DUKA LA ROHO
SEHEMU YA PILI
Ndani ya nyambizi ile, kulikuwa kuna pilika za hapa na pale hasa wale mafundi mitambo wanaongoza chombo kile maalumu kwa ajili ya kazi za kijeshi au kiusalama.
Naam, baada ya Lisa na kundi lake wakiwa sambamba na mtuhumiwa wao kuingia kwenye chombo kile, waliongozwa kwenye chumba maalumu na kuoneshwa nafasi zao za kukaa.
Baada ya kukaa, alitokea daktari mmoja akiongozana na kijana aliyebeba sinia dogo lililokuwa na sindano uwezazo kuzikamata kama bastola. Sindano hizo zenye dawa kiasi, kila mmoja alichomwa begani na baada ya dakika chache, macho ya hawa watu yakaanza kuwa mazito.
"Kazi za utumwa hizi. Hamtakiwi kujua hata ni wapi mnafanyia kazi na ndio maana mnapigwa sindano za usingizi ili msione mnapoenda. Stupid peoples." Sauti nzito iliyochanganyanyika na ulevi, ilimtoka yule mtuhumiwa aliyekuwa huru kuongea baada ya kutolewa ile gundi aliyozungushiwa na Mubah.
Hakuna aliyemjibu na badala yake, kila mmoja alibebwa na usingizi mzito.
****
FISSA (Federal Intelligence Secret Service Agencies)
Mlango mmoja mkubwa uliandikwa maandishi hayo ambapo ndipo hasa Lisa na Mubah wanafanya kazi zao. Ule usingizi mrefu ulikuwa umewapaa na sasa walikuwa wanatembea wenyewe huku wakimkwida vema mtuhumiwa wao ili asiwaponyoke.
"Kazi nzuri Agent Lisa. Mmefanya vizuri na kikosi chako." Sauti ya mtu mmoja mrefu kiasi na mweusi, ilisikika ikiwa kwenye jukwaa dogo ambalo mbele yake kulikuwa na watu wanachakalika na kompyuta zao huku skrini moja kubwa ikionesha kazi nzima wafanyazo wale wafanyakazi.
"Asante mkuu." Lisa alishukuru huku akiinama kidogo kuonesha heshima kwa mkuu wake wa kazi.
Mkuu yule akashuka toka kwenye lile jukwaa na moja kwa moja akamfuata yule mtuhumiwa na kumuangalia kwa macho makali kabla hajaanza kuongea.
"John Lobo. Nilishangaa sana nilipoambiwa kuwa u mzima.
Nilikuua kwa mikono yangu, lakini leo ni kama nakutana na mzimu." Sauti ya yule bwana ilipenyeza kwenye masikio ya kila mmoja aliyesikia vema maongezi yale. "Sina kesi na wewe. Nilishakuua kipindi kile, hapa naanza na kesi nyingine." Alimaliza Mkuu wa FISSA na kugeuka nyuma kurudi kwenye lile jukwaa dogo.
"Malocha Malingumu." Sauti ya John Lobo, mtuhumiwa aliyekamatwa na kundi la Lisa, ilimuita yule mkuu wa kitengo cha siri cha huduma za kipelelezi nchini Tanzania. Bwana Malocha akasimama kumsikiliza kimtokacho John Lobo.
"Siyo kosa langu kuua familia yako.
Nilinunua roho zao kwa kuamrishwa na shetani langu. Usilalamike sana. Hahahahahaaa." Lobo alimaliza kwa cheko lake la kukera kushinda hata la katuni au fisi.
"Mpelekeni Hell in Hell." Malocha akaamuru na kila mmoja alishituka baada ya kusikia amri hiyo.
"Hamjanisikia?" Malocha aliuliza baada ya kuona hakuna kinachotendeka baada ya amri.
"Lakini Mkuu huyu tutampoteza kule. Kumbuka CIA na FBi wanamtaka mzima." Lisa akiongea kumuelewesha mkuu wake.
"Kwa hiyo unashauri apelekwe wapi?" Malocha akauliza tena swali.
"Nadhani twende naye 123K." Alitoa wazo Lisa.
"Kwa hiyo akakae tu! Kaja kukaa hapa au kusema ukweli?" Malocha alimtupia swali Lisa.
"Lakini si kumpeleka Hell in Hell. Atasema nini kule?" Lisa alijitetea.
"Hivi mmenileta huku nije kusema kitu au nije kupiga story na 'school mate' wenzangu?" Lobo alifungua kinywa chake na kuwauliza wale wanaoshauriana wapi wampeleke.
