Rostam amgeuzia kibao Mch. Mtikila
Mchungaji Christopher Mtikila... habari kamili soma pembeni.
*Asema alimpa Sh 3 milioni kujenga Kanisa
*Aanika stakabadhi alizosaini hadharani
*Mtikila akiri kupokea hela, asema alimkopa
*Pia adai fedha hizo ni za serikali si zake
Na Ramadhan Semtawa
MBUNGE wa Igunga, Rostam Aziz, ameibua madai mapya na mazito, akisema kuna watu wazito na maarufu nchini wanapiga kampeni chafu dhidi yake huku akianika hadharani stakabadhi ya malipo ya Sh 3 milioni alizompa Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila.
Akizungumza kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari tangu awe mbunge kwa miaka 16 sasa, ikiwa pia ni baada ya kuibuka mjadala wa kudaiwa kutumia Kanisa kujisafisha, Rostam aliyaita matamshi ya Mtikila kuwa ni yenye uhusiano na kampeni chafu zinazoendeshwa na mtandao wa watu wazito na maarufu nchini dhidi yake. Hata hivyo hakuwataja.
Katika hotuba yake ya maandishi, Rostam alisema haoni kosa kuchangia Sh 7 milioni kwa Kwaya ya Amkeni katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKTT), Usharika wa Kinondoni, kwani hata Mtikila aliwahi kumwomba kiasi cha Sh 3 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kanisa, ambazo alimpa Aprili 14, 2008 kisha akatia saini.
"Fedha zangu ni pato halali linalotokana na jasho langu, kutokea mwaka 1852 huko Tabora kwa mababu zangu. Kwa kutambua fedha zangu ni halali, hata Mtikila mwenyewe Aprili 14, 2008, alikuja kuniomba nikampa na akaupokea mchango wangu wa Sh 3 milioni kuendeleza shughuli za kanisa lake," alisema Rostam na kuongeza:
"Hivi kuwaambia wengine kwamba, ni dhambi kuchukua mchango wangu wakati yeye mwenyewe amepokea fedha kutoka kwangu, tuiteje kama si unafiki, tena unaofanywa na mtu anayejiita Mchungaji. Maneno ya Mtikila ni yenye harufu ya chuki, wivu, ubaguzi na ufisadi."
Hata hivyo, Mchungaji Mtikila alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusiana na kupokea fedha hizo kutoka kwa Rostam, alikiri lakini akasema ni mkopo wake binafsi na wala hazikuwa za kuendeleza shughuli za Kanisa wala ujenzi wowote kwani wapo wafadhili wakiwemo kutoka nje wanafadhili Kanisa lake, ambalo linaitwa Full Salvation (Wokovu Kamili).
"Ni kweli, Rostam ni rafiki yangu sana, tena siku nyingi, lakini alinipa Sh 3 milioni kama mkopo, si fedha za kuendeleza Kanisa kama anavyosema. Muulizeni Kanisa gani, mimi sijengi Kanisa wala siendelezi, wapo wafadhili wa kanisa. Ni fedha za mradi wangu na ni mkopo," alisisitiza Mtikila.
Mtikila alipoulizwa tena katika mahojiano mafupi kwa njia ya simu, kwamba mkopo huo alipaswa kuurejesha kwa muda gani na ni mradi gani hasa aliufanya, alijibu tena: "Ni mradi wangu fulani hivi, muda wa kurejesha mkopo ulipaswa kuwa within two months (ndani ya miezi miwili)."
Katika mahojiano hayo, Mtikila alipoulizwa zaidi, kwamba hadi jana miezi miwili ilipita vipi hakuweza kurejesha fedha hizo, alijibu: "Ahaa ni kana kwamba mkopo ni mkopo tu, hata serikali bado inadaiwa na wafadhili na haijalipa hadi sasa, ila mimi nitamlipa ndani ya wiki moja hadi mbili kuanzia sasa."
Mtikila alipoulizwa zaidi, kwamba hata kama ni mkopo, vipi alikopa fedha kwa mtu ambaye amekuwa akimuita fisadi na mwenye kumiliki fedha chafu kwa kuwa pia alipinga Rostam kutoa fedha kwa KKKT, alijibu: "Ni kana kwamba zile fedha si chafu ni za nchi yetu, ni za serikali yetu, sema tu matumizi yake na amezipataje."
Wakati Mtikila akijitetea kwa hayo, Rostam aliweka bayana mambo mbalimbali, akimhusisha Mwenyekiti huyo wa DP na mtandao unaoendesha kampeni chafu dhidi yake.
