SEHEMU YA TANO
KIJIJI CHA MINDE - BAGAMOYO
“Babu! Babu!” kijana wa makamo alimwita babu yake huku akiwa anahema kama aliyefukuzwa na mbwa.
“We, nini?” babu yake aliyekuwa ameketi chini na wavuvi wenzake wakiwa wanasuka nyavu zao alimjibu kwa kumwuliza.
“Ame- ameam- amemka, yule mtu ameamka…”
Yule mzee akawatazama wale wavuvi wenzake na wote wakakurupuka na kukimbimbilia kwenye ile nyumba walimomlaza huyo mtu. Walipofika waliingia taratibu bila kufanya kelele na kumtazama.
“Oooh! Ameamka, asante binti kwa dawa ulizompatia,” Yule babu alimshukuru binti aliyekuwa kando na chungu chake kikubwa kilichojaa maji ya kijani.
“Bila asante, ni wajibu wangu kumsaidia,” akajibu.
Wale wazee wakasogelea kitanda na kumzunguka wakimtazama, naye pia alizidi kuwatazama kwa kuwashangaa.
“Niko wapi? Niko wapi hapa?” akauliza kwa ukali na kmkunja kanzu mzee mmoja aliyekuwa jirani nay eye.
“Aaah a a a! kijana tulia kwanza, hapa upo mahali salama kabisa,” mzee mwingine alimsihi mtu huyo kwa lugha ya pwani.
“Wewe ni nani kijana?” Yule mzee akauliza.
Yule mtu akawashangaa tena, akawatazama na kuwakazia macho, kisha akajitahidi kukaa na kuegemea ukutani.
“Naitwa Amata,” akajibu kwa kifupi.
“Amata! Pole sana Amata, tumekuokota baharini ukisukwasukwa na mawimbi makali. Mungu mkubwa kwani yalikupeleka mpaka kwenye mikoko nasi tumekuona huko, nini kilikupata kijana,”
Amata akanyamaza kimya akifikiria jambo, akijaribu kuvuta kumbukumbu kwa lile lililotokea.
SAA 20 ZILIZOPITA
Ajali ya ndege.
Mara tu baada ya kiti cha Amata kufyatuka na kutoka nje wakiwa angani, parachute alilokuwa akitumia Amata likagoma kufyatuka, akahangaika nalo huku msukosuko ukiendelea. Kutoka kwenye ile ndege akaanza kuanguka kwa kasi huku akielekea baharini.
“Scobaaaaaa!!!!” aliita kwa nguvu lakini mwito wake haukuwa na nguvu kwani Scoba naye alikumbwa na maswahiba wake. Kutokana na lile parachute kushindwa kufunguka, Amata alitua baharini kwa kishindo na kuzama kwa sekunde kadhaa kabla ya kuibuka juu. Kwa mbali aliiona kitu kama boti ikija kwa kasi na kupunga mikono kuomba msaada lakini badala ya msaada wale jamaa wakafyatua risasi kumshambulia, Amata akapiga mbizi na risasi mbili zikampata eneo la mgongoni. Jua lilififia machoni pa Amata, kiza kikayafumba macho yake, akajikuta anapoteza nguvu na ukimya mkuu ukamchukua.
“Nimekwisha!” akajitahidi kutamka kwa taabu.
“Ma-da-m S” akajitahidi kuita kwa nguvu lakini bado aliona giza likimzidi nguvu.
† † †
“Shabash, nimempata kwisha habari yake,” kijana mmoja alikuwa akishangilia kwenye ile boti. Huku akipiga risasi nyingine hewani.
“Una uhakika?” Mwenzake akauliza.
“We sogeza mashine pale uone, maiti tu ile,”
Ile boti ikasogea mpaka pale na kuukuta mwili wa Amata ukiwa kifudifudi. Wakautazama na kuondoka zao.
“Buriani, hatuna historia ya kubeba maiti,” Yule nahodha wa chombo akageuza na kuondoka zao mpaka katika kambi yao iliyojengwa katika moja ya visiwa vilivyozunguka eneo hilo.
† † †
Mawimbi ya bahari yakausukumasukuma mwili wa Amata na kuutupia kwenye mikoko iliyofungana katika pwani ya eneo hilo, na kunasa huko.
