Mkapa alipe kodi
2008-05-04 10:46:21
Na Simon Mhinda, Cynthia Mwilolezi, PST, Arusha
Mbunge wa Jimbo la Karatu, (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa, amesema Rais wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, anatakiwa kulipa kodi ya pango kwa serikali kwa sababu aliitumia Ikulu kama ofisi yake ya kufanyia biashara.
``Nasema hivi sababu nina ushahidi, na siropoki tu kwa sababu za kisiasa, hivyo Mkapa anatakiwa kulipa pango la ofisi ya serikali, kutokana na kufanya Ikulu kama ofisi yake ya biashara`` alisema Dk. Slaa.
Aliyasema hayo jana wakati akitoa mada kuhusu nafasi ya mbunge, wananchi na ushirikiano kitutendaji, kwenye mdahalo wa Ulingo wa Maendeleo Mkoani Arusha, ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la ANGONETI lililoko Mkoani hapa.
Alisema kuwa Mkapa aliandika barua akiwa madarakani kuomba fedha kwa anuani ya Ikulu kama mjasiliamali na sio Rais.
Dk. Slaa alisema kuwa hali hiyo ni hatari kwa uchumi wa nchi, kwani viongozi wa wanafanya kazi kwa manufaa binafsi.
``Halafu wanatudanganya wananchi kuwa nchi ya Tanzania maskini, si kweli, kama maskini wawekezaji wasingekuja kuwekeza... hiki ni kiini macho ili wananchi wasiwe na ufahamu`` alisisitiza Dk. Slaa.
Aidha, aliwataka wananchi kuwa makini katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, ili kuepuka kuchagua Marais wajasiliamali ambao watatumia madaraka yao kujinufaisha.
Aidha, alizitaka taasisi na mashirika ya watu binafsi kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuhoji maendeleo yao, bila kuogopa mtu yoyote kwani kwa kufanya hivyo itasaidia nchi kuondokana na ufisadi.
Pia alisema wananchi wengi hawajui wajibu wa wabunge wao na wengine huishia kuwaomba fedha za matumizi.
Dk.Slaa pia alisema uchumi wa nchi sasa upo kwenye mifuko iliyotoboka kwani viongozi wachache wamekuwa watumia vibaya madaraka na kujilimbikizia mali isivyo halali.
``Ili tuondokane na tatizo hili tushirikiane kuwafichua mafisadi kwa kutafuta nyaraka muhimu ili tukiwaeleza watu isiwe majungu`` alisema Dk. Slaa.
Naye Ofisa Mifugo Mkoa wa Arusha, Bw.Hargeney Chitukulo akisoma hotuba ya ufunguzi mdahalo huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Arusha, Bw. Isidore Shirima alisema kinachosababisha maendeleo ya nchi kurudi nyuma ni pamoja na kutegemea zaidi wafadhili.
Wakati huo huo, Mwandishi Simon Mhina anaripoti kwamba Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salamaa Mhashamu Methodius Kilaini, amemtaka Rais Benjamin Mkapa, na mkewe Anna kujibu tuhuma za ufisadi bila kusita kwa vile Watanzania wengi wana shauku ya kusikia neo kutoka kwao.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, kiongozi huyo alisema ni kweli usiopingika kwamba Rais mstaafu hawezi kujibu kila tuhuma inayotolewa barabarani au kwenye mikutano ya hadhara, lakini akasema kwa vile tuhuma hizo zimetolewa kwenye chombo muhimu kama Bunge haitakuwa vyema iwapo Bw. Mkapa atakaa kimya bila kutoa maelezo.
Askofu Kilaini alisema huenda taarifa iliyotangazwa na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kuwa Serikali inachunguza tuhuma hizo, ndizo zimemfanya Bw. Mkapa kukaa kimya hadi sasa.
Hata hivyo, alisema Watanzania wana shauku ya kusikia neno kutoka kwake.
``Nimesikia kwamba Waziri Mkuu amesema tuhuma hizo zitashughulikiwa, itakuwa jambo la busara mno iwapo atatumia fursa hiyo kutoa maelezo yake kwa nia ya kujisafisha,`` alisema.
Askofu Kilaini alisema kwa vile hizo ni tuhuma zinaweza kuwa za kweli au uongo, hivyo ni vema zikatolewa ufafanuzi, ili Watanzania waweze kuchuja pumba na mchele.
Alionya kuwa tuhuma hata kama ni za uongo zisipokanushwa katika utaratibu unaotakiwa, zinaweza kuhesabika kuwa ni za kweli.
Askofu Kilaini amewamwagia sifa wabunge wa CCM kwa kuanza kujadili hoja za kitaifa, bila kujali maslahi ya kisiasa kama ilivyozoeleka.
``Kwa kweli sasa siasa ni tamu, kitendo cha Mbunge wa CCM kumshutumu waziwazi Mwenyekiti wa zamani wa Chama chake, tena aliyekuwa Rais kinaashiria kuwa sasa Bunge halitaki mchezo,`` alisema na kuongeza ``Hivi ndivyo inavyotakiwa iwe.
Wabunge wawe huru kujadili mambo ya kitaifa, bila kufungwa kamba na mizengwe ya vyama vyao,��
Katika Kikao cha Bunge kilichopita, Mbunge wa Vunjo (CCM) Bw. Aloyce Kimaro, alimshutumu Bw. Mkapa na mkewe pamoja na Bw. Yona kwa kujiuzia kwa bei ya kutupa mgodi wa Kiwira.
Mgodi huo unakadiriwa kuwa na thamani ya Sh. bilioni nne lakini Bw. Mkapa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Daniel Yona, walijiuzia kwa Sh. milioni 70.
Askofu Kilaini alisema Kanisa linapenda watu wanaosema ukweli na daima tabia hiyo ikiendelezwa taifa litasimamama mahali pazuri.
Alisema utamaduni huo mpya ulioanzishwa na wabunge wa CCM, utakiletea heshima kubwa chama chao.
Alisema Watanzania walishaanza kukata tamaa, kwamba wabunge wa CCM wanakwamisha mambo mengi yenye maslahi kwa Taifa kwa sababu za kiitikadi, lakini sasa wamejivua aibu hiyo.
Aliwataka wabunge hao kuendelea kujikakamua kwa vile mwenendo mpya waliouonyesha katika kujadili mambo mbalimbali utawanufaisha Watanzania na CCM pia.
Kiongozi huyo alisema ukiachilia mbali Bw. Mkapa, wengine waliotajwa kama Bw. Yona hawana sababu yoyote ya msingi ya kuendelea kukaa kimya.
``Kwa upande wa Mkapa wanaweza kuzungumzia mambo ya itifaki, labda. Lakini hawa wengine nao wanakaa kimya kwa sababu gani?`` alihoji.
SOURCE: Nipashe