Riwaya ya Kijasusi; Mtoto wa Rais

RIWAYA; MTOTO WA RAIS
Imeandikwa na Halfani Sudy
Sinu 0652 212391

Sehemu ya Ishirini na Moja

"Tutaenda kuweka makazi yetu nje ya Ikulu kuanzia kesho alfajiri. Tutafata nyendo zake zote kutokea hapo. Kwa sasa turudi nyumbani" Daniel alisema.

***

Ni saa moja ilikuwa imepita tangu wamkose Mzee Kizito nyumbani kwa Donald Tengo. Walirudi maskani kwao. Wakina Karim walikuwa wamerudi na mtoto Aisha. Wote walikula na kuoga, kila mmoja akaenda kupumzika.

Chumbani kwa Daniel alipumzisha mwili tu, lakini akili ilikuwa kazini.

"Bado sijapata mwanga juu ya mkasa huu. Tangia mwanzo yametawala mafumbo tu ambayo ni magumu sana kuyafumbua. Pengine kesho tutapata kitu kwa kufatilia nyendo za Aneth. Bila shaka Aneth ana kitu ambacho kinawafanya wamsake na kutaka kumuua, ni kitu gani hiko? Lazima kesho nifahamu. Utata mwengine upo katika hadithi ya Salum Taiwan. Alisema jamaa wananunua kemikali kwa bei kubwa sana, je nini kazi ya kemikali hizo? Wamepanga kuzifanyia nini? Na wapi?. Fumbo lengine lipo kwa Zayiid Khalifa. Nadhani bado sijapata taarifa nyingi kumhusu huyu mtu. Taarifa alizonipa Hannan pekee sidhani kama zinatosha. Hadi sasa najua kwamba Zayiid anasakwa na C.I.A, pia zaidi ameletwa hapa nchini na wakina Donald Tengo. Kwa kazi gani? Yupo wapi kwasasa? Anafanya nini?. Maswali ni mengi, na yatupasa kuyatafuta majibu. Huu sio muda wa kupumzika!" Daniel alisema akinyanyuka kitandani. Akaanza kutembea taratibu akirejea ukumbini.

"Lazima tujue zaidi kuhusu ZAK, lazima tujue sababu ya kumuua Aneth. Lakini, kwanini nisiende kuongea na Aneth hukohuko Ikulu? Pia nimtahadharishe na nyendo zake ingawa tutakuwa tunamlinda kwa siri. Nafikiri ni wazo zuri" Daniel alifika sebuleni. Alibonyaza swichi moja ukutani. Ndani ya dakika moja wote walifika ukumbini mbiombio.

"Muda wa mapumziko umeisha" Daniel alisema akiwatazama usoni.

Watu wote walimshangaa.

"Niliwaambia mkapumzike. Sasa muda wa kupumzika umeisha. Huu ni wakati wa kazi" Daniel aliongea utani ukiwa mbali na yeye.

"Leonard na Hannan ninahitaji taarifa zaidi kuhusu Zayiid Khalifa. Ninawapa nusu saa. Mpekue mnavyoweza kutoka katika vyanzo vyenu vyote vya taarifa. Mje na taarifa hapa Zayiid ni nani hasa? Nendeni mkajifungie katika kile chumba cha mwisho" Daniel alisema, na wakina Leonard wakaelekea katika chumba alichowaonesha Daniel.

"Timu ya wadunguaji, Amin na Amani. Mimi pamoja nanyi" Daniel alisema akiwaonesha mkono Karim na Martin "Tunaenda kazini sasahivi. Kazi yetu ya kwanza ni kwenda kumsaka Aneth popote pale alipo. Aneth ni mtu muhimu sana kwetu kwa'sasa. Bila shaka ana taarifa ambazo zinamfanya atafutwe kwa udi na uvumba. Lazima tuwe wakwanza kumpata Aneth ili tuzipate taarifa hizo. Tunaingia mtaani sasahivi" Daniel alisema akiwatolea macho Karim na Martin.

"Wazo zuri Daniel, huu haukuwa muda sahihi wa kupumzika. Lakini kwanini tusimtumie Hannan kunasa simu ya Aneth ili tujue mahali alipo? Hii ni nzuri kuliko kwenda kuzurura tu huko mtaani" Martin alisema.

