Mwaka huu inabidi tuwe makini sana hapa JF....
Sumaye amtetea Mkapa
2008-06-02 09:39:20
Na Mashaka Mgeta
Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, ameibuka na kuutetea utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, kuwa uliharakisha maendeleo ya nchi na watu wake.
Kauli hiyo ya kwanza kutolewa na Bw. Sumaye, imekuja huku kukiwa na tuhuma nyingi zinazomkabili Bw. Mkapa, kutokana na madai ya matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa rais.
Baadhi ya tuhuma hizo ni kuingia mikataba `feki` na makampuni ya uwekezaji, hasa katika sekta ya madini huku naye akidaiwa `kujiuzia` mgodi, ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ununuzi unaotia wasiwasi wa rada na ndege ya Rais, na madai ya kuwa na mkono katika menejimenti ya kigeni iliyokuwa inaendesha Tanesco, Net Group Solutions.
``Utawala wa Mkapa ulileta maendeleo kwa kasi kubwa sana, na nchi ilikwenda mbele kweli kweli,`` alisema Bw. Sumaye, alipozungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Mkutano huo uliandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Tanzania Leo Limited, inayochapisha gazeti la Tanzania Leo, Bw. Venance Rwegoshora, kukanusha taarifa iliyochapishwa na gazeti hilo, toleo la Machi 31 hadi Aprili 6, mwaka juzi, kuwa Bw. Sumaye, anamiliki akaunti iliyopo nje ya nchi, ikiwa na Sh. Trilioni 10.
Bw. Rwegoshora, alisema baada ya mchakato wa hoja kati ya kampuni hiyo na Bw. Sumaye kushindikana kupitia usuluhishi wa Baraza la habari, suala hilo lilifikishwa mahakamani, ilipobainika kuwa habari hizo zilikuwa za uongo, zilitungwa, zikapotosha na kutokuwa na msingi wowote.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama Kuu iliamuru kufanyika kikao cha usuluhishi kati ya pande mbili hizo, na kukubaliwa masuala kadhaa, ikiwemo Tanzania Leo kumlipa Bw. Sumaye fidia ya Sh milioni 100, zitakazolipwa kuanzia kipindi cha kabla ya Desemba Mosi mwaka huu hadi juni mwaka ujao.
Bw. Sumaye, alisema utendaji wa Serikali ya Mkapa, ulikuwa makini, uliozingatia maslahi ya nchi, ingawa kuna uwezekano wa kuwepo viongozi binafsi, waliokiuka misingi na maadili ya utumishi wao.
``Kama kuna viongozi waliokiuka maadili ya utumishi, hawawezi kuwa sababu ya kusema serikali ilishindwa. Tumeambiwa kuna uchunguzi unafanyika, tusubiri matokeo yake na wahusika watashughulikiwa,`` alisema.
Alisema uchunguzi unaofanyika dhidi ya vitendo vya ufisadi vinavyodaiwa kufanyika wakati wa utawala wa Bw. Mkapa, ambapo (Sumaye), alikuwa Waziri Mkuu, unawahusu watu binafsi na si utendaji wa iliyokuwa serikali ya awamu ya tatu.
Miongoni mwa hatua za kiutendaji alizozitetea Bw. Sumaye, ni ununuzi wa rada, iliyoligharimu taifa kiasi cha Sh. bilioni 70.
Alidai kwamba kabla ya ununuzi wake, ndege za kimataifa zilitishia kukatisha safari zake kutokana na kulazimika kuzunguka angani, ili zionekane na waongozaji ndege, kabla ya kuruhusiwa kutua.
``Kwa hiyo ununuzi wa rada ile ulikuwa uamuzi wa msingi na muhimu, sasa kama kuna watu walifanya madudu yao, wanapaswa kushughulikiwa,`` alisema.
Hata hivyo, watanzania wamekuwa hawapingi ununuzi wa rada hiyo, isipokuwa kilichowashangaza ni gharama kubwa ya rada hiyo ya kijeshi, huku ikisemekana kuwa Tanzania ilihitaji rada ya kawaida yenye gharama ndogo.
Licha ya kutoa tathmini hiyo kuhusu utendaji wa serikali ya Bw. Mkapa, waziri Mkuu mstaafu Sumaye, alikataa kuzungumzia utendaji wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kwa madai kuwa hana utaalamu wa kufanya hivyo.
``Kwa bahati mbaya, nilipokwenda kusoma Marekani, sikuchukua somo hili la tathmini, hivyo suala hilo tuziachie taasisi kama zile za Chuo Kikuu,`` alisema wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Muda baada ya kumaliza kipindi cha uongozi akiwa Waziri Mkuu, Bw. Sumaye alijiunga katika Chuo Kikuu cha Harvard, nchini Marekani, ambapo alisomea masuala ya uongozi wa umma.
