Safari za Kikwete nje utata mtupu
Lula wa Ndali-Mwananzela Oktoba 1, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
Tukiweka utani wote pembeni, kejeli zote pembeni, na dhihaka zote pembeni, bado tunakabiliwa na swali moja muhimu: Ni kwanini Rais Jakaya Kikwete hawezi kukaa Dar kwa angalau wiki tatu mfululizo bila kwenda nje ya nchi?
Hivi ni kweli kuwa bila Rais Kikwete kwenda safari za nje ya nchi Taifa haliwezi kuendelea na bila ya yeye mwenyewe kufunga safari hizo, basi, misaada ya kigeni na uwekezaji hautafanyika nchini kama alivyoashiria Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, mapema mwaka huu?
Ninatatizwa, ninakerwa na niseme wazi kuwa baadhi ya ziara hizi haziingii akilini, na kwa hakika zinanifanya nianze kuhisi ninaishi katika ulimwengu wa kufikirika ambamo mambo yote yanawezekana.
Jibu jepesi ambalo limekuwa likitolewa mara kwa mara kubariki ziara hizi ni kuwa Rais Kikwete analazimika kwenda nje kwa sababu kwa kufanya hivyo anakutana na viongozi mbalimbali, anapokea misaada na pia analitangaza jina la nchi yetu. Na wengine wamefikia mahali pa kutaka wananchi waamini kuwa bila ya Rais Kikwete kufanya ziara hizo, basi, Tanzania haitakumbukwa katika medani za kimataifa.
Kwa wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka kuwa mwanzoni ilisemwa kuwa alikuwa anakwenda huko "majuu" kujitambulisha kuwa yeye sasa ndiye "Rais wa Tanzania" kana kwamba habari ya kuchaguliwa kwake ilikuwa siri.
Hebu tuangalie kama hoja zetu hizi ni za sisi waandishi tu au hata watu wengine wameanza kuziona? Taarifa ya ripoti ya Economic Intelligence ya Agosti mwaka huu inasema hivi kuhusu tathmini yake ya hali ya siasa za ndani "Rais Kikwete bado anatumia muda mrefu akisafiri nje ya nchi".
Kauli hiyo imetoka kwenye taasisi ya Economic Intelligence Unit ambayo iko chini ya Jarida maarufu la "The Economist". Ripoti yao hiyo inaelezea ni kwanini basi suala la Rais kuwa nje ya nchi mara kwa mara lina athari za aina fulani katika utendaji wa Serikali na ni kwanini sisi wengine tunahoji ulazima huu wa Rais Kikwete kuikimbia Dar es Salaam kila anapopata nafasi.
Jarida linasema hivi "baada ya Kikwete kukusanya madaraka makubwa kwake na kwa wasaidizi wake, basi, uwezo wa Serikali kufanya maamuzi muhimu wakati yeye hayupo unakuwa na kikomo".
Kwa maneno mengine ni kuwa kwa kadri Rais Kikwete anavyokuwa safarini nje ya nchi ndivyo hivyo hivyo baadhi ya maamuzi, hatua au maelekezo muhimu hayafanyiki hadi arudi.
Hapa tunaweza kupata mwanga kidogo wa kwa nini anapenda kusafiri nje ya nchi. Ni kwa sababu anakwepa kufanya maamuzi au hatua fulani yeye mwenyewe.
Kwa kadri Kikwete anavyokuwa nje ya nchi ndivyo vivyo hivyo maamuzi kadhaa yanaahirishwa kwa kisingizio cha "mpaka Rais arudi". Matokeo yake ni kuwa akirudi anakaa wiki chache halafu huyo anapaa tena!
Unaweza kuniuliza ni maamuzi gani hayo? Mengi tayari tunayafahamu, kuna suala la kufunguliwa mashtaka kwa baadhi ya viongozi wa juu wakati kesi dhidi yao ziko tayari na kinachosubiriwa (msiniulize ni kwanini) ni "go ahead".
Kuna suala la muafaka wa Zanzibar ambalo bila yeye kuingilia kati hilo haliendi; kuna masuala ya Dowans/Richmond, kuna suala la Rada, kuna masuala mengi tu ambayo tayari yanajulikana.
Kwa mujibu wa jarida hilo hilo inaonekana kuwa safari za Kikwete nje ya nje zinagusa masuala muhimu ya kiuchumi ya Taifa. Jarida hilo linazungumzia jinsi gani uamuzi wa Rais Kikwete kutuma vikosi vyetu kule Comoro vimempandisha chati kimataifa lakini wakati huo huo kusababisha madai kuwa kutokana na nafasi yake kama Mwenyekiti wa AU Rais Kikwete anaweka maslahi ya chati yake ya kimataifa mbele kuliko matatizo ya ndani ya Tanzania.
