Makapuku Forum

Makapuku Forum

Na Mimi siuachi Urais wa Makapuku ng'o ht muandamane


......................
1469303355800.jpg
 
SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE
.SIMULIZI: ANTI EZEKIEL
MTUNZI: George Iron Mosenya

SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE

Sasa leo ulipouleta ufunguo ulionisababishia majanga haya nikakuona kuwa wewe naye ni mmoja wa watu wabaya wanaofahamu siri yangu!! Sam kiuhakika nisingekutambua basi ungekufa kifo kibaya sana leo.” Alimaliza mzee yule kunieleza juu ya simulizi ile ya kutisha na kusisimua.
Mwili ulisisimka haswa nikijaribu kujenga picha juu ya mwanadamu kung’olewa jicho na kukatwa mguu.
Watu ninaokabiliana nao walikuwa wanyama haswa!!!

Wakati nikiendelea kufikiria juu ya tukio hilo la maajabu. Mara katika simu yangu ukaingia ujumbe!!
Hakuwa mwingine alikuwa ni Mama lao..
“SAM HALI SI SHWARI MZEE MATATA MATATANI”
Nilichoka!!!

Mzee akaishtukia hali ile ya hofu niliyokabiliana nayo, nami sikuona hiyana kumshirikisha. Nikamweleza juu ya Jojina na mkakati wetu. Na sasa amenasa huko jijini Dar.
“Mpigie simu tujue!! Kama ni hawa vijana niwaamnbie wakusaidie.” Alinishauri, nami nikapiga namba za Jojina.
Simu ikapokelewa!!
“Sam, huu mtandao ni hatari. Nasi tupo katika hatari kubwa sana. Mzee Matata amesimamishwa kazi, nyumba yake inauzwa juma lijalo.” Jojina alinieleza hayo kwa sauti ya chini tulivu!!
“Sikuelewi Jojina unamaanisha nini hata!!”
“Bosi wake mzee Matata ndo katoa tamko hilo la kumsimamisha kazi eti anaandika habari za kichochezi!!...” alijibu kinyonge.
Nikastaajabu, tangu zamani nilijua kuwa mzee Matata nd’o mmiliki wa ile kampuni, kumbe na yeye ana bosi wake. Nilistaajabu mno, kisha nikajenga picha ya huyo bosi wake na kujiuliza iwapo namfahamu ama nimewahi kuona Matata akiongozwa na mtu yeyote.
Hapakuwa na jibu la uhakika, na kama ningeamua kuwa na jibu basi ni kwamba ofisi kuu ya gazeti lile ilikuwa ile ya mzee Matata.
“Kwa hiyo sasa…” nilijikuta nikiuliza tu bila kuelewa kwa nini nauliza.
“Hatuna hata senti tano, akaunti zake zote zimefungwa. Mkewe tangu atoweke kwenda katika mambo ya vikao vya wanawake hajarudi na simu haipatikani.” Alizidi kunyong’onyea.
“Na mzee mwenyewe yupo wapi?”
“Nimemficha mahali Sam, hali si shwari na nimempa onyo asitoke hata kidogo. Hilo si jambo la kawaida. Amenielewa na ametii. Sam kiuhakika tunahitaji pesa kwa namna yoyote ile huku si kwema tena. Hawa watu wapo Tanzania nzima. Hakika ukiwajua ama ukitaka kuwajua tu unapotezwa!!” mama lao alisihi.
Sikuona haja ya kumweleza lolote ambalo mimi binafsi nilikuwa nimepitia, badala yake nilimuahidi pesa hiyo aliyoihitaji kuwa nitamtumia. Mzee Sendeu alitikisa kichwa kuunga mkono namna nilivyokuwa namjibu mama lao.
Jambo hilo likazidisha imani yangu kwake na mwisho akatokwa na machozi na kuniambia neno lililonifanya niingiwe uoga lakini na huruma vilevile.
“Natamani ningekuwa na miguu yangu yote miwili, natamani wasingeharibu jicho langu hili. Leo hii ningeongozana na wewe katika harakati hizi za kujua kuna nini kinafichwa hapa. Lakini wameniwahi na kunitia ulemavu wa maisha na bila shaka nikithubutu kutoka humu ndani wataniua kwanza mimi kabla ya kuwatesa sana ninyi!! Hawa si wanadamu wa kawaida Sam. Nakushauri kama ipo nafasi wewe jiweke mbali nao. Kaa mbali tu haidhuru kitu.
Sikukatishi tamaa lakini elewa kuwa namna yangu ya kupona na kuendelea kuwa hai si kila mmoja awezaye kupona hivi.” Alimaliza huku akinikazia jicho lake moja.
Chumba kilikuwa kimya kwa sekunde kadhaa kabla simu yangu haijaita tena!!
“Jojina..”
“Sam…. Nilisahau kukwambia kitu kimoja, katika purukushani hizi za hapa na pale nimegundua kitu, sijui kama ni chenyewe ama la!! Lakini hata kama ni chenyewe Sam, sikushauri uende mbele zaidi. “
“nini tena jojina…”
“Ni ule ufunguo chakavu, sina uhakika sana lakini nimekuta kitu kama hicho katika pochi langu!! Sijui kama ni wenyewe na hata kama ni wenyewe Sam nakusihi, tusitishe kwa muda kidogo harakati hizi hata pale tutakapoonana sote kwa pamoja…” kauli ya funguo ilituliza jazba zangu maana nilipanga kumkaripia mama lao kwa kuwa kigeugeu, mara juzi aniite mimi muoga leo hii tena anasema tuahirishe.
Na hapo likanijia wazo la kucheza na akili ya Jojina.
“Jojina ni kama ulikuwa katika mawazo yangu!! Umoja ni nguvu hakika, nitawangoja. Lakini nakusihi jambo moja ulifanye. Uagizie huo funguo kwa njia nyepesi uweze kunifikia huku. Nihakikishe kama ni wenyewe ili niachane na haya mambo ya kuchonga kisha nawasubiri…..fanya hima Jojina wakati hao wajinga wapo huko huko Dar.” Nikarusha maneno, yakamwingia Jojina…
Akakubaliana nami.
Hakujua kichwani mwangu nawaza nini. Nilikuwa na hasira na sikuwa na hofu tena.
Liwalo na liwe!!!!
Nikaagana na mzee Sendeu nikatoweka na kumwahidi kurejea tena kwake kwa ushauri zaidi.

BAADA ya siku mbili nikapokea funguo zile zikiwa zimetumwa kwa njia ya basi, ziliambatanishwa katika kitabu kikubwa katika bahasha, jina lililoandikwa ni Jonhson Fortunatus. Nami nikajitambulisha kwa jina lile nikapokea bahasha.
Swadakta!! Ulikuwa wenyewe, ufunguo alionipa Ezekiel maeneo ya Ubungo. Kitu ambacho sikujua matumizi yake lakini sasa natambua kuwa ni kitu muhimu sana ninachokihitaji.

Nikiwa na munkari ya hali ya juu sana, nikaondoka muda huohuo na kurejea nyumba ya kulala wageni. Huku nikaweka mikakati sawa. Mikakati ya kumhadaa Masawe tena ili nifanikiwe kutimiza jambo nililowaza!!
Kuingia katika hifadhi ile ya siri!!
Pombe!!
Ni hiki kitamfanya ahadaike na mimi niingie ndani!!
Nikasinzia na wazo hilo!!

*****

KINDO CHIZI

MASAWE alikuwa ameikubali ofa yangu, akaanza chupa ya kwanza, mara ya pili hadi ya sita akili yake ikawa imevurugika na akawa mcheshi sana. Mimi nilikuwa makini sikunywa kwa pupa. Nilitaka yeye alewe mimi nifaidike, wasiwasi ulikuwa kidogo maana nilishahakikishiwa kuwa watu wabaya walikuwa Dar es salaam wakinitafuta.
Nilibeba bia za kutosha na kuzileta katika banda la Masawe!!
Wachaga kwa pombe!! Mbona nilimuweza.
Masawe alipopendeza kichwani nami nikajifanya nimelewa nikaanza kumuuliza maswali hapa na pale.
Hatimaye akaanza kuropoka hapa na pale juu ya bosi wake.
“Bosi wangu mimi mpole sana lakini hataki tu kuchokozwa yule, yaani kingine hataki kabisa ujue mambo yake hovyohovyo, mimi sitaki kujua mambo yake kwa sababu ananilipa lakini mbili yangu, nakula na kulala bure. Bosi wangu mtu safi sana lakini watu wanamchokoza..” akasita kidogo kisha akabeua, akapiga funda jingine kisha akaendelea, “Mambo ya bosi ni ya bosi mimi hayanihusu, hata Kindo nilimwambia aache kuwa na kiherehere akaniona mimi bwege wa mwisho, eti kisa tu aliwahi kufanya kazi sijui wapi huko panaitwa eheee Michigani, nd’o huko na mimi niliambiwa nakuja kufanya kazi lakini nikaishia hapa, hata picha za hiyo hoteli sijawahi kuziona mimi. Kindo alikuwa ananihadithia, mara Michigani sijui inafanya nini mara huko Michigani nd’o kuna raha za dunia. Hebu tazama shehe wangu mfano mimi umeniajiri wewe halafu tena naleta mtu mwingine ndani ya duka lako, we utanielewa kweli. Sio mara moja au mbili, Kindo anamleta ndugu yake humu ndani, anaitwa nani vile sijui Alvin kitu kama hicho. Huyo Alvin akifika mara wananiambia nitoke nje, mara wananiambia mimi sijui mshamba.
Maneno yale yakanikera kweli ndugu yangu nikashindwa kuvumilia nikamweleza bosi.
Siku hiyo Kindo akaitwa na bosi, sijui waliongea nini hata lakini baada ya siku mbili akawa haji tena kazini, nikamkuta akiwa chizi huko anaokota makopo mtaani. Mimi siwezi kumchokoza mtu wa namna hii hata kidogo.”
“Na huyo Alvin wakasaidia kuokota makopo ama?” nikamuuliza Masawe mlevi.
“Alvin hakuonekana tena, bosi alikuwa haijui hata sura yake kwa jinsi alivyoniambia lakini alikuwa akimsaka sana. Nikamuuliza kama kuna tatizo. Akasema kuna vitu fulani havionekani mle ndani, huenda wameviiba…. Kuna kauli moja aliisema nd’o nikaamini kuwa si mtu mzuri huyu bwana. Akasema Kindo mwenyewe nshamtia uchizi hata hawezi kunisaidia kitu!!. Kwa maana hiyo ni yeye aliyemtia uhayawani yule jamaa. Wanadamu we acha tu…” alisikitika kisha akafakamia tena pombe!!
Akaniachia nafasi ya kufanya tafakuri, juu ya Kindo na jina hili la Alvini.
Sasa inamaana Alvin ndo Ezekiel kweli na hili ndo chimbuko lake, na je yawezekana baadhi ya vitu alivyochukua na ufunguo ulikuwa mmoja wa hivyo vitu? Pamoja na makaratasi yale labda!!
“Masawe!! Kwa hiyo Kindo yupo bado hapa Iringa na je akikuona hakukumbuki ama…”
“Hayupo yule, nilimsikia….. ujue bosi wangu ni rafiki yangu sana na ananiamini, nilimsikia akijisemesha ili nimsikie alisema kuwa hatimaye amemkamata huyo wa kuitwa Alvin, kisha akajisifu kuwa ameua ndege wawili wa jiwe moja jijini Dar yaani kindo na Alvin. Mimi kama unionavyo huwa simuulizi maswali na nadhani nd’o kitu anapenda yaani niwe bwegebwege hivi hivi.”
Majibu ya Masawe yakanitoa ukungu machoni!
Huyu bosi wake anajua kila kitu juu ya mkakati unaoisumbua akili yangu na anajua pia juu ya sakata zito la anti Ezekiel.
Nikataka kumhoji zaidi lakini alikuwa anakoroma tayari kwa usingizi.
“We Masawe wewe!! Masawe!!” nikajaribu kumtikisa lakini hakujibu kitu zaidi ya kuendelea kukoroma, hakika alikuwa amelewa!!
Ni hiki nilikuwa nahitaji, alewe sana ili aropoke mengi na kisha asinzie kabisa niweze kufanya yangu!!
Yote yalikuwa yametimia.
Ni mimi tu niliyesalia kuchukua maamuzi!!!!

Nikasimama kwa tahadhari, nikajipekua na kukutana na ule funguo kutoka jijini Dar es salaam.
Nikaingia hadi nikaufikia ule mlango wa siri, nikachomeka funguo ule. Mlango ukafunguka ulikuwa na kuselelesha kushoto na kulia. Nikauselelesha hivyohivyo. Nikapata upenyo nikachungulia ndani, palikuwa na mwanga hafifu sana, nikatega sikio nisikie kama kuna watu ndani yake lakini hapakuwa .
Nikajipenyeza vyema na kuingia ndani nikapokelewa na hewa murua si baridi sana lakini inayoburudisha. Nikashuka ngazi moja baada ya nyingine huku macho yangu yakitazama huku na kule, nilipoikanyaga ngazi ya tatu mara taa kali zikawaka, na mlango huku nyuma ukajifunga.
Hofu ikatanda!!!

**SAM amejitoa muhanga na kuingia katika mlango huo wa siri!!!
**NINI KITAJIRI HUMO!!! MILANGO IMEJIFUNGA!!!
 
SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO
.SIMULIZI: ANTI EZEKIEL
MTUNZI: George Iron Mosenya

SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO

Nikasimama kwa tahadhari, nikajipekua na kukutana na ule funguo kutoka jijini Dar es salaam.
Nikaingia hadi nikaufikia ule mlango wa siri, nikachomeka funguo ule. Mlango ukafunguka ulikuwa na kuselelesha kushoto na kulia. Nikauselelesha hivyohivyo. Nikapata upenyo nikachungulia ndani, palikuwa na mwanga hafifu sana, nikatega sikio nisikie kama kuna watu ndani yake lakini hapakuwa .
Nikajipenyeza vyema na kuingia ndani nikapokelewa na hewa murua si baridi sana lakini inayoburudisha. Nikashuka ngazi moja baada ya nyingine huku macho yangu yakitazama huku na kule, nilipoikanyaga ngazi ya tatu mara taa kali zikawaka, na mlango huku nyuma ukajifunga.
Hofu ikatanda!!!

