Makapuku Forum

Makapuku Forum

SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE
.SIMULIZI: ANTI EZEKIEL
MTUNZI: George Iron Mosenya

SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE

Sasa leo ulipouleta ufunguo ulionisababishia majanga haya nikakuona kuwa wewe naye ni mmoja wa watu wabaya wanaofahamu siri yangu!! Sam kiuhakika nisingekutambua basi ungekufa kifo kibaya sana leo.” Alimaliza mzee yule kunieleza juu ya simulizi ile ya kutisha na kusisimua.
Mwili ulisisimka haswa nikijaribu kujenga picha juu ya mwanadamu kung’olewa jicho na kukatwa mguu.
Watu ninaokabiliana nao walikuwa wanyama haswa!!!

Wakati nikiendelea kufikiria juu ya tukio hilo la maajabu. Mara katika simu yangu ukaingia ujumbe!!
Hakuwa mwingine alikuwa ni Mama lao..
“SAM HALI SI SHWARI MZEE MATATA MATATANI”
Nilichoka!!!

Mzee akaishtukia hali ile ya hofu niliyokabiliana nayo, nami sikuona hiyana kumshirikisha. Nikamweleza juu ya Jojina na mkakati wetu. Na sasa amenasa huko jijini Dar.
“Mpigie simu tujue!! Kama ni hawa vijana niwaamnbie wakusaidie.” Alinishauri, nami nikapiga namba za Jojina.
Simu ikapokelewa!!
“Sam, huu mtandao ni hatari. Nasi tupo katika hatari kubwa sana. Mzee Matata amesimamishwa kazi, nyumba yake inauzwa juma lijalo.” Jojina alinieleza hayo kwa sauti ya chini tulivu!!
“Sikuelewi Jojina unamaanisha nini hata!!”
“Bosi wake mzee Matata ndo katoa tamko hilo la kumsimamisha kazi eti anaandika habari za kichochezi!!...” alijibu kinyonge.
Nikastaajabu, tangu zamani nilijua kuwa mzee Matata nd’o mmiliki wa ile kampuni, kumbe na yeye ana bosi wake. Nilistaajabu mno, kisha nikajenga picha ya huyo bosi wake na kujiuliza iwapo namfahamu ama nimewahi kuona Matata akiongozwa na mtu yeyote.
Hapakuwa na jibu la uhakika, na kama ningeamua kuwa na jibu basi ni kwamba ofisi kuu ya gazeti lile ilikuwa ile ya mzee Matata.
“Kwa hiyo sasa…” nilijikuta nikiuliza tu bila kuelewa kwa nini nauliza.
“Hatuna hata senti tano, akaunti zake zote zimefungwa. Mkewe tangu atoweke kwenda katika mambo ya vikao vya wanawake hajarudi na simu haipatikani.” Alizidi kunyong’onyea.
“Na mzee mwenyewe yupo wapi?”
“Nimemficha mahali Sam, hali si shwari na nimempa onyo asitoke hata kidogo. Hilo si jambo la kawaida. Amenielewa na ametii. Sam kiuhakika tunahitaji pesa kwa namna yoyote ile huku si kwema tena. Hawa watu wapo Tanzania nzima. Hakika ukiwajua ama ukitaka kuwajua tu unapotezwa!!” mama lao alisihi.
Sikuona haja ya kumweleza lolote ambalo mimi binafsi nilikuwa nimepitia, badala yake nilimuahidi pesa hiyo aliyoihitaji kuwa nitamtumia. Mzee Sendeu alitikisa kichwa kuunga mkono namna nilivyokuwa namjibu mama lao.
Jambo hilo likazidisha imani yangu kwake na mwisho akatokwa na machozi na kuniambia neno lililonifanya niingiwe uoga lakini na huruma vilevile.
“Natamani ningekuwa na miguu yangu yote miwili, natamani wasingeharibu jicho langu hili. Leo hii ningeongozana na wewe katika harakati hizi za kujua kuna nini kinafichwa hapa. Lakini wameniwahi na kunitia ulemavu wa maisha na bila shaka nikithubutu kutoka humu ndani wataniua kwanza mimi kabla ya kuwatesa sana ninyi!! Hawa si wanadamu wa kawaida Sam. Nakushauri kama ipo nafasi wewe jiweke mbali nao. Kaa mbali tu haidhuru kitu.
Sikukatishi tamaa lakini elewa kuwa namna yangu ya kupona na kuendelea kuwa hai si kila mmoja awezaye kupona hivi.” Alimaliza huku akinikazia jicho lake moja.
Chumba kilikuwa kimya kwa sekunde kadhaa kabla simu yangu haijaita tena!!
“Jojina..”
“Sam…. Nilisahau kukwambia kitu kimoja, katika purukushani hizi za hapa na pale nimegundua kitu, sijui kama ni chenyewe ama la!! Lakini hata kama ni chenyewe Sam, sikushauri uende mbele zaidi. “
“nini tena jojina…”
“Ni ule ufunguo chakavu, sina uhakika sana lakini nimekuta kitu kama hicho katika pochi langu!! Sijui kama ni wenyewe na hata kama ni wenyewe Sam nakusihi, tusitishe kwa muda kidogo harakati hizi hata pale tutakapoonana sote kwa pamoja…” kauli ya funguo ilituliza jazba zangu maana nilipanga kumkaripia mama lao kwa kuwa kigeugeu, mara juzi aniite mimi muoga leo hii tena anasema tuahirishe.
Na hapo likanijia wazo la kucheza na akili ya Jojina.
“Jojina ni kama ulikuwa katika mawazo yangu!! Umoja ni nguvu hakika, nitawangoja. Lakini nakusihi jambo moja ulifanye. Uagizie huo funguo kwa njia nyepesi uweze kunifikia huku. Nihakikishe kama ni wenyewe ili niachane na haya mambo ya kuchonga kisha nawasubiri…..fanya hima Jojina wakati hao wajinga wapo huko huko Dar.” Nikarusha maneno, yakamwingia Jojina…
Akakubaliana nami.
Hakujua kichwani mwangu nawaza nini. Nilikuwa na hasira na sikuwa na hofu tena.
Liwalo na liwe!!!!
Nikaagana na mzee Sendeu nikatoweka na kumwahidi kurejea tena kwake kwa ushauri zaidi.