Hili linaweza kuwa na ukweli tukizingatia kuwa mara tatu sasa Rais Kikwete amefunga safari kwenda Kenya, Zimbabwe, na Sudan katika kujaribu kutatua migogoro ya nchi hizo. Wakati huo ameweza kukutana na viongozi waliogongana wa Kenya na wale wa Zimbabwe. Cha kushangaza hata hivyo ni kuwa hadi hivi sasa hajakutana na kusimamia mazungumzo ya Muafaka wa Zanzibar, hajatuma ujumbe wa nguvu kusuluhisha mapigano kule Tarime (isipokuwa kundi kubwa la waomba kura wa CCM wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Pius Msekwa).
Kwa wale ambao tulipata nafasi ya kuisikiliza na kuisoma hotuba ya Rais Kikwete kwenye Umoja wa Mataifa, hotuba iliyochukua karibu dakika ishirini hivi, ilituacha tujiulize kama alikuwa anazungumza kama Mwenyekiti wa AU au Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tukiachana na hayo hatuna budi kujiuliza swali jingine; Je, ziara zake hizi zinaendena na hali ya kiuchumi na vipaumbele vya Taifa letu? Ninaamini kuwa endapo tutapata mchanganuo wa gharama za ziara hizi tunaweza kupigwa na mshangao. Licha ya kutokuwa na hesabu mkononi ninaamini tunatumia fedha nyingi kweli kugharimia ziara hizi.
Hebu fikiria msafara wa Rais kwenda New York na Washington DC ukitanguliwa na safari ya mke wake ambaye yuko kimatibabu huko. Yeye Rais tu anaposafiri anakuja "standard". Wasaidizi, walinzi, watendaji wa Serikali (mawaziri), na wadandiaji wengine (wakiwemo wabunge na wanafamilia yake).
Hivi karibuni aliposafiri vyanzo vya uhakika vinasema kuwa alikwenda na mwanae aliyetoka kufunga ndoa hivi karibuni (sijui kama Serikali ilimlipia fungate hilo au zilitoka mifukoni mwa familia ya Rais).
Ukijumlisha watu wote hao walioambatana na Rais, gharama ya kuwaleta na kuwaweka Marekani kwenye mojawapo ya hoteli zenye hadhi ya juu kabisa si utani. Sitaki kukisia lakini Mkaguzi Mkuu wa serikali akithubutu kujumlisha gharama ya safari, malazi, chakula na matumizi mengine ya ki-Rais, sitashangaa jumla itakuwa kwenye mamilioni.
Katika hayo tusisahau kupiga hesabu za posho za wasaidizi mbalimbali na watumishi wanaosafiri na Rais au mawaziri wengine waliokuwa kwenye msafara huo.
Je, hawa wasaidizi wanalipwaje wanapokwenda nje ya nchi kwa siku? Kuna mtu anajua mahesabu haya na natumaini siku moja wataweka wazi kiasi kinachotumika kwa Rais kusafiri nje ya nchi.
Jambo jingine linalosumbua katika ziara hizi ni kile ambacho naweza kukiita "duplication" ya safari. Kuna wakati ndani ya miezi michache utaona Makamu wa Rais ameenda nchi fulani na siku chache baadaye Rais Kikwete yuko nyuma. Hili limetokea kwenye safari ya Rais Kikwete kule India na nikikumbuka vizuri hata alipokwenda Uarabuni. Hapa najiuliza kama yawezekana Rais Kikwete hawaamini watu wa chini yake (makamu na mawaziri) kwenda nchi nyingine na kuwakilisha maslahi ya Taifa?
Sasa hivi habari za uchunguzi zinasema huenda Rais akafanya ziara ya Marekani ya Kusini hivi karibuni. Inatarajiwa kuwa atatembelea nchi kama Cuba, Venezuela na Brazil. Nchi hizi zote zimetembelewa na Makamu wa Rais miezi michache tu iliyopita. Bila ya shaka huko hawamjui Rais wa Tanzania na ni eneo pekee ambalo Rais Kikwete hajatembelea tangu aingie madarakani.
Lakini hatuna budi kujiuliza kama Makamu wa Rais alikuwa huko ni kitu gani hiki kinacholazimisha Rais naye kwenda huko huko? Ni kitu gani ambacho Makamu wa Rais alishindwa kukifanya hadi Rais apitie huko? Kuna tetesi pia yawezekana akitoka huko atapitia tena Marekani!