Jioni ya saa kumi na mbili hivi wavuvi kutoka kijiji cha Minde walikuwa wakipita kuelekea katika shughuli zao huko katikati ya bahari, wakiwa na karabai zao wakipita pembezoni kabisa karibu na ile mimea ndipo walipouaona mwili huo.
“We hebu mulika pale,” mzee mmoja akamwambia nahodha wa chombo hicho.
“Nini?”
“Yule siyo mtu Yule?” wakatazama kwa makini na kugundua ni mwili wa binadamu, wakashuka na kutumbukia majini mpaka eneo lile.
“Oh Shit, si ajabu akawa hai huyu, mtazame!” wakamgeuza geuza na kuamua kumbeba. Safari ya kwenda uvuvini ikaghairishwa na wazee wale wakaamua kurudi kijijini. Walifika na kumshusha Amata kisha wakamlaza chini mkekani huku wakisogeza moto jirani ili kumpa joto. Mzee mmoja alikwenda kumwita binti anayesifika kujua dawa za asili, akaja na kuanza kumfukizia Amata moshi wa mchanganyiko wa majani na magome makavu ya miti.
“Hajafa bado huyu?” mzee mmoja akauliza.
“Hapana hajafa huyu, ila amezimia na yuko mbali sana katika mzimio wake, ninamwita polepole ataamka tu,” yule binti akajibu.
Matibabu hayo ya kienyeji yaliendelea mpaka asubuhi yake na mchana wa siku hiyo Amata alirudiwa na fahamu
SIKU ILOFUATA
Amata alitoka nje ya nyumba hiyo majira ya saa nne asubuhi, akasimama nje na kuangali upande wa baharini, akiwa hajui ni wapi alipo mpaka dakika hiyo. Akiwa bado hajisikii vyema sana hasa sehemu Fulani za mwili wake ambako kulikuwa na kitu kama jeraha aliendelea kutembea hapa na pale pale kijijini akiangalia hiki na kile. Nyuma yake akahisi mchakacho wa nyayo za binadamu, akasimama na kusubiri.
“Naona una nguvu sasa,” sauti nyororo ya kike ikasikika nyuma yake, akageuka na kugongana macho na mwanadada mrembo aliyekuwa ndani ya mavazi ya kawaida kabisa ya kijijini.
“Ndiyo, sasa najisikia nafuu zaidi, ila maumivu tu eneo hili,” akamjibu na kumwonesha eneo lenye maumivu.
“Pole, unywe ile dawa niliyokupa, ndani ya saa sita mpaka kumi zijazo utajisikia sawa kabisa, ni dawa nzuri kwa majeraha kama hayo,” Yule mwanadada akamweleza.
“Unaitwa nani?” Amata akauliza.
“Minde!” akajibu huku wakiwa wanatazamana na Amata.
“Asante Minde, umeokoa maisha yangu, unastahili zawadi, zawadi kubwa kabisa. Niambie hapa ni wapi?”
“Hapa ni Minde,”
“Minde tena?” Amata akauliza kwa kupata uhakika.
“Ndiyo, usishangae, kijiji hiki kinaitwa Minde na mimi naitwa Minde,” Yule mwanadada akamweleza Amata kisha akauchomoa mfuko wa plastiki ndani ya kanga yake kuukuu na kumpa Amata. Alipoupokea alihisi wazi uzito wa kiasi wa mfuko huo, akaufungua ndani na kuangalia, akatabasamu kisha akamwangalia binti Yule kwa kumkazia macho.
“Minde!” akaita kwa sauti tulivu.
“Umevipata wapi hivi?” akauliza.
“Nimevitoa kwenye nguo zako ulizovaa,” akajibiwa. Kamanda Amata akavimwaka juu ya jiwe lililokuwa jirani. Kwanza akachukua bastola iliyokuwa hapo, akaivuta slider yake na kuirudisha, akaifyatua kitako na kuchomoa magazine iliyojaa risasi, akazipachua moja moja na baadae akazirudishia tena. Akamtazama Minde akamwona jinsi alivyojawa na woga.
“Mbona unaogopa?” akamwuliza.
“Mmm umejuaje kama naogopa?”
“Nikimwangalia mtu usoni huwa najua kila kinachofanyika ndani ya ubongo wake,” wote wakacheka.
Amata akachukua waleti iliyokuwa pamoja na hivyo, akaifungua na kukuta kila kitu chake kipo salama, ndani yake licha ya vitambulisho kulikuwa na fuba la pesa za kitanzania kama shilingi laki tatu hivi, akachomoa noti kadhaa zilizofungwa vyema. Akazihesabu harakaharaka zilikuwa shilingi laki moja.
