SoC02 Muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva) unavyoweza kutumika kutatua tatizo la ajira nchini Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

tpaul

JF-Expert Member
Feb 3, 2008
21,818
18,241
Utangulizi
Leo nitaongelea mada inayohusu muziki wa kizazi kipya na jinsi muziki huo unavyoweza kutumiwa kikamilifu kutoa ajira kwa vijana ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana hapa nchini. Lakini kabla sijaendelea mbele, naomba nielezee mkwamo unaosababisha biashara ya muziki huu usipanuke kwa kasi.

Mkwamo wa muziki wa Bongo Fleva
Vijana wengi wanatamani na wameingia kwenye uimbaji wa muziki wa Bongo Fleva. Pamoja na ari hii, wanakabiliwa na changamoto kama vile ukosefu wa vifaa vya muziki, fedha za kurekodia na ubunifu (creativity). Hata wale vijana wachache wanaofanikiwa kurekodi, nyimbo zao zinakosa viwango na ubunifu ili kuvutia makundi yote katika jamii kuupenda na kuununua muziki wao. Mara nyingi vijana na baadhi ya watu wa umri wa kati kwa uchache, ndio wanaosikiliza nyimbo za Bongo Fleva.

Pili, vijana wengi wanaingia kwenye muziki kwa sababu ya kutafuta sifa za muda mfupi zinazopelekea kuwavimbisha vichwa na kuwafanya waanguke kimuziki ndani ya muda mfupi. Mojawapo ya sifa hizo za muda mfupi ni kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na ufuska. Kama mtakumbuka siku za hivi karibuni kuna mwanamuziki mmoja alijiingiza kwenye ufuska na kufikia hatua ya kushtakiwa mahakamani kwa kuvijisha video za ngono mtandaoni.

Kwa ufahamu wangu, haya mambo mawili ndiyo huwaangusha vijana kimuziki na kuwafanya waendelee kutopea sio tu kwenye umasikini lakini pia kwenye uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya na ufuska. Kuna mifano hai ya vijana wawili walikokuwa wasanii wakubwa wa muziki lakini kwa sasa wametumbukia kwenye madawa ya kulevya.

Kati ya hizi changamoto, ukosefu wa ubunifu wa kimuziki ndio chanzo kikubwa cha kuporomoka kimuziki kwa wasanii wa Bongo Fleva. Wengi wao hutunga nyimbo zilizo chini ya viwango na ambazo haziwezi kusikilizwa na watu wa rika zote kwa kuwa zimejaa matusi, kelele, na zinakosa ladha halisi ya kimuziki. Ndio maana baadhi ya nyimbo hufungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Kwa maana hiyo, kiwango kidogo cha ubora wa nyimbo pamoja na ujumbe dhaifu zinaoubeba husaidia kupunguza wasikilizaji na wafuatiliaji (wateja) wa nyimbo za muziki wa kizazi kipya. Ikumbukwe kwamba shabaha kuu ya mfanyabiashara yeyote yule siku zote ni kuhakikisha kuwa anajiongezea idadi ya wateja kila kukicha. Shabaha hii ni kinyume chake kwa wasanii wa Bongo Fleva. Badala ya kujitahidi kuongeza wateja, wanawapunguza kwa lazima kwa kulazimisha kutunga nyimbo zenye ujumbe wa matusi na ambazo hazielimishi. Nimekuwa nikijilazimsha kusikiliza nyimbo za kizazi kipya (kwa sababu za kiutafiti) na kubaini hazina mafundisho wala hazibebi ujumbe wowote wenye tija unaoweza kusikilizwa na mtu mtu mzima mwenye akili timilifu.

Utatuzi wa changamoto na kujiajiri kupitia muziki
Nyingi ya changamoto hizi zinaweza kutatuliwa bila kutumia hata senti moja. Ni uamuzi tu unaotakiwa kuchukuliwa na wahusika ili waanze kujiajiri kikamilifu kupitia sanaa hii ya muziki.

Mosi, vijana wanaoimba muziki na wanaotamani kuijiingiza kwenye muziki huu sharti wabadilike na kuanza kutunga nyimbo zenye mvuto kwa jamii na zitakazosikilizwa na watu wa rika zote. Utunzi wa nyimbo za kingono tu umepitwa na wakati. Kuna mambo mengi ya kuimba katika nchi hii yanayohusu uchumi, elimu, uwajibikaji, maisha ya kawaida kwa ujumla, nk. Ni afadhali hata wangekuwa wanatunga nyimbo za kimapenzi kama watunzi wa zamani walivyokuwa wanatunga. Nyimbo hizo za kale bado zipo na watu wa rika wanapenda kuzisikiliza. Hata mtu ukiwa na watoto wako unaweza kuzisikiliza bila wasiwasi. Kwa mfano, ukisikiliza wimbo huu wa jabali la muziki, Mbaraka Mwinshee utaukubali sana:


Chanzo: Mtandao

Pili, vijana hawa, kama nilivyogusia hapo awali, wanakabiliwa na tatizo la mtaji wa kurekodi na kununua vyombo vya muziki (kwa wale wachache wanaoweza kupiga vyombo). Hivyo, naomba serikali iwaangalie kwa jicho la huruma iwaondolee kodi kwenye vyombo vya muziki na pia iwaondolee tozo kwenye mauzo ya muziki, kama motisha ya kuwawezesha kujiajri kupitia muziki. Serikali haitapungukiwa chochote ikiwa itaamua kwa dhati kabisa kuwaunga mkono vijana kwa kuwapa unafuu wa kodi na tozo. Huwezi kumkamua ng’ombe pasipo kumlisha kwani kuna hatari ya kumkamua hadi damu na kumuua.

1662315762259.png

Mfano wa ng’ombe anayekamuliwa bila kulishwa
Channzo: Mtandao
Tatu, kumekuwa na tabia mbaya kwa baadhi ya wauza muziki kurudufisha kazi za wasanii waziwazi bila kuchukuliwa hatua zozote kwa mujibu wa sheria. Kurudufisha kazi ya muziki ya msanii (plagiarism) bila idhini yake ya kimaandishi ni kosa kisheria. Wasanii wamekuwa wakinyonywa kupitia urudufishaji kwa muda mrefu, hivyo kuwafanya wasinufaike na kazi zao za muziki. Kitendo hiki huwavunja moyo vijana ambao wanegependa kujiingiza kwenye biashara ya kimuziki hivyo kuongeza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana. Naomba wizara inayohusika na masuala ya muziki imulike tatizo hili kipekee kwani vijana wananyonywa sana kupitia urudufishaji wa kazi zao kinyume cha sheria.

Nne, kuendesha matamasha ya muziki ni njia nzuri ya kujipatia fedha papo kwa papo bila kutumia mtaji mkubwa. Wasanii hawatakiwi kutegemea kurekodi muziki tu bali wanapaswa kuendesha matamsha ya muziki kote nchini ili kujiongezea kipato. Kwa mfano, iwapo wasanii kadhaa wataamua kuungana na kuendesha tamasha walau moja tu kwa kila mkoa kwa Tanzania nzima watafanikiwa kuvuna makadirio ya chini ya Tsh 20,000,000 kwa kila tamasha, kwa mikoa yote 26 watavna jumla ya Tsh 520,000,000. Hizi fedha si haba zitawasaidia kujipanua kimuziki na kutoa ajira kwa vijana wenzao wa kitanzania.

Tano, wasanii kama raia wengine, nao wanahitaji kuwa na umoja madhubuti utakaosaidia kutetea maslahi yao ya kimuziki kwani wahenga walinena: Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Ipo haja kwa wasamii kupendana na kushikamana ili waweze kupambania sio tu haki za msingi bali maslahi ya kimuziki pia. Tatizo la sanaa ya Bongo Fleva ni kwamba kuna wasanii wengi wanaofanya muziki pekee yao kwa muda mrefu lakini hawatoboi. Natumia fursa hii kuwapongeza wanamuziki wawili wakubwa hapa nchini waliofikiria wazo la kuwaunganisha wasanii katika makundi makubwa mawili ili kuwaongezea nguvu. Kitendo hiki kimeongeza umoja na uwepo wa sauti moja inayotetea maslahi ya wasanii.

Hitimisho
Kwa maelezo haya mafupi, ni wazi kwamba endapo sanaa ya muziki wa kizazi kipya itatiliwa maanani, inaweza kuwa mkombozi wa ajira kwa vijana hivyo kupunguza wigo wa tatizo la ajira nchini Tanzania. Ni jukumu la kila mdau wa muziki kuhakikisha kuwa muziki wa Bongo Fleva unastawi na hivyo kutoa ajira kwa maelfu ya vijana wanaohitimu masomo na kukosa ajira.

Nawasilisha.​
 
Ndugu wadau wa JF naomba kura zenu kwenye uzi huu, naona mpaka sasa bila bila. Naomba walau kura moja nisiwe kama Prof Wajackoya aliyepata sifuri katika vituo vingi vya kupigia kura.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom