Wakili wa shetani
JF-Expert Member
- Nov 22, 2022
- 2,095
- 3,938
Miaka ya nyuma wakati wa ukoloni bonde la mto Rufiji lilijaa sana wanyama. Pengine nchi hii hakukuwa na sehemu yenye wanyama wengi kama bonde la Rufiji. Simba walikuwa wengi na waliua sana wenyeji. Wenyeji nao wakawa mafundi sana wa kuwinda na kuua simba. Hata kuna kipindi watu wa huko Singida walikuwa wanasumbuliwa na simba. Serikali ikaenda kuchukua wawinda simba kutoka bonde la Rufiji maana ndiyo walikuwa na uzoefu na hawakuogopa kupambana na simba. Hadithi moja ya simba wala watu ni ya simba aliyeitwa Zima-taa.
Mnyama huyo aliwashambulia watu bila ya kusitasita kokote alikokutana nao; mioto na taa ambazo kila mara huwatisha wanyama ndizo zilizomfanyisha ajue mahali walipo binadamu. Mara wenyeji wakaona bora wafunike taa zao na mioto waizime kila wakishamaliza kazi zao. Mambo yalileta taabu kubwa, wakaanzisha ‘Zima-Taa’ yao ya kienyeji, na hapo yule mnyama akapewa jina la ‘Zima- Taa’.
Wazungu wa serikali na wengineo wakujuao zaidi huku Afrika ya Mashariki wanakubali kwamba bonde la Rufiji limejaa wanyama wengi wa kila aina. Mzungu mmoja aliyenuia kukaa katika nchi ile zamani alitoroka kwa kuogopa wingi wa wanyama, lakini Warufiji na jamii ya wenyeji watokao katika nchi za jirani hukaa na kustahamili tabu za kila namna na kuwa tayari kuzitosa roho zao wanapolinda vyakula vyao vilivyomo mashambani.
Kijiji cha Mohoro ndicho cha zamani katika vyote hapo Rufiji. Kwa kuwa kijiji hicho kipo kusini kabisa ya nchi ya Rufiji, kimekuwa bandari kuu ya majahazi ya shehena na ofisi ya simu. Hapo, mapema usiku mmoja, huyo simba mla watu alijitokeza wasafiri wachache walipokuwa bado wamo njiani na wenyeji bado hawajalala. Mtu mmoja aliyekuwa akiitwa Hassani, aliyetoka Mohoro ya Zamani, alikuwa akivuka daraja la miti. Hassani alikuwa ametumwa kuja hapo kuleta habari fulani. Kabla hajaona taa za madukani ng’ambo, hatua chache chini ya daraja jahazi lilikuwa limefungwa kando ya mto na mlinda wa jahazi hili alikuwa amechutama nyuma ya jahazi.
Ghafla, katikati ya daraja, yule kijana akamwona simba mkubwa, viungo vyake vimekazana na mkia wake ukipigapiga huku na huku kwa kitisho! Hassani akasimama upesi, na hapo wakasimama wakitazamana. Hassani akafikiri kujitosa majini na aogelee mpaka kwenye jahazi, lakini mahali pale palikuwa pabaya sana kwa mamba; jamaa wengi sana wamekamatwa na mamba.
Dakika nyingi zikapita yule mtu na nyama walipokuwa wakitazamana; kisha yule mlinda wa jahazi akapiga kelele “Ruka majini na uogelee mpaka jahazini! Ndio salama yako!”
Yule simba akageuka kule kunakotoka sauti ile, Hassani akaona hakuna wakati wa kuporonyoka ila ule. Akajitupa majini. Kwa dhoruba kali za mikono alizokuwa akipiga alipokuwa akioegelea zilimsaidia kuwatisha mamba, akafika jahazini salama, akakamata mikono ya yule mlinda na akavutwa juu kwenye jahazi.
Wote wawili sasa wakakaa wakimuangalia yule simba aliyekasirika akilivuka daraja na kupotea mnamo vivuli vya miti iliyopandwa barabarani.