BAADA ya siku mbili nikapokea funguo zile zikiwa zimetumwa kwa njia ya basi, ziliambatanishwa katika kitabu kikubwa katika bahasha, jina lililoandikwa ni Jonhson Fortunatus. Nami nikajitambulisha kwa jina lile nikapokea bahasha.
Swadakta!! Ulikuwa wenyewe, ufunguo alionipa Ezekiel maeneo ya Ubungo. Kitu ambacho sikujua matumizi yake lakini sasa natambua kuwa ni kitu muhimu sana ninachokihitaji.

Nikiwa na munkari ya hali ya juu sana, nikaondoka muda huohuo na kurejea nyumba ya kulala wageni. Huku nikaweka mikakati sawa. Mikakati ya kumhadaa Masawe tena ili nifanikiwe kutimiza jambo nililowaza!!
Kuingia katika hifadhi ile ya siri!!
Pombe!!
Ni hiki kitamfanya ahadaike na mimi niingie ndani!!
Nikasinzia na wazo hilo!!

*****

KINDO CHIZI

MASAWE alikuwa ameikubali ofa yangu, akaanza chupa ya kwanza, mara ya pili hadi ya sita akili yake ikawa imevurugika na akawa mcheshi sana. Mimi nilikuwa makini sikunywa kwa pupa. Nilitaka yeye alewe mimi nifaidike, wasiwasi ulikuwa kidogo maana nilishahakikishiwa kuwa watu wabaya walikuwa Dar es salaam wakinitafuta.
Nilibeba bia za kutosha na kuzileta katika banda la Masawe!!
Wachaga kwa pombe!! Mbona nilimuweza.
Masawe alipopendeza kichwani nami nikajifanya nimelewa nikaanza kumuuliza maswali hapa na pale.
Hatimaye akaanza kuropoka hapa na pale juu ya bosi wake.
“Bosi wangu mimi mpole sana lakini hataki tu kuchokozwa yule, yaani kingine hataki kabisa ujue mambo yake hovyohovyo, mimi sitaki kujua mambo yake kwa sababu ananilipa lakini mbili yangu, nakula na kulala bure. Bosi wangu mtu safi sana lakini watu wanamchokoza..” akasita kidogo kisha akabeua, akapiga funda jingine kisha akaendelea, “Mambo ya bosi ni ya bosi mimi hayanihusu, hata Kindo nilimwambia aache kuwa na kiherehere akaniona mimi bwege wa mwisho, eti kisa tu aliwahi kufanya kazi sijui wapi huko panaitwa eheee Michigani, nd’o huko na mimi niliambiwa nakuja kufanya kazi lakini nikaishia hapa, hata picha za hiyo hoteli sijawahi kuziona mimi. Kindo alikuwa ananihadithia, mara Michigani sijui inafanya nini mara huko Michigani nd’o kuna raha za dunia. Hebu tazama shehe wangu mfano mimi umeniajiri wewe halafu tena naleta mtu mwingine ndani ya duka lako, we utanielewa kweli. Sio mara moja au mbili, Kindo anamleta ndugu yake humu ndani, anaitwa nani vile sijui Alvin kitu kama hicho. Huyo Alvin akifika mara wananiambia nitoke nje, mara wananiambia mimi sijui mshamba.
Maneno yale yakanikera kweli ndugu yangu nikashindwa kuvumilia nikamweleza bosi.
Siku hiyo Kindo akaitwa na bosi, sijui waliongea nini hata lakini baada ya siku mbili akawa haji tena kazini, nikamkuta akiwa chizi huko anaokota makopo mtaani. Mimi siwezi kumchokoza mtu wa namna hii hata kidogo.”