“Hii zawadi yako Minde,” akamkabidhi, Minde akamtazama Amata kwa jicho la uchu na kumshukuru kwa kibantu. Amata alimkumbatia Minde mikononi mwake huku akimwangalia usoni na kuyaona macho yanayojaa machozi.
“Minde, nahitaji kuondoka sasa, nitakuja kukusalimia tena,” akamuaga lakini ilikuwa ngumu kwa Minde kumruhusu Amata kutoka pale, alimbembeleza akae japo siku moja zaidi lakinia Amata alijua wazi kuwa kwa vyovyote wenzake watakuwa wakimtafuta. Akaichukua saa yake sasa hii ilikuwa ya mwisho kuitoa katika ule mfuko, akaizungusha mahala Fulani na kutazama kwenye kioo, kisha akamtazama Minde.
“Hapa ni Bagamoyo?”
“Ndiyo”
Baada ya kama saa tatu hivi, Minde alimruhusu Amata kuondoka kwa minajiri ya kuonana tena, Amata akaagana na wale wazee na kuanza kufuata barabara taratibu kuelekea barabara kubwa ambapo angepata usafiri wowote.
MASAKI - saa 1:30 usiku
MADAM S alisimamisha gari ndani ya uwa wa nyumba yake na kuruhusu lile geti lijifunge lenyewe nyuma yake. Aliposhuka garini akavuta hatua kuelekea mlango mkubwa wa kuingilia ndani huku akitumia simu yake ya mkononi kuzima kengele na kamera za hatari ambazo huziacha zikifanya kazi kama yeye hayupo. Akaufungua mlango na kuingia ndani alipouelekeza mkono wake kuwasha taa, taa zikawaka zenyewe na sebule yote ikang’azwa na mwanga wa kupendeza.
Madam S alipigwa na mshangao, akabaki akikodoa macho huku mkono wa kuume ukiwa tayari na bastola kiganjani.
“Amani!” sauti ya Amata ikasikika.
“Uhhhhh! Siku nyingine utakuja kufa wewe, kwanza ulikuwa wapi?” Madam S akaanza kufoka.
“Nilikuwa kuzimu, na sasa nimefufuka katika wafu,” Amata akajibu.
“Shiiiit! Mzima wewe? Au mzuka!”
“Njoo unipapase maana mzuka hauna mifupa wala nyama,” Amata akajibu.
“Oh! No.”
Madam S akainua simu yake na kubofya tarakimu Fulani kisha akaweka sikioni.
“Hello (…) sawa, njoo haraka nyumbani kwangu,” alipomaliza hayo akakata simu.
Moja kwa moja akakindea kiti kilicho mbele kinachotazamana na Amata.
“Nini kilikupata Amata, na ulikuwa wapi?” akauliza. Amata akainua fulana yake aliyoivaa na kumuonesha Madam S jeraha la risasi kwenye nyama za ubavu wake.
“Sifi tena kama hii haijaniua,” akajibu huku akifunika na kumwacha Madam S akiwa kinywa wazi kisha Amata akamsimulia kila kilichomsibu.
“Kamanda Amata, nilishatakiwa kutangaza kifo chako lakini nilikataa na kuwahakikishia kuwa upo hai kwa sababu najua wazi kuwa ni Mungu atakayeichukua roho yako lakini binadamu mwingine awaye yote,” madam akaeleza.
“Umenea sawa, vipi kuhusu Scoba?”
“Scoba tulimpata usiku wa siku hiyohiyo, sasa ni mzima na anaendelea vyema, hataki kabisa kusikia habari za kuwa wewe umekufa,”
“Yuko wapi?”
“Shamba, bado yuko shmba na hatuwezi kumwacha hadharani tuliliweka hivyo ili kuhakikisha kuwa tumekupata kama siwewe basi mwili wako,” Madam akaeleza.
“Nipo hai, ninaishi kwa mara nyingine tena, je mlifanya lolote kwa kumsaka Pancho?”
“
“Hapana kamanda, tuliliacha kama lilivyo, japo mpenzi wako Gina hana raha kabisa kwani hata yeye ana huzuni na kifo chako,” Madam S akaendelea kuzungumza na Amata juu ya tukio hilo liliwapa mshtuko mkubwa na kuwafanya kiasi Fulani kutikisika.