Wakati ule ubishi ukaanza huko ng’ambo, na makelele ya watu waliokuwa wakibishana yaliweza kusikilikana mpaka pale mtoni, na taa ilikuwa ikionekana katika nyumba ya Mzungu mmoja aitwaye ‘Mtawa Maporini’. Kwa kujua kuwa yule simba amekwendea upande ule ule, Hassani akaweka mikono mbele ya kinywa chake akapiga ukelele kuwajuvya wakaao pamoja na Mtawa Maporini’. “Juma Juma! Angalia simba darajani!”
Juma alikuwa mwindaji mashuhuri, akienda kuwinda pamoja na bwana wake huweza kuifanya kazi ikiwa bwana wake amechoka: akiwa peke yake huitumia gobore yake vyema.
Baada ya kelele za Juma kukawa kimya; kisha wakasikia mwanamke anawaita watoto wake na kuwakamata akijaribu kuwarudisha nyumbani na kuwaficha. Kwa mara ya pili sauti ya Juma ikasikiwa akitoa amri zake na huku watoto wakilia na kupiga kelele wakiwasikia wakubwa zao wakibabaika kwa woga wa simba. Milango ikafungwa; taa ya ‘Mitwa Maporini’ ikazimwa na kote kukawa kimya. kabisa, ji!
Baada ya dakika chache Juma akajitokeza darajani na gobore lake na wenzie waliobeba mikuki mikali kama wembe. Akasema “Yuko wapi huyo mtu aliyeniita?” Mlinda pahazi akamjibu “Yupo hapa. Tungoje.” Kisha yeye na Hassani wakapanda mtumbwini wakaenda kusini ya pwani. Humo mtumbwini Hassani akaanza kueleza hadithi, akasema, “Nilipambana na simba uso na macho hapo darajani, nikarukia majini na kuogelea mpaka jahazini na yule simba akaaendea huko.”
Juma akaitikia kwa makini, kisha akasema, “Vyema, hatuwezi kufanya jambo lolote sasa hivi, lakini kesho asubuhi lazima tufanye sako kubwa.”
Hassani akashuka mtumbwini akaenda nyumbani kwake hata dukani hakuenda usiku ule. Yule mtu wa jahazini akarudi na mtumbwi wake mpaká chomboni mwake, na kwa kutaka salama, akakisukuma chombo chake katikati ya mto, na akatupa nanga yake yenye kutu. Mabaharia wengine waliokuwako mjini waliweza kuivuta ile jahazi kama wangerudi lakini alidhani kwamba hawatarudi kwa kuogopa simba.
Kabla Juma na wenzie hawajafika nyumbani kwa ‘Mtawa Maporini’ wakasikia kelele zingine za kustusha zikitokea kitambo cha maili moja kusini. Juma akasema “Kelele hizi zinafikirisha kwamba simba yumo mashambulioni!” na mara Juma akawaongoza wenzie kule kule kwenye matata yale. Kabla hawajafika kule waendako wakasikia ngoma ya kujulisha kuwa simba amekamata mtu!
Walipofika katika kijiji kidogo karibu na mto Shera wakawakuta watu wameshika silaha zao, bunduki na mikuki. Mwanamke aliyekuwa ameshikwa na uchungu wa kulia hakuweza kusema neno. Hakuna alilokuwa akijua ila mumewe amekamatwa na simba.
Juma akamwuliza yule bibi, “Tuambie yaliyotokea, tunataka kukusaidia. Yule mnyama amekimbilia upande gani?”
Mwishowe yule bibi akakazana maana maneno ya yule Juma yalikuwa yakimwingia moyoni sana, na akawa anaanza kufahamu kuwa Juma alikusudia kumsaidia kweli. Akasema, “Sote tulikuwa tumekaa nje tukiongea nikamwona simba akitokea kizani akitujia. Kabla sijaweza kumwambia kuwa simba anakuja alikuwa amekwisharukiwa mgongoni na yule mnyama… Sikuweza kusema wala kupiga kelele; Nikakimbilia ndani ya nyumba… Sikujua wapi alikimbilia.”
