Hebu angalia Tanzania Daima ambaoa katika kichwa chao cha habari sehemu ya chini wamesema, Sumaye amtetea Mkapa, lakini ndani ya habari yenyewe kuna sentesi inayosema "mimi si mtoto wake, siwezi kumsemea". Nilikuwapo katika huo mkutano na niliongea na Sumaye baada ya mkutano, akasema sasa hivi ukimtetea mtu unaweza kupata matatizo makubwa, ni bora ukajitetea mwenyewe na ukawa mkweli hata kama unamuudhi mwenzako. Kwa ujumla Sumaye alitetea SERIKALI YA MKAPA AKIWA WAZIRI MKUU WAKE." na alipoulizwa kuhusu tuhuma za viongozi akiwamo Mkapa, alisema, "UNATAKA MIMI NIMSEMEE? ALISHASEMA KULE LUPASO, LAKINI KWANI MIMI NI MTOTO WAKE NIMSEMEE?" sasa hao wanaoandika amemtetea wapi kuna quotation? Mbona quotation zote wameandika serikali ya awamu ya tatu blah!!! Blah!!!
Sumaye: Urais basi
na Martin Malera
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema hana mpango wa kuwania tena nafasi ya urais hata ifikapo mwaka 2015, na badala yake anataka kuwa mtu wa msaada kwa nchi za Afrika, ili ziweze kujikwamua katika lindi la umaskini.
Sambamba na hilo, Sumaye amesema katika kipindi alichokuwa madarakani kwa nafasi yake ya uwaziri mkuu, hakuwahi kufungua akaunti nje, kama ilivyo kwa baadhi ya viongozi waliopo madarakani hivi sasa.
Sumaye alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Protea, zamani Court Yard, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulikuwa na lengo la kutangaza hatua yake ya kulisamehe gazeti la Tanzania Leo, lililowahi kuchapisha taarifa kuwa Sumaye anamiliki kiasi cha dola za Marekani trilioni 10 kwenye akaunti nje ya nchi.
Akifafanua azima yake ya kutowania tena urais, Sumaye alisema hatua yake ya kwenda kusoma, imetafsiriwa vibaya na baadhi ya watu kuwa anataka na anajiandaa kuwania tena kiti hicho ifikapo muda huo, ambapo Rais Jakaya Kikwete, atakuwa amemaliza mihula miwili, iwapo atachaguliwa tena mwaka 2010. Mwaka 2005 Sumaye alikuwa mmoja wa wana CCM waliowania nafasi hiyo.
"Nilipoamua kwenda kusoma, lengo langu halikuwa kuwania urais, bali ni kutaka kuwa mtu wa msaada kwa nchi za Afrika, hasa katika harakati za kujikwamua kiuchumi kupitia taasisi nitakayoianzisha baadaye.
"Hebu fikiria, mwaka 2015, Rais wangu Jakaya Kikwete atakuwa anamaliza muda wake, yaani miaka kumi ijayo kutoka sasa, mimi niwanie tena urais, haiwezekani. Nataka kuwa mtu muhimu kwa nchi za Afrika kwa lengo la kusaidia mapambano dhidi ya umaskini," alisema.
Akizungumzia taarifa za gazeti kuhusu kumiliki sh trilioni 10 nje ya nchi, Sumaye alisema katika kipindi chote cha miaka kumi alichokuwa madarakani kama waziri mkuu, hajawahi kufungua akaunti yoyote nje ya nchi, kwani hakuona sababu ya kuwa na akaunti hiyo kwa wakati huo.
Hata hivyo, alisema alipokuwa masomoni, nchini Marekani katika Chuo Kikuu cha Havad, alifungua akaunti nje iliyopo hadi sasa, ili kumwezesha kuweka fedha alizokuwa akizitumia kwa ajili ya masomo na huduma nyingine alipokuwa nje.
"Sijawahi kuwa na akaunti nje, sikuona sababu ya kuwa nayo na ndiyo maana nilishtuka sana kusikia gazeti la Tanzania Leo limeniandika eti namiliki akaunti ya dola trilioni 10 nje ya nchi. Hizi ni hela nyingi sana, hata tajiri kama Bill Gates sijui kama anazo, sijui hata hao walioziandika kama wanajua wingi wake, na ndiyo maana niliwafikisha mahakamani, nikataka wanilipe sh bilioni 20 tu, wakasema, hizo nyingi sana, ila dola trilioni 10 waliona ni fedha ndogo za kumiliki mtu kama mimi," alisema Sumaye.