Wakati huohuo honi za gari zikasikika getini Madam S akabonya swichi maalumu iliyowekwa ukutani na kuruhusu geti hilo kufunguka. Gari ndogo aina ya RAV 4 ikajitoma ndani. Amata akasimama pale alipo na kuitazama gari hiyo ikiingia taratibu, ‘Jasmine,’ akawaza na kurudi kitini. Hali ya Jasmine ilikuwa ileile pindi tu alipoingia nyumbani kwa Madm S, alipatwa na mshtuko alipomuona Amata pale kitini. Baada ya mazungumzo ya kina alilitazama jeraha la Amata.
“Inabidi tusafishe,” akamwambia.
“No, nina dawa nimepaka hapo, huo weusi sio uchafu,” akamjibu.
“Ok, hata hivyo inabidi sasa kwenda pamoja Shamba tukaweke mikakati yetu vizuri hakuna kulala,” Madam aliwaeleza vijana wake na wote wakajipanga kuondoka. Chiba na Gina nao wakapewa taarifa za kufika huko usiku huo.
USIKU HUOHUO
SHAMBA
ILIKUWA FURAHA YA AINA YAKE walipokutana tena na Kamanda Amata, kila mmoja alikuwa na hamu ya kutaka kujua hasa ni nini kilimsibu mwenzi wao huyo hata kutoweka kwa siku hizo tatu kama sio mbili. Gina ndiye haswa aliyeonekana kuchanganyikiwa zaidi kwa kumwona Amata hakuamini kabisa kwani alishajua mtu amekufa alikuwa akisubiri tu taarifa ya kiofisi.
“Mmefurahi sana ee?” Madam S akawauliza.
“Ndiyo maana yake, hii ni furaha ya kukutana pamoja maana tulikwishachanganyikiwa,” Chiba akaeleza.
“Ok basi sherehe iishe na sasa tuangalie kazi,”
Wote wakaketi vitini katika meza yenye umbo la yai huku wakimwacha madam S upande wa peke yake kama kiongozi.
“Hatutakiwi kuchelewa kwani adui yetu anaweza kututoroka na tusimwone tena,” ilikuwa ni sentensi ya kwanza katika kufungua kikao hicho kutoka kwa Madam S.
“Tunapaswa kuingia kazini, tukamsake huyu mwanaharamu, tumtie nguvuni, hastahili kuishi nje ya gereza,” akaendelea kuongea mara hii akionekana wazi kuwa ana hasira moyoni mwake.
“Sawa Madam, sasa tunajipangaje kwa maana bila shaka pale walipodunguliwa Scoba na Amata ndipo kwenye makazi ya mtu huyo ijapokuwa hapajaonekana wazi,” Chiba akaeleza wasiwasi wake.
“Ndio, msako huu utafanyika katika eneo hil…”
“Ina maana mpaka sasa Pancho atakuwepo bado? Nina wasiwasi atakuwa keshaondoka nchi hii,” Gina alimkata kauli Madam S.
“Yupo hajaondoka, tulidhibiti njia zote za kutokea nje ya nchi kuanzia viwanja vya ndege, bandari mpaka stendi za mabasi na hasa kule mipakani, kila basi linapekuliwa kwa umakini na kila abiria anafanyiwa uchunguzi wa kina kwani anaweza kujibadilisha sura na akaondoka. Kwa jinsi hiyo hatujapata jibu kama amekamatwa,” Chiba alieleza.
“Kwa hiyo yupo,” Scoba akaeleza.
“Kamanda Amata ana jeraha yampasa kupumzika kwani hawezi mikikimikiki kwa sasa,” Jasmine aliliambia jopo, ndipo na wengine wakapata kujua kuwa Amata alikuwa amejeruhiwa.
Wote wakageuka kumtazama kwa huruma.
“Alikwambia nani, hii show tunaingia wote jukwaani na lazima mtu huyo akamatwe ndani ya saa 24 kutoka sasa,” Amata akawajibu.
“Ndio maana nakupenda mpenzi,” Gina akamalizia.
“Art of War,” Kamanda akamwambia Gina huku akimtazama usoni kisha wote wakacheka.
