SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI
SIMULIZI: ANTI EZEKIEL
MTUNZI: George Iron Mosenya
SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI
Aliponipa mgongo, nami nikaanza kufanya kilichonipeleka, nikatazama huku na kule bila mafanikio. Nikaituliza akili yangu na hatimaye nikaona kitu.
Tundu la funguo katikati ya makablasha ya kuwekea bidhaa, nikajaribu kuvuta pakawa pagumu kufunguka, nilijaribu tena na tena lakini bado hali ilikuwa ileile.
Nikachukua funguo zilizokuwa pale ndani lakini hazikufanania na tundu lile!!
Nguvu zikaniishia tena, nilitamani dakika za mwisho za uhai wangu ziishie ndani ya huo mlango ilimradi nijue tu ni kitu gani huwa kinaendelea katika maficho yale.
Wakati nawaza juu ya ufunguo.. nikakumbuka kuwa kuna funguo nilipewa na Ezekiel Ubungo na kunisihi mambo kadha wa kadha. Nilipotazama kile kitasa hakika kiliendana na ule ufunguo!!
Nikakumbuka kuwa ufunguo ulipotea ukiwa ndani ya bahasha!!
Kazi ikawa ngumu zaidi!!
****
Nilirejea kimaficho katika nyumba ya kulala wageni niliyokuwa nimefikia, lakini9 nikakumbuka kununua magazeti kadha wa kadha, nikatilia maanani gazeti la yule mzee Matata, mzee ambaye kwangu mimi alikuwa kama adui tayari.
“MZIMU WA SAM WAONEKANA DAR UKIZURURA”
Nilishikwa na hasira kuiona picha yangu tena katika kurasa za mbele za magazeti. Nikajikuta nakabiliana na donge la hasira kooni, nikakumbuka kuwa funguo nimepoteza tayariu ambazo zingenisogeza karibu na ukweli na sasa gazeti la kipuuzi la mzee Matata linaandika ujinga tena kuwa nimeonekana Dar.
Huyu mzee na shahada zake za kutosha bado anashikiliwa akili na wajinga wajinga hawa. Haoni uchungu mwanaye amepotea? Ama nd’o upendo uliopoa?
Ghafla nikavamiwa na wazo kuwa huenda Anitha alirejeshwa nyumbani kwao, na huu msala umebaki kuwa mzigo wangu mwenyewe!!
Wazo hili halikutaka kutoka kichwani mwangu hata kidogo!! Nikajiaminisha kuwa namuwaza mtu ambaye yu huru!!
Nd’o maana baba yake anaendelea kufanya upumbavu huu!!
Nilijihisi kutetemeka mwili mzima, huku lile gazeti mkononi mwangu nikiliona kuwa mzigo mzito sana tena mzigo wa miiba unaochoma kwa hasira.
Mwendo mfupi wa kuifikia ile nyumba ya kulala wageni niliona ni sawa na kilometa kumi. Nilitamani kukifikia chumba nikivamie kitanda na kujilaza. Sikuwa na la ziada.
Hatimaye nikafika chumbani, nikalifunua lile gazeti. Kama ilivyo kawaida ya wasiojiamini, akaandika kuwa habari ile imeandikwa na ‘MWANDISHI WETU’
Nikasonya kwa ghadhabu na kulichana vipande vipande gazeti lile, kisha nikalala! Bila hata kuvua viatu vyangu!!
HARAKATI ZA JOJINA DAR
Nilikuja kushtuka masaa kadhaa mbele, usiku ulikuwa umeingia tayari na sikuwa nimepata walau hamu ya kula, niliumiza sana kichwa nisijue ni wapi pa kuweza kuanzia tena ili niufungue mlango ule, nikajiuliza mara mbili zaidi na kukosa majibu. Nikaingia bafuni na kujimwagia maji huenda kuna jambo jipya limezibwa na uchovu wa mwili litajitokeza.
Hakuna kilichojitokeza. Nilishika hiki na kuacha kile labda nitapata ufumbuzi lakini sikuwa na ujanja wowote, nikafikiria juu ya kuchongesha funguo za bandia lakini ajabu hata ramani ya tundu lile sikuwanayo na haikuonekana kuwa kazi nyepesi kuchonga funguo zahali pale. Funguo za maajabu.
Simu yangu ya mkononi ambayo namba yake alikuwanayo Jojina pekee ilipatwa na uhai na kuanza kuimba! Nikaisogelea kwa hofu maana sikutarajia simu kutoka Dar es salaam niliamini Jojina alikuwa mwenye ghadhabu na labda hakutaka kusema nami lolote.
Naam hakuwa mwingine aliyepiga simu ile.
Alikuwa Jojina!
“Nambie Mama lao…” nilimuanza kiutani ili kama ana jazba azitulize kidogo
“Safi tu Sam vipi ulikuwa umelala tayari.” Alinijibu kwa uchangamfu, ile saauti yake ya kimahaba ikanituliza woga wangu.
“Hapana nilikuwa bafuni ….”
Nikajirusha kitandani na kujilaza simu sikioni niweze kusikia Jojina ana lipi jipya!!