Kuna safari ambazo naamini ya kuwa zinamuhitaji Rais kwenda kama siku chache pale Umoja wa Mataifa. Lakini kuna safari nyingine zingeweza kufanywa na Makamu au Waziri Mkuu. Huu ulazima wa visafari hivi vyote kuwa aende yeye kunaonyesha tatizo kama lilivyoonyeshwa katika hiyo ripoti ya EIU.
Pamoja na hayo ni lazima tutafute njia nzuri ya kupima mafanikio ya ziara hizi tukilinganisha na gharama yake. Sijui ni kwa kiasi gani safari hizi ziko tayari kwenye bajeti na kwa kiasi gani bajeti inazingatiwa.
Hapa naamini kazi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali itaonyesha umuhimu wake mkubwa sana. Mkaguzi Mkuu atalifanyia taifa hisani kubwa kama akiweza kuchanganua matumizi ya safari hizi za Rais na misafara ya watu anaoandamana nao ambao wanagharimiwa na fedha za walipa kodi wa Tanzania.
Ni lazima tuwe na utaratibu wa kujali fedha za wananchi kuliko kufikiria kuwa kwa vile zipo basi "tutumbue". Mnapokuwa na baba ndani ya nyumba au mama ambaye anasafiri mara kwa mara watoto hamna budi kujiuliza kama yote hayo ni mazuri kwa familia au la.
Kama kila wakati baba akirudi nyumbani watoto mkifurahia na kabla hamjaanza kumueleza yaliyowakuta shuleni au matatizo na majirani yeye anatimka kwenda kwingine mwisho kila mtoto ataanza kufanya mambo yake. Mwisho wake baba atashindwa kusimamia nidhamu ya watoto wake.
Ndugu zangu hilo ndilo linalotokea sasa hivi Tanzania kiasi kwamba watu wana shaka kama Rais Kikwete ana udhibiti wa Serikali na chama chake. Kwa kadiri mambo yanavyokwenda inaonekana kana kwamba Rais amefanya uchaguzi; uchaguzi wa kufuata safari zake na si maslahi ya wananchi na kuliongoza Taifa.
Tunapokabiliwa na changamoto za maamuzi magumu na hatua nzito Rais wetu anapokuwa hapatikani, kunatufanya tuamini kuwa aidha hatujali au hajali ule wajibu ambao tumempa.
Kama hadi hivi sasa ameshindwa kusimamia mazungumzo ya Muafaka wa Zanzibar huku Uchaguzi Mkuu ujao ukisogea karibu kabisa na matokeo ya kuingia katika uchaguzi huo bila Muafaka tukiwa tunayajua wote, kama hadi hivi sasa ameishia kuambia ulimwengu kuwa "tunapambana na rushwa" wakati ripoti ya Transparency International ya mwaka huu inaonyesha kuwa rushwa imeongezeka, basi, tuna matatizo.
Na bahati mbaya nyingine ni kwamba inaelekea hakuna watu wanaoweza kumwambia kwa yakini, kwamba kwa uzuri wote anaodhani anawafanyia Watanzania, wangependa wamwone akishughulikia matatizo ya ndani zaidi, isifike mahali umma ukamchoka wakati kimsingi yeye ni bora kuliko viongozi wengi waliopo kwa maana ya uadilifu.
Rais Kikwete anahitaji kuliongoza Taifa katika mambo haya magumu yanayolikabili Taifa na kufanya maamuzi magumu ambayo yataonyesha kuwa yeye kweli ana udhibiti wa Serikali yake. Kama anaona hili ni gumu na "kuruka" kila baada ya wiki ndiyo uongozi wenyewe, basi, Bunge letu liamue kupitisha sheria ya kujenga Ikulu ndogo Ulaya, Marekani na Asia ili Rais wetu awe anaishi huko huko majuu na arudi nyumbani kutusalimia akijisikia. Kwani hadi hivi sasa, mambo yanakwenda kama hayaendi bila yeye.
Unapomaliza kusoma makala hii Rais atakuwa amerudi nyumbani kwa Sikukuu ya Idd. Lakini sitashangaaa ndani ya wiki moja ijayo au mbili tukasikia ameondoka tena kwenda mikoani au "kwa mjomba".
Vyovyote vile lazima tukubali kuwa kuna kitu kinamfanya Rais wetu asipende kukaa Dar es Salaam na kupenda kukimbilia mikoani au kwenda nje ya nchi. Bado natafakari ni kitu gani hicho kinachomfanya apaone Dar es Salaam pachungu.
Vyovyote vile, sitoshangaa kuwa kina Marco Polo na Vasco Da Gama wanaweza kuwa wanasikia wivu. Angalau wao walikuwa ni wafanyabiashara na wavumbuzi; wa kwetu ndiye Rais mwenyewe.