RIWAYA; MTOTO WA RAIS
IMEANDIKWA NA HALFANI SUDY
SIMU 0652212391
Sehemu ya Thelathini
Mwili wote wa Inspekta Adrian ulisisimka. Nywele zilimsimama. Kama mpigaji alidhamiria kumtetemesha Inspekta Adrian, basi alikosea sana. Ari ya Adrian kumsaka muuaji wa Aneth ilianza kupanda taratibu baada ya simu ile kukatwa. Simu hii ilikuwa ni kama kupandisha moto wa kipelelezi. Mara zote tangu aanze kuichunguza kesi hii hakuwa na pa kuanzia. Wauaji walifanya mauaji kiustadi sana. Wakiziba mianya yote ya kupatikana kwa muuaji. Lakini sasa, walimpa pakuanzia. Kuichunguza simu hii.
Simu ya onyo!
Moja kwa moja Adrian alimpigia simu afande Simon. Alikuwa ni askari katika kitengo cha TEHAMA. Simon alimhakikishia kwamba yupo ofisini.
"Nakuomba njoo ofisini kwangu mara moja." Inspekta Adrian alisema simuni.
"Nipo njiani afande." Simon aliitikia wito.
Dakika nne zilitosha kumfikisha afande Simon ofisini kwa Inspekta Adrian.
"Karibu sana Simon," Adrian alisema huku akimuonesha kiti Simon.
"Ahsante sana." Simon alisema huku akikaa kwenye kiti.
"Simon, nimekuita hapa kama ndugu yangu. Tunayoongea hapa naomba yabaki kuwa yetu tu, kama ndugu."
"Sawa Adrian. Amini upo na mtu sahihi wa kumwambia lolote lile." Simon alisema, macho yake yakiwa kwa Adrian.
"Simon, najua unafahamu nimepewa kazi ya kuchunguza kifo cha Aneth. Ukweli ni kwamba kesi hii imekuwa ngumu sana kuipeleleza kuliko kesi yoyote ile niliyowahi kupewa kabla. Hadi muda huu tunapoongea sijapiga hatua yoyote ile. Kila ninapojaribu kusonga mbele lakini kuna vikwazo vingi vinatokea. Ninajikuta ninazunguka katika duara lisilo na mwisho. Sasa leo nikiwa hapa nimepigiwa simu kutoka kwa mtu nisiyemfahamu. Mpigaji wa simu kaongea maneno machache sana, yenye dhamira ya kunipa onyo."
"Onyo gani?" Simon alidakia.
"Nisiendelee na kazi hii. Kama ninapenda kuishi basi nisichunguze kifo cha Aneth." Adrian alisema.
"Kabisa amethubutu kumwambia maneno hayo askari Polisi?"
"Ni dakika tano tu zilizopita hayo yametokea. Lakini simu ya onyo imenipa ari zaidi ya kupambana. Kujua chanzo cha kifo cha Aneth. Na kuwatia hatiani watu wote waliohusika katika mauaji ya Aneth. Sasa, kuna kitu nataka unisaidie, lakini iwe nje ya kazi. Unisaidie kama kaka yako, unisaidie kama ndugu yako." Adrian alisema.
"Usihofu Inspekta Adrian, nitakusaidia chochote kile ili kuhakikisha unawapeleka katika vyombo vya sheria wote waliohusika katika mauaji ya Aneth."
"Nashukuru sana Simon. Ninachohitaji kutoka kwako ni msaada wa kiteknolojia. Kitu cha kwanza ninachotaka kutoka kwako ni kuichunguza simu hii niliyopigiwa. Tujue ni simu ya nani? Na imepigwa kutoka wapi? Lakini iwe kazi yetu isiingie katika rekodi ya ofisi yenu. Iwe kazi yetu mimi na wewe." Adrian alisema.
Simon alifikiria kidogo, kisha akasema, " Daah mwanzoni nilikubali kukusaidia. Lakini hilo jambo nahisi litakuwa gumu kidogo. Kutumia tarakilishi za ofisi yetu bila kuweka rekodi sio utaratibu wa ofisi. Afande Bosco anahitaji kujua kila tulifanyalo."
"Simon, najua hayo yote mdogo wangu. Na hiyo ni sababu ya kukuita hapa wewe na kutokuja ofisini kwenu. Lengo ni tuongee sisi wawili, kutokana na utata wa kifo cha Aneth na jinsi mambo yaliyozunguka kifo hiki sitaki kuwajumuisha watu wengi. Nakuomba tufanye jambo hili kwa siri, matokeo yake ndio tutawashirikisha wengine."
"Sawa, nimekuelewa Adrian. Naomba hiyo namba iliyokupigia nitajua kwa namna gani nitafanikisha hilo."
"Ahsante sana kwa kukubali kuifanya kazi hii Simon. Nitakutumia namba ya huyo jamaa."
Wakaongea kidogo na Adrian kisha Simon akaondoka.
Simon alipofika tu ofisini alipokea ujumbe kutoka kwa wafanyakazi wenzake. Alikuwa anahitajika katika ofisi ya Bosco.