Alinieleza mambo kadha wa kadha kuhusu uwepo wake jijini Dar na mimi nikamweleza juu ya hali ya hewa ya Iringa, kisha akachukua nafasi kuel;ezea nia ya kunipigia simu usiku ule pasi na matarajio.
JOJINA.
SAM, kwanza sahau kuhusu yaliyopita, nadhani tulipishana lugha tu, nilipokukosea nisamehe nami nishasamehe uliponikwaza. Sam ni siku kadhaa hatujazungumza na ni kama siku yangu ya nne ama ya tano huku Dar es salaam. Kubwa zaidi la kukupigia hii simu ni kwamba hatimaye nikafanikiwa kuonana na mzee Matata. Sam yaleyale ya mzee Madati kurukwa akili ndo huku pia lakini afadhali huyu hajawekewa madawa lakini kupotea kwa mtoto wake kumemchanganya sana. Nilipofika kule mara ya kwanza nilizuiliwa kuingia eti kwamba mzee hatakiwi kuonana na watu madaktari wamekataza.
Nikaondoka kapa siku hiyo! Lakini sikufa moyo.
Sikukata tamaa Sam. Mara ya pili nikajieleza kuwa shida yangu kuonana na mzee ni kuhusu mwanaye. Wacha wee! Hapo sasa nikaonekana lulu mchangani, kila mtu ananiuliza kulikoni. Nikagoma kusema lolote hadi niongee na mzee. Kama yeye atawaeleza ni juu yake! Lakini mimi simwelezi mtu tofauti na yeye, na kama sitaruhusiwa siku hiyo basi tena hawataniona mimi kukanyaga pale nyumbani kwao.
Sam niliyasema haya huku natetemeka, maana najua kuwa maaskari watakuwa wameshirikishwa juu ya jambo hili, hivyo wakisikia kuna mtu anajua wanaweza kumweka kizuizini ili asaidie upelelezi. Nikaamua kujitoa muhanga huku nikiamini kuwa Mungu anamshika mkono mwenye haki.
Ama kweli damu nzito kuliko maji!!
Mzee akaelezwa nikakubaliwa kuingia japo walinionya kuwa ana tatizo la kubadilika badilika yule. Sikujali kuhusu hilo nilichotaka kuonana naye kwanza.
Sam, yule mzee amekwisha na hapa sasa naamini alikuwa akimpenda sana mtoto wake, yaani amekuwa dhaifu sana. Akanikodolea macho nami nikajiweka sawa, tulikuwa wawili tu, nikaanza kumweleza kilichonileta hadi pale, nikamsimulia baadhi ya matukio hadi ujio wa Anitha Iringa, sikukutaja wewe hata kidogo kwanza, nikadanganya kuwa alikuwa amekuja kufanya biashara huko.
Nikamwelezea juu ya mikasa ya ajabu ya Anti Ezekiel mjini Iringa. Mikasa ambayo inasemekana kuwa ni ya kishirikina ama mauzauza mengine!
Hapo akakodoa macho yule mzee, na kwa mara ya kwanza akasema na mimi. Kumbe na yeye ni mtu wa Iringa ni Mbena yule mzee. Hapa tukabadili lugha tukahamia katika kabila, nikasema naye kibena. Ushirikiano ukawa mkubwa sana tukawa marafiki.
Nikamweleza kuwa nauhitaji sana msaada wake maana hata mimi nimepoteza mtoto na kuna mwenzangu familia yake yote inateketea. Kufikia hapa nikaona hakuna haja yoyote ya kuendelea kuficha siri hii ilhali mzee ameonyesha ushirikiano na nilichokisema hakikuwa katika maandishi ningeweza kukibadili muda wowote ule!!!
Nikamtajia jina lako, sikumpa nafasi ya kusema lolote bali nikamlaumu kwa kutotaka kukusikiliza nikamweleza juu ya tuhuma unazozushiwa na watu wabaya na nd’o haohao wamemchukua mtoto wake. Kufikia hapo nikamweleza kuwa Anitha alikuwa katika harakati za kukusaidia wewe na wao wakagundua nd’o wamemshikilia.
Macho yakamtoka mzee na akatoa ushirikiano!!
Akakiri kuwa kuna watu walikuwa wakileta taarifa zile ofisini, na hakujua kama ni watu wabaya. Nikamuonya asithubutu kumweleza mtu yeyote juu ya hili maana hao watu ni hatari, wakigundua umewajua tu wanaanza kukuonya kimatendo, mzee akakiri kuitambua skendo hiyo ya UKIMJUA UNAPOTEA. Akajionya!!! Aliwahi kuisikia Iringa miaka hiyo!!
Kumbe ni mchezo wa miaka mingi tu huu Sam!! Na bado umefumbiwa macho. Anti Ezekiel ni nani hadi alibabaishe taifa letu!! Yeye ni nani katika ardhi hii huru??
Baada ya mazungumzo marefu tukapanga mikakati kabambe! Mkakati wa kumvumbua huyo Anti Ezekiel.
Mzee alichangamka na hakuna hata ndugu mmoja aliyeweza kuamini kuwa yule alikuwa mzee wao.
Leo asubuhi mikakati hiyo imeanza kufanya kazi!
Gazeti la mzee Matata limeandika taarifa zako kuwa umeonekana maeneo ya Dar es salaam mjini ukizurura.
Nia yetu kubwa ni kuwavuta hawa watu waje huku ili tuweze kushughulika nao vyema. Baada ya taarifa hiyo ofisi ya mzee Matata ikapokea simu kutoka kwa watu wanaojiita wapelelezi kutoka Iringa, mmoja akazungumza Kiswahili na mwingine akasema kiingereza. Wakadai wanahitaji kuonana na huyo mtu aliyekuona wewe waweze kujua wapi pa kuanzia ili kuujua ukweli, walilalamika kuwa wao wanaamini umekufa hivyo uzushi kama huo unashusha thamani ya utendaji kazi wao.
Kufikia hapo mzee Matata ameniamini sana na kujua ni kweli kuna jambo linafichwa nyuma ya pazia..
Hao mabwana wakawasili kutoka Iringa na kukutana na watu wa mzee Matata, ni mzungu mmoja na muafrika na wamekuja na gari binafsi aina ya Nissan patrol! Kwa leo wametoa tu salamu, kesho watakuwa ofisini kwa mzee Matata, japo mzee hatakwenda amewaambia wakitoka huko wamtembelee nyumbani kwake.
Kwa hiyo Sam hapo nd’o tumefikia!!
JOJINA AKAMALIZA.,
Nilikuwa natetemeka sana, ilikuwa ni sababu ya baridi pamoja na uoga tele huku kihoro cha matumaini kikinipagawisha. Mwanzoni nilikuwa na hasira wakati namsikiliza mama lao kwa sababu nilihisi mzee Matata ni mnafiki na anamhadaa lakini kumbe ile habari gazetini imepikwa maksudi ili kuwaweka karibu maadui kuwa marafiki ili shambulizi likifanyika wawe katika taharuki bila matarajio wala maandalizi ya kujikinga!!
Watu waliotajwa nilikuwa nimewaona asubuhi hiyohiyo katika kijumba cha Michigan!!
Cheupe dawa na yule mwenzake wapo Dar tayari.
Nikamweleza Jojina juu ya mkasa wangu kwa ufupi sana, nikamwelezea juu ya watu hao na jinsi wanavyoishi kimaajabu katika kibanda cha Michigan. Nikamwelezea kila nilichofanya hadi kufikia hatua ya kukuta tundu la kufunguliwa na funguo. Sikusita kumhakikishia kuwa cheupe dawa huyo ndiye aliyemkamata mke wangu jijini Dar…
“Jojina, tumekaribia kulipata jibu lakini kuna kitu kimoja ambacho kinanipa utata na kuniumiza kichwa, sehemu ya kufungulia geti la kuingia katika maficho yao imeonekana tayari na ninaweza kujua namna ya kupaingia tena. Lakini Jojina funguo hakuna Jojina, ile bahasha tuliyopoteza katika chumba chako kwenye operesheni mbwa okoa, ndani yake kulikuwa na funguo!!
Ni hizo na ninao uhakika kuwa Ezekiel alimaanisha kitu aliponipatia zile funguo!!
Nilimaliza kuongea nikamsikia Jojina akishusha pumzi zake kwa nguvu sana. Ni kama alikuwa ameungana nami katika kukata tamaa.
“Kweli huo ni mtihani mgumu, lakini Sam unakumbuka kuwa kila jaribu linalokuja kwa mwanadamu huwa linayo njia yake ya kutokea? Basi amini kuwa hata kikwazo hiki tukakiruka. Kama unaweza kwenda tena kwa huyo Masawe basi hakikisha kuwa unachukua alama ya hilo tundu ili tuweze kuchonga ufunguo wa bandia…….” Alianza kushauri Mama lao. Nikaingilia kati na kumweleza kuwa kile kitasa ni cha aina yake na hata ule funguo ulikuwa wa aina yake. Mama lao akasihi kuwa ni heri kujaribu kuliko kupuuzia.
Nikakubaliana naye, lakini kila nilivyoujengea picha ule ufunguo chakavu alionipatia Ezekiel na umbo lake la kustaajabisha niliamini kabisa kuwa zile zilikuwa mbio za sakafuni tulizokuwa tunajaribu kukimbia.
Lazima ziishie ukingoni tu!!
Tukaagana na mama lao, na kuahidia kupeana matokeo kwa siku inayofuata.
Huo ukawa usiku wenye matumaini kiasi fulani, lakini sikujua kama asubuhi ya siku inayofuata ingekuwa asubuhi ya kustaajabisha ndani ya jiji la Dar es salaam na wakati huo mjini Iringa!!!
Ni heri tusingefikia maamuzi yale!!
Lakini hatukujua!!!
***
**HARAKATI zinaendelea kushika kasi!! Je uwepo wa Matata utaleta unafuu ama utata mpya??
***SAM atafanikiwa katika harakati za kuupata ufunguo kwa kuchonga??
**Hii ni ya jana..... Itaendelea tena kesho saa KUMI KAMILI