Nilimsikia Mchungaji Gwajima kwenye video akisema ana vyeti vya mtu anayeitwa Daudi Bashite na Paul Christian Muyenge akimlenga Paul Makonda pamoja na kwamba alitumia umakini mkubwa katika maelezo yote kutolitaja jina la Paul Makonda ili asiingie kwenye mkono wa sheria.
Gwajima alifahamu kama angesema ana vyeti vya Paul Makonda basi angejikuta kwenye kosa la kuhodhi cheti/vyeti vya Paul Makonda bila idhini yake.
Haya ni maelezo mazuri sana kisiasa lakini kwa watu wanaofahamu sheria wataanza kujiuliza maswali mengi kwa sababu madai ya Gwajima yanamuingiza kwenye makosa ya jinai ambayo yameorodheshwa kwenye Kanuni ya adhabu Sura ya 16 katika sehemu ya 258-259 inayohusu wizi na pia sheria ya Usalama wa Taifa namba 3 ya mwaka 1970, Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa namba 3 ya mwaka 2002, Sheria ya Utumishi wa Umma namba 8 ya mwaka 2002 na Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma.
Sheria hazina siasa pamoja na kwamba siasa wakati mwingine hazina sheria lakini pia hoja zangu hazimtetei Paul Makonda kama kweli ametumia vyeti vya mtu mwingine kitaaluma.
Kuhodhi cheti cha mtu mwingine bila idhini yake ni kosa la jinai kama ilivyo kutumia cheti cha mtu mwingine kwa idhini yake.
Ifahamike kuwa, hata kama ukiokota cheti/vyeti vya mtu mwingine lazima utoe taarifa mapema kwenye vyombo vya serikali na kushindwa kufanya hivyo utakuwa unahesabiwa ni mwizi kama ilivyoainishwa katika kanuni ya adhabu Sura ya 16.
Ninaamini Gwajima hawezi kutoa vyeti vya Paul Makonda bila idhini yake pamoja na kwamba amesema atavitoa.
Nimesikia anasema ameleta watu waliokuwa watumishi wa umma watoe ushuhuda kuhusu ukweli wa Daudi Bashite na Paul Christian Muyenge lakini hao watu lazima waelewe wanaweza kujikuta katika mikono ya sheria kama hawatapata wanasheria wazuri wa kuwaeleza jinsi ya kuruka mitego ya kisheria.
Nimalizie kwa kusema, watoa ushuhuda wa Mchugaji Gwajima lazima waelewe kuwa wakoloni walipoondoka katika makoloni yao hawakufuta sheria walizozitunga na kikubwa zaidi, serikali zilizorithi utawala wa kikoloni ziliongeza zaidi sheria zinazoweza kuwaingiza matatani kama watawala wakiamua kuzisimamia kikamilifu.
Nimalizie kwa kuwatakia ushuhuda mwema !