Hivi sasa limezuka tatizo la wananchi kukimbilia kwa viongozi wa juu kabisa pindi yanapotokea matatizo hata yale madogo tu. Lakini kibaya zaidi hivi sasa ni Pinda na JK , nahisi hata Shein ingawa imekuwa ni nadra sana kusikia wananchi wakimtaka akawatatulie matatizo yao labda kutokana na upole wake. Ni kawaida kusikia wananchi wakidai kama haji Pinda / JK patachimbika hapa, Mtu atakaa akijiuliza je hii ni nini hasa?
Tukuchukulie mfano wa Kwembe Kati, Wakazi wa eneo hilo walikumbwa na matatizo ya watendaji wabovu wa Wizara ya Ardhi na tamaa zao walizoweka mbele. Wakazi hao walikimbilia kwa viongozi mbali mbali kuomba msaada bila ya suluhisho lolote la maana. Wananchi hao wanafahamu kuwa Ardhi ni msingi wa maendeleo. Hivyo kwa muda mrefu wametunza ardhi yao ili iweze kuwasidia kusukuma siku mbele hasa wakati huu ambapo kuna tatizo kubwa la ajira. Wengi wao wanajihusisha na kilimo cha msimu katika maeneo ya mabondeni yasiyofaa kwa ujenzi wa nyumba na majengo mengine, wakitumia maeneo yao kwa maendeleo endelevu.
Ghafla kulitokea miradi ya kujenga chuo Muhimbili, kujenga mji wa Luguruni, kujengwa kwa Chuo kikuu cha Mt. Joseph n.k. Hii ilipelekea mafisadi wa wizara ya ardhi kuanza kulimezea mate eneo hilo, na hivyo kuanza kupiga jalamba ili kulipora toka kwa wananchi, Hivi sasa wanatumia mbinu mbali mbali kufanikisha wizi huo.
Mbinu ya kwanza ilikuwa kuwatisha wananchi kuwa kuwa kuna mpango wa kutwaa maeneo yao kwa malipo ya shilingi 300,000/= kwa eka moja ama mtu akikataa basi eneo husika litatwaliwa na Raisi kwa manufaa ya umma. Baada ya madai haya wananchi wengi waliogopa na kuanza kuuza maeneo yao kwa bei ya kutupa, na hivyo kuwapa mwanya maofisa wa wizara ya Ardhi kutwaa maeneo hayo kwa manufaa yao kwa bei ya kutupa.
Baada ya hapo maofisa hawa walikuja na kuanza zoezi la uthamini huku bei ikiwa siyo ile waliyowatishia wananchi wakati ule. Hata hivyo walitumia mbinu mbali mbali kuwanyonya wananchi huku wakikiuka sheria na taratibu zote zilizowekwa na mamlaka husika.
Baadhi ya mambo ya wazi ni kama ifuatavyo:
1) Wametwaa eneo la Veterinary lililokaribu na shule ya Joha lililotengwa kwa ajili ya kuhamishia watu waliobomolewa Luguruni na kuwagawiana viwanja pale, viwanja hivi wamevipima kwa ujazo wa chini baadhi ya hivyo ni 70 x 70. wao wanadai eti ni makazi ya viongozi nao wameainishwa ikiwemo baadhi ya viongozi wenye heshima zao ambao hatuamini hata kidogo kuwa wanashiriki katika ubatili huu. Hii ndiyo sababu ya Ramani kufichwa kinyume na utaratibu ambapo ramani inatakiwa iwe wazi kwa muda wa miezi miwili kabla ya kuitumia. Lakini hadi sasa bado ramani hiyo ni siri ya Mama Mushi na wenzie.
2) Watu wengi wamelipwa chini ya kiwango ambapo wengi wamelipwa kidogo kupindukia na kupelekea kuwekwa kwa walipwaji hewa. Hapa mtu akikutwa na ekari moja yenye minazi ishirini, anadanganywa kuwa ataongezewa minazi hadi 40 hapa anapigwa changa la macho kwani kwenye ardhi anaandikiwa nusu eka na nusu nyingine anapewa mtu wa ardhi ama jamaa yake.