Alipomaliza kusema maneno hayo kwa sauti ya kutetemeka, akaanza kulia machozi tena. Juma hakuweza kupata habari zaidi kutoka kwa yule bibi. Alipozungusha kichwa chake akakiona kitabu kimelala chini nje ya kibanda cha yule bibi; pia aliweza kusikia harufu ya mafuta ya taa. Mtu mmoja alimwambia kuwa yule mtu aliyekamatwa alikuwa akisoma pale nje na akitumia taa ya kandili, basi yule simba alipokuja kumshambulia, aliipiga chini na kuizima. Jina hilo la ‘Zima-Taa’ lilimstahili sana simba yule!
Juma akazisoma sura za wenziwe wote waliokuwa wakimzunguka na akasema, “Kila ajionae kuwa ni mwanamume asiogope kunisaidia kumtafuta yule mnyama. Tutaanza sasa hivi.”
Wale watu wote pamoja na silaha zao wakausaka msitu kwa saa mbili lakini hawakufanikiwa kumwona yule mnyama. Mwezi mchanga ulipokuwa ukizama chini ya msitu wale wawindaji wote wakashangaa mmoja wao aliponyoosha kidole chake mbele kwa hofu na huku akinong’ona, “Angalieni !”
Dudu moja kubwa jeusi lilikuwa likiwakabili, waliweza uona mgongo usiokuwa na nyele uking’ara kwa maji. Juma akasema taratibu, “Kiboko yule.” Yule mnyama aliposikia sauti ile akageuka na akakimbia mpaka ziwani. Hatimaye kiongozi akaona kuwa hakuna faida yoyote kuendelea kusaka usiku ule, kwa hiyo akawaruhusu wale watu warudi makwao na kufanya mashauri ya kukutana tena subuhi ya pili. Mwangaza wa jua ndio waliotumainia kutafutia nyayo za yule simba.
Juma aliamka alifajiri sana na alikuwa tayari nje akiwazungukia wenziwe na kuwaweka tayari kwa sako la simba. Aliona tabu kidogo kuwapata watu wale wale aliokuwa nao tangu kwanza; wengine walikuwa wamechoka kwa mwendo wa usiku uliopita na hawakuweza kuamka asubuhi mapema. Jamaa wengine walikuwa wamepata habari ya mshindo ule na wakatoka makwao mbali kuja pale kuungana na wenzao kumtafuta yule ‘nduli’ mla watu. Ndugu wa marehemu pia walikuwapo, mioyo yao imejaa ghadhabu nao pia walikuwamo katika sako hilo hilo. Kwa kuwa haikujulikana wapi ataweza kuonekana yule simba, Juma aliona heri ajitulize kidogo mpaka ipatikane habari safi ya yule simba ndipo ajiunge katika kundi mojapo.
Basi Juma akakaa kitako karibu ya moto akijishughulisha kujaza baruti nyingi katika gobore lake ili mshindo mmoja tu umwue simba au kiboko. Baadaye watu wengine wakajiunga naye kushindilia baruti zaidi ndani ya mago- bore yao na kuinoa mikuki yao, na wakaleta habari kuwa hakuna aliemwona simba.
Mchana akaja kijana mmoja mwenye habari nyingi, akasema, “Nimeuona mwili wa Mtungute, ulikuwa kitaruni. Nilikwenda huko kukata kuni nikaona matambara meupe yametanda. Nilipokaribia nikaona kichwa chake na vipande vipande vya kanzu yake…” Juma akamwuliza, “Je uliona upande uliokwendea nyayo,” “ndio” akajibu, “Nilizifuata nyayo zake mpaka nikakuta mabaki ya mwili wake… nikawaita ndugu zake wakakusanya mabaki ya maiti wakenda kuzika.” “Kwa hiyo haina maana kumtafuta yule mnyama mahali pale” Juma akasema. “Madhali maiti yameondolewa, simba yule atakwenda kumtafuta mtu mwingine amle.”
