ACT Wazalendo
JF-Expert Member
- May 5, 2014
- 610
- 1,540
Zuio la TCRA Matumizi ya VPN linakandamiza uhuru wa habari Nchini.
Chama cha ACT Wazalendo kupitia Wizara Kivuli ya Habari na Mawasiliano tunapinga vikali taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania -TCRA ya kukataza matumizi ya Mtandao binafsi maarufu kama VPN (Virtual Private Network) iliyotolewa jana Oktoba 13, 2023. ACT Wazalendo tunaona taarifa hiyo pamoja na vifungu vya kanuni vilivyotajwa ni kandimizi na mwendelezo wa kuzuia wananchi kufurahia haki na uhuru wa kupata habari na kujieleza bila hofu na faragha za watumiaji.
Tunafahamu VPN zinatumiwa na watu binafsi na taasisi kama benki, mashirika katika shughuli zao za kila siku na kwamba kusalimisha itifaki hizo kwa TCRA kunaweza kurahisisha kuingilia faragha na taarifa binafsi za watumiaji kinyume kabisa na sheria za nchi.
Serikali ya CCM imekuwa ikizuia wananchi kupata au kutumia mitandao mbalimbali mara kwa mara bila maelezo yoyote. Wananchi hutumia VPN kuendelea kufikia habari, taarifa na kupata faragha. Mfano mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu Serikali ilifungia mitandao ya kijamii ili kuzuia wananchi kupata taarifa za kiuchaguzi. Hatutaki yajirudie tena.
ACT Wazalendo inashangazwa na kitendo cha Serikali badala ya kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu usalama na Ulinzi wa taarifa za kimtandao kama vile wizi wa taarifa, utapeli na ulaghai wa kimtandao, usiri wa taarifa zinazotembea katika mitandao na kuzuia udukuzi wa aina yoyote. Serikali inakuja na tamko la ajabu linalolenga kurudisha nyuma hatua na kurahisisha udukuzi wa taarifa. Hii haikubaliki na inapaswa kupingwa kwa nguvu zote.
Hivyo, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kusitisha mara moja kanuni hizo kandamizi na kuacha wananchi, taasisi na mashirika waendelee kuvinjari haki ya faragha, kupata na kutoa habari kama ilivyotolewa na katiba ya nchi.
Mwisho, tunatoa wito kwa wadau wote kushikamana ili kulinda uhuru wa kupata habari nchini kwa kupinga katazo hili haramu na kutaka kanuni zifanyiwe marekebisho.
Imetolewa na;
Ndg. Philbert Simon Macheyeki,
Waziri Kivuli wa Habari na TEHAMA,
ACT Wazalendo.
14 Oktoba, 2023.
Ndg. Philbert Simon Macheyeki,
Waziri Kivuli wa Habari na TEHAMA,
ACT Wazalendo.
14 Oktoba, 2023.