Alisema aliamua kulifikisha gazeti hilo mahakamani ili kusafisha jina lake, hasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wameamka, kiasi cha kufikia hatua ya kuwarushia mawe watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi wanapopita mitaani.
Alisema katika kipindi chote alichokuwa waziri mkuu, alijitahidi kuwa mvumilivu, lakini mara baada ya kumaliza muda wake, hatakubali kuona akichafuliwa jina lake alilolijenga kwa muda mrefu na kwa gharama kubwa.
Kuhusu shutuma za ufisadi wa maamuzi ya mikataba mibovu iliyoliingiza taifa katika hasara kubwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, Sumaye alisema hajutii maamuzi yote waliyofanya wakati huo, kwani kila uamuzi uliofanywa ulikuwa na lengo zuri na kuongeza kuwa chini ya Mkapa walikuwa wakichapa kazi na nchi ilisonga mbele.
"Uamuzi wa ununuzi wa rada, ndege ya rais na mengine yote yalikuwa sahihi. Kwa mfano ununuzi wa rada, ilifika mahala ndege za nje zilitishia kuacha kutua, hali ilikuwa mbaya, lakini sasa hali ni nzuri na wote tunaona pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
"Hata hivyo, pamoja na maamuzi mazuri tuliyoyapitisha, kama kuna watu waliojipatia fedha kwa njia zisizo halali kutokana na mikataba hiyo, wachukuliwe hatua, lakini hatuwezi kusema kwamba tulifanya uamuzi mbaya," alisema Sumaye.
Alipotakiwa kuelezea tuhuma za Mkapa kama msadizi wake, Sumaye alisema: "Mimi siwezi kumzungumzia Mkapa, maana mimi si mtoto wake, ila mkitaka niizungumzie serikali yake kama taasisi hiyo naweza kuwa na maelezo yake. Hata hivyo si amejibu, lakini bado watu mnataka ajibie Dar es Salaam… mimi nadhani amejibu," alisema Sumaye.
Aidha, Sumaye, ambaye sasa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), pia alikataa katakata kutoa tathmini ya uongozi wa Rais Kikwete, kwa madai kuwa haikuwa sehemu ya elimu yake aliyoipata hivi karibuni nchini Marekani, na kuwa kufanya tathmini ukiwa nje ni ngumu kidogo.
Pamoja na kukubali kulisamehe gazeti hilo ambalo hata hivyo halipo mitaani kwa sasa, Sumaye alisema linalipa fidia ya sh milioni 100, na fedha hizo atazitumia kwa ajili ya kuchangia Jukwaa la Wahariri, ili kutoa semina kwa waandishi wa habari katika kusaidia kujenga maadili ya kazi hiyo, kuepuka kile alichokiita habari za kuingizwa mkenge.
Pia alisema fedha nyingine atazitoa kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa jamii ya Kimasai, ambao wengi hushindwa kuendelea na masomo kutokana na wazazi wao kushindwa kuwalipia karo za shule na huduma nyingine.
"Kwa kweli hata kama ingetokea muujiza wakanilipa sh bilioni 20, ningefungua kituo cha watoto yatima, baada ya kukata gharama zangu za uendeshaji wa kesi," alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Leo Limited, Venance Rwegoshora, alisema wameamua kumwangukia Sumaye baada ya kujiridhisha kwamba habari zilizochapishwa katika matoleo yao mawili namba 341 la Aprili 7, 2006 na Aprili 13 mwaka huo, zilikuwa za uongo, za kutungwa, za kupotosha na zisizo na msingi wowote.
"Sisi Tanzania Leo tunaamini kuwa kuomba radhi kwetu hakuwezi kufuta kabisa machungu na madhara aliyoyapata Sumaye na tunaelewa kwamba taarifa pekee kwa vyombo vya habari, haziwezi kurudisha heshima na hadhi iliyoharibiwa na gazeti letu. Hata hivyo, tunaomba radhi kwake kwa dhati kabisa," alisema Rwegoshora.
umaye amtetea Mkapa
2008-06-02 09:39:20
Na Mashaka Mgeta
Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, ameibuka na kuutetea utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, kuwa uliharakisha maendeleo ya nchi na watu wake.