Kutwa nzima ikapita bila ya kupatikana habari yoyote zaidi, na jioni majirani walijikusanya barazani kwa Juma kama ilivyo kawaida yao, na kama kawaida ya watu wengine, walikuwa hawana jambo la kulizungumza ila lile la simba mla watu. Kiza kilipokuwa kikubwa, wote wakajimwaga wakaenda zao majumbani mwao; pia kazi ya kulinda viboko ilibidi ifanywe, maana wangeiacha, viboko wangeliviharibu vyakula vyao vyote mashambani.
Juma aliwasindikiza watu wale kwa kiasi cha maili hivi; kisha alipokumbuka kuwa hakuchukua silaha yoyote alirudi nyuma. Kiasi ya hatua mia baada ya kuachana na wale jamaa, akakutana na mtoto aliyetumwa na mkewe mwenye busara kumpelekea bunduki yake, pembe ya baruti na mfuko wa risasi. Yule mwanamke mwema kila mara alikuwa akimuasa asitembee usiku bila ya silaha katika nchi ile yenye wanyama wabaya.
Jamaa Wakirufiji ni watu wasiogopa hata kidogo wanyama wakali. Mambo yaliendelea kama kawaida tu mle mjini, kama kwamba hakukutokea jambo lolote la kustusha. Usiku ule hakukuwapo jambo lolote. Mbwa walilia huko na huko, na katika vibanda vilivyokuwa mbali kidogo, wanawake walikuwa wakiimba nyimbo zao kwa huzuni sana. Walikuwa wakitumaini kumsikia simba mla watu saa zozote.
Juma alipokwisha ipokea ile bunduki yake kwa yule mtoto, akamwambia arudi nyumbani akamwambie mkewe kuwa yungali na hamu ya kuwinda. Makelele ya madebe yalimjulisha Juma kuwa walinda viboko wamo kazini.
Hapo hapo akakutana na dudu moja kubwa likitokea kwenye Ziwa Shera, akishughulika kung’oa mipunga. Alipotambaa mpaka karibu Juma akawa tayari kumpiga na mara debe likapigwa na yule mnyama akaporomokea ziwani. Bahati ya Juma ikapotea!
Alipokwenda kwenye dungu alilokuwa akikaa mwinda viboko aliyepiga lile debe, wakaanza kuzungumza na wakala ndizi za kuchemsha. Kisha akateremka dunguni akaenda upande mwingine wa ziwa ambako alifikiri kuwa ataweza kupata viboko wengine. Hapo pote palikuwa hakuna miti mingine ila mikoche tu. Mwezi ulikuwa uking’ara zaidi kuliko usiku uliopita na kulikuwa na vivuli vya kuogopesha sana chini ya mikoche hata ilimbidi aende kwa uangalifu sana.
Wakati huo Juma alikuwa amekaza macho kwenye kitu kilichokuwa kikitembea polepole mbele yake. Kilikuwa si kiboko alikuwa na hakika kabisa lakini kwa mwangaza wa baramwezi hakuweza kusema kilikuwa ni nini kabla hakijajipoteza. Juma akasimama kimya kwa dakika chache akisikiliza sana lakini hakuweza kusikia sauti yoyote. Alipokaribia kuondoka kwenda zake kusikia sauti kitu kile kile kikaanza kutembea tena na kujijulisha mbele yake, karibu hatua thelathini. Upepo ulikuwa ukivuma polepole ukijia alikokuwa yeye.