***

Hofu ikaanza kutanda, nikageuka nilipotokea palikuwa na mwanga mtupu sikuuona mlango.
Maajabu. Nikaendelea mbele huku nikitetemeka. Kwa mbali nikajihisi kujutia kile kitendo cha kuzama katika mkasa huu ambao mama lao alikuwa amenishauri tuungane pamoja kuweza kuumaliza taratibu na kiuhakika.
Njia zilikuwa nyingi sana na sikujua njia ipi inaenda wapi, kila njia ilikuwa na herufi zake tofauti!!
Jumba la maajabu!! Nikakiri hata kabla ya kuelewa kama nitatoka salama ama la!!
Nikacheza pata potea nikachagua njia ya kuifuata. Niliponyanyua uso wangu juu. Mara macho yangu yakaiona ile picha fulani hivi, nikaamua kusogea taratibu ili niweze kuitambua kama ni yenyewe ama la. Sikuhiotaji kutembea sana kabla sijahakikisha kuwa ile picha ninayoiona mbele yangu ilikuwa picha ya mtoto. Si mwingine ni ya mtoto ambayo kwa mara ya kwanza niliiona katika makablasha ya Ezekiel ambaye naaminishwa kuwa jina lake lilikuwa Alvin.
Picha hii haikuishia pale tu, pia Anitha alinitumia picha ambayo inaonyesha picha hii, na akadai hajui wapi alipo. Kisha akatekwa na wanaume waliovaa suti nyeusi!!
Hata mimi sijui nilipo!! Mungu wangu!!.. nikahanika nisielewe kama nipo sahihi kuwa eneo lile ama sipo sahihi. Na hata kama sipo sahihi bado nilitakiwa kuwa pale maana mlango haukuwa ukionekana tena.
Nikajiuliza ilikuwaje Anitha akafika eneo kama lile na nkupiga picha, ama kuna eneo jingine zaidi aliwahi kufika maana picha ile ni kama ile aliyonitumia katika barua pepe. Pangekuwa na hali ya kawaida kidogo tu jasho lingeweza kunitoka lakini hali ya hewa ilikuwa baridi la kiyoyozi. Ukimya ulitanda sana.
Hapakuwa na kelele hata kidogo!!
Nikaendelea mbele kidogo, mara nikasikia kama mchakato fulani hivi, nikatega sikio vyema nitambue ni kitu gani kinafurukuta ndani ya jingo lile. Sikuwa nimejiandaa kwa majibu yoyote endapo nikikamatwa pale. Maisha yangu niliyaweka rehani.
Mara ule mchakato ukaongeza kelele na nikasikia vishindo nyuma yangu!! Macho yakanitoka nikataka kukimbia lakini sikwenda mbali, nikakanyaga kamba za viatu vyangu na kupiga mweleka chini!! Nikataka kusimama, macho yangu yakakautana na viumbe wawili. Waliponiaona wakageuza na kurudi walipotoka kwa mwendokasi wa kutisha. Nikasimama na kutabasamu kidogo huku nikiunyoosha mkono wangu na kusikitika sana kupiga mweleka nikiwakimbia panya buku!! Wasiojua hata maana ya uwepo wangu ndani ya jumba lile la siri kubwa!!