3) Maofisa wa wizara ya ardhi wamepima upande wa pili wa eneo la mradi la Luguruni na baadaye wanaviuza kwa watu tunaoporwa hapa kwembe kwa bei ya juu sana, ukikutwa na maendelezo yeyote yasiyokamilika waambiwa bomoa haraka ili wapime viwanja wakauze kwa bei ya kujipangia. Hii iangalie na kufanyiwa utafiti kwani haya siyo majungu bali kweli tupu, Ukikutwa na robo eka (30x50) unapewa chini ya shilingi milioni mbili, wengine wamepewa milioni moja Ukienda upande wa pili unaonyeshwa kiwanja nusu ya hicho (30x20) kwa bei kati ya Mil. 6 hadi 8.
4) Wamekuwa wakichagua nani aandikiwe eneo gani. Mzee mmoja alilazimishwa akachukue shilingi Millioni 21 naye akakataa akidai eneo hilo si lake naye hataki kufungwa. Haya yalielezwa mbele ya aliyekuwa mkuu wa Wilaya, Masawe naye aliahidi kushughulikia ingawa hakufanya chochote kile.
5) Maeneo waliyonunua wakati wa vitisho kutohusishwa katika uporaji kwa madai kuwa watapima na kuuza wenyewe kwa bei watakayo hapo baadaye. ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA YA KINONDONI analo eneo kubwa karibu na kinapojengwa chuo cha Muhimbili ambalo analihodhi yeye na mama Mushi, Pamoja na eneo lingine kubwa katika mtaa wa Kibwegere ambalo nalo ni la mama Mushi, Haya hayahusiki ila yetu sisi wanyonge ndiyo yanatwaliwa kwa bei ya kutupa, huku tukinyimwa haki ya kupewa angalau kiwanja kimoja katika maeneo yetu yanayotwaliwa kwa madai kuwa hatujamalizia kujenga, hii ni kinyume cha kanuni na sheria. Waziri husika hataki kutolea tamko jambo hili . Kanza analo eneo kubwa karibu na maduka sita mtaa huu wa Kwembe kati ambalo halijausishwa na wizi huu.
6) Kutishia wananchi watoe pesa la sivyo maeneo yao yatafanya maeneo ya miundo mbinu kama barabara, na hivyo nyumba zao kuvunjwa. Wananchi wamelalamika katika vikao halali juu ya hili bila kutokea mtu wa kuwafuta machozi.
7) Waliwaeleza wananchi kuwa wale waliokuwa na majengo ambayo hayaisha wasubiri hadi pale michoro mipya itakapokuwa tayari. Lakini sasa wamewageuka wananchi wakisema wayabebe majengo yao ambayo hayajawa tayari wayapeleke porini, Huu ni uonevu ambao hautavumiliwa hata kidogo, kwani wote tunajenga pole pole kwa ukosefu wa pesa, kutugeuka na kuvunja maendelezo yetu bila malipo ni suala gumu sana linaloweza kuhatarisha amani.
8) Maeneo ya mabonde ambapo watu maskini walikuwa wakilima mbonga mboga wanadai watapewa watu wengine ili wayaendeleze ingawa hakuna viwanja hapo. Wanasikitisha eti kuna wawekezaji toka India wanataka lima pili pili kwa ajili ya kusafirisha nje, hili lilisemwa na Mama Bura mbele ya Massawe lakini pamoja na wananchi kuwazomea hakuna kauli dhabiti iliyotolewa hadi sasa kupinga uhuni huu. Hapa mtu atajiuliza hivi kwa nini aliyekutwa asiwezeshwe kufanya mradi huo. Eti kiwanja kilichopo karibu na hapo lazima apewe mwekezaji
9) Maofisa wa ardhi ambao wanalipana posho kubwa za "Special Duty" kila mmoja kati ya 80,000/= hadi 150,000/= kwa siku gharama zitakazobebwa na wakazi, na hii imepelekea wao kutomaliza kazi hii kwa muda mrefu ili siku ziwe nyingi. Kwa utaratibu wa sheria gharama za mradi zafahamika hivyo ziwekwe wazi tujue ni utaalamu gani hasa wanaoleta hadi walipwe mshahara wa mwalimu mmoja kwa mwezi wao walipwe kwa siku moja kama siyo wizi mtupu.
10) Kwa kulipana kiasi hiki kikubwa imepelekea watu wengi kuchukuliwa maeneo yao bila kulipwa kwani pesa imetumika kuwalipa hawa wahuni malipo hewa na sasa wanadai kuwa wenye maeneo watalipwa pindi wakimaliza kuuza viwanja, na wenye maeneo hawapewi kipaumbele.
11) Wamekuwa wakipita maeneo ya Kibamba na Luguruni wakinadi viwanja ambavyo tunavimiliki wakitumia ramani hewa, hivyo Kamati ya Wananchi ikitaka marekebisho wanagoma kwani wameishaahidiwa fedha. Wengine maeneo yetu yameuzwa tukiwapo bila aibu yeyote. Wanaoendesha uhuni huu ni Kanuti na Kamala ambao hata siku za jumapili wanakuwa site wakinadi viwanja vyao, bila aibu yeyote.
12) Mwananchi akikutwa ameishajenga nyumba hilo ni kosa kwani wanahakikisha anabakiwa na sehemu yenye nyumba tu na sehemu nyingine wanawapa wapendwa wao, hata kama kuna maendelezo mengine kama vyoo n.k tena bila kulipwa. Hii inatuletea umaskini wakutisha kwani pale tulipotumia kufugia kuku, ngombe na mifugo mingine wametwaa na kuwapa wapendwa wao sisi tukiachwa bila utetezi wowote ule. Hivi maisha bora ni kwa watu wa Wizara ya Ardhi tu ama ni kwa kila Mtanzania kama alivyotangaza mtukufu Raisi.
13) Wamekuwa wakibabaika kila mara katika kauli zao, Waziri amekuwa akidai kuwa watu wa Kwembe Kati wanapangwa wakati maofisa wa ardhi wanahaha kupora maeneo ya watu kwa ajili ya kuuza viwanja vya watu. Waziri aliyedai Kwembe kati watapimiwa naye kaingia mitini.
14) Wamekiuka taratibu zote zinazotakiwa kufuatwa ili kuweza kufanya ufisadi wao, sasa wanadai eti eneo linalojulikana kama Kwembe Kati eti ni sehemu ya Luguruni wakati wao wanafahamu kuwa maeneo hayo ni tofauti kabisa.
15) Kwa kuwa kamati iliyoundwa Kihalali na ni kimbilio la Wananchi wanyonge hawataki kuisikia kwani wanataka wananchi wawafuate wao ili wawaombe hongo. Ikumbukwe sheria za ardhi namba 4 ya 1999 inatambua kamati hizi, lakini watu wa Wizara ya ardhi wanadai kuwa itawazuia kufanya usanii wao.
16) Waliwauzia wananchi waliohamishwa Luguruni viwanja walivyokuwa wameodhi na hivi sasa wanahaha kutafuta viwanja vingine kwa ajili ya kulangua hapo baadae, wakitumia mbinu chafu zisizokubalika hata kidogo.. Kama kuvunja maendelezo ya watu na kudai hongo wazi wazi.
17) Wamekuwa wanadai wananchi waliofanya maendelezo ambayo hayajakamilika hongo ili eti yatambuliwe ukikataa unakiona cha moto kwani wanavamia na kudai yavunjwe mara moja.
Undumilakuwili wa viongozi
Baada ya kero zote hizi wananchi waliwakimbilia viongozi wao wakidhani kuwa watasikilizwa jambo ambalo halikuwa hivyo hata kidogo. Hii inatokana na kuwa mafisadi wa Wizara ya Ardhi wameishajua dawa yao. Nayo ni kuwaahidi viwanja, wakishafanya hivi viongozi hawa uwageuka wananchi mara moja na kuungana na mafisadi hawa kuwakomoa wananchi waliowachagua. Hawa viongozi kwa ahadi ya viwanja ni kama mbwa kwa chatu hawachomoki hata kidogo. Wakifika na kuwasikiliza wananchi ukweli wanauona mfano Ni kitu gain kinasababisha mwananchi mmoja aambiwe avunje endelezo lake ili apewe mwingine? Hapa jibu liko wazi lakini wakishaelezwa kuwa tukifanya hivyo wewe upati kiwanja hapa wanashindwa kuchukua maamuzi ya busara na kulegea kabisaaaa. Hii imepelekea wananchi kuanza kukimbilia kwa Waziri Mkuu, na Mheshimiwa Rais kwa matatizo madogo yaliyokuzwa kwani wana maamuzi yasiyoteteleka, na hivyo kuwafanya wawe na majukumu mengi isivyotakikana. Kwa Kwembe Kati mifano ya viongozi hao ni kama ifuatavyo:
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya
Alipoombwa kuingilia kati baada ya mambo kwenda mrama yeye aliingia pale kwa mbwembwe akionekana ni mtetezi wa wananchi, alifika akifuatana na maofisa wa TAKUKURU, na maofisa wengine. Alionyesha uelewa wake katika masuala ya Ardhi akibainisha wazi mapungufu mengi katika zoezi la Kwembe Kati. Aliahidi kuwa yote yatawekwa sawa.
