Hakikisha yafuatayo kabla hujaamua kupata mtoto

Diwani

JF-Expert Member
Oct 25, 2014
2,672
2,697
Kumekuwa na ongezeko kubwa la wanaume na wanawake wenye watoto, ndio ni wanaume na wanawake, na si wakina baba na mama. Kwa sababu, kuwa na mtoto hakukuvishi maana zote za kuwa mzazi moja kwa moja. Kuna kuwa mzazi kwa maana ya kuwa na uzao, yaani watoto na kuna kuwa mzazi kwa maana ya kuwa katka majukumu sahihi ya kulea; japo waleaji huitwa walezi tu, ila unaweza kuwa mzazi na usiwe mlezi, lakini mlezi ni mzazi.

Ulimwengu tulio nao sasa, hususan hapa Tanzania, jukumu la malezi si la jamii nzima kama ilivyokuwa zamani, siku hizi mtoto ni mali ya mzazi husika. Ule wito wa kuguswa na maendeleo ya mtoto wa mtu mwingine umefifia pakubwa sana. Sasa; kabla ya kukileta kiumbe cha Mungu duniani, tathmini na ufanye mambo yafuatayo.

1. Hakikisha upo kwenye mahusiano na mwenza aliyekomaa kihisia, kiakili na kiroho; jukumu la malezi si tu kuwa na mtoto/watoto, hapana malezi yaanzia rohoni, ni jukumu lenye picha ya wito ndani yake. Wito ni pale unapodhani wewe ndiye mtu pekee unayeweza kutekeleza jukumu lililopo mbele yako, na si mwingine. Ili wote muitikie wito wa malezi, ni lazima muwe mmekomaa kiakili; yaani kuweza kutafsiri wito husika.

2. Wekeza kwenye afya yako binafsi, uchumi na elimu ya malezi; jaribu kufikiria pale kiumbe huyu anazaliwa na kukuta afya dhoofu ya mzazi wake, ufanisi wa kuhudumia kiumbe hiki utakuwa mdogo sana, kitu ambacho kinaweza kukufanya ukamuingiza matatani na matatizoni. Siku hizi zipo elimu nyingi za malezi zinazotolewa kupitia taasisi kama shule, dini na mashirika. Chagua na amua kwa hekima.

3. Weka mipango ya muda mrefu kabla ya kiumbe hiko kuzaliwa au kuamua kuzaa; jaribu kutazama baada ya miaka kumi, unamuona wapi mtoto wako anayekaribia kuzaliwa? Wewe kama baba/mama, unataka awe wapi? Ikiwa umewekeza katika mipango ya muda mrefu, hapa ndipo utapata hekima ya kuwekeza taratibu ili kufanikisha lengo lako, kwa mfano kuwa akaunti maaulumu ambayo wewe na mwenzako mnawekeza. Mipango hutoa dira.

4. Punguza kundi la marafiki na jamaa wasio na tija; kwanza elewa maana ya tija. Tija ni maana au faida inayojengeka pale ambapo jambo Fulani hupangwa kufanyika. Penye marafiki hapakosekani ushauri, je kila ushauri unaopokea kuhusu malezi una tija? Yaani una maana kwa ustawi wa familia yako hapo baadae? Kama ndiyo, mtunze aliyeutoa, na vilevile, kundi la wazazi wenzako ndilo liwe marafiki wapya.

5. Chagua vigezo (standards) za malezi ya mwanao; amua kabla na mwenzako, mtataka mtoto alelewe kwenye misingi ipi? Je ni dini? Kikabila? Ikiwa mtachagua mapema, itakuwa rahisi pia kutengeneza maadili ya mtoto, kwa sababu kutakuwa na kanuni maalumu ya kuifuata, si kwamba ataishi tu ilimradi. Hii itamsaidia mtoto kujengeka katika misingi maalumu katika dunia yenye mchanganyiko wa tamaduni nyingi. Lengo ni kumuepusha na maadili yasiyofaa, lakini kwanza, na ajue yafaayo ni yapi.
 
Back
Top Bottom