RIWAYA; DUKA LA ROHO
SEHEMU YA KUMI NA TATU
"Usijali. Tayari nimekwishawaambia mbwa wako mwanao alipo. Wapo njiani wanaelekea huko." Gunner akaongea na wakati huo mvua ya manyunyu ilikuwa imeanza kushika namba eneo hilo. "Zimebaki dakika kumi za Lobo kichukua roho yako. Umefanya maamuzi sahihi sana kwa kununua roho ya Martina." Lobo akazidi kutiririka.
"Fanyeni haraka. Sina muda wa kukaa na hii roho, ni yenu." Lisa akafoka tena.
"Hapana mke wangu, sheria zinasema masaa ishirini na nne. Bado dakika saba tu, utakuwa kuzimu. Lobo yumo mle, anasubiri kazi yake." Gunner alipoonesha sehemu Lobo alipo, taa za gari zikawashwa mara moja na kuzimwa.
"Mi' si mke wako pia." Lisa aliongea kwa kujiamini mbele ya Gunner ambaye alimpiga kofi zito lililompeleka Lisa chini ya rami. Mara baada ya kofi hilo, akaanza kumpiga mateke mazito binti yule kana kwamba hamjui.
"Mjinga wewe. Nitakuua mimi." Gunner aliongea kwa hasira huku akimtemea maji ya mvua Lisa. Radi nazo zilikuwa zinawaka huku na huko na kuonesha vazi la suti nyeusi aliyovaa Gunner. "Muda wa Lobo umewadia, kwa heri Lisa." Gunner alimuaga mkewe na kwenda kwenye gari alilopo Lobo. Wakati anaingia, John Lobo akawa anatoka upande mwingine.
Koti lake jeusi na refu linalochagizwa na kung'aa kama la majambazi, lilimfanya kumchora Lobo kama katili la hatari sana. Kila radi zilivyocharaza anga, uso wa Lobo ulionekana na mkononi kwake akiwa kakamata bastola iliyofungwa kiwambo cha sauti.
"Muda wa kufa Lisa. Imebaki dakika moja." Alipoongea hayo, radi ikapiga tena na uso wake mweupe kiasi huku kichwani akiwa hana nywele, zikamfanya Lisa aamini kuwa muda wake kweli umeisha.
Akanyanyuka pale alipokuwa kalala baada ya kupigwa na Gunner, akapiga magoti tayari kwa kukipokea kifo chake.
"Kumi, Tisa, Nane, Saba, Sita, Tano ......" Lobo akawa anahesabu sekunde ambazo zilikuwa zimebaki. Lisa akafumba macho yake baada ya sekunde kufikia nne.
Akiwa kajiandaa kufa mtoto wa kike, na wakati huo kifyatulio cha risasi kikiwa tayari kufyatuliwa na Lobo, muujiza wa ajabu ukatokea. Hakika ulikuwa muujiza wa aina yake.
Lobo akiwa anaanza kufyatua kifyatulio cha bastola yake, mara mkono wake wa kushoto ukachomwa na vitu kama nyota zenye ncha kali. Maumivu aliyoyapata dakika hiyo, yalikuwa hayaelezeki. Akiwa katika hali hiyo akajikuta akidondosha bastola yake na kuanza kutazama ni wapi vitu vile vimetokea. Wakati anatazama huku na huko, radi ikapiga na hapo akaona kitu mfano wa mtu aliyevaa nguo nyeusi anakuja kwa kasi ya popo mbele yake. Nasema ni mfano wa mtu kwa sababu kilikuwa kina kasi ambayo mtu wa kawaida hana hata kidogo lakini umbile hilo la mtu lilikuwa limetunukiwa kasi hiyo.
Kuja kutahamaki, kitu hicho kikampiga mateke mawili mazito John Lobo. La kwanza lilimkuta kifuani, kitu hicho kikiwa bado kipo angani, kikammalizia teke la pili la hatari shingoni. Lobo akapaishwa hadi kwenye boneti ya gari walilokuja nalo.