Kabla hajaanza kutembeatembea, Juma akavumbua kuwa kile kitu kikubwa kilichokuwa kikitembea polepole kilikuwa simba mkubwa. Alipokuwa bado akimwangalia, yule simba akajinyoosha kama paka aliyetoka usingizini; kisha akaunguruma mlio wake wa hatari. Juma aliposikia mngurumo ule akajua jinsi jamaa walio vibandani wakijitahidi kufunga milango yao, na wasafiri wakiomba Mungu wafike mwisho wa safari zao salama waone jua siku ya pili.
Alipohakikisha kuwa gobore lake limeshindiliwa sawa sawa akazidi kumchungua yule mnyama. Mara yule simba akageukia upande aliokuwako Juma, naye akailinga bunduki polepole. Ingawa alikuwa mwindaji wa siku nyingi lakini hofu ilimwingia na ikampata taabu kidoko kuiweka sawa bunduki yake. Bwana wake alikuwa akimwambia kuwa hao wasiopata kujua hofu ni walevi au wapumbavu; ingawa alikuwa amejawa hofu moyoni mwake alijaribu kujikaza ili asiharibu kazi yake ya kumwua yule mnyama mkali aliyemkalia mbele yake.
Na bunduki yake mkononi, Juma alisimama kama sanamu ya askari iliyoko Dar es Salaam ya ukumbusho wa vita, yule simba alikuja mpaka hatua chache tu kutoka alikokuwa Juma na mara akapata harufu yake akasimama. Juma tena hakungojea kitu, aliifyatua tu, ukatokea mshindo wa ajabu na ulimi mrefu wa moto ukatoka kwenya mdomo wa bunduki. Harufu ya baruti ikajaa pote na kumpalia Juma; moshi ukajaa na kumziba kabisa.
Juma akanyamaa kimya akingoja. Kama asingemwua yule mnyama au angemjeruhi kidogo angekufa yeye; yule simba asingempa nafasi ya kushindilia tena bunduki yake. Lakini risasi ilimwingia simba barabara hata hakuweza kusogea, akalala kama mtu aliyechoka kwa mwendo. Huku akimshukuru Mungu kwa kumsalimisha, Juma akauegemea mkoche akishindilia bunduki yake tena; kisha akasogea majanini kwa uangalifu sana.
Hapo simba kubwa limelala maiti! Kwa hatua fupi alizokuwa yule simba, ile risasi ya Juma ilimwingia sawa sawa. Lakini yote yale Juma aliona bure, maana kama alivyoona yeye, simba yule aliemwua hakuwa ‘Zima-Taa’.
Akajua kwamba madhali yule amekufa mwenzie atataka kulipa kisasi kwa kuuliwa rafiki yake, Juma hakupoteza wakati, akajirudia nyumbani. Nusu ya njia akasita kidogo, akasikiliza kwa makini. Mbali sana ikatokeza sauti ya ngoma hafifu lakini wazi, ikimwambia kuwa huko maporini mtu ameliwa na simba katika kijiji cha Mbwara!
Juma akasema, “Maisha ni jambo la ajabu sana, huku simba ameuawa na mtu; na huko mtu ameuawa na simba.”
Saa mbili asubuhi habari zikafika Mohoro kuwa simba mkubwa aliyejulikana kuwa ndiye yule yule ‘nduli’ mla watu, alishambulia kundi la watu waliokuwa wamekaa karibu ya moto pembeni ya njia huko Mbwara, wakipumzika walipokuwa wakitoka Kilwa kwenda Mohoro. Mtu mmoja alikamatwa na ingawa yule simba alifukuzwa na watu ili amwachie mwenzao alizidi kwenda naye.
Kwa njia hii, kwa miezi mingi, simba yule alikuwa akikamata watu, alikuwa akitembea bila ya woga Rufiji nzima. Askari wa nyama waliletwa katika vijiji vyote walikuwa wawindaji hodari waliozoea sana kazi hiyo na waerevu sana kwa kutega simba. Mitego ya simba ilikuwa ikirushwa ovyo na simba huyo hata ilikuwa haiwezi kumkamata. Kwa ubaya wake hakuogopa taa wala moto, alikuwa akiwakamata watu popote alipopenda na mtu yoyote amtakae.