"Upo Sahihi Martin. Karim kamwite Hannan, mwambie aje na tarakilishi yake" Daniel alisema. Karim alienda katika chumba walichokwenda wakina Hannan.

Ndani ya dakika moja Hannan na Karim walirejea. Hannan akiwa na tarakilishi mkononi.

"Samahani kwa kuwakatisha kazi yenu. Kuna kazi ya dharura imejitokeza hapa" Daniel alisema akimwangalia Hannan.

"Kazi gani Daniel?"

"Tunataka utafute mahali alipo Aneth sasahivi. Tunataka tumfate hapohapo alipo" Daniel alisema.

Hannan hakuongea kitu. Aliiweka tarakilishi yake juu ya meza na kuanza kuichezea.

"Anaitwa Aneth Mark Mwazilindi" Hannan alisema.

"Ndio" Daniel alijibu.

"Sawa, nimeipata namba yake" Hannan alisema huku akiwa ameiinamia tarakilishi.

Ukumbi ulikuwa kimya, wote wakimwangalia Hannan akifanya mambo yake.

"Kwasasa Hannan yupo Masaki, katika nyumba namba hamsini na tisa. Najaribu kuangalia mmiliki wa nyumba hii" Hannan alisema huku akiendelea kubonyaza tarakilishi yake kwa kasi kubwa sana.

Baada ya muda mfupi akasema "Kwa mujibu wa taarifa kutoka mamlaka ya nyumba. Hii nyumba namba hamsini na tisa iliyopo Masaki, inamilikiwa na mtu anayeitwa Joash Mtoto..."

"Yule mbunge kijana machachari?" Daniel aliuliza.

"Bila shaka ni huyohuyo. Joash Mtoto ni mbunge mdogo zaidi bungeni. Joash akijipatia umaarufu mkubwa sana bungeni baada ya kupeleka mswaada binafsi juu ya namna ya kuzuia biashara ya madawa ya kulevya hapa nchini. Ingawa mswaada ule ulikataliwa bungeni, lakini Joash Mtoto alikubalika sana kwa wananchi. Hadi leo wananchi wanashangaa kwanini mswaada ule ulikataliwa?" Hannan alisema.

"Yatupasa twende huko Masaki. Nahisi kuna kitu kinaendelea kati ya Aneth na Joash" Daniel alisema.

"Wazo zuri. Nitawaambia endapo simu ya Aneth itahama eneo" Hannan alisema.

"Sawa Hannan, kaendelee kufanya kazi ya kumchunguza Zayiid, lakini pia usiache kuangalia mienendo ya simu ya Aneth" Daniel alikubali.

Hannan alirudi chumbani. Hakukumkuta Leonard. Alipochungulia dirishani alimwona akiongea na simu bustanini. Akaendelea na kazi.

Wakati Martin, Daniel, Amini, Amani na Karimu walitoka nje. Safari ya kuelekea Masaki nyumbani kwa Joash Mtoto ilianza. Walitoka na gari mbili, ya mbele ilikuwa imepandwa na Daniel Mwaseba, Martin na Karim. Wakati nyuma walifuatiwa na wakina Amini.

Kutokana na foleni waliyokutana nayo barabarani iliwachukua wakina Daniel saa zima kufika Masaki, nyumbani kwa Joash Mtoto. Wakiwa njiani mara kwa mara waliwasiliana na Hannan, na mara zote Hannan aliwaambia kuwa simu ya Aneth bado ilikuwa ndani ya nyumba namba hamsini na tisa, Masaki.

Walifika Masaki, walipaki gari mita chache nje ya nyumba ya Joash Mtoto. Na kama kawaida wakina Amini wao walipaki kwa mbali kidogo wakifatilia kila kitu.

"Timu ya wadunguaji wametuambia kila kitu kipo sawa. Sasa tunaenda kuingia katika hii nyumba, ambayo tunaamini Aneth yupo ndani yake. Umakini unahitajika kama ilivyo ada ya Mpelelezi yeyote yule duniani" Daniel aliwapa tahadhari.