Radi nyingine ikapiga, hapo kile kitu kikaonekana kimesimama wima kwa mtindo wa kupigana. Lobo akagonga boneti la gari ile, na Gunner akawasha taa. Sasa alionekana mtu ambaye kafunikwa sura lakini kavaa suti ya gharama.
Kwa kasi, Lobo akashuka toka kwenye boneti na kumfuata yule mtu asiye na sura na kuanza kupambana naye wakati huo Lisa maswali kibao yaliendelea kutiririka katika kichwa chake asijue kile ni kitu gani au ni mtu gani na kaja sehemu ile kufanya nini.
Lobo akarusha teke, lakini cha kushangaza mtu yule alilidaka teke hilo kwa mguu wake wa kushoto na kulibana nyuma ya goti. Lobo akawa hana ujanja wa kutumia miguu yake. Akaanza kurusha ngumi ambapo yule mtu asiye na sura alikuwa akizitoa nje bila hata kurusha zake.
Ngumi ambayo Lobo aliivuta kwa nguvu zake zote, mtu yule aliidaka na sasa akawa kakamata mkono na mguu wa Lobo. Lobo akawa kakamatika hana la kufanya. Mara yule mtu alirudisha kichwa chake nyuma na kukipeleka mbele kwa kasi, kikatua kwenye pua ya Lobo. Damu zikamchuruzika Lobo lakini hakuenda popote kwa sababu alikuwa kabanwa ipasavyo na mtu yule.
Wakati damu zinaendelea kumtoka, Lobo akajikuta akipokea kichwa kingine palepale alipopigwa mwanzo. Maumivu yaliyompata, hakusita kupiga kelele na nadhani angesimulia hadi kwa wajukuu zake.
Hapo yule mtu alimuachia mkono na kisha akaanza kutandaza ngumi zisizo na idadi kwenye kifua cha Lobo. Ngumi ya mwisho ilitua tena kwenye pua, na hapohapo mtu yule akamuachia Lobo mguu wake na kuruka teke zito la kuzunguka. Lobo akapaa juu na kisha akatua chini kama mzigo akiwa kachafuka kwa damu na hali yake ikiwa wazi ni mbaya.
Yule bwana akawa bado kasimama palepale akiwa kakunja ngumi na sura yake iliyofungwa na sijui nini, ikiwa imeinama kwa kusubiri jambo lingine.
Mvua sasa ilikuwa hainyeshi tena bali kubaki miungurumo ya hapa na pale. Gunner akafungua mlango wa gari yake na kwa madaha akachomoka toka mle ndani na kisha akaenda kwa Lobo na kumuingiza ndani ya gari.
"Safi sana. Yaonekana una uwezo mkubwa wa kupigana. Haijalishi, lakini sasa unapambana na mzimu." Gunner aliongea na muda huohuo akachomoka kwa kasi na alipofika mbele ya yule mtu, alisimama ghafla na kuanza kurusha ngumi nyingi zisizo na idadi. Zilikuwa zinarushwa kuelekea kichwani, kifuani na kila mahali ambapo Gunner aliona patamsaidia kumnyamazisha mpinzani wake aliyekuwa anakazi ya kuzitoa na kuzikwepa.
Kuna ngumi moja ya hatari Gunner aliirusha na jamaa yule aliikwepa kwa kuinama kidogo, lakini kwa bahati mbaya alipoinama, Gunner akaachia ngumi ya mkono mwingine ambayo ilimkuta jamaa yule kidevuni na kumrusha hadi alipo Lisa. Alipotua chini, tayari Gunner alikwishafika, akamkalia kwa juu na kuanza kumtwanga ngumi za usoni.
Ilikuwa ni 'kimuhemuhe' au patashika kwa shimo kuchimbika. Mtu yule ambaye alikuwa kazibwa na mask, ni wazi alikuwa taabani hasa pale mwanaume wa shoka Gunner aliposhika ile mask iliyoungana na suti yake na kutaka kuiondoa.
Alipoishika, ndipo alipogundua inaseli za umeme ambazo ni hadi ubonyeze kitu fulani ndizo nazo zijifungue. Gunner akajaribu kuzamisha vidole vyake kwenye ile mask kwa kutaka kuirarua lakini kwa bahati mbaya alipokea pigo hafifu toka kwa Lisa lililopigwa kwa teke baada ya Lisa kuona mtu anayemsaidia kuzidiwa maarifa. Ni pigo hafifu kwa sababu si lile ambalo ungepigwa nalo na Lisa wakati yu mzima.