Akizungumzia fidia atakayolipwa na kampuni ya Tanzania Leo, Bw. Sumaye, alisema baada ya kutoa gharama zilizotumika kudai haki yake, sehemu ya `vijisenti` vitakavyobaki atavikabidhi kwa Jukwaa la Wahariri ili kufanya semina ya maadili ya uandishi kwa vyombo vya habari.
Alisema fedha nyingine atazipeleka kufanikisha miradi ya kuwawezesha wasichana wa kabila la Kimasai, kupata fursa zaidi za kujiendeleza kielimu.
Wakati huo huo, Bw. Sumaye, amesema hajiandai kuwania urais, baada ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
Bw. Sumaye ni miongoni mwa wanachama 10 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walioshindana na Rais Kikwete kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama hicho, kuwania urais mwaka 2005.
Wakati Bw. Sumaye akitoa tamko hilo, habari za ndani ya CCM zilinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi, zikidai kuwapo wanasiasa waandamizi, wakiwemo waliowania uteuzi wa kugombea Urais mwaka 2005, kujipanga kushindana na Rais Kikwete, katika uteuzi wa kuwania kiti hicho mwaka 2010.
``Sijiandai kuwa Rais, kwanza sasa hivi tunaye Rais Kikwete tuliyemchagua, sasa hadi atakapotoka madarakani mwaka 2015 mimi niingie tena, yaani kama ni urais nikae miaka 10 mingine, nitapona kweli,`` alihoji bila kufafanua.
Alisema hivi sasa, anakamilisha mipango itakayofanikisha azma yake ya kuwa mwanaharakati wa kuwasaidia viongozi waliopo madarakani katika nchi za Afrika, kupambana na umaskini.
Aidha, Bw. Sumaye, alisema katika kipindi alichokuwa madarakani, hakuwahi kujihusisha na biashara za kimataifa wala kufungua akaunti nje ya nchi.
``Sikuwahi kuwa na akaunti hata ya Dola moja, ama isiyokuwa na fedha kabisa nje ya nchi, ndani ya kipindi chote nilipokuwa Waziri Mkuu,`` alisema wakati akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari.
Hata hivyo, alisema hivi sasa anamiliki akaunti moja nchini Marekani, aliyoifungua wakati alipokwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini humo.
Alisema bado anaendelea kuihudumia akaunti hiyo, kutokana na kuwa na shughuli mbalimbali anazozifanya na Chuo Kikuu hicho nchini Marekani, ambazo hata hivyo hakuzitaja.
Pia Bw. Sumaye, alisema hana hofu kuhusishwa na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma, akiwa msaidizi wa karibu wa Bw. Mkapa wakati wa utawala wa awamu ya tatu.
``Mkiniandika kama mnavyomwandika (Mkapa) andikeni tu, ali mradi muwe na taarifa za kweli, vinginevyo, hivi sasa mimi ni raia wa kawaida. Mkifanya hivyo kwa kunichafua, tutafikishana mahali pa kusafishana,`` alisema.
Bw. Sumaye, alitetea usiri unaoainishwa katika Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kwamba unasaidia kulinda utu wa mtu.
``Dunia hii kila mtu ana privacy yake (mambo binafsi), kama kuna wasiwasi na kiongozi fulani kuna vyombo vya uchunguzi kupata na kutumia zile taarifa, vinginevyo ukisema iwe kwa kila mtu, itakuwa vurugu,`` alisema.
Hata hivyo, alisema bado kuna haja ya kuangalia mapungufu yaliyopo katika sheria hiyo na kuyarekebisha kwa maslahi ya umma.
Tayari Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta, ameiagiza Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala, kuipitia sheria hiyo na kutoa mapendekezo ya uboreshaji wake.
Kwa upande mwingine, Bw. Sumaye alisema tuhuma dhidi ya ufisadi, zinazowakabili wanasiasa, zina athari kubwa katika maisha yao binafsi.
Alisema athari zake ni kubwa zaidi inapotokea tuhuma hizo `zimepandikizwa` na watu kwa maslahi yao binafsi.
``Hali ikiwa hivyo unaweza kujikuta kila unapopita unazomewa na pengine kupigwa mawe... Watu wakikuona wanasema huyo alikula fedha zetu,`` alisema.
SOURCE: Nipashe
http://www.ippmedia.com/ipp/nipashe/2008/06/02/115635.html