Habari hii hapa inaweza pia kusaidia baadhi ya hoja za wajumbe, hasa kuhusu ELIMU...kama ilivyoripotiwa na Mwananchi...
Rais Kikwete aonya kuhusu mifarakano ya dini
Na Shadrack Sagati
RAIS Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kufahamu kuwa katika mifarakano na uhasama wa kidini, hakuna atakayeibuka mshindi bali wote watakuwa ni watu walioshindwa.Akihutubia Baraza la Eid el Fitr lililofanyika Jijini Arusha jana, Rais Kikwete alisema watu wa imani tofauti katika jamii wataendelea kuwepo; hivyo kila mtu lazima aukubali ukweli huo na akubali kuishi na mwenzake wa dini na dhehebu tofauti.
"Hili linawezekana kwani ndiyo ilivyo hivi sasa hapa kwetu," alisema Rais Kikwete na kusisitiza kuwa serikali anayoiongoza, haitarudi nyuma katika kuheshimu uhuru wa raia wa kuabudu na kuhubiri dini bila kuchochea chuki na uhasama miongoni mwa wafuasi wa madhehebu na dini nyingine.Alisema yeye na wenzake serikalini, watakuwa wakali na wepesi wa kuchukua hatua kuhakikisha watu wachache wakorofi hawavurugi nchi kwa kuchochea uhasama na kutokuelewana kati ya Waislamu na Wakristo.
Rais amewaonya watu hao aliowaita waovu, kuwa serikali haitakuwa na ajizi bali itaendelea kulinda amani bila woga, huba au upendeleo kwa dini yoyote. "Tumefanikiwa miaka yote huko nyuma, hatuwezi kushindwa sasa."Hivyo, Rais aliwataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao wenye mwelekeo wa kuhubiri na kupandikiza chuki dhidi ya dini na waumini wa dini au madhehebu mengine, waache kufanya hivyo.
Akizungumzia mchango wa dini katika kuleta maendeleo, Rais aliwaambia Waislamu kuwa mchango wa dini yao hasa madhehebu ya Suni ambao ndio wengi sio mkubwa katika masuala ya elimu, afya ukilinganisha wa dini nyingine au madhehebu mengine.Aliwapa changamoto kuwa ili waweze kushiriki katika dini zingine ni lazima wawe na uongozi thabiti na makini wa Baraza Kuu la Waislam (Bakwata) ili liwe na mwelekeo wa kisera unaotoa kipaumbele stahiki kwa masuala ya kuendeleza elimu na afya.
Jambo lingine alilolitaja ili Bakwata ifikie malengo yake ni kuwepo kwa mikakati na programu za utekelezaji wa mipango hiyo na pawepo pia na mfumo maalum wa uendeshaji wa kuongoza na kusimamia utekelezaji wa programu na miradi ya utekelezaji wa mipango watakayojiwekea.
Rais alisema mambo hayo matatu aliyoyaita ya msingi yamekuwa pungufu katika Bakwata; ndio maana Waislamu hawakupiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta za elimu na afya.
Alitaja mapungufu mengine kuwa ni kutokuwepo kwa uaminifu wa uongozi na watendaji wa baraza hilo, kutokana na baadhi ya viongozi wake kutokuwa waaminifu katika kudhibiti na kusimamia fedha na mali za baraza hilo."Matokeo yake ni kukosekana kwa misaada muhimu kutoka kwa watu wenye nia njema ndani na nje ya nchi," alisema Rais ambaye alimtaka mufti na viongozi wenzake kuwa waaminifu na wawe na mfumo mzuri wa usimamizi wa fedha na mali za baraza.
Kuhusu Waislam kujiimarisha kiuongozi, Rais Kikwete alisema Bakwata ndicho chombo kikuu cha uongozi wa Waislamu na angependa kuona baraza hilo linaaminiwa na kuheshimiwa na waumini wote wa dini hiyo.Aliongeza kuwa Bakwata ndicho chombo kikuu kinachotegemewa cha kuwaunganisha na kuwaongoza Waislamu katika kuendeleza maslahi yao ya kiimani na kimaendeleo "Bakwata haina budi iwe ndilo kimbilio la Waislam kwa matatizo yao ya kiroho na kimwili."