Simu ya mkononi ya Madam S ikaita, akaitazama kwenye kioo na kukunja sura kisha akawatuliza kwa ishara ya mkono na uiweka sikioni ile simu wakati huo Chiba akiwa tayai keshapachika kifaa chake cha kurekodi sauti hiyo.
“…na kwa sababu mnajifanya mnajua, sasa sikilizeni redio usiku huu mtaelewa kuwa sitaki kutaniwa…” na ile simu ikakatika baada ya sauti hiyo ya mkoromo kukoroma sikioni mwa Madam S. ‘Private number’ akawaza Madam S na kuishusha taratibu.
Sura ya Kamanda Amata ikabadilika na kuwa sura ya kazi, akatazamana na Madam S wasipate jibu wakatia huo, Chiba aliondoka na simu ya Madam S na kuingia katika chumba chake cha kazi kuifanyia uchunguzi simu hiyo ilipigwa kutoka uelekeo gani.
“Pancho Panchilio au kibaraka wake, hawezi kuwa mwingine, atapatikana tu,” Chiba akajibu.
“Gina, fanya kazi niliyokupa sasa,” Madam S akampa amri Gina naye hakuchelewa akasimama na kuondoka katika chumba hicho.
Saa 7 Usiku
Usiku huo Gina aliegesha gari eneo la Upanga katika barabara ya Ally Hassan Mwinyi, karibu kabisa na hoteli ya Palm Beach. Kamanda Amata akiwa ameketi upande wa kushoto katika kiti cha abiria, aliiweka vizuri bastola yake tayari kwa lolote.
“Vipi?” Gina akauliza.
“Sina utani na mtu sasa hivi,” Amata akamjibu Gina, kisha wakateremka garini.
“Vijana wako wapi?” akauliza.
“Wameshafika tayari wapo kwenye pozisheni zao,” Gina akajibu. Kisha wakavuta hatua kuielekea hoteli hiyo ambayo siku hiyo ya wikiendi watu walijazana kwa starehe mbalimbali.
† † †
KAMBA SEBULE alikuwa akifurahia maisha ndani ya ukumbi mkubwa uliokuwa na michezo mbalimbali ya kujipatia pesa. Akiwa na walinzi wake alijumuika pamoja na wengine wengi waliokuwa hapo kutafuna maisha. Furaha ilionekana wazi kati nyuso za wote waliozunguka eneo hilo huku wadada warembo wakitumbuiza kwa muziki uliokuwa ukipigwa ‘live’ kutoka jukwaani, wakicheza kwa minenguo ya Kikongo huku wakiwa wamevalia nusu utupu. Mijanaume yenye uchu ilikuwa imezunguka jukwaa hilo lililojengwa juu kidogo na kutazama wadada hao wakifanya mambo yao hadharani.
Kamba Sebule aliendelea kuburudika na rafiki zake waliofanana na yeye waliokuwa wakicheza ‘poker’na kufurahia pesa waliyokuwa wakiivuna. Mmoja wa walinzi wake alionekana kuchezwa na machale kidogo, akatoka kitu kama picha katika mfuko wake wa shati na kuiangalia kwa sekunde kadhaa kisha akairudisha mfukoni, na kumwinamia Kamba Sebule, akamnong’oneza kitu.
† † †
“Nahisi wametugundua,” Gina akamwambia Amata.
“Ndiyo nimeona, Yule mtu inaonekana ana picha ya mmoja wetu, kwa nini katembea nayo? Lazima tuipate na tujue kaipataje,” Kamanda Amata akamwambia Gina.
“Wanatutazama,” Gina akamwambia Amata.
“Ndiyo, ondoka nenda chooni, wakija name nakuja hukohuko,” Amata akatoa maelekezo na Gina akayafuata bila kuhoji. Akavuta hatua kuelekea chooni, kama alivyofikiria Amata ndivyo ilivyokuwa.
Yule mlinzi mmoja akambonyeza mwenzake na wote wawili wakatoka kuelekea kule chooni wakamwacha Kamba Sebule na mlinzi mwingine mmoja, wakiahidi kuwa wanarudi muda tu. Kamanda Amata naye akajinyanyua taratibu na kuelekea upande uleule.
Gina aliingia ndani ya choo akafungua maji na kusimama kando, dakika moja ikapita, akafunga maji, akajiweka tayari huku akipiga mruzi na kufuatisha wimbo uliokuwa ukisikika kutoka ukumbini. Akafungua mlango kutoka nje na ndipo alipokutana na vijana hao. Gina akajifanya kupita katikati yao kama hajui kinachoendelea.
Mmoja wa wale walinzi akamzuia kwa kifua chake kipana hasipite, Gina hakuuliza wala hakupoteza muda, alimsukuma kando akadakwa na Kamanda Amata kwa nyuma. Amata akamgeuza na kumpiga kichwa kisha akamdaka kolomeo kwa kono lake la kulia na kumfanya mtu huyo aanze kutapatapa kutafuta pumzi.
Gina aligeuka ghafla na kumchapa ngumi nzito Yule wa nyuma yake, Yule jamaa nae akajibu shambulizi lakini Gina alikanyaga mguu wake ukutani na kuepa shambulizi hilo, alipotua chini alimpa pigo moja la karate lililompata barabara na kumwacha akiweweweseka alipotulia alijikuta mbele ya domo la bastola ya mwanamke huyo. Kamanada Amata aliendelea kumbana kolomeo Yule jamaa.
“Nani bosi wako?” Amata akauliza.
“Kamba, Ka-ka-mmmbbba!” akajibu kwa tabu huku akianza kulegea.
“Makazi ya Kamaba yako wapi?”
“U-pa-ngggga!”
“Ofisi yake iko wapi?”
“Mtaa wa Ka-ka-lu-ttttaaaa namba 25!” akajibu na kuanza kutapatapa kwa nguvu.
Yule jamaa aliyetazamana na domo la bastola ya Gina akajaribu kutafuta mbinu ya kujiokoa wakati huo nje ya choo hicho walisikika watu wakiingia kujisaidia. Gina akashusha bastola yake na kuifutika kiunoni, kosa. Yule jamaa akarusha ngumi iliyompata Gina usoni na kumyumbisha kiasi Fulani. Ngumi ya pili Gina akaudaka mkono na kuuzungusha kwa nguvu.
“Aaaaaiiiiigggghhhh!” akatoa yowe la uchungu, huku mifupa ya mkono ikiachana, akamrudisha mbele na kumpiga futi la kwenye korodani kabla hajajibwaga chini na kujipigiza kwenye sinki la kunawia maji na kutulia sakafuni akikoroma. Kamanda Amata akafungua mlango wakatoka na Gina na kuwaacha watu wakitukana na kusonya huku wakiingia ndani kujisaidia.
“Mama majambaziiiiiiiii!” ilisikika sauti ya kike ikipiga yowe kutoka chooni. ‘Pameharibika!’ Kamanda akawaza na moja kwa moja akamshika mkono Gina na kurudi ukumbini, hali ya taharuki ikaugubika ukumbi huo, walinzi wa hoteli wakaingia kuangalia kulikoni.
“Ita vijana,” Kamanda akamwambia Gina, naye akachomo simu yak e ya upepo na kuwaita waingie. Moja kwa moja walisimama kwenye ile meza ya ‘poker’.
“Upo chini ya ulinzi, Kamba Sebule,” Gina alimwambia huku Kamanda Amata akiwa kasimama pembeni, bado kulikuwa hakujatulia.
Kamba Sebule alitulia kimya macho yake yakiwa juu ya ile meza yakiangalia karata zilizopangwa juu yake.
“Wewe ni nani, na una mamlaka gani ya kuniambia mimi hayo?” Kamba akauliza bila kugeuka.
“Tii sheria bila shuruti, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo iliyonipa malaka hayo,” Gina akaunguruma.
“We mwanamke hivi ushawahi kuzaliwa?” kamba akalalama.
“Kamba Sebule sitaki kutumia nguvu kwani nimekuja na nguvu kubwa kuliko unavyofikiri,”
Kamba Sebule akageuka taratibu na kukutana na sura ya Gina, sura ya mwanamke mrembo lakini isiyoonesha hata chembe ya tabasamu, nyuma ya Yule mwanamke Yule alikutana na macho ya kijana shababi aliyesimama kwa utulivu huku mikono yake kaifumbata mbele chini ya kitovu.
“Huna adabu msichana!” Kamba akaunguruma na kuchomoa simu yake lakini kabla hajaiweka sikioni ilinyakuliwa na Amata, na alipotaka kuleta tabu Gina alimtandika pigo moja uso na kumrudisha mezani akiwa hoi.
“Tia pingu,” akawaambia vijana wa polisi nao wakatekeleza na kuondoka naye.