"Kama mnataka mnijue au niseme chochote, hilo mmekosea. Hapa hampati kitu wajinga nyie." Lobo akamaliza na hapohapo ngumi nzito ya tumbo ilitua. Alikuwa ni Mubah aliyemuadabisha.
"Utalipa hii dogo." Lobo alimwambia Mubah na Mubah badala ya kutilia maanani yale maneno, alimuongeza konde lingine zito la tumboni.
"Big Mistake(Kosa kubwa) Lakini bado unanafasi ya kulisawazisha." Lobo alimwambia tena Mubah baada ya kuinuka alipokuwa kainama kwa sababu ya kupigwa ngumi ile.
"Mpelekeni 123F6."Malocha aliamuru tena. Na kitendo bila kuchelewa, Lisa na Mubarak walimkamata kushoto na kulia na kuanza kumkokota kwenda chumba walichokiita 123F6.
HELL IN HELL
Hichi ni chumba kipana kilichopo ndani ya FISSA. Ndani ya chumba hiki kuna kiti cha umeme ambacho hutumika kuwasulubu watuhumiwa nguri na saa nyingine kuwaua.
Pia kuna tank kubwa ambalo limejengwa kwa vioo, na tank hilo ndani yake kuna maji. Pia hutumika kusulubisha watuhumiwa kwa kuwazamisha humo au wakiona haongei, hufungulia umeme uliyoungwa ndani ya tank hilo na kuanza kumpiga shoti mtuhumiwa. Hizo ni silaha chache zilizopo katika chumba kiitwacho Hell In Hell. Mbali na hayo, kuna vifaa vya kunyongea na kuchania ngozi.
Ni chumba ambacho kinaogopwa hata na wafanyakazi wenyewe. Kinatisha kwa matendo yanayofanyika huko.
123K
Hiki pia ni chumba kilichopo hukohuko FISSA. Chumba hiki pia ni kipana na kina meza moja kubwa pamoja na kioo ambacho ukiwa ndani huwezi kumuona wa nje lakini wa nje anamuona wa ndani.
Chumba hichi ni kwa ajili ya kumuhoji mtuhumiwa kwa mdomo bila kumsulubisha. Na hata kama watataka.kufanya hivyo, basi hutumia viungo vyao kama ngumi na mateke.
123F6
Hiki ni chumba kipana pia kwa ajili ya mahojiano na watuhumiwa. Ndani ya chumba hiki, mahojiano huwa ni ya kulazimisha uongee ukweli kwa kubanwa na silaha mbalimbali pamoja kuchomwa na vitu vyenye ncha kali lakini lengo likiwa utoke mzima.
Na mara nyingi kama mtuhumiwa ni mgumu, basi hupigwa sindano yenye dawa kali ambayo hufanya ubongo na akili ya mtuhumiwa iwaze kusema ukweli tu.
Humo ndimo ambamo John Lobo kapelekwa. Nyuso mbili ambazo hazina utani zilikuwa zimesimama pembeni ya chumba hicho huku wakijaribu jaribu vifaa vyao.
Mzee mmoja ambaye alikuwa anapuliza gesi yenye moto juu, aligeuka haraka baada ya kusikia mlango wa chumba kile ukifunguliwa.
"Ooh! Lisa. Umefanikiwa kumkamata Lobo. Kazi nzuri sana binti." Mzee yule aliongea kumpongeza Lisa.
"Asante Babu Pujini, hakuleta shida wakati wa kumkamata." Lisa alimjibu Mzee Pujini ambaye alikuwa ana asili fulani ya Kihindi lakini ni Muafrika halisi kutoka Tanzania.
"Good Lisa. Ndio umemleta kwenye shughuli eeh." Mzee Pujini aliongea huku akianza kuchezea tena ile gesi kwenye kibubu maalumu kinachotengeneza moto huo wa gesi.
"Ndio babu. Fanya yako." Lisa alijibu na wakati huo Mubah alikuwa anafungua pingu alizokuwa kamfunga John Lobo.
Licha ya Lisa na Mzee Pujini kuongea mengi yanayomhusu John Lobo, lakini Lobo mwenyewe hakuwepo kwenye dunia yao bali macho yake yalikuwa yakipepesa huku na huko, chini na juu ya chumba kile.
"Huyu hapa Mzee." Sauti ya Mubarak ilisikika huku ikifuatiwa na kumsukuma Lobo kwa mzee yule bingwa wa kutoa adhabu kwa watuhumiwa mbalimbali.
"Beda. Muondoe misuti yake huyu bwana." Mzee Pujini alimsukumia Lobo kwa Beda, jamaa fulani wa makamo na kwenye mwili mkubwa kutokana na kunyanyua vitu vizito.