"Tunaingiaje? Kwa kuvamia au kistaarabu?" Karim aliuliza.

"Tutaingia kistaarabu kwa kwenda kugonga geti. Mbinu itabadilika kutokana na tutakavyopokelewa huko ndani. Lengo la kwanza la misheni hii ni kumpata Aneth akiwa hai. Lengo la pili la misheni hii ni kumpata Aneth akiwa hai. Na lengo la tatu la misheni hii?" Daniel aliuliza.

"Ni kumpata Aneth akiwa hai" Martin na Karim walijibu kwa pamoja.

Walishikana mikono huku Daniel akigawa majukumu. Na misheni ilianza. Karim alibana upande wa kushoto wa geti. Daniel alibaki upande wa kulia, wakati Martin alienda kugonga geti. Kila mmoja alikuwa karibu sana na bastola yake. Hawakujua nini kitatokea katika sekunde inayofuata.

"Ngo ngo ngo" Martin aligonga geti kwa mkono wake wa kushoto.

"Ngo ngo ngo ngo" Aligonga tena kwa mara ya pili baada ya ile ya kwanza kupokelewa na ukimya. Lakini bado iliendelea kupokelewa na ukimya.

"Jaribu kusukuma geti" Daniel alisema kwa sauti ndogo iliyofikiwa na masikio ya Martin Hisia.

Martin akasukuma geti dogo. Geti likafunguka. Martin aliutumia upenyo huo kuchungulia ndani. Hakuona kitu chochote zaidi ya maua yaliyopangiliwa kwa mpangilio mzuri.

"Ingia ndani, kuwa makini sana Martin" Daniel alisema kwa kunong'oneza.

Martin alinyata taratibu, bastola ikiwa mbele. Aliingia mle ndani na kwa kasi alielekea katika kibanda cha mlinzi. Ilianza kufika bastola yake kibandani kabla ya yeye. Akiwa kibandani aliangalia mazingira yote ya mle ndani. Kulikuwa kimya kabisa, kimya, kimya, kimya.

"Mnaweza kuja kuko salama" Martin aliongea kwa kutumia vifaa walivyovaa masikioni. Wakina Daniel nao wakaingia ndani na bastola zao mikononi. Wote wakichukua tahadhari kubwa sana. Walielekea pale katika kibanda cha Mlinzi.

"Haujakuta mtu hapa?" Daniel aliuliza naye alipofika.

"Hapana, hakuna mtu" Martin alijibu.

"Yatupasa kwenda ndani. Bila shaka Aneth yupo ndani ya nyumba hii. Hannan kanitumia meseji kusisitiza bado simu yake ipo humuhumu ndani" Daniel alisema kwa uhakika.

"Sawa, tunaenda ndani kwa kulindana. Tuhakikishe hakuna anayefanya kosa lolote lile, kosa moja tu litaamua hatma ya mwengine" Martin alisema akitoa tahadhari.

Alianza Daniel Mwaseba, alijibiringisha kwa namna ya ajabu hadi mlangoni. Ilikuwa ni mithili ya tairi la gari likisukumwa na mtoto mdogo. Martin naye akafata kwa mtindo uleule, mwisho Karim alienda, lakini hakuweza kuwaiga wale wanaume wawili. Wakipekee. Yeye alitambaa kama nyoka wa kijani.

"Tunaingia ndani, umakini zaidi unahitajika. Nitapiga hodi, isipojibiwa tutaingia kwa namna yetu" Daniel alisema.

Alijaribu kupiga hodi. Lakini kulikuwa kimya. Akabisha tena hodi, bado kulikuwa kimya. Akajaribu kuufungua ule mlango. Ulikuwa umefungwa. Akatoa rundo la funguo mfukoni. Akajaribu funguo ya kwanza, ikakataa. Akajaribu ya pili, ikakataa, akajaribu funguo ya tatu, mlango uliitika. Mlango uliwachekea.

Daniel alitangulia kuingia ndani akifatiwa na Karim, kisha Martin. Wote bastola zilikuwa zimetangulia mbele ya vifua vyao. Walikuwa makini sana.


Itaendelea...
Kazi nzuri inapatikana wapi
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom