Nimemaliza mwaka huu kwa Kupata Mtoto wa kiume; huu ni Muhtasari wa Safari tangu mwezi Februari mwaka huu

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,895
NIMEMALIZA MWAKA HUU KWA KUPATA MTOTO WA KIUME; HUU NI MUHTASARI WA SAFARI TANGU MWEZI FEBRUARI MWAKA HUU.

Anàandika, Robert Heriel
Shahidi

Andiko hili liwe tumaini kwa waliokata tamaa. Liwe faraja kwa wasio na mfariji. Liwe funzo kwa wenye kupenda ufahamu. Basi nikasema, hili nalo nitaandika kwa kifupi ili yule atakayehitaji kitu kama hiki asipate sababu ya kukikosa ikiwa atakitafuta. Nina furaha. Mwenye kufurahi afurahi pamoja nami. Kwa maana maisha ni kufurahi na kuwapa wengine furaha.

Kumtegemea Mungu kuna faida kubwa. Kumtegemea Mungu ni tafsiri ya kumuamini. Nimefunzwa hivyo, nimejifunza mwenyewe jambo hili. Nami nitawafunza wote wapendao na watakao kumtegemea Mungu na kumuamini. Mungu aliyewaumba, aliyeumba huu ulimwengu wa ajabu. Mungu wa maajabu. Ukiweza kumuamini huyo umeyaweza maisha. Ukifanikiwa kumjua huyo basi umetoboa kwenye maisha.
Kwa maana kuyaweza maisha ni kumuamini Mungu muumba, na kutoboa(kufanikiwa) kwenye maisha ni kumjua Mungu. Na huko ndiko kuishi.

Wakati ninapanga mambo yangu siku zote ninajua yale ambayo Mungu atayaruhusu ndio yatakayokuwa ya maana kwangu. Hiyo ninaiita mipango yangu inapofanana na mipango ya Mungu. Mipango yenye maana ni ile ambayo Mungu ameipanga kwangu. Lakini nani ajuaye mipango ya Mungu? Hakuna! Mipango ya Mungu hujulikana baada ya kutokea, na hiyo inanifundisha kusubiri wakati sahihi(wake). Subira, imani na tumaini.

Mwezi Februari ndipo safari ya Uhai ndani ya uhai ilianza. Mimi na Mke wangu, ndiye Binti Kimoso. Mipango yetu na ya Mungu iligongana. Wakati sahihi ulikuwa mbele yetu. Basi taarifa ya kubeba mimba nikapewa. Furaha yenye hofu vikachanganyika. Mtu fulani ataniuliza hofu kwenye furaha inawezekana vipi?
Hilo liliwezekana kwetu, kwanza ugeni wa jambo lenyewe, lakini pili, taarifa ya ujauzito huo uliendana na masharti makali ya Daktari ambaye ni specialist wa mambo ya kina Mama.

Daktari alitupa sharti kubwa moja ambalo alisema lazima tulizingatie kwa gharama yoyote. Sharti hilo ni mke wangu hapaswi kufanya kazi yoyote ile, alipewa bedrest. Hiyo ilimpasa aache kazi mimba ikiwa na mwezi mmoja tuu.Hiyo ilimaanisha pato la familia lingeathirika.

Tukasema Mungu ndie anaongoza. Yeye ndiye kiongozi wa Watibeli. Hivyo mke wangu akaacha kazi(kazi katika kampuni binafsi). Kipato cha familia yetu sio kikubwa lakini uwepo wa Mungu umetufanya tupate mahitaji yetu ya msingi kwa wakati. Naweza nisieleweke.

Kazi za kupika, kufua, kuosha vyombo, kwenda sokoni, yaani kazi yoyote hiyo ingekuwa juu yangu. Kuna wakati Binti Kimoso alikuwa akihitaji kunisaidia lakini nilimkataza, sipendi kupuuza taarifa ya kweli hasa inayotolewa na wataalamu. Sipendi Kujilaumu.

Kufanya kazi za nyumbani zote hiyo ilimaanisha kwenye kazi za uzalishaji kipato zingeathirika kwa kiwango fulani. Kumaanisha Economic Crisis kwa miezi ya mbele ilikuwa ni dhahiri.

Ilikuwa muhimu kuandaa mpango wa kukabiliana na wakati ujao ambao hatuujui. Lakini kwa vile tulikuwa tunamuamini Mungu ajuaye wakati na nyakati tukawa na imani kuwa kila kitu kitaenda Sawa. Tulichomuomba Mungu ni kutujulisha wajibu wetu katika safari hii.
Wajibu wetu ulikuwa kama ifuatavyo;

1. Kufuata taratibu zote za kiafya kama inavyoshauriwa na Mungu mwenyewe kisha na wataalamu wa afya aliowaweka.

2. Kuhakikisha tunatumia baraka na riziki atupazo Mungu kwa akili ikiwa ni pamoja na kuweka Akiba.

3. Kujiepusha na uzembe, kuwa Makini.

4. Kumjenga na kumlinda mtoto(aliyetumboni) kiafya(mwili), kihisia, kiakili, na kiroho.
Kiafya, kutumia vyakula, virutubisho vyote kama tulivyoshauriwa na wataalamu wa afya.
Kihisia, Kuhakikisha Mke wangu anafuraha muda wote, kuepusha migogoro, na muda wote kuwa na amani.
Kiakili, kufanya shughuli zinazohitaji utulivu wa akili kama kuchora, kuandika au kufuma.
Kiroho, kuweka ratiba ya maombi, kusoma neno la Mungu, na kuimba.

5. Kujiepusha na maneno au elimu ambazo hazitoki kwa wataalamu wa afya, au zenye ushirikina na uchawi.
Hii ni kwa vijana. Mtu kama hana utaalamu wa mambo ya udaktari usiuendekeze ushauri wake. Watalaamu wa ishu hizo wapo.

6. Wakati mwingine usiwaamini hata Madaktari. Hii nitaandika siku nyingine.

Safari hii ilinifundisha kuwa kila mtu unayekutana naye maishani anamchango hasi au chanya katika maisha yako. Hivyo lazima uwe Makini. Kama isingekuwa Mungu basi Mtoto huyu asingezaliwa.
Wakati mhusika mbaya fulani anapozuka kwenye maisha yako basi elewa kuwa hapohapo kuna mhusika mzuri atazuka kwenye maisha yako ili akusaidie.

Na mara nyingi wahusika watakaokupa msaada ni wale ambao hamjawahi kujuana. Na hiyo ikakazia falsafa yangu ya kuwa Wapende Watu wote na wafanyie wema Watu wote kwa maana hata wewe utafanyiwa wema na mtu yeyote.

Kuna furaha kubwa ukiwa unatekeleza majukumu yako kwa familia yako. Kuna furaha kubwa kuihudumia familia yako. Ilikuwa miezi tisa kama mwezi mmoja. Sikuona urefu wowote.
Mhudumie mkeo, ihudumie familia yako. Na kumfanyia hayo iwe kwa upendo ili usione mzigo. Kwa sababu upendo hauhitaji faida, upendo ni ukweli.

Vijana, kukosa kwako kipato sio sababu ya kuiangusha ngome yako, wewe ndiye Rais na mfalme wa nyumba yako. Kipato changu sio kikubwa mbele za Watu lakini ni kikubwa kwangu sababu kinatoka kwa Mungu wangu, yeye aliyemlezi, yeye ndiye anajua ninatakiwa niishije kwa muda huu ili niwe na furaha.

Nilimuomba Mungu tangu nikiwa mtoto kuwa nataka maisha yangu yawe ya amani na furaha. Hivyo hivi ninavyoishi naamini ni sehemu ya uratibu wake.

Vijana, hauhitaji pesa nyingi kuwa na familia yenye furaha. Familia hasa ukiwa katika nafasi ya mkeo ni mjamzito inahitaji mambo yafuatayo;

1. Upendo
2. Utayari huo itakupa Ujasiri wa kukabiliana na changamoto.
3. Akili ya kutumia baraka atakazokujalia Mungu wako. Kwa sababu Mungu ni lazima akupe riziki au baraka. Namna ya kutumia ni wewe mwenyewe.

Nakiri kuwa pamoja na namna nijionavyo kuwa ni mwanaume bora wa wakati wangu, lakini hata huyu Mwanamke ni bora zaidi.

Na hii inanifanya niseme kwa wanawake yakuwa, kwenye familia mnamchango mkubwa sana hasa mkiwa na tabia zifuatazo;

1. Watiifu
2. Wenye kumuamini Mungu na mumeo
3. Kutokuwa na tamaa
Wanawake wenye tamaa ndio huwahangaisha waume zao kwa vitu vilivyo nje ya uwezo wao.
4. Kujidhibiti

Mkishirikiana lazima mambo yaende. Na siku zote Watu wanaoabudu Mungu mmoja lazima washirikiane. Mkiwa na ratiba za kumuomba Mungu pamoja kwa imani yenu. Ninakuhakikishia lazima muwe na familia bora yenye furaha.

Kama mume unamheshimu Mungu hiyo automatically itamfanya mkeo akuheshimu.

Ndani ya familia tatizo kuu sio kipato kama inavyoripotiwa. Isipokuwa tatizo kuu ni kukosekana kwa Mungu ndani ya familià.

Familia inaweza isiwe na chakula wala pesa ndani lakini ikawa na furaha kama Mungu yu ndani ya nyumba hiyo. Lakini familia inaweza ikawa na vyote vya dunia hii lakini kama haina Mungu haiwezi kuwa na furaha na Amani.

Sisemi kujimwambafai kuwa labda familia yangu ina Mungu kuliko wengine. Nop! Bali naandika kwa wale ambao wanatafuta furaha ndani ya familia zao na hawajui wanaipataje. Jibu ni moja, msitafute pesa, sijui, magari, sijui majumba, sijui nini, nop! Mtafuteni Mungu. Huyo ndiye atawapa furaha ya kweli.

Wakati mimba imeingia ilibidi tuanishe vitu ambavyo lazima tununue kwaajili ya kufurahisishia majukumu ya nyumbani. Vitu kama Brenda, Jokofu, mashine za kufulia, Oven, n.k. lakini vyote tuliponunua hatukuona badiliko lolote la ndani katika nafsi zetu. Ni vitu vya kawaida.

Vijana, maisha yako yalipo ndio furaha yako inapopatikana. Usisuburi uwe na magari sijui vitu vizuri vya ndani ndio ufurahi. Hutokuja ufurahi kamwe kama mtazamo wako utakuwa hivyo.

Furaha ya kweli ni kuishi na mkeo kwa amani. HAKI, KWELI, UPENDO NA AKILI ndio viww nguzo ya familia yenu. Lazima mfurahie hata mngekuwa kwenye kijumba cha udongo.
Lakini kikikosekana kimoja kati ya hivyo hata mngeishi Mbinguni bado msingekuwa na furaha.

Mimi nimemaliza, Mwaka huu umeisha kwa mpango mkubwa kukamilika. Na hii inafanya Mungu atekeleze mipango yangu kwa asilimia 80%. Ikiwepo mipango ya kijamii, kiuchumi, na kifamilia.

Mungu awabariki.
Nawatakia Sabato Njema.

Ni yule shahidi kutoka Nyota ya Tibeli.
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Dar es salaam
 
Ili Mungu akubariki na kukunyooshea njia zako basi fuata na fanya yanayompendeza.

Wakati mwingine vijana hufeli kwa kufanya dhambi na kumchukiza Mungu.

Isingekuwa rahisi kwa kuomba tu, huku unafanya mambo ya ajabu kama ushirikina, wizi na utapeli na hata usinzi. Kijana kamvuta tu binti wa watu kamjaza.

Kama hujapata changamoto basi hesabu ni upendeleo wa wazi.

Hongera sana Mtibeli. Andiko lako limejaa maarifa na ushauri mwingi sana. Ubarikiwe. Mtoto pia.
 
Ili Mungu akubariki na kukunyooshea njia zako basi fuata na fanya yanayompendeza.

Wakati mwingine vijana hufeli kwa kufanya dhambi na kumchukiza Mungu.

Isingekuwa rahisi kwa kuomba tu, huku unafanya mambo ya ajabu kama ushirikina, wizi na utapeli na hata usinzi. Kijana kamvuta tu binti wa watu kamjaza.

Kama hujapata changamoto basi hesabu ni upendeleo wa wazi.

Hongera sana Mtibeli. Andiko lako limejaa maarifa na ushauri mwingi sana. Ubarikiwe. Mtoto pia.

Nashukuru sana mkuu.
Ni kweli udhaifu wa kibinadamu wakati mwingine unakulazimisha kuasi ili njia yako iwe ngumu
 
Ili Mungu akubariki na kukunyooshea njia zako basi fuata na fanya yanayompendeza.

Wakati mwingine vijana hufeli kwa kufanya dhambi na kumchukiza Mungu.

Isingekuwa rahisi kwa kuomba tu, huku unafanya mambo ya ajabu kama ushirikina, wizi na utapeli na hata usinzi. Kijana kamvuta tu binti wa watu kamjaza.

Kama hujapata changamoto basi hesabu ni upendeleo wa wazi.

Hongera sana Mtibeli. Andiko lako limejaa maarifa na ushauri mwingi sana. Ubarikiwe. Mtoto pia.
Upo sahihi Mkuu.

Sometimes watu wanapata matatizo kwasababu ya kufanya mambo mazuri na mabaya kwa makusudi.

Fanya mema na wema utakuwa wako.

N.b binadamu hatujakamilika lakini haimaanishi tufanye mabaya kwa kusudi.
 
Back
Top Bottom