Naye Beda bila kuchelewa, akaanza kumwondoa nguo John Lobo na wakati huo Lisa na Mubah walishatoka katika chumba kile na Mzee Pujini alishakifunga.
****
"Lobo. Nia yako na washirika wako ni nini?" Sauti ya kiume ilisikika katika chumba kiitwacho 123F6.
Ilikuwa ni sauti ya Malocha ikitoka kwenye spika zilizopo kwenye chumba kile.
Lobo alikuwa akivuja damu nyingi kifuani na maeneo ya usoni. Alikuwa kalegea kwa mateso makali ambayo yalitoka mikononi mwa Beda na Mzee Pujini.
"Kazi yangu ni kuuza au kununua roho tu!
Sina kazi nyingine. Sina nia na wala sijui washirika wangu ni wakina nani." Lobo alijibu swali la Malocha na baada ya jibu hilo, Malocha alitoa ruhusa ya mateso kuendelea.
Mzee Pujini akachukua kile kibubu chenye gesi na kuwasha gesi ile. Baada ya kuweka moto fulani kwenye kibubu kile cha gesi, akamfata Lobo na kuanza kumpitishia machoni bila kumdhuru bali kumsikilizisha joto litokalo mle kwenye kibubu.
"Joto hili linaenda kwenye maungo yako ya uzazi." Mzee Pujini akiwa kavalia kama Daktari, akaongea huku taratibu akianza kushusha moto ule kwenye maeneo ambayo kayataja.
Licha ya hayo yote kutukia, uso wa John Lobo ulikuwa si wenye mashaka wala uoga. Ni kama alishazoea yale mateso, lakini yote ni sababu alikuwa mkomavu katika nyanja kama zile.
Mzee Pujini akafika maeneo ya uzazi ya John Lobo, na bila kusita akapulizia gesi ya moto maeneo yale na kumfanya John Lobo atoe sauti kali iliyochanganyika na maumivu. Hakika mkomavu na kamanda wa mateso, alikuwa anaumia.
"You fu**n, motherfu***r you're hurting me. (We mpumbavu, (tusi). Unaniumiza)." Sauti ya maumivu makali ilisikika kutoka kwenye kinywa cha Lobo ikifuatana na matusi mazito ya wazazi kumuelekea Mzee Pujini.
"Sema ukweli tuache hili zoezi." Mzee Pujini aliacha kuchoka maeneo nyeti ya Lobo na kumuomba aseme ukweli.
"Pale nitakapofanikiwa kusimama kwenye hiki kiti, wewe ndio utakuwa wa kwanza kufa." John Lobo alimwambia Mzee Pujini maneno ambayo yule mzee alitabasamu kwa dharau kisha akaangalia kile kioo ambacho wa ndani hamuoni wa nje ikiwa ni ishara ya kuwaambia waulize swali lingine.
"Lobo. Hatupo hapa kukuumiza. Ni rahisi tu! Unashirikiana na nani na nini nia yako kwa ufanyayo." Swali lilelile lilitoka kwenye kinywa cha Malocha.
"Hahahaaa. Malocha, mbona unajiumiza sana. Nimekwisha kwambia, sina nia zaidi ya kuuza na kununua roho za watu.
Au unataka nikwambie duka la roho lilipo?" Lobo aliuliza huku uso wake ukielekea kwenye kile kioo kana kwamba anawaona wale wanaomtupia maswali kwa kunong'onezana.
"Lobo. Hatupo katika utani. Umemuua Kamanda wa Kikosi cha Upepelezi kanda ya kati. Umewatishia amani mawaziri mbalimbali na kauli yako ya kununua roho zao. Ukawaua baadhi ya viongozi hao. Ukaona haitoshi, ukaanza kuwaondoa mabalozi mbalimbali wa nchi hii kwa kuwaua. Sasa umegusa pabaya zaidi. Marekani.
Umegusa nchi ambayo hatuiwezi kwa kitu chochote....." Sauti ya Malocha ilikuwa ikielezea baadhi ya maovu ya John Lobo lakini kabla hajamaliza maongezi yake, sauti yenye hasira kupindukia, ilimkata kauli.
"Eti hatuiwezi kwa chochote.
Ni ujinga gani ambao umekujaa kichwani we' mpumbavu? Marekani anachotuweza ni nini? Au ndio kasumba zenu za uoga bado zimewatawala kichwani mwenu?
Huyu Frank anapambana na kutafutwa kwa udi na uvumba na watu gani? Si ni hawahawa Wamarekani? Mbona hawampati? Mbona hata wakimpata wanamshindwa? Kaua makomando wangapi Wakimarekani. Usiwe mjinga Malocha. Umiza kichwa fala wewe." Kauli chafu zilitiririka toka kinywani mwa Lobo na hakuna aliyethubutu kumkatiza hadi alipomaliza mwenyewe.