Baada ya kuahaidiwa kiwanja aligeuka ghafla na kufanya mambo mengi ya ajabu, alianza kwa kudai kuwa watu wa ardhi ni kama baba akijamba wananchi wasihoji hivyo hata kama sheria zimekiukwa hakuna shida watu wavumilie. Aliendelea kutisha wananchi kuwa yeye ana uwezo wa kumweka ndani mtu saa 48. Lakini aliwacha watu hoi pale alipodai kuwa hata kama ujalipwa uache tu kwani utalipwa watakapouza viwanja watakavyopima. Mambo mengine ya ajabu ni pamoja na:
1) Alikimbiliwa tangu mwezi Septemba 2008 akiombwa msaada lakini yeye aliingia mitini pamoja na kupewa barua. Baada ya kuona wananchi wameungana kupinga ufisadi akaja bila kuitwa na kuanza kutugawa akidai atawasikiliza wenye nyumba tu na wale wengine watajiju.
2) Alipanga mamluki (wengi wao wakiwa madalali na vibaka) siku ya Idd El Haji (3-3-09) ili ionekane kuwa wananchi tumekubaliana na madai yao ya kupora ardhi yetu, ila kuna wakorofi wachache lakini janja yake iligunduliwa na wananchi baada ya siri kuvuja na hivyo kujikuta uso kwa uso na wananchi wenye mabango pale serikali ya mtaa, aliumbuka na kuondoka na waandishi wa habari aliowaita kufanya usaniii ule. Vile vile alitoa hongo ili habari hiyo isiandikwe magazetini, hapa waweza kupata ukweli toka kwa OCD wilaya ya Kipolisi ya Kimara aliyefika siku ile. Vile vile amekuwa akitumia mamluki hao hao kuwapeleka ktk ngazi mbali mbali za serikali ili ionekane kuwa taratibu zilifuatwa wakati si kweli, vibaraka wake twawajua akiwemo mtendaji na madalali
3) Aliandika barua kuwa tumekubali kuporwa maeneo yetu kuwapa watu "hewa" wa Kibamba na Luguruni. Baada ya wanakamati kukataa barua hiyo yeye alielekeza wasishirikishwe tena bali itumike mitutu ya Polisi katika zoezi husika.
4) Amekuwa akimdanganya Waziri husika kuwa mambo yapo sawa wakati hiyo yote si kweli kwani mabango aliyokutana nayo siku ya Idd yanaeleza ukweli halisi. Aliyachukua mabango yetu kuwa atayafikisha kwa waziri husika lakini hakuyafikisha sehemu husika kwani aliumbuka siku hiyo.
5) Amehongwa kiwanja na MAMA MUSHI ambaye amekuwa akilalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu bila mafanikio, wala hatua zozote kuchukuliwa dhidi yake, alivuruga sana pale Luguruni bila kuchukuliwa hatua yeyote ile, huyu mama ni hatari kwani amekuwa akifanya vikao na Kijana wa Uru Kishumundu pale Rombo Green View kupanga jinsi ya kuwaumiza watu wanyonge.
