🎙️ MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI:
Baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya Yokohama kumalizika Kocha Arne Slot alizungumza na waandishi wa habari na baadhi ya mambo aliyozungumza ni kama yafuatayo:
Anazungumziaje Kuhusu Mechi Na Kiwango Cha Timu Yake:
🗣️ “Ilikuwa mechi nzuri dhidi ya wapinzani ambao tayari wako katikati ya msimu na wamezoea mazingira ya hapa. Walifanya mchezo kuwa wa ushindani mkubwa kwetu, jambo ambalo ni zuri sana kipindi cha maandalizi ya msimu kwa sababu tunahitaji mechi za aina hiyo. Tunataka timu zinazoweza kutupa changamoto, na hii bila shaka ilikuwa moja wapo."
"Nimeona mambo chanya kadhaa – kwa mfano, namna tulivyorejea mchezoni baada ya kufungwa bao la kwanza. Hili ni jambo tulilofanya mara kadhaa msimu uliopita. Pia, kuona wachezaji wanaoingia kutoka benchi wakibadilisha mchezo."
"Kulikuwa na vipindi kadhaa vya ujenzi mzuri wa mashambulizi, lakini pia katika bao tuliloruhusu na nafasi kubwa tuliyowapa wapinzani kipindi cha kwanza, niliona hatukufanya kazi ya kutosha kurudi kwa kasi kwenye ulinzi. Hili pia lilitokea dhidi ya AC Milan. Inaweza kuwa ni kutokana na mazoezi magumu ya kambi au joto kali – lakini ni jambo tunalopaswa kuboresha kabla ya kumenyana na Athletic Bilbao ambaye ni mpinzani wetu anayefuata.”
Kuhusu Kama Kikosi Kinajua Nani Atakuwa Nahodha Msaidizi Mpya Na Mabadiliko Yoyote Kwenye Kundi La Uongozi:
🗣️ “Timu halijajulishwa bado. Lakini tayari nimezungumza na watu binafsi, kwa hiyo yule atakayekuwa nahodha msaidizi tayari anajua. Kila mtu anapenda kuwa na viongozi kwenye timu, na katika soka la kisasa hilo huwa halionekani sana tena. Nina bahati kuwa na baadhi yao — wachezaji wenye uzoefu ambao si tu wana uzoefu, bali wanaelewa mchezo na wanaweza kuwa sauti ndani ya kundi na uwanjani. Hilo linasaidia sana."
“Nikisema sasa itakuwa vigumu, kwa sababu tupo mwanzoni mwa mwezi wa nane, na bado kuna mwezi mzima. Mambo mengi yanaweza kutokea ndani ya mwezi mmoja kwenye soka, kwa hiyo tusubiri tuone. Kwanza tunarejea nyumbani, kisha wiki ijayo tutacheza mechi pale Anfield. Ingawa nimefurahia sana kuwa hapa — heshima kutoka kwa mashabiki, jinsi walivyotukaribisha, na idadi yao — lakini naweza kukuambia Anfield ina uwanja bora zaidi kuliko viwanja viwili vya mwisho tulivyocheza!”
Anazungumziaje Kiwango Kiwango Alichokionyesha Rio Ngumoha:
🗣️ "Kama nilivyosema, hakuwa peke yake aliyebadilisha mchezo alipoingia. Trey Nyoni pia, kijana mwingine, alifunga goli akipewa assist na Jeremie Frimpong. Katika goli la kwanza, nafikiri Curtis Jones alihusika sana kwa kuupoka mpira katikati. Rio tena alionyesha ubora wake na hilo ni jambo zuri kwetu kwa sababu tuna wachezaji wengi wenye ubora mkubwa."
"Lakini kuwa na wachezaji bora wanaotokea kwenye academy kila mara huwa msaada mkubwa na huleta nguvu mpya kwenye timu. Ni jambo la kufurahisha kuwaona vijana wa miaka 16, 17 au 18 tayari wakibadilisha mechi. Kulikuwa pia na tukio ambapo alipaswa kumpasia Macca [Alexis Mac Allister] au Curtis, kwa hiyo kuna maeneo ya kujifunza kwake pia. Ukiwa na miaka 16 na unaweza kuathiri mchezo namna hiyo, hakika unastahili pongezi.”