BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,376
- 8,118
Siku chache tangu aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Simai Mohammed Saidi kujiuzulu nafasi hiyo leo, Jumamosi Januari 27.2024 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefanya mabadiliko ya Baraza la Mapinduzi kwa kuteua Mawaziri wapya wawili (2) na kumbadilisha Wizara Waziri mmoja (1), pia ameteua Naibu Mawaziri wapya wawili (2) na kumbadilisha Wizara Naibu Waziri mmoja (1)
Taarifa iliyotolewa Ikulu Zanzibar ambayo imesainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi SMZ Mhandisi Zena Ahmad Saidi imeeleza kuwa Rais Mwinyi amemteua Mudriky Ramadhan Soraga kuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya kale ambapo kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, wakati Ali Suleiman Ameir (Mrembo) akiteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Ikulu ambapo kabla ya hapo alikuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango
Aidha, Shaaban Ali Othman ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi akitokea kuwa Naibu Waziri wa Nishati, Maji na Madini, naye Juma Makungu Juma aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi sasa anakuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango
Mwakilishi wa Viti maalum kutoka kundi la Vijana Kusini Unguja Salha Mohammed Mwinjuma ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, wakati Mwakilishi wa Jimbo la Konde, mkoa wa Kaskazini Pemba Zawadi Amour Nassor yeye anakuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini,
Taarifa hiyo imeeleza kuwa wateule hao wataapishwa kwa Tarehe itakayotangazwa hapo baadaye