Kwaheri 2025, Ulikuwa Mwaka wa Majanga!. Yaliyopita si Ndwele, Tugange Yajayo!. Karibu 2026, Uwe Mwaka wa Kheri!. Ni Mwaka wa Katiba Mpya!, Inakuja..!

Kwaheri 2025, Ulikuwa Mwaka wa Majanga!. Yaliyopita si Ndwele, Tugange Yajayo!. Karibu 2026, Uwe Mwaka wa Kheri!. Ni Mwaka wa Katiba Mpya!, Inakuja..!

Pascal Mayalla

Platinum Member
Joined
Sep 22, 2008
Posts
57,101
Reaction score
128,716
Wanabodi
Hii ni makala yangu ya kufungia mwaka kwenye gazeti la Mwananchi la Leo ikiwa ni makala ya 52 kwa mwaka huu.
Screenshot 2025-12-31 at 08.34.02.png

Hii ni Makala yangu ya mwisho kwa mwaka huu wa 2025, ambapo Jumatano ya leo,ndio siku ya mwisho ya Mwaka huu wa 2025, usiku wa leo,ni mkesha wa mwaka mpya tunauaga mwaka huu wa 2025 ,na kuukaribisha mwaka mpya wa 2026 kesho Alhamisi,kwa kuianza safari mpya ya 2026.
Mwaka 2025 ulikuwa ni mwaka wenye mengi,makubwa mazuri pia na changamoto kadhaa, kubwa kuliko yote la mwaka 2025, ulikuwa ni mwaka wetu wa Uchaguzi Mkuu wa rais, Wabunge na Madiwani.
Siku ya uchaguzi kulitokea mambo ambayo sii mazuri, yametutia doa sisi Tanzania kama nchi, hivyo nasisitiza, tuufunge mwaka kwa “yaliyop[ita sii ndwele, tugange yaliyopo na yajayo, ili tuuanze mwaka mpya wa 2026 kwa nia njema na dhamira safi.

Kilichotokea ile siku ya uchaguzi, October, 29, kimewashangaza wengi, lakini kufuatia msemo wa Kiswahili, usemao, “Mwenda pole hajikwai, na akijikwaa haanguki, na akianguka haumii”, na msemo wa “haraka haraka haina baraka”, “mkamia maji hayanywi” na “mwenye pupa hadiriki kula tamu”, tukubali tukatae, kilichotokea October 29, badala ya Tanzania kuwa ni mwenda pole, sisi tulikwenda mbio sana, tukachukua maamuzi ya pupa, tukataka kuyakamia maji, tukashindwa kuyanywa, haraka haraka yetu ikatukosesha baraka, tukajikwaa, tukaanguka, tukaumia, na badala ya kurudi nyuma kuangalia pale tulipo jikwaa, ili tusije kujikwaa tena pale pale, sisi ni tumeamka, tumeangalia pale tuu tulipoangukia, na kuendelea na safari yetu.

Kwa vile kwa kipindi cha mwaka mzima wa 2025, tumekuwa tukiuzungumzia uchaguzi mkuu, kwa kushauri, nini kifanyike, ili uchaguzi wetu mkuu uwe ni uchaguzi huru na wa haki, wenye amani na utulivu, mapendekezo yetu mengi hayakuzingatiwa.

Moja ya pendekezo kubwa kabisa, lililopendekezwa na wengi, ni kufanyika kwa mabadiliko madogo ya katiba, sheria, taratibu na kanuni, za uchaguzi, ili kuusawazisha uwanja tenge wa mchezo wa uchaguzi wetu ukae sawa, lakini wenye maamuzi wakagomea, hivyo tukaingia tena kwenye uchaguzi mkuu wetu kwenye uwanja tenge na matokeo yake ni matokeo tenge.

Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni, kwa vile mkubwa ni jalala, lawama zote anatupiwa Rais Samia, lakini kiukweli kabisa, yeye kwa upande wake, alifanya kila alichoweza, aliunda kikosi kazi, kikawaita wadau, wakatoa maoni, wakajadili sheria taratibu na kanuni, wakaja na mapendekezo, pendekezo kubwa likiwa ni kufanyika kwa mabadiliko madogo ya katiba, “minimum reforms”.

Hili lilikataliwa, serikali ikaleta mabadiliko ya sheria ya uchaguzi, sheria ya vyama vya siasa, ikaleta mabadiliko ya kawaida ya sheria, ikaivunja Tume ya zamani ya Uchaguzi NEC, na kuunda Tume mpya Huru ya Uchaguzi, INEC.

Kwa vile NEC ni zao la katiba, kikatiba na kisheria, jambo ambalo liko ndani ya katiba, haliwezi kuondolewa kwa sheria ya kawaida bila ya kufanya mabadiliko madogo ya katiba, kuivunja kwanza NEC, na kuinda kwanza INEC, ndani ya katiba, kisha ndipo tuje tutunge sheria ya kuinda INEC kwa mabadiliko ya sheria.

Niliandika Makala humu kuhusu “Kufanya Mabadiliko ya Sheria Bila Mabadiliko ya Katiba, ni Sawa na Kula Bila Kunawa”. Kilichofanyika ni tulibadili sheria kwa pupa, tukaunda Tume mpya ya Uchaguzi kwa pupa, na matokeo yake, tukafanya uchaguzi kwa sheria mpya na tume mpya ya INEC ambayo mpaka hapa ninapoandika leo, INEC haitambuliwi na katiba yetu, kwenye katiba yetu bado kuna NEC.

