mbaroni kwa kumzomea Mkapa
Na Mwandishi Wetu, Masaki
VIJANA watano wa jijini Dar es Salaam wanashikiliwa na Polisi kwa madai kwamba walimzomea Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa kwa kumwita kuwa ni fisadi.
Tukio hilo la aina yake limetokea jana saa 11 jioni,katika maeneo ya Masaki karibu na kituo cha Daladala cha Masaki ambapo vijana hao kama kawaida yao walikuwa kijiweni wakipiga stori zao.
Imedaiwa kuwa kundi hilo la vijana wakiwa eneo hilo la stendi ya daladala walianza kupiga kelele baada ya kuona msafara wa Mkapa ukipita n kuanza kuzomea kwa mayowe wakisema fisadi huyo!!!, fisadi huyo!!!.
Tukio hilo lililoshtua watu waliokuwepo karibu na kituo hicho ambapo baada ya muda mfupi polisi walifanya msako mkali kituoni hapo na kufanikiwa kuwasomba vijana watano lakini wengine baada ya kuona hivyo walitimua mbio wakielekea kusikojulikana.
Rais huyo mstaafu amekumbwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi kwa siku za karibuni ingawa mara zote amekuwa mkimya huku wananchi vikiwamo vyama vya upinzani vikimtaka azijibu tuhuma hizo.
Katika mkutano wa Bunge lililopita mjini Dodoma alishambuliwa na Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro akisema yeye na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona walinunua mgodi wa Mawe wa Kiwira kwa sh. milioni 70 wakati thamani yake ni sh. bilioni 4.
Katika madai hayo Kimaro alisema kwamba viongozi hao wawili walitumia nafasi zao za uongozi kuiingiza nchi katika matatizo makubwa ya kiuchumi. Akasema kwamba ilikuwa wanunue mgodi huo kwa sh. 700 lakini hadi sasa wamelipa sh. milioni 70 tu.
Mkapa pia anakabiliwa na tuhuma za kutumia nafasi yake alipokuwa Ikulu kufanya biashara ikiwa ni pamoja na kupata mkopo wa Sh milioni 500 benki ya NBC ili awekeze katika biashara zake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum Dar es Salaam, Jamal Rwambow alipopigiwa simu kuelezea tukio hilo alisema kuwa yupo kwenye msafara na ataelezea kwa undani taarifa hizo pindi atakapozipata.
" Nipo kwenye msafara na taarifa hizo bado sijazipata nitakapozipata nitaelezea kwa undani,"amesema Rwambow alipopigiwa simu leo asubuhi.
source:
http://www.darleo.co.tz/kurasa.php?soma=habari&habariNamba=795