Rais alisema Waislamu wanapokosa chombo cha kuwaunganisha wanakosa umoja, mshikamano na wanayumbishwa. Alisema hali hiyo inawafanya baadhi yao kuangukia katika mikono ya watu wabaya na wakatumika kwa mambo yasiyokuwa na maslahi kwa Waislamu.Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete alisema uendeshaji wa dini ya kiislam hasa ya dhehebu la Suni ni tofauti na zile za dini ya Kikristo na hata za madhehebu mengine ya dini ya Kiislamu. Alisema wengine wana uongozi wa kuanzia chini mpaka juu kitaifa na hata kimataifa jambo ambalo haliko kwa Suni.
Akionyesha umuhimu wa kuwa na chombo cha kuwaunganisha waumini mbalimbali, Rais alitoa mfano wa uongozi kwaWakristo kuwa wana Paroko au mchungaji kiongozi wa kanisa, wana jimbo linaloongozwa na Askofu, wana Jimbo Kuu linaloongozwa na Askofu Mkuu na wana Mkuu wa Kanisa kwa nchi na wana uongozi wa kimataifa. Alisema hata Bohora, Ismailia, Wahindu na hata Shia wako karibu hivyo hivyo.
Lakini kwa upande wa Waislam wa Suni, Rais Kikwete alisema uongozi huanzia na kuishia msikitini na wala hakuna msikiti mkubwa wenye mamlaka kwa mdogo. Pia alisema hakuna sheikh mkubwa mwenye mamlaka ya amri kwa wenzake."Ni dini iliyojengeka kwenye msingi wa usawa wa waumini wa misikiti yao. Katika mazingira hayo kuwepo chombo cha kuwaunganisha Waislam baada ya ngazi ya msikiti ni jambo jema na la manufaa ya aina yake," alisema.Katika hotuba yake hiyo Rais Kikwete aliwataka viongozi wa Bakwata kutambua umuhimu na unyeti wa baraza hilo na kuishi na kufanya kazi kwa shabaha na malengo yake ili kulinda maslahi ya Waislamu wote.
Wakati huo huo, Mussa Juma anaripoti kutoka Arusha kuwa Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaban Simba amewataka Waislam nchini, kuendeleza matendo mema na umoja kama walivyokuwa katika mwezi wa ramadhani na kuacha vurugu za mara kwa mara katika misikiti.
Akizungumza na waumini wa Kiislam mara baada ya sala ya Idd el fitri iliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jana, Mufti alisema kama Waislam watarejea kutenda maovu itamaanisha kuwa hawakubadilishwa na mwezi wa ramadhani."Tumetoka kwenye ibada sasa sote ni wasafi hatutarajii kurejea tena kule tulipokuwa ...kama uliacha madhambi ni vyema ukaendelea kuacha na hiyo ndio itadhihirisha ramadhani imekubadilisha kwa dhati," alisema Mufti Simba.
Sheikh Mkuu pia aliwataka Waislam kuacha kuendeleza vurugu misikini kwani vitendo hivyo ninaendelea kuwagawa waumini wa dini hiyo na ni makosa makubwa mbele ya Mungu."Amani hii ambayo tuliyonayo iendelee hata katika misikiti yetu, tuache vurugu, tuwe kitu kimoja kwani umoja ni nguvu," alisema Mufti.Alisema migogoro na vurugu isipewe tena nafasi miongoni mwa Wasilamu na wasio Waislam ili nchi iendelee kuwa ya amani na utulivu wakati wote.
Awali, akisoma hutuba ya Idd, Sheikh Khadiu Hussein, aliwataka Waislam kuongeza juhudi katika kutafuta elimu na kufanya kazi kama ambavyo mwenyezi Mungu ameagizaSheikh Khadiu ambaye ni Imam wa Msikiti Mkuu wa Arusha, alisema tangu enzi za adamu, moja ya masuala yaliyopewa kipaumbele ni elimu na kazi hivyo ni lazima kufuata maagizo hayo.
Alisema Mtume Mohamad (SW), katika maisha yake, aliagiza waislam kuwa ni lazima kutafuta elimu popote inapopatikana duniani.