Kila baada ya siku chache habari mpya za ubaya wa huyo simba ziliwasili Mohoro. Safari moja, mtu mmoja aliacha duka lake wazi kwa upumbavu wake na taa ikiwaka; simba aliruka mpaka ndani akamata mtu mwingine. Mwanamke mmoja aliyekuwa akimkogesha mwanawe kibandani mwake alinyakuliwa na simba. Vifo viwili havikupata kutokea mahali pamoja hata mara moja: ‘Zima-Taa` alikuwa simba mtembezi sana.
Askari nyama walizidi kumiminika, na mitego ikazidi kutegwa lakini ‘nduli’ mla watu aliendelea kufanya kazi yake kwa kitisho sana; uhodari wake wa kujua tabia za binadamu ulimsaidia kuepukana na vifo vingi. Woga ulizidi kutangaa kote kijijini na usiku watu walijifungia mnamo vibanda vyao vyenye kiza.
Jioni moja ngoma ya sherehe ilichezwa karibu maili mia kutoka Mohoro katika kijiji cha Kwangasi. Ilikuwa ngoma ya kusherehekea harusi ya kijana mmoja, wanaume na wanawake waliuzunguka moto na huku wakicheza ngoma. Ghafla, simba mkubwa akaruka mpaka katikati ya wacheza ngoma. Bila ya kuogopa moto, yule simba akamvamia mtu mmoja ambapo wengine walitawanyika ovyo kwa woga.
Mwishowe yule ‘Nduli’ akamkamata mwanamke mmoja aliyekuwa akipigia kelele sana na akaruka naye kizani. Wale waliomwona akichukuliwa walipiga kelele kama walivyoweza, wakijaribu kuwaita wenzao kusaidia kumwokoa yule mwanamke. Wabantu ni watu wenye moyo mgumu sana na shime nyingi; kila mwanamke au mwanamume aliyekuwako alikamata kijinga cha moto na kwanza kumfuata yule simba. Hata wapiga ngoma walikwenda na huku wakipiga ngoma zao.
Lile kundi halikufika mbali kabla hawajasikia mshindo wa bunduki. Wakaharakia mbele wakitazamia kumkuta aliyemuona yule simba. Lakini bila ya kutazamia wakamkuta yule simba na yule mwanamke wamelala wakivuja damu maiti. Uzi uliotegwa na askari nyama ulifyatua risasi kwa shabaha njema, na hapo yule mnyama na mwanamke wakauawa!
‘Zima-Taa’ alikuwa na urefu wa futi kumi; jino moja kubwa lilivunjika, jicho moja limetoka, na mwili umejaa makovu.
Baada ya hapo uuaji wa simba ukamalizika; ‘Zima-Taa’ aliyekuwa akiogopwa hawezi kuitisha Rufiji tena.
Hii hadithi ipo ndani ya kitabu Masimulizi ya Mtawa Maporini kitabu cha 4. Unaweza kisoma chote ndani ya Maktaba
16. ZIMA-TAA
Katika mwaka 1943 kwa muda wa mwezi mmoja tu, simba mla watu ambaye hadithi yake itaelezwa mbele aliuwa watu arubaini na saba (wanaume, wanawake na watoto) katika nchi ya Rufiji na akajeruhi kumi na saba.Mnyama huyo aliwashambulia watu bila ya kusitasita kokote alikokutana nao; mioto na taa ambazo kila mara huwatisha wanyama ndizo zilizomfanyisha ajue mahali walipo binadamu. Mara wenyeji wakaona bora wafunike taa zao na mioto waizime kila wakishamaliza kazi zao. Mambo yalileta taabu kubwa, wakaanzisha ‘Zima-Taa’ yao ya kienyeji, na hapo yule mnyama akapewa jina la ‘Zima- Taa’.