fanya utafiti wanao mtukana nyerere wengi ni dini moja hapa bongo kwa kisingizi aliwadandamiza
halafu sijiamini kwani mimi nyerere
siyo kweli maneno yako. Na huyu mwandishi je?
Kama si Nyerere, tusingekuwa na ombwe hili la uongozi!
Evarist Chahali
Uskochi
29 Jun 2011
Toleo na 192
WIKI hii ninazungumzia jambo linaloweza kuwakera baadhi ya wasomaji wa safu hii; ninajaribu kumkosoa mwasisi wa Taifa letu, Mwalimu Nyerere na itikadi yake ya Ujamaa na Kujitegemea, na jinsi ilivyojenga msingi wa ufisadi na utapeli wa kisiasa.
Nimetahadharisha kuwa mada hii inaweza kuwakera baadhi ya wasomaji kwa sababu kuu mbili. Kwanza, hata baada ya kifo chake, Nyerere ameendelea kubaki na heshima ile ile aliyokuwanayo katika siasa za nchi yetu, na neno lolote baya dhidi yake linaweza kukusababishia hasira kubwa.
Kimsingi, kumsema Nyerere vibaya kunaweza kutafsiriwa sio tu kama ukosefu wa heshima; bali pia sawa na kutafuta laana.
Sababu ya pili ni ukweli kwamba kwa mujibu wa mila na desturi zetu za Kiafrika, si vyema kumsema vibaya marehemu. Sifahamu kwa nini jamii inapendelea kuzungumzia mema tu ya waliofariki na kuepuka mabaya yao, lakini inawezekana ni miongoni mwa njia za kuwaliwaza wafiwa.
Kumzungumzia Nyerere na Ujamaa kunahitaji zaidi ya makala moja, na kwa minajili hiyo nitaelemea zaidi kwenye hoja ninayojaribu kuitengeneza kwamba kwa kiasi fulani (na pengine kiasi kikubwa) kuna mambo ambayo laiti Nyerere angeyafanya vyema, basi, leo hii tusingekuwa tunashuhudia nchi ikipelekeshwa na mafisadi huku uongozi wa nchi ukiwa katika mtindo wa bora liende.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanakwenda mbali na kumtuhumu Nyerere kuwa alipoamua kungatuka mwaka 1985 hakufanya hivyo kwa minajili ya kupisha wengine waongoze; bali ilikuwa ni dalili ya kukubali kimya kimya kuwa jaribio lake la Ujamaa limeshindikana na nchi ilikuwa imemshinda.
Wachambuzi hao wanafikia hatua ya kumshutumu kuwa, kwa hakika, wakati anastaafu alipaswa kuwaomba radhi Watanzania kwa baadhi ya makosa aliyofanya, na ambayo kwa sasa yanaisumbua sana Tanzania.
Kwa minajili ya makala hii, naomba niweke kando mazuri mengi ya Nyerere. Sifanyi hivyo kwa ajili ya kumfanya aonekane mbaya tu; bali kuepusha mkanganyiko katika uwasilishaji wa hoja yangu. Na kwa upande mwingine, takriban kila Mtanzania anafahamu mema ya Baba wa Taifa, lakini yayumkinika kuhitimisha kuwa mabaya yake yameendelea kuwa kama mwiko.
Kosa moja kubwa la Ujamaa wa Nyerere lilikuwa katika namna jamii ilivyotakiwa kuwanyenyekea viongozi. Wengi tunakumbuka kibwagizo zidumu fikra za mwenyekiti... Leo hii tunaweza kujiuliza pasi hofu kuwa zidumu hata kama ni hovyo?
Ujamaa ulifanikiwa kutengeneza matabaka yasiyoonekana. Kwa vile Chama kilishika hatamu, na uongozi wa Chama kubaki kwa wateule wachache, kilichojitengeneza ni hali ya u-Mungu mtu kwa viongozi wetu. Japo Nyerere alikuwa mcha Mungu, kama Mjamaa alijitahidi sana kupunguza nguvu ya dini kwenye harakati za jamii.
Kimsingi, Nyerere alitaka dini ibaki kuwa suala la mtu binafsi lakini isiwe jambo linaloweza kukinzana na siasa na uongozi wa nchi. Ni kwa minajili hiyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaamini kuwa hata hujuma dhidi ya taasisi muhimu kwa Waislamu ya East African Muslim Welfare Society (EAMWS) zililenga kuepusha uwezekano wa asasi hiyo kutoa uongozi mbadala kwa jamii (hususan Waislamu).
Kadhalika, baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa hata kile kinachodaiwa kuwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kugeuzwa chombo cha kuwakilisha maslahi ya dola badala ya waumini, ni matokeo ya jitihada hizo za kupunguza nguvu za dini kwenye jamii.
Kwa hiyo, kwa makusudi au bila kukusudia, Ujamaa ulifanikiwa kuzalisha miungu watu ambao fikra zao zilipaswa sio tu kuwa sahihi; bali kunyenyekewa na kuabudiwa kwa nguvu. Ni wazi kuwa laiti dini zingekuwa na nguvu sawa na itikadi, wananchi - ambao pia ni waumini wa dini hizo, wangeweza kumtanguliza Mungu zaidi badala ya kulazimishwa kuwaabudu watawala; hata wazembe na wale wenye mapungufu ya uadilifu.
Tofauti na sasa ambapo baadhi ya viongozi wameamua kujidhihirisha rangi zao halisi kwa kutetea hata yasiyopendeza masikioni mwa wananchi (kwa mfano, kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutetea posho za waheshimiwa, hii ya Spika Anne Makinda kuwafananisha baadhi ya wabunge na watu (Waswahili) wa Kariakoo, na ile ya Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kutetea malipo kwa kampuni ya Dowans), enzi za Nyerere tulishuhudia watendaji wake wakituhadaa majukwaani kuhusu Ujamaa; ilhali mioyoni walikuwa mabepari wanaosubiri Nyerere aondoke waanze kutafuna nchi.
Na dua zao zilisikilizwa mwaka 1985 pale Nyerere alipoamua kustaafu. Bila aibu wala uoga, Awamu ya Pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, ikaanzisha operesheni ya nguvu ya kuua Ujamaa. Ikumbukwe kuwa hadi wakati huo Ujamaa ulikuwa bado kama ndoto na hadi unauawa, haukuweza kufikia hatua ya kuwa kitu halisi. Ndio maana Mwinyi na wenzake waliopitisha Azimio la Zanzibar hawakupata wakati mgumu kutekeleza mauaji ya itikadi ya Ujamaa.
Lakini hata kabla ya Mwinyi na wenzie kuuzika Ujamaa, utawala wa Nyerere ulishatengeneza mazingira ambayo yalikwaza utekelezaji kamili wa itikadi hiyo. Kwa mfano, pamoja na kauli kali dhidi ya mabepari na mabeberu, Tanzania iliendelea kuwa tegemezi wa misaada ya mabepari na mabeberu haohao tangu tunapata Uhuru hadi Nyerere anaondoka madarakani.
Utegemezi huo kwa kiasi kikubwa haukuwekwa hadharani pengine kwa kuchelea kuwa ungeleta mgongano na msisitizo wa sera ya Kujitegemea. Lakini hilo ni dogo kulinganisha na ukweli kwamba miaka kadhaa kabla ya kuwekwa hadharani, Serikali ya Nyerere ilikuwa ikifanya mashauriano ya siri na mashirika ya fedha ya kimataifa kuhusu mipango ya kurekebisha uchumi (kibepari) ambayo kimsingi ilikinzana moja kwa moja na itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea.
Lakini lililo baya zaidi ni kwamba Nyerere alikuwa amezungukwa na matapeli mbalimbali wa kisiasa (political conmen). Hawa ni watu walionukuu ki-kasuku kila alilosema Nyerere na tukawaamini kuwa ni Wajamaa kama yeye, lakini ukweli ni kwamba walikuwa na mawazo ya kibepari na kinyonyaji. Kwa faragha, walifanikiwa kuwekeza utajiri mkubwa nje ya nchi; huku subira ikivutwa Nyerere aondoke madarakani ndipo uanze kutumika.
