Utaratibu wa njia tatu umesababisha vifo 11
MBUNGE JIMBO LA SAME MASHARIKI
na Irene Mark na Rahel Chizoza, Dodoma
MBUNGE wa Same Mashariki, Anne Malecela (CCM), ameitaka serikali kuweka wazi idadi ya vifo vilivyotokana na ajali zinazobabishwa na utaratibu wa njia tatu jijini Dar es Salaam.
Aidha, mbunge huyo alisema hakubaliani na utaratibu huo uliowekwa na serikali kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari na foleni katikati ya jiji hilo na kwamba haujasaidia kupunguza tatizo.
Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohamed Abood, katika majibu yake, alisema baada ya kuanza kwa utaratibu wa njia tatu, foleni za magari zimepungua katika jiji hilo.
Aidha, alibainisha kuwa kati ya Mei na Oktoba 29, mwaka huu, jumla ya ajali 107 zilizosababisha vifo vya watu 11 zilitokea baada ya kuanza kwa utaratibu wa njia tatu kutokana na mwendo kasi na uzembe wa madereva kutofuata sheria za barabarani.
Abood alisema utaratibu wa njia tatu hasa nyakati za asubuhi na jioni, umezoeleka jijini Dar es Salaam na kumtaka mbunge huyo kuondoa hofu, huku akiwaomba madereva na watumiaji wengine wa barabara zinazohusika na utaratibu huo kuwa makini.
Alisema jumla ya sh bilioni 10 zimetengwa na serikali kwa ajili ya kuboresha utaratibu huo kwa muda wakati wakitizama namna ya kuondoa tatizo la msongamano na foleni za magari.
Hata hivyo, majibu hayo hayakumridhisha mbunge huyo na kueleza kuwa utaratibu wa njia tatu haujazoeleka wala kusaidia kupunguza foleni badala yake umeongeza idadi ya ajali na vifo huku akiitaka serikali kubuni mbinu mpya.
Mwanzo mwa mwaka huu, Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliagiza uwepo utaratibu wa njia tatu katika baadhi ya barabara jijini Dar es Salaam, ili kupunguza msongamano na foleni, hasa wakati wa asubuhi na jioni.
Barabara zinazohusika na utaratibu huo ni Morogoro na Ali Hassan Mwinyi.