Taarifa ya kuitwa ghafla katika ofisi ya afande Bosco ilimstua sana Simon. Bosco alikuwa ndiye mkuu katika kitengo cha TEHAMA katika kituo kikuu cha Polisi.
Bosco alikuwa ni askari mmoja mrefu, mweusi mwenye mwili mkakamavu. Kwa bahati mbaya sifa zake kuu zilikuwa ni roho mbaya, ujivuni na unyanyasaji. Askari yeyote yule katika kitengo cha TEHAMA kuitwa katika ofisi ya Bosco halikuwa jambo jema hata kidogo. Watu walikuwa wanamuogopa Bosco kuliko askari yeyote yule pale kituoni, hata mkuu wa kituo mwenyewe alikuwa anaongea kwa namna ya pekee pindi aongeapo na Bosco. Alikuwa anaongea kwa heshima na taadhima. Na sababu kuu ya yeye kumheshimu Bosco ilikuwa ni moja tu, ukaribu wa Bosco na watu wakubwawakubwa kivyeo.
Simon alielekea ofisini kwa Bosco akiwa na mashaka tele ndani ya moyo wake. Lakini ungejaribu kumuuliza sababu ya mashaka hayo, pengine asingekuwa na majibu sahihi ya kukupa. Alifika nje ya mlango wa ofisi ya Bosco. Juu ya mlango kulikuwa na kibao kidogo cha rangi ya kahawia kilichoandikwa kwa maandishi ya rangi nyeusi.
'Mkuu wa kitengo cha Tehama.'
Taratibu, Simon alishika kitasa na kukizungusha kuelekea upande wa kulia. kwa macho yake aliushuhudia mkono wake mwenyewe ulivyokuwa unatetemeka uliposhika kitasa. Ilikuwa ni hali mbaya sana kwake. Alikuwa mithili ya ng'ombe anayepelekwa machinjioni.
Akagairi kushika kile kitasa.
Aligonga hodi.
"Ingia.." Sauti nzito ya Bosco ilisikika ndani. Sasa ndipo Simon alielekeza tena mkono wake kwenye kitasa. Akakizungusha na kusukuma mlango. Mlango haukumsaliti, ulifunguka taratibu. Akapiga jicho ndani, moja kwa moja akakutana na sura ya Bosco. Akajitutumua na kuingia ndani. Alipofika katikati ya ofisi alijikaza hasa. Akapiga saluti ambayo wala haikupokelewa na Bosco. Yeye, alikuwa bize akiongea na simu yake. Kwa mkono wake wa kushoto akamuonesha kiti. Akajua anaambiwa akae.
Simon akakaa, akimsubiri Bosco amalize kuongea na simu. Iwe zamu yake kuongea na yeye. Na zaidi asikie ni kitu gani alichoitiwa na Bosco?
Sidhani kama Simon alilisikia neno lolote kutoka kwa Bosco wakati akiongea na simu. Ilikuwa ni simu ya upande mmoja. Mara chache Bosco aliitikia ama kuguna. Maneno matatu tu yakapita katika akili ya Simon.
'Simu ya maagizo.'
Dakika saba za simu ya upande mmoja ziliisha. Sasa zikaanza dakika zingine mpya, dakika za yeye na Bosco, bosi wake katika kitengo cha TEHAMA.
"Karibu sana Simon," Bosco alisema huku akijiweka vizuri kitini.
"Ahsante sana." Simon alijibu, huku kwa mbali sauti yake ikimsaliti kwa uwoga.
"Simon, nimekuita hapa kama ndugu yangu. Tunayoongea hapa naomba yabaki kuwa yetu tu, kama ndugu." Bosco alisema akimkazia macho Simon.
Kauli hii ilimstua sana Simon. Pengine alipaswa astuke tangu mwanzo. Kwa maana hata ule ukaribisho ulikuwa na mfanano fulani na maneno haya. Kwa maana maneno haya yaliongelewa na Inspekta Adrian dakika chache zilizopita alipoenda ofisini kwake.
Simon hakujibu, ila mshangao wake ndio uliojibu.
"Naijua sababu ya mshangao wako. Najua umepewa kazi na Inspekta Adrian. Sasa kama mimi ni ndugu yako naomba achana na hiyo kazi. Najua una familia, kufuata maelekezo hayo ni sawa na kuipeleka familia yako katika matatizo." Bosco alisema huku akimkazia macho Simon, ambapo yeye alishindwa kumwangalia usoni.
Alibaki kimya.
"Onyo! Usimwambie chochote Inspekta Adrian juu ya ujumbe huu. Unachotakiwa kufanya ni kumwambia Inspekta Adrian kwamba kazi yake imeshindikana kufanyika.
Nukta!"
Bosco alisema huku akiipiga meza.
"La mwisho, kuanzia sasa unatembea na malaika wa kifo. Kuwa makini sana Simon.Wewe ni kijana mdogo, napenda kuona ukizifikia ndoto zako bila kuyaingilia maisha ya watu. Unaweza kwenda." Bosco alisema huku akimwonesha Simon mlango wa kutokea.
