Ongezeko la asilimia 5.2 la uchumi wa China kwa mwaka 2023 ni habari njema kwa Afrika na dunia

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
1709088799427.png


Serikali ya China imetangaza kuwa uchumi wa China kwa mwaka 2023 ulikuwa na ongezeko la asilimia 5.2. Habari ambayo wachambuzi wa maswala ya kiuchumi duniani wanaiona kuwa ni habari inayoleta ahueni kwa dunia, hasa ikizingatiwa kuwa hali ya uchumi wa dunia kwa ujumla bado haijatengemaa.

Kwenye mkutano wa Davos uliofanyika mapema mwaka huu, mkurugenzi wa Shirika la Fedha duniani IMF, Bibi Kristalina Georgieva akizungumzia uchumi wa China alisema, kufikia ongezeko la uchumi la zaidi ya asilimia 5 ni habari njema kwa China, na pia habari njema kwa Asia na dunia kwa ujumla kwa sababu uchumi wa China unachangia theluthi moja ya ukuaji wa kimataifa. Hali hii ni habari njema pia kwa ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika, kwani kutokana na mafungamano ya kina ya uchumi wa pande hizi mbili, ni wazi kuwa changamoto za kiuchumi kwa China zinaweza kuwa na matokeo hasi kwa nchi za Afrika.

Wachambuzi wa maswala ya uchumi wa Afrika walionesha wasiwasi mara kwa mara kuhusu maendeleo ya uchumi wa China na athari zake kama China ingechelewa kufufuka kutokana na athari za janga la COVID 19, na hata baadhi kuanza kuhimiza maendeleo ya biashara ya ndani ya Afrika kama moja ya njia ya kuepuka athari kama zikitokea, lakini kwa mshangao wa wengi mafungamano ya kiuchumi na China yameendelea kuwa imara na hata kukaribia kurudi katika hali ilivyokuwa kabla ya janga la COVID 19. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2023 China ilikuwa imetenga karibu dola bilioni 1 za mikopo kwa ajili ya nchi za Afrika ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mwanzoni mwa mwaka jana kulikuwa na hofu kuhusu uwezekano wa China kufikia malengo yake ya kiuchumi hasa kutokana na changamoto za uchumi wa dunia, madhara ya janga la COVID-19 na hata migogoro inayoendelea duniani na athari zake kwa uchumi. Hata hivyo kutokana na mabadiliko ya muundo wa uchumi wa China, wa kuifanya sekta ya matumizi ya ndani kutoa mchango mkubwa kwenye ongezeko la uchumi, na kupunguza utegemezi wa kuuza bidhaa nje, inaonekana kuwa na matokeo mazuri, kwani ongezeko ililopata China limepatikana katika mazingira ya dunia yenye changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa vitendo vya kujilinda kibiashara.

Kauli ya Bibi Georgieva kuhusu ongezeko la uchumi wa China sio ngeni, kwani mwaka jana aliwahi kusema kuwa China na IMF ni washirika wakubwa kwenye maswala ya uchumi, na China ina uwezo mkubwa wa kuleta tija na kuweka mazingira thabiti yenye tija zaidi kiuchumi. Lakini pia alipongeza China kwa kuendelea kutekeleza sera ya mageuzi, ufunguaji mlango na ushirikiano katika uchumi wa dunia, ambavyo alivitaja kuwa ni njia sahihi kwa China, na pia ni jambo lenye manufaa kwa dunia.

Moja kati ya mambo ya muhimu ambayo Bibi Georgieva ameyataja ni kuwa China inachangia theluthi moja ya uchumi wa dunia. Kauli hii inaonesha kuwa uchumi wa China umefungamana na unaingiliana kwa kina na uchumi wa nchi nyingine dunia, na kwamba uchumi wa China ni injini muhimu ya uchumi, ambayo ni muhimu katika kuhimiza ajenda ya kimataifa ya kupunguza umaskini na kuhimiza maendeleo ya uchumi.
 
Back
Top Bottom