Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema Ofisi ya Mkoa kwa kushirikiana na TANESCO haitabaki kimya kufuatia kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Padri Charles Kitima, kuhusu tukio la uvamizi alilodai lilihusisha kuzimwa kwa umeme na Shirika hilo.
Akizungumza leo Desemba 5, 2025 katika Hafla ya Uzinduzi wa Mita Janja za Umeme kwa Wateja wa TANESCO katika Ukumbi wa JNICC, RC Chalamila amesema kauli hizo ni nzito na zinahitaji kuchunguzwa kwa kina.
Chalamila amesema alimsikia Padri Kitima akieleza kuwa siku aliyovamiwa kulikuwa na “conspiracy” (mpango) kati ya wavamizi na TANESCO, na kwamba Shirika lilizima umeme ili wahalifu waweze kumdhuru haraka.
Chalamila amesema amezungumza na Mkurugenzi wa TANESCO, Lazaro Twange, na kukubaliana kuwa kauli kama hizo zinapaswa kufanyiwa kazi ipasavyo kwa kuwa zinagusa taswira ya Shirika.
“Kauli kama hizo ni ngumu sana ambazo tunapaswa kuanza kuzifanyia kazi vizuri sana. Tumeawaambia wanasheria wafanye kazi yao bila kubaki kimya,” amesema RC Chalamila.
Amesema TANESCO anayoifahamu haiwezi kuhusika katika tukio lolote la kuzima umeme kwa lengo la kumdhuru raia, hivyo ni muhimu kupata maelezo ya ziada kutoka kwa Padri Kitima ili taswira ya Shirika hilo iendelee kuwa njema.
“Ukikuta kuna hayo maneno ndani ya mkoa unaouongoza, there is something to do (kuna la kufanya). Lazima kama Mkoa na Wanasheria tukae pamoja tumuulize vizuri ndugu yetu Padri Kitima, labda ana maelezo ya ziada,” amesema.
Ikumbukwe, Desemba 1, 2025 TANESCO ilikanusha vikali taarifa kuhusiana na Mahojiano ya Padri Kitima, ambapo Shirika hilo lilihusishwa na matukio ya kihalifu.
TANESCO ilieleza kuwa kukatika kwa umeme mara nyingi husababishwa na sababu za kiufundi kama hitilafu za dharura au matengenezo yaliyopangwa, na kwamba mambo hayo hayana uhusiano wowote na vitendo vya uhalifu.