“Na huyo Alvin wakasaidia kuokota makopo ama?” nikamuuliza Masawe mlevi.
“Alvin hakuonekana tena, bosi alikuwa haijui hata sura yake kwa jinsi alivyoniambia lakini alikuwa akimsaka sana. Nikamuuliza kama kuna tatizo. Akasema kuna vitu fulani havionekani mle ndani, huenda wameviiba…. Kuna kauli moja aliisema nd’o nikaamini kuwa si mtu mzuri huyu bwana. Akasema Kindo mwenyewe nshamtia uchizi hata hawezi kunisaidia kitu!!. Kwa maana hiyo ni yeye aliyemtia uhayawani yule jamaa. Wanadamu we acha tu…” alisikitika kisha akafakamia tena pombe!!
Akaniachia nafasi ya kufanya tafakuri, juu ya Kindo na jina hili la Alvini.
Sasa inamaana Alvin ndo Ezekiel kweli na hili ndo chimbuko lake, na je yawezekana baadhi ya vitu alivyochukua na ufunguo ulikuwa mmoja wa hivyo vitu? Pamoja na makaratasi yale labda!!
“Masawe!! Kwa hiyo Kindo yupo bado hapa Iringa na je akikuona hakukumbuki ama…”
“Hayupo yule, nilimsikia….. ujue bosi wangu ni rafiki yangu sana na ananiamini, nilimsikia akijisemesha ili nimsikie alisema kuwa hatimaye amemkamata huyo wa kuitwa Alvin, kisha akajisifu kuwa ameua ndege wawili wa jiwe moja jijini Dar yaani kindo na Alvin. Mimi kama unionavyo huwa simuulizi maswali na nadhani nd’o kitu anapenda yaani niwe bwegebwege hivi hivi.”
Majibu ya Masawe yakanitoa ukungu machoni!
Huyu bosi wake anajua kila kitu juu ya mkakati unaoisumbua akili yangu na anajua pia juu ya sakata zito la anti Ezekiel.
Nikataka kumhoji zaidi lakini alikuwa anakoroma tayari kwa usingizi.
“We Masawe wewe!! Masawe!!” nikajaribu kumtikisa lakini hakujibu kitu zaidi ya kuendelea kukoroma, hakika alikuwa amelewa!!
Ni hiki nilikuwa nahitaji, alewe sana ili aropoke mengi na kisha asinzie kabisa niweze kufanya yangu!!
Yote yalikuwa yametimia.
Ni mimi tu niliyesalia kuchukua maamuzi!!!!

Nikasimama kwa tahadhari, nikajipekua na kukutana na ule funguo kutoka jijini Dar es salaam.
Nikaingia hadi nikaufikia ule mlango wa siri, nikachomeka funguo ule. Mlango ukafunguka ulikuwa na kuselelesha kushoto na kulia. Nikauselelesha hivyohivyo. Nikapata upenyo nikachungulia ndani, palikuwa na mwanga hafifu sana, nikatega sikio nisikie kama kuna watu ndani yake lakini hapakuwa .
Nikajipenyeza vyema na kuingia ndani nikapokelewa na hewa murua si baridi sana lakini inayoburudisha. Nikashuka ngazi moja baada ya nyingine huku macho yangu yakitazama huku na kule, nilipoikanyaga ngazi ya tatu mara taa kali zikawaka, na mlango huku nyuma ukajifunga.
Hofu ikatanda!!!

**SAM amejitoa muhanga na kuingia katika mlango huo wa siri!!!
**NINI KITAJIRI HUMO!!! MILANGO IMEJIFUNGA!!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom