyote, bali watauza sehemu moja ambayo inamkutanisha mkulima kupitia chama hicho na mnunuzi wa mazao.

Utaratibu huu una lengo jema la kulinda maslahi ya wakulima lakini kwa asili ya urasimu uliopo katika utendaji wa serikali, inachukua muda mrefu kwa wakulima kupata fedha zao ili kuendesha maisha yao.

Zamani kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, wakulima walikuwa huru kuuza mazao yao kwa mtu yoyote kwa bei ambayo watakubaliana na mkulima aliweza kupata fedha zake papo hapo kwa bei waliyokubaliana.

Faida za mfumo wa soko huria ni kwamba mkulima ana uwezo wa kupanga bei ya mazao yake kwa bei ambayo anaona itamlipa. Licha ya kwamba wakulima wamekuwa wakionewa katika suala la bei, kuna haja ya kuuangalia mfumo uliopo ambao ulianzishwa ili kulinda maslahi ya wakulima.

Katika soko huria kuna watu ambao shughuli yao ni kununua mazao ya wakulima. Watu hawa ambao wanajulikana kama “kangomba” kwa sasa wanapigwa marufuku kwa madai kwamba ni wanyonyaji wa wakulima.

Ni kweli, wapo ambao wanawadhulumu wakulima lakini wengine wanafanya biashara zao kama wafanyabiashara kwenye maeneo mengine, wanahitaji kutengenezeza faida ya haki kwa kununua mazao kwa wakulima na kuuza kwenye masoko wanayoyajua.

Moja ya mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wakulima kwenye mfumo wa uuzaji mazao wa pamoja, ni ucheleweshaji wa fedha za wakulima ambapo wanasema inachukua muda mrefu kupata fedha zao.

Pia, baadhi ya viongozi kwenye vyama vya msingi wamekuwa wakiwadhulumu wananchi fedha zao ambazo wanazitegemea kuendesha maisha yao na kwa ajili ya kujiandaa na msimu wa kilimo unaofuata.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa elimu katika kuongeza thamani ya mazao yao. Biashara kubwa katika sekta ya kilimo ipo kwenye usindikaji wa mazao hayo na kuyaongezea thamani kabla ya kuyapeleka sokoni.

Kukosekana kwa elimu hiyo kumewafanya wakulima wengi waishi maisha ya kawaida licha ya jitihada kubwa wanazozifanya katika kuzalisha mazao. Wameendelea kuwa masikini kwa sababu uzalishaji wao ni mkubwa lakini hauna faida.

Nadhani sasa ni wakati mwafaka kwa serikali kuangalia namna bora ya kutatua changamoto hizo za wakulima ili wakulima watajirike na kilimo wanachokifanya na kuwawezesha kubadilisha maisha yao na familia zao.

Vilevile, serikali iangalie namna bora ya kuboresha vyama vya msingi au kurudisha mfumo wa soko huria kwa kuliwekea misingi bora ambayo haitaruhusu ukandamizaji kwa wakulima wadogo hapa nchini.

Serikali iweke mikakati ya kuwezesha kilimo cha kisasa hasa kilimo cha umwagiliaji kwa kuhakikisha kwamba pembejeo za kutosha zinapatikana kwa gharama nafuu na masoko ya mazao na bidhaa za kilimo zinazozalishwa yanapatikana ndani na nje ya nchi.

Tuwasaidie maelfu ya vijana wasio na ajira waone kilimo kama fursa kubwa ya kubadilisha maisha yao ili wasikae wakisubiri kuajiriwa. Nchi za wenzetu zimepiga hatua kwenye kilimo hasa kilimo cha shamba kitalu (greenhouse).

Mabadiliko yaanzia kwenye fikra, hatuwezi kubadilisha kilimo chetu kama tutaendelea kuwa na fikra zilezile za kutegemea mvua ili kuendesha kilimo chetu. Maisha yanabadilika, nasi tubadilike.

Kwa karne ya sasa, ni vizuri tukajielekeza kwenye kilimo ambacho hakitegemei mvua ambazo zimekuwa hazitabiriki. Nchi yetu imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya maji ambavyo vinaweza kutumika katika kilimo cha umwagiliaji.

MAKALA HII ILICHAPISHWA KATIKA GAZETI LA MWANANCHI, SEPTEMBA 14, 2021.

Umwagiliaji.jpg
 
Back
Top Bottom