Kauli hiyo ya kwanza kutolewa na Bw. Sumaye, imekuja huku kukiwa na tuhuma nyingi zinazomkabili Bw. Mkapa, kutokana na madai ya matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa rais.
Baadhi ya tuhuma hizo ni kuingia mikataba `feki` na makampuni ya uwekezaji, hasa katika sekta ya madini huku naye akidaiwa `kujiuzia` mgodi, ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ununuzi unaotia wasiwasi wa rada na ndege ya Rais, na madai ya kuwa na mkono katika menejimenti ya kigeni iliyokuwa inaendesha Tanesco, Net Group Solutions.
``Utawala wa Mkapa ulileta maendeleo kwa kasi kubwa sana, na nchi ilikwenda mbele kweli kweli,`` alisema Bw. Sumaye, alipozungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Mkutano huo uliandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Tanzania Leo Limited, inayochapisha gazeti la Tanzania Leo, Bw. Venance Rwegoshora, kukanusha taarifa iliyochapishwa na gazeti hilo, toleo la Machi 31 hadi Aprili 6, mwaka juzi, kuwa Bw. Sumaye, anamiliki akaunti iliyopo nje ya nchi, ikiwa na Sh. Trilioni 10.
Bw. Rwegoshora, alisema baada ya mchakato wa hoja kati ya kampuni hiyo na Bw. Sumaye kushindikana kupitia usuluhishi wa Baraza la habari, suala hilo lilifikishwa mahakamani, ilipobainika kuwa habari hizo zilikuwa za uongo, zilitungwa, zikapotosha na kutokuwa na msingi wowote.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama Kuu iliamuru kufanyika kikao cha usuluhishi kati ya pande mbili hizo, na kukubaliwa masuala kadhaa, ikiwemo Tanzania Leo kumlipa Bw. Sumaye fidia ya Sh milioni 100, zitakazolipwa kuanzia kipindi cha kabla ya Desemba Mosi mwaka huu hadi juni mwaka ujao.
Bw. Sumaye, alisema utendaji wa Serikali ya Mkapa, ulikuwa makini, uliozingatia maslahi ya nchi, ingawa kuna uwezekano wa kuwepo viongozi binafsi, waliokiuka misingi na maadili ya utumishi wao.
``Kama kuna viongozi waliokiuka maadili ya utumishi, hawawezi kuwa sababu ya kusema serikali ilishindwa. Tumeambiwa kuna uchunguzi unafanyika, tusubiri matokeo yake na wahusika watashughulikiwa,`` alisema.
Alisema uchunguzi unaofanyika dhidi ya vitendo vya ufisadi vinavyodaiwa kufanyika wakati wa utawala wa Bw. Mkapa, ambapo (Sumaye), alikuwa Waziri Mkuu, unawahusu watu binafsi na si utendaji wa iliyokuwa serikali ya awamu ya tatu.
Miongoni mwa hatua za kiutendaji alizozitetea Bw. Sumaye, ni ununuzi wa rada, iliyoligharimu taifa kiasi cha Sh. bilioni 70.
Alidai kwamba kabla ya ununuzi wake, ndege za kimataifa zilitishia kukatisha safari zake kutokana na kulazimika kuzunguka angani, ili zionekane na waongozaji ndege, kabla ya kuruhusiwa kutua.
``Kwa hiyo ununuzi wa rada ile ulikuwa uamuzi wa msingi na muhimu, sasa kama kuna watu walifanya madudu yao, wanapaswa kushughulikiwa,`` alisema.
Hata hivyo, watanzania wamekuwa hawapingi ununuzi wa rada hiyo, isipokuwa kilichowashangaza ni gharama kubwa ya rada hiyo ya kijeshi, huku ikisemekana kuwa Tanzania ilihitaji rada ya kawaida yenye gharama ndogo.
Licha ya kutoa tathmini hiyo kuhusu utendaji wa serikali ya Bw. Mkapa, waziri Mkuu mstaafu Sumaye, alikataa kuzungumzia utendaji wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kwa madai kuwa hana utaalamu wa kufanya hivyo.
``Kwa bahati mbaya, nilipokwenda kusoma Marekani, sikuchukua somo hili la tathmini, hivyo suala hilo tuziachie taasisi kama zile za Chuo Kikuu,`` alisema wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Muda baada ya kumaliza kipindi cha uongozi akiwa Waziri Mkuu, Bw. Sumaye alijiunga katika Chuo Kikuu cha Harvard, nchini Marekani, ambapo alisomea masuala ya uongozi wa umma.