Hofu ikatoweka tena nikaendelea na njia ile hatimaye upande wa kulia nikaiona njia iliyonyooka vyema nikaifuata huku nikiwa na hofu juu ya uhai wangu, lakini nisingeweza kurudi nyuma hata kidogo maana niliamini hiyo ilikuwa njia ya kwenda kuikomboa familia yangu. Njia hii ilitia matumaini kiasi fulani, ilikuwa imetandikwa zulia jekundu.
Sam, nikajikuta natembea katika zulia jekundu. Lakini sikuwa na amani bali hofu na uoga tele. Kwa mbali nikamuona mtu!!
Nikashtuka sana kwa mara ya kwanza kumuona mtu katika kasri ile ya maajabu!! Nikataka kukimbia na yeye akataka kufanya hivyo, nikaanza kurudi kinyume nyume na yeye akaniiga, halafu na yeye alikuwa na hofu kubwa. Hili likanipa matumaini ya kutomuogopa, nikaamua kwenda mbele. Na yeye akaenda mbele ili tukutane.
Na hapo nikagundua kuwa nilikuwa naiona taswira yangu katika chumba kilichojengwa kwa kutumia vioo.
Nikatabasamu na ile taswira nayo ikatabasamu!!
Mapigo ya moyo yakapungua mwendo kasi. Nikaacha kuitazama ile taswira nikalitazama lile jengo la kuvutia.
Nikanyanyua macho juu ili nione urefu wake unafikia kimo kipi, mwisho wa jingo lile nikakutana na maneno makubwa ya kung’ara. Yaliyoniduwaza, nikayasoma mara mbili mbili.
“MICHIGANI HEAD OFFICE”
Moyo ukapiga kwa nguvu sana.Nikagutuka na kutaka kukimbia, ile Michigani niliyokuwa naitafuta miezi kadhaa, michigani inayosadikika kuchomwa moto ilikuwa mbele yangu. Badala ya kufurahia nikahofia kukumbwa na mambo mabaya katika jumba hilo la aina yake, nilikuwa ndani ya ile Michigan niliyokuwa naitafuta siku zote kwa ajili ya kung’amua siri juu ya Ezekiel.
Nikakisogelea kile kioo na kuangaza ndani kwa namna ya kuchungulia.
Nikaona kiti cheusi cha kuzunguka kilikuwa wazi na kuna koti lilitundikwa juu yake, bila shaka kuna mtu alikuwa hapo.
Nikaendelea kuangaza nyuma yake juu nikaona picha iliyotundikwa, niliwahi kuiona mahali sura ile.
Nikajitahidi sana kutuliza akili nikatambua kuwa niliiona nyumbani kwa Ezekiel, hiyo picha ya mwanaume wa kizungu, na pia hiyo picha ilikuwa katika yale makablasha niliyokuwa nimeyabeba kutoka nyumbani kwake ambapo nilikutana na maiti yake. Lakini si hivyo tu hii picha kuna mahali pa ziada kabisa nilipata kuiona kwa dharula sana, nikakifinyafinya kichwa changu nikumbuke kama ni kweli niliona picha ama mtu halisi mahali.
Hakuwa cheupe dawa, huyu alikuwa tofauti sana!!
Alikuwa anatabasamu!! Bila shaka ile ofisi ilikuwa yake na yeye ndiye alikuwa kinara wa kasri hilo la Michigani.

Ile hali ya kuamini kuwa ndani ya hilo kasri kuna watu wanaishi iliniletea wasiwasi mkubwa sana. Nikajitabiria kifo iwapo nitagundulika kuwa eneo lile kiholela na si mwenzao bali adui yao. Wazo likanijia la kuvujisha baadhi ya siri ambazo zinaweza kuwawezesha mama lao na mzee Matata kuweza kugundua kambi hiyo hata Kama nikiwa nimekufa kinyama waweze kuyapata maiti yangu. Na ukweli uwe wazi. Nikajiahidi kuwa nitapiga picha na kisha kama itawezekana nizitume kwa njia ya email nikiwa humohumo Michigani. Na litakalotokea baada ya hapo ni kuwaachia walio hai walifikishe kwa walio hai wenzao. Sikuwa naogopa tena kufa iwapo tu mama lao atanielewa.
Nikajipekua na kuitoa simu yangu nitazame uwezekano wa kuwasiliana. Nikajaribu kubofya vitufe kadhaa nimpigie Jojina lakini simu haikuwa na mtandao. Nikainyanyua huku na kule lakini tatizo likabaki kuwa lilelile.
Hapakuwa na uwezekano wa kuzungumza kwa njia ya simu ukiwa ndani ya ficho lile la ajabu!!
Nikaanza safari ya kurudi kutoka nje!! Nikajiapiza kuwa nitauvamia mlango na iwe isiwe mpaka niufungue tena.
Nikajipekua na kuushika vyema ule ufunguo wenye kutu ambao kwa tahadhari kuu niliuchomoa pale mlangoni baada ya lango kukubali kufunguka. Sasa nilihitaji kufungua tena niweze kutoa nje na kisha kufanya mawasiliano na mama lao kisha nirejee tena kikamilifu. Nikajipa imani kuwa nitakumbuka kila hatua niliyokuwa nimepita kabla kuingia eneo la ofisi ile.
Hapa nilitamani kulia, maana nilipotea njia huku na kule, nikajaribu kutuliza akili lakini sikuweza hata kidogo kukumbuka ni wapi nilitokea hadi kufika humo ndani. Kila upande niliojaribu kwenda ulikuwa mrefu kuliko mwingine, na karibia kila kona ilifanana na kona nyingine.
Nikahaha huku na huko, bado hali ilikuwa tete, nikafikia mahali nikakutana na ukumbi mwingine ukiwa umezungukwa vioo pia. Nikiwa pale nikashangaa kuona watu kwa ndani, kabla sijajua nifanye nini niliwaona wakinijia kwa kasi sana, nikaanza kurudi kinyumenyume.
Nikagota katika vioo vingine, nikawa natazamana ana kwa ana na wale watu! Walikuwa uchi na wote niliowaona kwa harakaharaka walikuwa watoto wa kiume.
Walikuwa wakinisihi jambo fulani lakini sikuweza kuzisikia sauti zao, nilitamani kuwasikiliza zaidi lakini hata mimi nilikuwa matatani na sikuwa natambua ni wapi nimetokea na wapi sahihi natakiwa kwenda.
Masaa yalikatika nisijue nimekaa humo ndani kwa muda gani.
Hali ya mule ndani haikubadilika ili kuwezesha kutambua kama ule ni usiku sana ama ni mchana au asubuhi, hali ilikuwa ileile, nilipanda na kushuka lakini sikuweza kuuona mlango wa kutokea. Michigani ilikuwa Michigani haswa.
Nikaendelea kuhaha na hatimaye nikakutana na mlango mwingine na huu nikaufungua baada ya kuona kitundu kikifanana na ufunguo wangu, nikadhani kuwa hata ile yaweza kuwa njia ya kutokea.
Looh!! Nikakutana na mwanaume akiwa amechoka sana na bila shaka alikuwa amekata tamaa, nikastaajabu mambo mawili. Ule ufunguo na yule bwana aliyefungiwa mle ndani ya kile chumba kidogo. Alikosa nini hadi atendwe vile.
“Nisa….saidie..” aliongea sauti ya chini, alikuwa amekonda na ngozi yake kubabuka kama aliyemwagiwa mafuta ya moto.
“Wewe ni nani….” Niliuliza kiuoga huku nikijiweka mbali naye.
“Anti…..Anti…Ezekiel….” alijitambulisha kwa shida sana, nikashangaa utambulisho huu. Kivipi hawa wa kuitwa Anti Ezekiel wawe wengi kiasi hiki. Nikainama na kumtazama vyema nikidhani kuwa ni yule aliyeniingiza matatani na familia yangu kutokomea kwa sababu yake. Lakini hata kama alikuwa amechakaa namna gani, hakufanania na yule Ezekiel ninayeaminishwa kuwa anaitwa Alvin. Huyu alikuwa tofauti kabisa.
Hawa jamaa vipi? Nilijiuliza huku nikihisi hasira kali ikinitwaa kwa sababu ya fumbo ambalo nilidhani kwa kuwa ndani ya michigani nitakuwa nimelifumbua badala yake hali iliendelea kuwa tete.
“Sikuelewi…sikia wewe ni mwenyeji humu ndani? Niambie niambie tafadhali natoka vipi ili niweze kukusaidia..” nilimsihi kwa sauti ya chini kiasi.
“Ni ngumu … wanafunga kila upande wa jumba hili…wanaiita nchi yao…” alilalama kwa sauti ya kunong’ona.
“Kina nani wanaoiita nchi yao eeh!! Ni akina nani hao.” Nilihoji upesi upesi sasa nikiwa nimechuchumaa.