Rostam alisema, amekuwa akihusishwa na tuhuma mbalimbali na kutoa ruksa kwa wenye ushahidi kuupeleka katika vyombo vya dola ili ashughulikiwe na kuongeza kwamba, tuhuma za kumiliki Kampuni ya Kagoda inayohusishwa na ufisadi wa wizi wa Sh 40 bilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hawezi kuzungumzia kwani kuna timu ya Rais inafanya kazi ya uchunguzi wa tuhuma hizo.
Alipoulizwa kwamba, kama azma yake ya kwenda kanisani haikuwa kujisafisha, kwa nini aliamua kwenda kuzungumzia mambo hayo kuhusu tuhuma dhidi yake na baadhi ya watu wengine kwamba ni chuki badala ya kuzungumza siku zote tangu kuibuka kwa sakata la Richmond mwaka 2006, alijibu: "Kwanza sikwenda kujisafisha, nilialikwa, nilitaka viongozi wa dini wajenge maadili mema katika nchi."
"Nimeamua kuwaita ili kuweka rekodi sahihi, kutokana na matukio ya wiki hii inayomalizika leo (wiki iliyopita iliyoisha jana), nimeamua kufanya hivi baada ya Mchungaji Mtikila kuitisha mkutano na kuamua kunitukana na hata kuhoji uhalali wa KKKT kunialika kuwa mgeni rasmi katika sherehe za uzinduzi wa albamu ya Kwaya ya Amkeni," alisema Rostam, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rostam alisema baada ya mkutano huo, KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, walipata shinikizo wakatoa taarifa ya kuukana mwaliko wa kanisa hilo, Usharika wa Kinondoni.
"Huu ni mwendelezo tu wa kampeni chafu inayoendeshwa na watu wachache, ambao ni maarufu na wazito katika jamii yetu, waliojiunga pamoja katika ushirika usio mtakatifu, ambao kwa kutumia malengo yao wanayojua wao, wameamua kuchafua majina, hadhi na heshima ya baadhi yetu," alisema.
Mbali na Mtikila, Rostam alisema ndani ya kikundi hicho, wamo ambao hawaridhiki na nafasi za uongozi walizonazo na ambao wamejenga chuki kwa kudhani na kujiaminisha kuwa, labda alihusika (Rostam) kuwazuilia, kujichukulia fursa za ufahari na hadhi wasizostahiki kwa vyeo vyao.
"Siweki visasi na kutaka kumkomoa mtu eti kwa sababu tu kampuni yangu ilikosa zabuni fulani katika mchakato wa ushindani wa kibiashara au katika kubinafsisha mashirika ya serikali," alisema bila kufafanua zaidi.
Alifafanua kwamba, mjadala uliozushwa kuhusu kuchangia fedha katika KKKT umekusudiwa kutimiza ajenda za kisiasa na wivu wa kibiashara. Hata hivyo, hakutaja ni nani mwenye wivu wa kibiashara na ajenda binafsi dhidi yake zaidi ya kuongeza kuwa: "wahusika watajijua."
Rostam aliongeza kwamba, hakuanza leo kulisaidia Kanisa hilo kwani hata katika ujenzi pia alishiriki na pia amekuwa akishirikiana na madhehebu mengine, ikiwemo ya dini ya Kiislamu.
"Leo hii kushiriki katika shughuli za Kanisa lile lile nililochangia kunapofanywa kama vile ni kitu cha ajabu na kunidhalilisha kwamba, kuna ajenda nyingine wanayoielewa hao waliozusha mjadala huu. Ufanisi wa haraka wa Mtikila kukusanya watu na kutoa tamko lazima uwe unaratibiwa na watu wanaoelewa wanachofanya," alisema.
Alisema hana matatizo yoyote na KKKT na kwamba mikakati hiyo michafu na kifisadi haiwezi kumfanya arudi nyuma, bali atazidi kuipenda nchi yake na kusema ukimya wake haukuwa woga wala haogopi kitu.
Wiki iliyopita, Rostam alihudhuria hafla ya uzinduzi wa albamu ya Kwaya Amkeni katika Usharika wa Kinondoni. Pamoja na mambo mengine, alilishukuru Kanisa kwa kumwalika na kutambua usafi wake na kuachana na maneno aliyoita ya kijiweni, uzushi, chuki na kuchafuana.
Kauli hiyo iliibua mjadala mzito hadi KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani kukana mwaliko wa Rostam. Hata hivyo, mwenyewe jana alisisitiza ni msafi na kwamba mwenye ushahidi wa uchafu wake aende mahakamani, zikiwemo tuhuma za kumiliki kampuni za Richmond na Dowans.