"Sound like it's true. But none of it is real. (Sauti kama ya ukweli. Lakini hakuna kati hivyo chenye uhalisia)." Malocha aliongea kwa kutumia lugha ya ughaibuni.
"Frank, never killed any commander from America. He just killed the terrorists, and bad guys. (Frank hakuua kamanda yeyote wa Kimarekani. Aliua wavamizi na watu wabaya pekee)." Sauti ya Lisa iliunga maelezo ambayo Malocha aliyaacha kati.
"Inaonekana hamjui lolote la kwa nini Frank anatafutwa na kwa nini kajificha. Na mbaya zaidi, hao anaowaua ndio mimi na baadhi yenu nyie wapelelezi mnawasujudia. Mtakufa kama panya kwenye sumu kwa mkono wangu." Lobo aliongea kwa hasira huku akijaribu kuchomoa mikono yake toka kwenye kiti alichokuwa kafungwa barabara na wazee wa kazi wa chumba 123F6.
Hali ya kujikakamua ili atoke pale kwenye kiti, ilifanya mwili wake ututumke na kusambaa misuli kama ananyanyua vitu vizito.
"Mzee Pujini. Fanya yako." Malocha aliongea kumruhusu tena Mzee Pujini aendeleze adhabu zake.
Mzee Pujini naye bila kusita, akajaribu moto wake angani kabla hajaanza kazi ya kuchoma ngozi nyeusi ya John Lobo.
****
"Hahahahahaa. Kuna muda hamna haja ya kulia bali kucheka kwa sababu maumivu uyapatayo, ni sawa na kukutekenya tu." Sauti ya John Lobo iliongea baada ya Mzee Pujini kumaliza kumchoma kwa gesi maeneo ya ndani ya mapaja na kifuani.
"Look like you are so tough. Lets see. (Unaonekana kama mgumu. Ngoja tuone)." Sauti ya Beda, mshirika au msaidizi wa Mzee Pujini ilisikika ikiongea hayo huku ye' mwenyewe akivaa grovu tayari kutimiza majukumu yake.
Beda akachukua visu fulani vidogo vilivyo kwenye mkoba maalumu kwa ajili ya kuvihifahidhia. Na baada ya kukamata visu hivyo viwili, akawa anavinoa kwa kuvisugulisha vyenyewe kwa vyenyewe huku akitembea mbele ya Lobo huku na huko.
Visu vilivyokuwa vinang'aa kama almasi lakini ni vya siliva, vilipita kifuani mwa Lobo haraka na kuacha alama kama ya X kifuani hapo, na kabla hata Lobo hajalia kwa sababu ya maumivu, akamwagiwa mafuta fulani spesheli ambayo yanauma si kawaida pale yawekwapo kwenye vidonda, lakini ni tiba tosha kwa ambaye anavuja damu.
"Fuc*** you FISSA. And fuc** you all and your mama."Lobo alitukana matusi mazito ya Kimarekani kwa sababu ya maumivu makali yaliyokuwa yanampata kwa wakati ule. Hakika alikuwa katika mateso, lakini bado hakuwa tayari kusema ukweli wowote.
"Lobo. Nia yako ni nini na washirika wako ni wakina nani?" Malocha aliuliza kwa sauti kali tena.
"Nia yangu ni kusafisha pasafi kwa kuweka uchafu. Washirika wangu ni uchafu, umenielewa?." Lobo alijibu kwa hasira kali zilizokuwa zimemjaa moyoni sababu ya kuchanjwa na kuteswa na FISSA.
"Mkuu, niachie mimi nikamuhoji mlemle." Mubarak alitoa ombi ambalo halikukataliwa kwa sababu majibu ya John Lobo yalikuwa hayana mashiko hata kidogo vichwani mwao.
"Ooh! Mubah. Umekuja kuchukua ujumbe wako." Lobo alitoa tabasamu pana baada ya kumuona Mubarak kaingia ndani ya chumba kile.
Mubah hakuongea chochote zaidi ya kuchukua chuma chenye ncha kali kwenye ule mkoba wa kuhifadhia vifaa hivyo vya mateso.
"Nauliza swali. Nataka jibu sahihi." Mubah alimwambia Lobo huku akikaa kwenye kiti ambacho alikivutia mbele ya Lobo.
Lobo badala ya kujibu, alitabasamu tena. Tabasamu la kukereketa hata ubongo wa kichaa.
ITAENDELEA