SEHEMU YA 135...
Hawakuchukua muda mwingi, wakafika mahali hapo. Kendrich alikuwa amekwishafikishwa, aliteremshwa, akawekwa juu ya machela na kuanza kuingizwa ndani. Hata kabla watu wengine hawajaingia ndani, Amanda akasimama, akaliona gari moja la wagonjwa likiingia mahali hapo, alitaka kuondoka kuelekea ndani ila moyo wake ukaa mzito kufanya hivyo, akajikuta akianza kulisogelea gari lile.
“Amanda, let’s get inside,” (Amanda, twende ndani) alisema mwandishi mwenzake aliyeitwa Henry.
“No! Just wait,” (hapana! Subiri kwanza)
Mlango wa gari lile ukafunguliwa, machela ikashushwa kutoka ndani ya gari lile, alipoangalia juu ya machela ile, macho yake yakatua kwa mgonjwa aliyekuwa hoi, alikonda mno, alionekana kama mfu pale alipokuwa, dripu ilikuwa juu yake na mwili wake ulikuwa na vidonda vingi.
“What the hell with her?” (nini kimempata?) alijikuta akiuliza Amanda huku akimwangalia mgonjwa huo. Alishangaa, ni kweli aliwahi kukutana na wagonjwa wengi lakini wa siku hiyo alionekana kuwa tofauti na wengine.
“She is very sick,” (anaumwa sana) alijibu daktari mmoja.
“What?” (nini)
“Sickle Cell and Leukemia.”
“Ooh! My God!” (Ooh Mungu wangu!) alisema huku akishangaa.
Wakati akiuliza maswali hayo, mlango wa mbele ukafunguliwa na wanaume wawili kuteremka, mmoja alivalia suti na mwingine alikuwa katika mavazi ya kawaida. Kichwa chake kikamwambia kwamba watu hao ndiyo walikuwa ndugu wa mgonjwa huo.
Hakuamini kama mtu aliyekuwa akiumwa kansa ya damu na sickle cell angekuwa katika hali aliyokuwa nayo mgonjwa yule, alishangaa, alitaka kujua mengi kwani aliona kabisa kulikuwa na kitu zaidi ya hicho kilichokuwa kikiendelea.
Hakutaka kusimama, kwa kuwa alikuwa na kiu kubwa akaanza kuwafuatilia watu hao, alitaka kujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea. Machela ikasukumwa mpaka katika chumba cha upasuaji, akabaki nje na wanaume wale.
Alitamani kufahamu kilichokuwa kimetokea, alisahau kabisa kuhusu Kendrich, upepo ulibadilika na alichotaka kujua zaidi kilikuwa ni kuhusu mgonjwa yule.