Mwasisi wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Edwin Mtei amesema kuwa chama
hicho kitaendelea kuwafukuza wote
wanaokihujumu huku akieleza kwamba,
anaunga mkono kuvuliwa uongozi kwa Zitto
Kabwe na Dk Kitila Mkumbo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na
gazeti hili, nyumbani kwake jana, Mtei
aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu (BOT) na
Waziri wa Fedha katika utawala wa awamu ya
kwanza wa Mwalimu Julius Nyerere, aliweka
wazi kuwa daima ataunga mkono dhamira ya
kukisimamia chama hicho aliyoitaja kuwa ni
safi.
Naunga mkono uamuzi wote wa Kamati Kuu,
kuwasimamisha na kuwavua uongozi Naibu
Katibu Mkuu wetu Zitto Kabwe na Dk Kitila
Mkumbo. Na kwa sababu Chadema inataka
kusonga mbele, lazima iwafukuze mafisadi na
wezi wanaoshirikiana kukihujumu chama,
alisema Mtei.
Bila kufafanua zaidi au kutaja majina,
mwenyekiti huyo wa kwanza wa Chadema
alisema: Hatuwezi kuendesha chama wakati
viongozi wengine wanapokea pesa na
kuzihifadhi kwenye akaunti za siri.
Alisisitiza
kwamba kwa nafasi yake akiwa mwasisi wa
Chadema ni lazima ahakikishe anaunga mkono
dhamira safi ya kukisimamia chama.
Kuhusu Arfi kujiuzulu
Akizungumzia hatua ya Makamu Mwenyekiti wa
Chadema (Bara), Saidi Arfi kujiuzulu, Mtei
alisema kuwa inafaa kiongozi huyo ajitazame
upya na kujisahihisha badala ya kuwa
mlalamikaji kila siku.
Aache kulalamika kwa sababu, wakati
alipochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti
mimi nilisimamia uchaguzi. Kama alikuwa na
ndoto kwamba siku moja atakuwa mwenyekiti
wa Chadema taifa alipaswa kujichunguza
kwanza, alisema.
Mtei aliongeza kuwa iwapo kuna watu
wanadhani Chadema itakufa hiyo ni dhana
potovu, lakini kwa sasa chama hicho
kimejipanga kuchukua dola na tayari
wamejiimarisha kimkakati.
Katika suala la kushughulikia watu
wanaokihujumu chama hakuna
compromise (mjadala), alihitimisha Mtei.
Juzi Chadema ilitangza uamuzi wa Kamati Kuu
yake kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila,
huku Arfi akitangaza kujiuzulu nafasi ya
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania
Bara.
Mtei amewahi kumkemea na kumwonya Zitto
katika mambo mbalimbali aliyofanya ndani ya
Chadema, moja ikiwa Oktoba mwaka jana
ambapo mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini,
alipotangaza kuwania urais mwaka 2015.
Alisema kuwa hatua hiyo itasababisha mzozo
na mpasuko ndani ya chama, huku akiongeza
kwamba amekuwa akimshauri Zitto mara kwa
mara kuhusu hatua yake hiyo akimtaka
kuwaunganisha wana-Chadema na siyo
kuwagawa au kuwavuruga.
Hakuna shida kuonyesha hisia, lakini
unatengeneza mzozo mkubwa sana ukitangaza
sasa. Mimi nimeshamshauri sana Zitto,
ahakikishe anakiunganisha chama na siyo
kukigawa wala kukivuruga, alisema Mtei.
Mtei alisema hatua ya mbunge huyo kutangaza
kutogombea tena ubunge na badala yake
kujipanga kuwania urais mwaka 2015, imekuja
mapema mno na kuonya kuwa itaibua mzozo
ndani ya Chadema, akiweka wazi kuwa wakati
ukifika chama hicho kitafanya uchaguzi sahihi.
Siyo vibaya kwa Zitto kuonyesha hisia zake,
lakini ndani ya Chadema kwa sasa, kuna watu
mbalimbali wanaopenda kuwania urais, lakini
hawajatangaza. Dk Slaa (Willbrod) anataka,
Freeman (Mbowe) anataka, Zitto anataka, hata
mimi huenda nikataka kugombea.
Hapa hakuna
upendeleo, sifa ndizo zitakazoamua, alisema.
Hata hivyo, Zitto alipinga kauli hiyo akisema:
Demokrasia haileti mizozo kwenye vyama vya
siasa hata siku moja, bali humaliza mizozo.
Udikteta, kuminya fikra huru na mawazo huru,
ndivyo huleta mizozo kwenye vyama vya siasa.
Alisema ni muhimu wazee wakawaacha vijana
wawe huru kusema wanachofikiri, kwa kuwa
uhuru wa fikra na mawazo ni moja ya haki za
msingi na moja ya nguzo za demokrasia.
Ninarudia, nitaomba kupeperusha bendera ya
chama changu kwenye uchaguzi wa urais
mwaka 2015. Naamini kwamba ninaweza
kuwezesha chama chetu kushinda na kuongoza
dola na Chadema kutoa rais wakati baadhi ya
waasisi wetu wakiwa hai na kuona vijana wao
tunavyobadili maisha ya Watanzania na
kutimiza ndoto zao, alisema Zitto.
Alisema ana uwezo, uadilifu na uzalendo wa
kutosha kuwa Amiri Jeshi Mkuu na kuunganisha
Watanzania kuwa wamoja bila kujali rika, dini
wala makabila yao... Nimejiandaa kisaikolojia
kukabili changamoto za ufukara wa nchi yetu.