Akizungumzia fidia atakayolipwa na kampuni ya Tanzania Leo, Bw. Sumaye, alisema baada ya kutoa gharama zilizotumika kudai haki yake, sehemu ya `vijisenti` vitakavyobaki atavikabidhi kwa Jukwaa la Wahariri ili kufanya semina ya maadili ya uandishi kwa vyombo vya habari.
Alisema fedha nyingine atazipeleka kufanikisha miradi ya kuwawezesha wasichana wa kabila la Kimasai, kupata fursa zaidi za kujiendeleza kielimu.
Wakati huo huo, Bw. Sumaye, amesema hajiandai kuwania urais, baada ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
Bw. Sumaye ni miongoni mwa wanachama 10 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walioshindana na Rais Kikwete kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama hicho, kuwania urais mwaka 2005.
Wakati Bw. Sumaye akitoa tamko hilo, habari za ndani ya CCM zilinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi, zikidai kuwapo wanasiasa waandamizi, wakiwemo waliowania uteuzi wa kugombea Urais mwaka 2005, kujipanga kushindana na Rais Kikwete, katika uteuzi wa kuwania kiti hicho mwaka 2010.
``Sijiandai kuwa Rais, kwanza sasa hivi tunaye Rais Kikwete tuliyemchagua, sasa hadi atakapotoka madarakani mwaka 2015 mimi niingie tena, yaani kama ni urais nikae miaka 10 mingine, nitapona kweli,`` alihoji bila kufafanua.
Alisema hivi sasa, anakamilisha mipango itakayofanikisha azma yake ya kuwa mwanaharakati wa kuwasaidia viongozi waliopo madarakani katika nchi za Afrika, kupambana na umaskini.
Aidha, Bw. Sumaye, alisema katika kipindi alichokuwa madarakani, hakuwahi kujihusisha na biashara za kimataifa wala kufungua akaunti nje ya nchi.
``Sikuwahi kuwa na akaunti hata ya Dola moja, ama isiyokuwa na fedha kabisa nje ya nchi, ndani ya kipindi chote nilipokuwa Waziri Mkuu,`` alisema wakati akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari.
Hata hivyo, alisema hivi sasa anamiliki akaunti moja nchini Marekani, aliyoifungua wakati alipokwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini humo.
Alisema bado anaendelea kuihudumia akaunti hiyo, kutokana na kuwa na shughuli mbalimbali anazozifanya na Chuo Kikuu hicho nchini Marekani, ambazo hata hivyo hakuzitaja.
Pia Bw. Sumaye, alisema hana hofu kuhusishwa na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma, akiwa msaidizi wa karibu wa Bw. Mkapa wakati wa utawala wa awamu ya tatu.
``Mkiniandika kama mnavyomwandika (Mkapa) andikeni tu, ali mradi muwe na taarifa za kweli, vinginevyo, hivi sasa mimi ni raia wa kawaida. Mkifanya hivyo kwa kunichafua, tutafikishana mahali pa kusafishana,`` alisema.
Bw. Sumaye, alitetea usiri unaoainishwa katika Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kwamba unasaidia kulinda utu wa mtu.
``Dunia hii kila mtu ana privacy yake (mambo binafsi), kama kuna wasiwasi na kiongozi fulani kuna vyombo vya uchunguzi kupata na kutumia zile taarifa, vinginevyo ukisema iwe kwa kila mtu, itakuwa vurugu,`` alisema.
Hata hivyo, alisema bado kuna haja ya kuangalia mapungufu yaliyopo katika sheria hiyo na kuyarekebisha kwa maslahi ya umma.
Tayari Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta, ameiagiza Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala, kuipitia sheria hiyo na kutoa mapendekezo ya uboreshaji wake.
Kwa upande mwingine, Bw. Sumaye alisema tuhuma dhidi ya ufisadi, zinazowakabili wanasiasa, zina athari kubwa katika maisha yao binafsi.
Alisema athari zake ni kubwa zaidi inapotokea tuhuma hizo `zimepandikizwa` na watu kwa maslahi yao binafsi.
``Hali ikiwa hivyo unaweza kujikuta kila unapopita unazomewa na pengine kupigwa mawe... Watu wakikuona wanasema huyo alikula fedha zetu,`` alisema.