Watangulizi wote wa Nyerere, kwa maana ya Mwinyi, na Marais Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, ni watu waliolelewa na Baba wa Taifa. Swali la kujiuliza ni je: Waliwezaje kuficha rangi zao halisi na kudumisha imani ya Nyerere kwao hadi walipofanikiwa kupata urais na kubainisha wao ni watu wa aina gani?
Lakini pia tunafahamu udhaifu wa Nyerere ambao umerithiwa hadi sasa ambapo viongozi aliowapenda walipoboronga sehemu fulani waliadhibiwa kwa kuhamishiwa mahala pengine. Kiongozi anavurunda kuongoza shirika la umma; kisha anaadhibiwa kwa kupewa ubalozi!
Kuna wanaodhani kuwa huenda Nyerere hakujua kuwa baadhi ya wafuasi wake ni mbwa mwitu wenye ngozi ya kondoo.Wengine tunadhani kuwa Nyerere alifahamu kuhusu hilo, lakini, kama ilivyo kwa Kikwete na mafisadi, alikuwa na huruma kwao.
Labda aliamini kuwa ni utoto wao tu katika kuuelewa Ujamaa, wakikua wataacha. Kwa bahati mbaya hawakuacha, na Nyerere alipoondoka watoto hao watukutu wa Ujamaa wakageuka majabali ya siasa zisizojali kabisa utu wa Mtanzania wa kawaida.
Na kwa vile Ujamaa ulikuwa na chembechembe za Ukomunisti - mfumo wa kibabe usioruhusu kukosoa au upinzani, CCM aliyoasisi Nyerere ikageuka taasisi ya ki-Mungumtu ambapo licha ya kiminya fursa ya kukosoana, inawaona wanasiasa wa Upinzani kama maadui wa Taifa. Kila anayejaribu kukosoa anaonekana kama mhaini.
Ugonjwa huo ukahamia na kwenye taasisi za dola (kama Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi) ambapo badala ya kuwekeza nguvu kupambana na maovu katika jamii, raslimali kubwa inaelekezwa kuwadhibiti wazalendo wanaokemea au kupambana na maovu hayo.
Matapeli zaidi wa kisiasa zaidi ya wale waliokuwemo kwenye mfumo wametambua kuwa sehemu salama ya kuifisadi Tanzania, ni kuwemo ndani ya CCM ambapo sio tu watapatiwa ulinzi na vyombo vya dola, lakini pia watafanikisha madili yao ya kifisadi (kama ilivyokuwa kwenye skandali za Richmond, EPA, nk), na pindi wakijisikia kujiuzulu watapongezwa kwa ujasiri wao na kuambiwa hizo ni ajali tu za kisiasa (rejea kujiuzulu kwa Lowassa).
Migongano tunayoshuhudia hivi sasa kati ya wanasiasa na viongozi wa dini ni mwendelezo tu wa jitihada zilizoanzishwa nyakati za Ujamaa. Kadhalika, uzembe wa wabunge wengi wa CCM kupitisha kila kinacholetwa na serikali bungeni (hata kama kina madhara kwa wapigakura wao), ni mwendelezo huo huo wa Chama kushika hatamu.
Na udikteta wa Spika Makinda dhidi ya wabunge wa vyama vya Upinzani, ni utekelezaji tu wa imani hasi kuwa vyama hivyo ni mithili ya maadui wa taifa (na sio umasikini, ujinga na maradhi kama alivyotusisitizia Nyerere).
Hali kadhalika, utetezi wa waheshimwa kuhusu posho kubwa wanazolipwa na zisizoendana na utendaji kazi wao unachangiwa zaidi na imani potofu kuwa stahili zao hazipaswi kwa namna yoyote ile kufanana na za walalahoi.
Kibaya ni kwamba tumebaki kuwa taifa lisilo na mwelekeo. Kwenye Ujamaa hatupo kwa vile ulishazikwa na Azimio la Zanzibar. Kwenye ubepari hatupo kwa vile Ubepari hauhalalishi utapeli wa kisiasa na ufisadi mwingineo unaoshamiri kwenye nchi yetu.
Kama ambavyo tunaotegemea kudra za Mwenyezi Mungu kutusaidia kutatua tatizo la mgao wa umeme, hatma ya nchi yetu nayo inaelekea kutegemea kudra za Muumba.