“Wazungu na vibaraka wao wa kiafrika….fungua ofisi chukua nyaraka ukifanikiwa kutoka kaitangazie dunia… ”
“Ofisi ipi..na nyaraka ipi sasa eeh!!…” sikuelewa kabisa yule bwana anajaribu kuniambia kitu gani. Kila aliochokisema kilikuwa kipya.
“965901” alizitaja namba zile kwa tabu na hakuweza kuongea tena akabaki kunitazama huku mikono yake inayotetemeka ikinisihi kurejea nilipotoka.
Nikatamani kumbeba lakini ningempeleka wapi, nikarejea njia niliyotoka, nikaifuata kwa muda na kukutana na tena na ile ofisi kubwa ya vioo. Safari hii sikupotea sana. Nikachungulia na kuona kablasha kubwa mezani.
Huenda ni hilo!!! Nikajiongeza!! Na hapo nikaona mahali pa kufungua mlango kwa kutumia namba za siri.
Nikaanza kubofya!!
96…..59….. Mungu wangu!! nikasahau namba mbili za mwisho. Nikajaribu kukumbuka lakini haikuwezekana, yule bwana alizitaja mara moja, na hapo nikatambua kuwa sikumsikiliza kwa makini na sasa niliuona umuhimu wa namba zile.
Nikatimua mbio hadi kwa yule bwana tena, nikamkuta akiwa bado amekodoa macho, hakuyapepesa hata kidogo.
“Nimesahau namba mbili za mwisho ndugu yangu….namba za siri…TISA SITA TANO TISA…….” nikamtajia ili amalizie lakini hakuwa akiweza tena kusema , akabaki kukodoa macho, mkojo kidogo unitoke kwa kutamani aweze kusema ili nijue ni nini katika makablasha yale.
Nikamtikisa lakini hakuonekana kupatwa na hisia zozote zile!!
Mkojo ukachuruzika!! Sikuweza kuuzuia!!
Na hapo nikasikia vishindo kwa mbali!!!!
Hofu ikazidi.

**SAM amesahau namba za siri za kuingia ofisi kuu ya MICHIGAN… Anayezijua namba amenyamaza kimya tayari……

NINI KITAJIRI KATIKA CHIMBO HILO!!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom