Mkapa anapochuuzwa na kina Hiza
Nkuzi Kwanzi
KWA aliyesoma utumbo wa mtu anayetapatapa kwa kujifanya msemaji wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, aitwaye Tambwe Hiza, atakuwa amesikitika na kuwashangaa Mkapa na Hiza.
Licha ya utetezi wake kuwa mfu na usio na mashiko, ni tahadhari kwa Mkapa kuwa kama hatakuwa makini, waganga njaa watamtumia wakijionyesha wanampenda, kumtetea na kumjali ilhali ukweli ni kwamba wanapaza sauti ili awasikie na awatupie makombo.
Hakuna mtu aliyetapatapa kipindi hiki kama Hiza. Alianza na kuvizushia vyama vya upinzani huku akijirejesha kundini alikokuwa kwa kulamba matapishi yake.
Hakujua kuwa CCM waliishaistukia janja uchwara ya wachumia matumbo na matapeli wanaohama hama vyama kukidhi njaa zao.
Kutokana na usuhuba na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, Hiza na makapi wengine walifinyangiwa ofisi na idara ya uani ya propaganda!
Jaribio la kuuza machukizo ya kundi hili wakati wa kutapatapa kutetea bajeti mikoani, waliishia kuzomewa.
Hiza hakuchoka kuusaka mkate na kuridhisha wasitiri wake. Aligombea ujumbe wa NEC na kubwagwa kama taka. Ameona hii janja ya nyani kutofanikiwa, amedandia utetezi mfu wa Mkapa.
Kwa mtu mwenye akili timamu na hekima na anayemjua Mkapa vizuri na zigo la madhambi yake, hawezi kupoteza muda wake kutaka kufanya muujiza wa kumsafisha.
Hiza ni nani akilinganishwa na vigogo kama Daudi Mwakawago, Jaji Mark Bomani, Joseph Butiku na watu wengine wenye majina na waliomuonya Mkapa kuwa anachojaribu kufanya ni kujichimbia kaburi na hakistahili kufanywa na mtu wa nafasi yake?
Watetezi wa Mkapa wanamdhalilisha sawa na wapambe wa utawala wa sasa wanavyousukumizia motoni. Hakuna kitu kibaya kama kumdanganya mtu. Maana ni kumfanya ********.
Kibaya zaidi ni kudanganya nawe ukajidanganya. Adui yako kweli muombee njaa. Hiza anajifanya kama Mtanzania aliyekuwa ughaibuni wakati ukweli kuhusu Mkapa ukiwekwa njia panda ili kila mpita njia ajionee na kuhukumu.
Hiza ataleta jipya gani iwapo akina Kingunge, Makamba, Mwanri, Warioba wamechemsha? Hiza anajua nini zaidi ya kuendeshwa na mkuno wa njaa tumboni?
Bahati mbaya CCM nayo imekula hasara. Maana kama kuna fasheni inayotumika kuiibia na kuitapeli si nyingine ni watu kuhama vyama au taaluma zao tayari kupewa kazi ya kuzoa uchafu wake wasiuweze. Dawa ya yote haya ni kusafisha nyumba yako na kuwa msafi.
Hiza asiyejua hata kujenga hoja zaidi ya kulalamika na kusifia, ana msaada gani kwa Mkapa iwapo ameshindwa kujisaidia mwenyewe kiasi cha kusaidiwa kwa njia ya kudhalilishwa? We Hiza we, tafuta njia ya uhakika ya kuishi na siyo salata na urongo.
Hata bata bingwa wa kuchokoa taka huwa halali chooni wala kujisifia matendo yake. Yeye kama hayawani hana jinsi. Hayo ni majaliwa yake. Nepi siku zote ni nguo ya aibu si vizuri kujisifia unepi wala fisi mpenda mizoga hajisifii ufisi wake. Hiza ni mahuluku wa ajabu anayeonekana kuendeshwa na njaa kiasi cha kuvuka mipaka!
Na hili inabidi liwe somo kwa watawala wasio waadilifu. Ufisadi unamtoa mtu utu na heshima kiasi cha kutetewa na majambazi wa kisiasa. Tangu lini kuku akamtetea mwewe hata ahaidiwe kutoliwa vifaranga vyake? Visipoliwa vyake vya wenzake vitaliwa. Je, kuna usaliti mchafu kama huu?
Mkapa kwa kutetewa na vyangu wa kisiasa, anazidi kumomonyoka na kuonekana mhalifu japo hataki aeleweke hivyo. Hakanushi wala hata kuwakemea kimya kimya huko wanakokutana kama wanakutana.
Je, Mkapa anawatuma akina Hiza kufanya kazi chafu kwa ajili yake au wanajikomba na kujipendekeza ili lau waambue makombo? Kama ni mkakati, basi umeshindwa hata kabla ya kufanyiwa kazi.
Hivi nani anadhani Watanzania ni majuha na wendawizimu kumsikiliza au kumwamini kiumbe asiyejiamini wala kuamini anachosema? Nani mpuuzi amuamini mkaanga sumu na majungu.
Hiza anadhani kuwa alipokuwa Mbeya hivi karibuni alijivua nguo hadharani kwa kukiri kuwa alikuwa mpika majungu mkuu alipokuwa CUF? Je, ameokoka lini kuacha kilema hiki cha akili hadi tumwamini?
Mkapa, kwa viwango vyovyote ni msomi, hata kama elimu yake aliitumia vibaya. Tangu lini msomi akatetewa na mbumbumbu mzungu wa reli? Ni ajabu kipofu kumtetea mwenye macho au shehe kutetewa na mlevi! Hii inazidi kumfanya Mkapa aonekane si Mr Clean kama tulivyoaminishwa.
Wazungu husema show me your friends I will tell you who you are. Na Mkapa japo amekataa kujitetea, bado hajahukumiwa kiasi cha kutetewa na vibaka na wasaka mkate. Ni aibu na hatari kwake.
Watu wenye majina yao, japo walipotea njia kama akina Jaji Joseph Warioba walijaribu wakazomewa na kusutwa, sasa wamenywea itakuwa Hiza!
Aliponiacha hoi Hiza ni pale alipowasingizia marehemu. Anadai Oscar Kambona alikuwa mwanazuoni! Pia anadai alipomtuhumu mwalimu JK Nyerere eti Mwalimu alinyamaza! Uongo, tena unaonuka.
Kama Hiza kaishiwa hoja afunge mdomo. Kwani Nyerere alieleza bayana kuwa hana tatizo na madai ya Kambona bali anachoomba auleze umma na vyombo vyake zilipo na zikiwapo basi wazichukue.
iza anachokifanya ni kujenga mazingira mazuri ya kuweza kujuana na Mkapa (kama atakuwa naye ameishiwa kiasi hicho) kwa kujifanya ni mtetezi wake. Tumewaona wengi hata waliofanya utapeli kwa kusingizia walitekwa na CCM kumbe ilikuwa ni kuwachuuza wenzao.
Ila tunakokwenda mchezo huu ni hatari. Maana ni usaliti. Wanachofanya ni kujipaka mafuta halafu wanakwenda kupita kati kati ya moto.
Kwa mtu anayeunga mkono mambo ya Mkapa na biashara zake za Ikulu iwe ni kwa njaa zake au upenzi wake au kwa vile alinufaika chini ya utawala wake, ni adui wa umma.
Nafasi haitoshi. La muhimu ni wananchi kuanza kuongeza idadi ya maadui wao kama umma ambapo hili genge jipya linalotumiwa au kujipandikiza kutetea uoza na kuhujumu harakati zao inabidi liangaliwe kwa jicho baya.
nkwazigatasha@yahoo.com
www.mpayukaji.blogspot.com