Gunner akajikuta akimuachia yule mtu na kumfuata Lisa ambaye alikuwa kasimama pembeni kidogo na pale. Kwa hasira nyingi, Gunner alimpiga kofi zito Lisa na lile kofi yule mtu aliyechini aliliona na likamshtua vilivyo. Mwanamke kupigwa kama mwanaume, yule mtu alistaajabu ya Filauni sasa baada ya kuyashuhudia ya Mussa.
Gunner hakuishia kwenye kofi pekee, Lisa alipoyumba baada ya kofi lile, Gunner akaruka teke la kutanguliza mguu mbele na likakita nyuma ya kiuno cha Lisa. Lisa masikini ya MUNGU akadondoka chini na kugaa gaa kwa maumivu.
Gunner akazidi kuonesha ukatili wake dhidi ya wanawake. Na hakika alikuwa katili. Mateke mazito kwenda tumboni, kifuani na saa nyingine kumkanyaga Lisa kichwani kama mwenye kuua nyoka kwa kumkanyaga na kiatu, usingeweza kusema huyu jamaa ana roho ya utu hata kidogo.
"Heeeey." Sauti kali ilisikika nyuma ya Gunner aliyekuwa anamsulubu Lisa. Akiwa anapumua haraka, Gunner akageuka nyuma kumuangalia anayemuita huku bado mguu wake upo juu ya mwili wa Lisa.
Akamtazama Lisa aliyekuwa anagaragara kwa maumivu, kisha Gunner akampiga teke dogo kama anatoa pasi ya mpira. Akamuacha na taratibu akaanza kwenda alipo yule mtu aliyekuwa kasimama na kuweka mguu mmoja mbele kama wafanyavyo wacheza mapigano ya miguu na mikono (karate).
"Hivyo ndivyo mama yako alivyokufundisha kucheza na mwanamke?" Yule bwana kwa mara ya kwanza aliongea baada ya kufoka.
"Oooh! Mama? Namchukia mama yangu kwa sababu alinitelekeza nilipozaliwa tu. Nampenda sana baba." Gunner alijibu huku akivaa vizuri groves zake nyeusi.
"Kwa hiyo baba yako ndio kakufundisha kuwapiga wanawake? Eti we' tasa." Yule jamaa aliongea maneno ya kukarahisha na Gunner yakamuuma.
"Usiniite hivyo."
"Tayari nimekwisha kuita sasa." Jamaa yule safari hii alikuwa anaongea huku akizunguka kwa hatua ndogondogo akimtazama Gunner kwa makini. "We' ni mgumba tu, hahahaaa." Jamaa akacheka kwa dharau.
"Mmmh! Yaonekana mswahili sana kijana. Lakini mbona hauvui hicho kiuchafu kichwani? Unaogopa nini?" Gunner aliuliza na wakati huo Lobo alikuwa ndani ya gari akifatilia ule mpambano kwa makini japo alikuwa katika maumivu makali ya kuvunjwa mfupa wa pua.
"Ooooh! Nimesahau kuwa ulikuwa unataka kuvua hii sura. Usijali Mgumba, ngoja nitimize." Jamaa yule aliongea na kufunua koti lake la suti sehemu ya mkononi, akaanza kuiobonyeza saa yake na sekunde kadhaa, ile mask ikaanza kutoa sauti za shoti ya umeme na baadaye ikapotea kabisa na kubaki sura ya yule bwana akiwa katika suti mwanana na ya kumpendeza pia.
Ni yuleyule Pirlo wa Italia na Hyung wa China, ndiye sasa alioneokana vema kwenye uso wa Gunner aliyebaki katabasamu tu bila kusema chochote.
"A coward's back. (Muoga karudi)" Gunner aliongea huku bado katabasamu.
"Karudi kuangamiza zao la wagumba na matasa." Pirlo au Hyung akajibu.
"Huwezi kunisimamisha Man'Sai, tayari nina kila kitu." Gunner akaongea akilitaja jina la Man'Sai ambalo ni jina alilojipa Frank Masai. Lisa kusikia jina hilo, akajikuta akipata hata nguvu na kutazama kule Frank Masai alipo.
Tabasamu la shida likamtoka mwanamke yule alipothibitisha sura ya Frank Masai.
"Oooh! Kumbe wanijua eeh. Sasa ndio nimerudi hivyo. Naanza na SGT kisha namalizia na Jet P112. Zote naziharibu." Frank aliongea kwa utulivu na sasa alikuwa kasimama akimuangalia adui yake.
"Hahahaaa. Wameshindwa makundi kama FBI, we bwege utaweza." Gunner akaongea kwa dharau.
"Hizo ni akili za Wagumba wengi wa dunia hii. Wanadhani kufanya kazi katika makundi ndio kufanikiwa. Njia ya kufanikiwa ni kuwa peke yako na kufanya kila kitu peke yako. Sihitaji msaada kutimiza nilichokitaka. Msaada wangu ni MUNGU tu." Masai aliongea kwa utulivu na Gunner akacheka tena.
"Okay Man'Sai. Lisa huyo hapo, nimekulindia sana. Ni mtamu mnooo, hahahaaa." Gunner akajidai anatoa maneno ya kejeli.
"Hahahaa. Usemayo ni ya kweli, ila unapewa utamu unashindwa kuleta matunda ya utamu huo. Mwanaume suruali wewe. Hahahaaa." Masai akakejeli naye jambo lililomfanya Gunner apandwe na hasira na kujikuta akikimbia kwa haraka kwenda kwa Masai ambaye safari hii alimuonesha huyu bwana kwa nini anatafutwa kwa udi na uvumba kwenye hii dunia na hapatikani.
Gunner akiwa katika kasi hiyo, akamfikia Frank Masai na kuanza kurusha ngumi nzito kama kawaida yake, lakini ubaya alimkuta hata Masai akiwa katika hasira za kumuona akimpiga Lisa kama mwanaume mwenzake.
Ngumi nyingi alizorusha Gunner, Masai alizipangua na yeye akawa anarusha zake kwa chati, yaani kwa kumendea. Gunner akajichanganya kidogo kwenye kurusha ngumi hizo, Masai akapangua na kutupa yake ambayo ilimkuta jamaa kwenye pua. Gunner akashika pua yake na kujisahau kuwa yupo mpambanoni. Frank akatupa ngumi nyingine ambayo hiyo ikatua kwenye shavu la kushoto na kumfanya Gunner aegemee upande wa kulia. Kosa kubwa kwa Gunner kwani wakati anaegemea upande huo, tayari Man'Sai alikuwa katupa ngumi nyingine nzito zaidi na kupiga shavu la kulia ambapo alikuwa anaegemea Gunner.
Damu kiasi zikamtoka Gunner lakini haikumaanisha ndio mpambano umeisha. Man'Sai akaruka teke zito lililompeleka Gunner hadi kwenye gari la Lisa.
Frank akiwa katika ubora wake wa kwenye riwaya ya Jina na Ukurasa wa Hamsini, akamuonesha Gunner kuwa yeye si wale aliowategemea katika maisha yake, bali yeye ni yule ambaye hakupaswa hata kumuota ujio wake.
Gunner alisikia sauti ya maji na sauti kama ya karatasi inayopepea ikija nyuma yake. Alipogeuka, kwa msaada wa taa za gari alizoziwasha wakati Lobo anasulubishwa, aliona viatu vya gharama alivyovaa Frank vikichapua katikati ya maji ya mvua iliyokata muda mchache uliopita. Maji hayo kila Frank alipotua mguu wake huku akikimbia, basi yaliruka kwa pembeni kuonesha kuwa zile mbio zilikuwa ni nzito. Sauti kama karatasi inayopepea, ilikuwa ni suti mwanana aliyotinga Man'Sai, ilikuwa inatoa sauti hiyo wakati anakimbia kwa hatua ndogondogo kumfuata Gunner aliyekaribu na gari la Lisa.
ITAENDELEA