Naibu Kamishna wa Ardhi ( Shewio)
Katika maofisa wote waliowahi kuhusika na mgogoro huu huyu ndiye aliyeonekana kuwa na afadhali kwani alisikiliza na kukubali masuala yote ya msingi. Akisistiza kuwa kiwanja cha mwananchi ambaye ajalipwa akitauzwa bali atapewa yeye mwenyewe naye alipie gharama za upimaji. Katika mkutano mmoja ambapo wananchi walikuwa na hasira kali yeye aliwakonga nyoyo wananchi kwa kueleza wazi wazi kuwa sheria lazima zifuatwe. Akifuatwa ofisini anasisitiza kuwa hakuna haja ya kumwondoa aliyeendeleza hata sehemu ndogo na kumkabidhi mtu mwingine eneo husika. Alishangiliwa pale aliposema lengo ni kuepuka Manzese nyingine hapa. Alidai kama kuna maendelezo yeyote yule aliyendeleza atapewa kipaumbele kwanza, akasema labda akatae kupewa kiwanja husika mwenyewe, alida kiwanja cha aina hiyo kitakuwa "reserved". Lakini baadaye nae ameonekana kulega lega katika msimamo wake.
Kamala, Kanuti / Mama Mushi / Mama Mmbaga
Hawa ndiyo maharamia ambao watu wa Kwembe Kati watawakumbuka kwa maisha yao yote. Mwanzoni waliwaongopea wananchi kuwa kiwanja cha ukubwa wa chini (high density) kitakuwa na ukubwa wa meta 35 x 35 na kuendelea na kudai kuwa tutapewa kila aina ya huduma za jamii. Kwa sasa ndiyo wanaoongoza kwa kutumia kila hila kupora wakazi hawa na kuendelea kuwatwisha jiwe zito la ufukara. Wanatumia ramani zisizo halali na kutumia maneno ya vitisho ili mradi wapore wananchi, usipokubali kuwaonga unajuta kuwafahamu kwani watakufanyia visa vya kila aina kama vile kupitisha barabara sebuleni kwako, kukupunja kiwanja hata kama kipo katika viwanja vya ujazo wa chini na kutenganisha choo chako na nyumba yako ili mradi ujute kwa kutowapa hongo. Kwao cha msingi ni kupata viwanja vya kuodhi ana kulangua na pesa nyingi ili walipwe posho kubwa kubwa walizojipangia. Baada ya zoezi la kwanza kwisha na kufanikiwa walirudia zoezi husika ili wapate viwanja vingi hasa vya mbele kwa ajili ya kuuza na kuwapa watu wao, lakini hii ndiyo iliyoamsha hamasa ya wananchi. Hili ni kundi la maharamia ambao wanaweza hatarisha usalama katika jamii. Wanawatumia madalali hivi sasa kunadi maeneo waliyoyatayarisha kwa ajili ya kupatia pesa kwani hivi sasa kama ulikuwa na eneo lako sehemu nzuri basi ujue atapewa mteule wao. Kati ya watu watakaojuta juu ya ujio wa maharamia hawa ni akina mama na wajane wanyonge ambao hatuna nguvu ya kupamba na maharamia hawa huku viongozi wetu wakiwa hawakotayari kutusaidia hata kidogo.
Katibu tarafa / Mtendaji wa Mtaa Mw/kiti mtaa / Baadhi yaWajumbe
Hawa wote wamehaidiwa ama viwanja ama posho za shilingi 5,000/= na hivyo kuwasaliti wananchi moja kwa moja bila aibu hata kidogo. Hawa wengi wao hawatafaidi lolote zaidi ya kupata pesa ya kuganga njaa na kuwatongoza wafanyakazi wa ndani na watoto wa shule basi.
Aliyekuwa mkuu wa Mkoa (Kandoro)
Huyu alifanya kila analoweza kuondoa kadhia kwa wananchi na kuagiza kuwa yule atakayekutwa apewe kipaumbele kwanza katika kugawa kiwanja, na wengine wapewe sehemu itakayobaki. Vile vile amesisitiza kuwa yeye ni mtu wa mungu hawezi kudhulumu watu maskini Alionyesha uadilifu wake na kumwogopa mungu, kwani mambo mengi ni suala la kumwogopa mungu tu. Haya aliyafanya kwa matendo siyo maneno watu wa Mwanza watanufaika na busara / kuridhika / uadilifu na ucha mungu wake.
Waziri wa Ardhi
Waziri wa Ardhi alifika Kwembe kufafanua juu ya ujio wa Mradi wa ujenzi wa chuo cha Muhimbili na kiwanda cha dawa pale. Wananchi walimuuliza juu ya utwaaji wa ardhi Kwembe Kati naye alikanusha na kusema kuwa wananchi wa kwembe kati tulieni hamtaporwa bali mtapimiwa viwanja vikubwa alidai kuwa pale tu miundombinu itakapopitia ndipo watapatwaa. Alishangaa ni kwa nini watu wanafanyiwa tathmini, bali maofisa wa ardhi walisema kuwa ni kwa ajili ya sehemu zile tu zitakazopitiwa na miundo mbinu pekee ndipo wanalipa.
Hatujui kama ni kuahidiwa kiwanja ama kuwa na kazi nyingi lakini naye ameonyesha dalili ya kuwahadaa wananchi kwani anadai atasimamia uuzwaji wa viwanja hivyo bila kubainisha wale waliopimiwa bila kupewa fidi itakuwaje, wataachiwa maeneo yao ama la.
Madai yake kuwa watapewa kipaumbele watu waliohamishwa Luguruni ni ya kutilia mashaka kwani wengine hawakuwa na majengo bali ardhi tupu, iweje wao wapewe kipaumbele bali wale walioko Kwembe Kati na hawajamalizia majengo yao wabomoe kama siyo kuleta mwanya wa watu hewa wa Luguruni??. Vile vile kuna watu ambao wamevamiwa na hivyo taarifa zake hazipo wizarani kwani hawakulipwa yeye amenyamaza kimya bila kutoa ufafanuzi.
Ameombwa iwekwe wazi kiwanja kimetokana na mlipwa yupi kwa namba ya uthamini ipi lakini amepuuza kwani madudu yalofanywa kwenye uthamini ni ya kutisha mno. Kuna uwezekano kuwa watu wengi wamenufaika na fungu hili ndo maana wanagwaya kuchukua hatua.
Katibu tarafa / Mtendaji wa Mtaa / Baadhi yaWajumbe
Hawa wote wamehaidiwa ama viwanja ama posho za shilingi 50,000/= na hivyo kuwasaliti wananchi moja kwa moja bila aibu hata kidogo. Hawa wengi wao hawatafaidi lolote zaidi ya kupata pesa ya kuganga njaa na kuwatongoza wafanyakazi wa ndani na watoto wa shule basi.
Kutokana na watendaji hawa wabovu kumepelekea kuendelea kufedheheshwa kwa serikali mbele ya wananchi wake, ambao wanatazamia kupata huduma safi kutoka kwa watumishi wa serikali badala ya kuombwa rushwa, kuporwa ardhi, kupunjwa malipo ya fidia kutokana na kuwepo vitendo vya malipo hewa, baadhi ya watu maeneo yao kutwaliwa bila kulipwa kwa madai kuwa watalipwa pindi viwanja vikiuzwa, na baadhi ya watu kuzidishiwa malipo isivyo halali. Utawala bora kama ilivyokusudiwa na Serikali yetu tukufu usiwe kwa kauli mbiu tu bali kwa vitendo na mlengwa awe ni huyu mtu wa chini anayekandamizwa na mafisadi hawa.
Hii ndiyo sababu wananchi wanakimbilia kwa Waziri Mkuu na Raisi hata kwa mambo ambayo Mkuu wa Wilaya angeweza kabisa kuyatatua kwa urahisi zaidi. Kama suala la kupima viwanja ambalo taratibu ziko wazi kuwa anayekutwa apewe kipaumbele kama hajapitiwa na miundo mbinu.
Vile vile kuhamishwa kwa kijana wa Uru Kishumundu baada ya kuongwa viwanja hivyo suala hili tayari lilikuwa limemshinda, kumefanya watu wadhanie kuwa JK kaliona hili na kumwondoa , na hivyo kuwaonea huruma huko aendako, mwenyezi mungu mwingi wa rehema awasaidie awape ushupavu wa kutambua na kukabiliana na hila zake.
Mkuu wa Wilaya aliyekuja asikubali kuongwa kiwanja hata kidogo. Ashirikiane na Serikali kuwanyanganya viwanja walivyopora kwenye mradi wa viwanja 20,000 ili wauziwe wanyonge, hakuna haja ya kumwita mkuu wa mkoa hapa. Kama mkuu wa wilaya atasimamia vizuri basi mambo yataenda vizuri..
Halima Songambele
Kwembe Kati
Kata ya Kibamba