Akiwa amefadhaika, Simon alinyanyuka kitini. Akatoka nje huku akiwa katika mawazo makuu. Ni swali moja lenye maneno kumi ndilo liliomjia kichwani.
"Ina maana Bosco anahusika na mauaji ya mtoto wa Rais?.
Simon alienda hadi ofisini kwao. Mtu yeyote yule angeweza kugundua kwamba Simon alikuwa na mawazo. Lakini hakuna aliyeshangaa kwa wafanyakazi watatu wa ofisi ile ya TEHAMA. Wote walijua kwamba Simon aliitwa na Bosco, na mawazo ni kitu pekee unachorudi nacho ukitoka katika ofisi ya Bosco.
Kwa Regina, askari Polisi pekee wa kike katika idara hii mawazo haya ya Simon kwake yalikuwa nafuu. Yeye siku alipotoka katika ofisi ya Bosco alitoka na mawazo yaliyoambatana na kilio.
Ilikuwa ni siku ya tatu baada ya kuhamishiwa katika idara ya Tehama kutoka katika majukumu yake ya awali. Ndipo alipogundua kwamba bosi wake alikuwa anampenda kimapenzi, hapana, neno sahihi kulitumia ni bosi wake alikuwa anamtamani kimwili.
Regina, mhitimu wa shahada ya kwanza katika chuo kikuu cha Dar es salaam. Kwa bahati nzuri sana, Regina alikuwa kinara katika kitivo cha teknolojia ya mawasiliano na habari kwa mwaka aliomaliza. Lakini bahati mbaya ikafata, Regina akaja kuwa wa mwisho katika soko la ajira. Siyo kwamba hakuajirika. Hapana, aliajirika, lakini hakuajiriwa.
Mwaka wa kwanza ulipita, wa pili ukafuata, watatu ukaingia lakini Regina hakupata ajira pamoja na kuitwa katika sahili kibao, zote aliangukia pua. Mwaka wa nne ndipo alipoamua kurusha kete yake katika nafasi za ajira katika jeshi la Polisi. Huko alipata zari, aliajiriwa.
Ukazuka mgogoro mpya baada ya kupata ajira ndani ya jeshi la Polisi. Mgogoro wenyewe ulitokana na mpenzi wake, Boniface au Bonny kama mwenyewe alivyopenda kumwita. Bonny hakutaka mpenzi wake awe askari Polisi.
Mvutano ulikuwa mkubwa sana ndani ya mahusiano haya. Bonny alikuwa anamkataza Regina asifanye kazi bila sababu. Regina alitaka kufanya kazi kwa sababu.
Mgogoro ulikuwa siku baada ya siku.
Kitu kizuri ni kwamba, mgogoro huo haukuvunja mahusiano yao, ingawa yalitetereka kwa kiasi fulani.
Pamoja na kuwa na mgogoro lakini Regina alianza kazi kama Polisi wa kawaida, na baadaye kuhamishiwa katika kitengo cha TEHAMA katika kituo kikuu cha Polisi, huko ndipo akakutana na bosi mpya, Bosco.
Mwanzoni, Regina alihisi Bosco alikuwa anamtamani. Jinsi akivyomtazama, jinsi akivyomsemesha ilikuwa ni sawa na mwanaume yeyote yule anamyemtamani mwanamke kwa mara ya kwanza.
Regina alijiweka bize na kazi, akimkwepa Bosco mara kwa mara.
Lakini ikatokea siku aliyoitwa ofisini na Bosco.
Hakurudi salama.
Ni dakika mbili tu za kumkataa Bosco zilimfanya arudi na mawazo yaliyoambatana na kilio. Kwani bado hujaelewa Bosco alimfanya nini Regina?
Alimbaka!
Kitendo hiko kilimfanya Regina ajisikie mnyonge sana. Sio tu kilimuondolea hamu ya kufanya kazi, bali pia hata hamu ya kuishi. Kwake, kilikuwa ni kitendo cha udhalilishaji mkubwa sana. Kilimdhalilisha yeye na mchumbaye, Boniface.
Hapakuwa na pakwenda kushtaki. Mkuu wa kituo mwenyewe alikuwa anamwogopa Bosco, sasa angeenda wapi?
Hakumsimulia hata Boniphace maana alijua ungekuwa mwisho wa wa penzi lao, na Bonny angejiona nabii kwa kumkataza mapema kufanya kazi hii.
Regina aliamua kukaa kimya huku akiugulia ndani kwa ndani. Lakini siku zote akiomba kwa Mungu amfanye kitu Bosco. Ikapita miezi Mungu hakumfanya kitu Bosco, hadi leo hii Simon anaporudi akiwa na mawazo tele.
Simon akiwa katikati ya mawazo, akapokea ujumbe kutoka kwa inspekta Adrian.
'0710896977, namba ya kimeo hiyo.'
Simon akawa katika mtihani. Pengine unaweza kuwa mtihani mkubwa zaidi katika maisha yake. Kama alikuwa anaupenda uhai wake na familia yake, basi inampasa aache kazi ya kuipekua ile namba kama alivyoonywa na Bosco.
Mtihani.
Itaendelea..