Wataalamu wa habari wa Tanzania waona maamuzi yanayotolewa katika Bunge la Umma la China yanaleta athari za moja kwa moja duniani

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
VCG11463967990.jpg


Wakati Mikutano miwili mikubwa inayofanyika kila mwaka hapa nchini China yaani Bunge la Umma (NPC) na Baraza la Mashauriano ya Kisiasa, ikiwa imefunguliwa na kuendelea kufanyika katika Jumba la Mikutano ya Umma hapa Beijing, nchi mbalimbali duniani zimeanza kufuatilia kwa karibu zaidi mwenendo wa mikutano hii wakiwa na matumaini makubwa huku wakisubiri kwa hamu juu ya ajenda zitakazojadiliwa na kupitishwa ikiwa ni pamoja na kuona matokeo kamili ya mikutano hii.

Si jambo la kushangaza kuona macho yote duniani sasa yameelekezwa kwenye kikao cha bunge, kwani kama inavyofahamika kuwa China ni nchi kubwa na inayotegemewa zaidi duniani, hivyo maamuzi yoyote yatakayotolewa ama kupitishwa basi pia yataathiri moja kwa moja pande nyingine za dunia katika masuala ya biashara, uwekezaji, usalama na hali ya uchumi duniani.

Akizungumzia kuhusu athari ya mikutano hii miwili ya China kwa dunia, mwanahabari wa Gazeti la Mwananchi, Tanzania Ephrahim Edward Bahemu ambaye mwaka jana alikuja kushuhudia vikao hivi vikipitisha ajenda zake mbalimbali, anasema nchi za Afrika ni lazima zifuatilie zaidi mikutano hii, kwasababu ukiangalia kwenye masuala ya biashara katika muongo mmoja uliopita, China imekuwa mbia namba moja kati yake na bara la Afrika, hivyo hatua zozote zile za kimaendeleo zinazohusiana na taifa hili zinakuwa na athari ya moja kwa moja kwa mataifa ya Afrika.

“China ni mzalishaji namba moja duniani, hivyo sera zake zinazohusiana na masuala ya uzalishaji, ama maamuzi yake ya ndani yanaathiri dunia kwa ujumla, hasa ikizingatiwa kwamba dunia inategemea bidhaa nyingi kutoka katika taifa hilo. Hivyo yote haya yanafanya ushawishi wa China duniani kuendelea kuongezeka” anasema Ephrahim Edward Bahemu

Kama alivyotangulia kusema Bahemu kwamba ni jambo muhimu kuendelea kufuatilia na kujua kinachoendelea katika taifa hili ili pindi China ikija na mikakati mizuri itakuwa na manufaa kwa dunia nzima.

Katika ufunguzi wa kikao cha bunge, moja ya mambo yaliyojadiliwa ni nia ya China kutaka kufikia kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa cha karibu asilimia 5 katika mwaka huu wa 2024, ikiashiria nchi hii ambayo ni ya pili kwa uchumi mkubwa duniani imedhamiria kupata maendeleo ya hali ya juu licha ya sintofahamu zilizopo ndani na nje ya nchi.

Lengo lililokadiriwa, ambalo halina tofauti na lengo la ukuaji la mwaka uliopita, ni mojawapo ya malengo muhimu ya maendeleo yaliyozinduliwa katika ripoti ya kazi ya serikali iliyotolewa bungeni na Waziri Mkuu Li Qiang.

Bila shaka hii tunaweza kusema ni habari njema kwa mataifa mengine pia, kwasababu kukua kwa uchumi wa China pia kutatuliza ukuaji wa uchumi wa nchi nyingine duniani. Lakini kubwa na muhimu zaidi ni kwamba kwa sasa watu wanatega sikio kwa makini kujua China itatangaza sera gani za nje pamoja na uhusiano wake na nje.

Kwa upande wake Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya serikali Zanzibar, Ali Haji Mwadini anaona kupitia mikutano hii miwili ya China, nchi za Afrika pia zitanufaika pakubwa, hasa kwa kuwa miongoni mwa mambo yanayojadiliwa bungeni ni maendeleo ya kiuchumi na viwanda ya China.

Si miaka mingi sana iliyopita ambapo China pia ilikuwa ni miongoni mwa nchi masikini lakini kwa sasa imeweza kujikwamua na kupiga hatua kubwa hasa kwasababu ya uongozi wake imara, hivyo kwa nchi za Afrika pia zinaweza kutumia fursa hii kujifunza jinsi gani uongozi wa China ulivyoweza kuleta mabadiliko au maendeleo ya kiuchumi na ya viwanda.

“Utaalamu na teknolojia za China zimechangia sana katika maendeleo ya kiuchumi na kufikia hatua ya maendeleo ya viwanda” alielezea Ali Haji Mwadini

Wachina ni watu wabunifu na wenye mikakati imara, na ndio maana hata uendeshaji wa kikao chao cha bunge unachukua muda mfupi sana, ambao unaondoa porojo nyingi bungeni na kuepuka kutumia gharama kubwa katika kipindi hiki. Mwadini anaona hili ni jambo ambalo kwa nchi za Afrika zinaweza kuona ni dogo lakini umuhimu wake ni mkubwa sana hasa ikizingatiwa kuwa nyingi zao ni masikini.
 
Back
Top Bottom