Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika leo ameongea na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam ambapo amehoji kwanini Bunge limedharau ushauri wa Wananchi wa kufanya mjadala kwanza kabla ya kuidhinisha mkataba wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uendeshaji wa Bandari.
"Waziri Mkuu amesema anakaribisha ushauri kuhusu jambo la Bandari, sasa ni vizuri Waziri Mkuu akalieleza Bunge maana ile hotuba ameitolea kwenye nyumba ya Ibada, ni vizuri atoe hotuba Bungeni alieleze Taifa kwamba wao wanakaribisha ushauri sasa hivi lakini kabla tulitoa ushauri kabla ya kuidhinisha na Bunge tuwe na mjadala sasa wameacha ushauri wa Wananchi wakaidhinisha na sasa wanataka mjadala, Waziri Mkuu aeleze ni sababu zipi zilifanya wapuuze ushauri na wakaidhinisha”
"Waziri Mkuu amesema hili suala limeibuka sasa kwasababu Serikali hii tofauti na Serikali iliyopita imeamua kulipeleka jambo hili Bungeni, kwahiyo Wananchi wakisikiliza wanasema mjadala huu ni mkali kwasababu Rais Samia amemua mikataba ipelekwe Bungeni na kuwa wazi mjadala umekuwa mkali, kitu ambacho sio kweli, Mimi nikiwa Bungeni 2017 Serikali ilipeleka makubaliano ya mkataba kama huu wakati Rais akiwa Magufuli kuhusu ujenzi wa Bomba la mafuta, sasa kwanini mkataba ule haukuwa na utata mkubwa kama huu wa sasa jibu lipo kwenye masharti ya mkataba wa sasa"
"Waziri Mkuu amezungumzia kwamba hakuna hatari ya kiusalama kuhusu mkataba huu kwamba kuna Kituo cha Polisi Bandari wataendelea kuwepo, Jeshi la Wanamaji lipo pale , jambo la msingi ambalo Waziri Mkuu anatakiwa alitolee maelezo ni kifungu cha 6(2) cha mkataba ambacho kinaeleza mazingira ya usalama lazima yawe yamekubaliwa na pande zote mbili"
"Sasa Waziri Mkuu atueleze Serikali ya Tanzania akiona shida halafu Serikali ya Dubai ikaona hakuna shida kwa mazingira ya kiusalama kwa mkataba huu, je kifungu hiki hakiibani Tanzania kiusalama, Marekani iliingia kwenye ubishani kama huu, DP World ilinunua kampuni inayoendesha Bandari kadhaa Marekani lakini Bunge likasema hili jambo ni hatari kwa mazingira ya kiusalama, Bunge likamkatalia Rais Bush, kampuni ya DP World ikauza ile kampuni iliyonunua kwa kampuni nyingine ya Marekani"