Huyu dereva wa lori si inatakiwa akabiliwe na kosa la kuua (sio kuua bila kukusudia)? Maana kama alijua gari ina matatizo ya brakes na bado akalipeleka barabarani, basi Tanzania tuna hatari kubwa mno.
Watu 15 wafa katika ajali Mbeya
*Yumo askofu wa Wasabato
Brandy Nelson na Hawa Mathias, Mbeya
WATU 15 wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa akiwamo Askofu Mkuu wa kanisa Wasabato Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, William Mtani baada ya lori kuligonga kwa nyuma basi dogo la abiria Toyota Hiace maarufu kama kipanya katika eneo la Kinyala Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya.
Waliokufa katika ajali hiyo na majina yao kutambuliwa ni pamoja na Katibu wa kanisa hilo la Wasabato Golden Mwangwilima, kondakta wa Kipanya, Friday Siwakwi (23) mkazi wa Mwanjelwa jijini Mbeya, Salome Mgala mkazi wa Ihumwe jijini Mbeya, Atupakisye Sege, Salum Ramadhani, Frank Mwasege, Hussein Amani, Elizabeth Mwakalukwa, John Poles, Andrwe Mwalukama na wengine wanne bado majina yao hayajatambulika.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni pamoja na Veronika George, Lucy Ndenga, Upendo Isaya, Amani Mwasanga, Hezron Masawe, Amani Salehe ambao wote wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na dereva wa Hiace, Remijo John (41) ambaye amelazwa katika Hospitali teule ya Ifisi iliyopo Mbalizi nje kidogo ya Jiji la Mbeya na hali zao zinaendelea vizuri.
Akielezea tukio hilo dereva wa Lori, Elipamphrey Samky mkazi wa jijini Dar es Salaam alisema ajali hiyo ilitokea saa 12:00 juzi baada ya kushindwa kufunga breki kutokana na gari hilo kuwa na matatizo ya breki wakati mbele yake kulikuwa na basi la abiria lililokuwa linaingia barabarani kutoka kituoni.
�Baada ya kuona Hiace inaingia barabarani na gari yangu ilikuwa na tatizo la breki nilipoonyesha ishara ya hatari kwa kuwasha taa ya kuwa gari yangu haiwezi kusimama, lakini dereva wa Hiace aliendelea kuingia barabarani ndipo nilipomgonga kwa nyuma,�alisema.
Alisema magari yote mawawili yalikuwa yanatokea barabara ya Tunduma ambapo yeye alikuwa amepakia matofari aliyoyatoa wilayani Mbozi kuyapeleka eneo la Kwa Mama John, jijini Mbeya ndipo alipokutana na ajali hiyo katika eneo hilo.
Naye dereva wa kipanya, Remijo John akiwa katika Hospitali teule ya Ifisi alisema anachokumbuka ni kishindo tu na baada ya kupata fahamu aliona kuna lori ambalo limeanguka lakini alikuwa hajui kama ndilo lililomgonga mpaka alipoambiwa na watu waliompeleka hospitalini hapo.
Alipohojiwa kama aliliona lori hilo nyuma yake alisema hakuliona kwani yeye alikuwa anatoka katika kituo kupakia na kushusha abiria akiingia barabarani kuendelea na safari ndipo ghafla alisikia kishindo mara kapoteza fahamu na baadaye alipopata fahamu akaona lori lililoliganga basi lake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova alisema baada ya lori hilo kuigonga Hiace liliseleleka umbali wa meta 350 na kuanguka upande wa pili wa barabara umbali wa mita 20 wakati Hiace ilipogongwa iliburuzwa umbali meta 50 na baadaye likarushwa pembene mwa barabara.
Kova alisema waliokufa papo hapo katika ajali hiyo ni saba na wanne walifia njiani walipokuwa wakipelekwa hospitalini watatu walifariki jana usiku walipokuwa hospitalini wanapatiwa matibabu na mmoja amefariki dunia leo asubuhi katika hospitali ya Rufaa Mbeya.
Muuguzi wa zamu aliyejulikana kwa jina moja la Zambi alisema kuwa majeruhi hao wanaendelea vizuri lakini hawataweza kuruhusiwa kwa sasa.
Mkoa wa Mbeya umekuwa na matukio kadhaa ya ajali ndani ya mwaka huu wa 2007 na kwambva mpaka sasa jumla ya ajali tano na kusababisha vifo vya watu wengi. Novemba 8, mwaka huu lori aina ya Scania liliparamia nyumba na kusababisha vifo vya watu watatu.
Naye Gasper Andrew, anaripoti kutoka Singida wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi ya Kasasida iliyoko Kijiji cha Kisasida katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida, wamefariki dunia na abiria wengine 17 wamejeruhiwa vibaya baada ya gari hilo kushindwa kupanda mlima wa Kisasida kiasha kuacha barabara na kupinduka.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Celina Kaluba alisema ajali hiyo imetokea juzi jioni saa 12.00 jioni wakati abiria hao ambao wengi wao ni wafanyabiashara waliokuwa wanatokea mnadani.
Aliwataja wanafunzi hao waliofariki kwenye ajali hiyo kuwa ni Swaa Ally (13) na Juma Hamisi (13) na wote ni wanafunzi wa darasa la tano.
Kamanda Kaluba, alisema chanzo cha ajali hiyo ni gari hilo kukosa breki hivyo kumfanya dereva kushindwa kulimudu na hivyo kupinduka.