Na INEC yenyewe iliyosimamia uchaguzi, kusema la ukweli ni ile ile NEC, viongozi ni wale wale, kuanzia Mwenyekiti na Katibu na ma Kamishna wa INEC ni wale wale wa NEC!, kikiundwa chombo kipya, ilikuwa lazima kuwateua viongozi wapya hata kama ni wale wale, lakini baada ya kuvunjwa NEC na kuundwa kwa INEC, viongozi wa NEC wanapoteza uteuzi, na kuteuliwa viongozi wa INEC, hata kama watakuwa ni wale wale waliokuwa NEC walipaswa kuteuliwa upya.

Ukiangalia muda uliokuwepo, ulikuwa ni muda wa kutosha kabisa kufanya minimum reforms, ukijiuliza ni sababu zipi zilizopelekea kusifanyike mabadiliko madogo ya katiba, hakuna!, ila kilichopo ni kama kiburi tuu na jeuri ya madaraka na mamlaka kwa vile kuna watu wametangaza shinikizo la bila mabadiliko, hakuna uchaguzi (NRNE), serikali ikaona ikifanya mabadiliko madogo ya katiba, ni kama kuwanyenyekea na kukubali shinikizo, hivyo ikaamua kufanya kiburi, na kiburi sii maungwana, badala yake tukaingia kwenye uchaguzi bila mabadiliko ya katiba, na huu ndio mzizi wa yote yaliyotokea ile tarehe 29 October, yale ni matokeo tuu sio chanzo, hatukuziba ufa, sasa tunajenga ukuta.

Na hata sheria mpya ya uchaguzi iliyopitishwa, bado ilikuwa na vipengele batili vinavyokwenda kinyume na katiba yetu, ambavyo niliviainisha humu kwenye Makala za nyuma.

Funzo kwa serikali yetu, tujenge utamaduni wa kuwa serikali sikivu, Nchi ya Tanzania ni mali ya Watanzania, ndio wenye nchi, wenye katiba na wenye kila kitu, mamlaka kuu inatoka kwa wananchi, rais, serikali, Bunge na Mahakama wote ni watumishi wa wananchi, kama wananchi walitaka mabadiliko madogo ya katiba, walipaswa wapewe, na kama kuna sababu za msingi kwanini wasipewe, basi walipaswa waelezwe ili waelewe.

Haya maji ya October 29, yameisha mwagika, hayazoleki, kwa vile sasa ni mwisho wa mwaka, tuyaache yaliyopita sii ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Kwa vile kuna tume ya uchunguzi wa kilichotokea, wale wenye maoni, pelekeni kwenye Tume, itoe matokeo hili liishe.


Kubwa, la mwaka huu ni Katiba Mpya. Baada ya CCM kushinda uchaguzi kwa kishindo cha asilimia 98%, na kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM 2025-2030, hoja ya katiba mpya ipo, na Rais Samia akilizindua Bunge jipya, aliahidi kuuanza mchakato wa katiba mpya ndani ya siku 100 za kwanza. Hii katiba mpya itaukata mzizi wote wa fitna, tunakwenda kwenye Mwaka Mpya wa Tanzania Mpya na Mambo Mapya.

Heri ya Mwaka Mpya.

Mungu Ibariki Tanzania

Paskali
 
Inakuja kweli? Mbona mishangao mingi kwenye mwanzo habari hii?Kwa kiburi cha Mtanzania na kwa uwepo wa kazi ya tume,isiwe tu kisingizio cha kukosa kuanza mchakato wa katiba.Umenena mengi mazuri ya kushauri ila tu viburi wasikuteke ili usiendelee kuwapigia kelele wasizozipenda.
 
Katiba itakayoundwa na huyu chura kiziwi itakuwa kiini macho tu kama alivyofanya kwenye tume huru ya uchaguzi.

Suluhu ni Suluhu kung'atuka, halafu serikali ya mpito ije kushughulika katiba na reforms nyingine.
 
Bila kusahau ukosefu wa mvua, maji, maisha magumu, huduma mbovu kutoka serikalini (hasa customer services)! Namba zipo, jaribu kupiga ushuhudie...
Ulikuwa mwaka mbaya TZ haijawahi tokea kutoka kupata uhuru!
Somebody or some people are responsible for that!
Watawajibishwa?!
We don't think so...
 
Kubwa, la mwaka huu ni Katiba Mpya. Baada ya CCM kushinda uchaguzi kwa kishindo cha asilimia 98%, na kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM 2025-2030, hoja ya katiba mpya ipo, na Rais Samia akilizindua Bunge jipya, aliahidi kuuanza mchakato wa katiba mpya ndani ya siku 100 za kwanza. Hii katiba mpya itaukata mzizi wote wa fitna, tunakwenda kwenye Mwaka Mpya wa Tanzania Mpya na Mambo Mapya.

Heri ya Mwaka Mpya.

Mungu Ibariki Tanzania

Paskali
Hii aya ndiyo ulipoharibu kaka. Inaonesha kuwa umekuja hapa kufanya damage control trajectory pamoja na kudivert situation ya yanayoendelea kujjri nchini
  1. Ahadi ama matarajio ya Katiba Mpya unayatoa wewe kama nani?
  2. Kwa nini unathibitisha ushindi wa wahaini CCM wakati unaujua ukweli kura hazikupigwa?
  3. Kikatiba na kisheria, majeshi yanaingiaje kwenye mchakato wa uchaguzi?
  4. Hii project ya kupaka rangi mzoga unalipwa kiasi gani?
  5. Tukueleweje Paskali?
 
Back
Top Bottom