Mara nyingi sana huwa nasoma makala za Jenerali Ulimwengu lakini kinachonigusa zaidi kwenye makala zake ni ile hoja yake kwamba "watanzania tumejipa likizo ya kufikiri". Kimantiki hali hiyo utaiona sana kwenye mabandiko yanayohitaji kufikiri kama hili la
Mzee Mwanakijiji kwani mwisho wa siku Yanadoda! Ni rahisi kujaza kurasa kwa kurasa kwa kushabikia au kushutumu chama fulani,kundi au mtu fulani bila kuwa na ushahidi wa kutosha kuliko kujadili kwa kina hoja zenye kuchanganua chanzo cha tatizo. Hata humu tunapenda kujipa raha kwa kuishi kwenye dunia ya kufikirika!!
Kwa mtizamo wangu CHADEMA inakabiliwa sana na vikwazo viwili vikubwa. Katiba ya chama na utendaji wa sekretarieti ya chama pale makao Makuu. Katiba ya CHADEMA ilitungwa juu ya msingi wa imani au Falsafa ya kuondoa mtindo wa kufanya maamuzi toka makao makuu badala yake maamuzi yafanywe kwenye ngazi za chini na Makao kuwe kunafanyika uhakiki tu maamuzi hayo.
Bahati mbaya waandishi wa Katiba ya CHADEMA wakaiandika kwa mtindo wa kurundika maamuzil yote Makao Makuu na kuacha ngazi za chini bila maamuzi. Mfano rahisi ni suala la Madiwani wa Arusha na Mwanza. Kama katiba ingeandikwa kwa mfumo wa kumaliza matatizo ya Majimbo na wilaya kwenye ngazi ya mkoa basi bila shaka Kamati Kuu ya chama isingehusika na migogoro hii ya Mwanza na Arusha.
Lakini Katiba imeandikwa katika mfumo kwamba jambo likishindikana kwenye ngazi ya jimbo ngazi inayofuatia ni Kamati Kuu. Mikoa na Wilaya zenye jimbo zaidi ya moja kazi yao ni kufanya "mashauriano" na katiba inaelekeza kwamba kama maamuzi yakifanywa kwenye ngazi ya Jimbo au wilaya taarifa inapelekwa moja kwa moja Makao Makuu na Mkoa unapewa Nakala!!
Na makao makuu nao wanapeleka maagizo Majimboni na wilayani na Nakala mikoani.
Kwenye ngazi ya mkoa hakuna chombo cha kufanya kazi za kila siku za chama badala yake kuna watu wawili Mwenyekiti na Katibu ambao kwa pamoja na Wenyeviti (waratibu) wa mabaraza ya chama wanaunda kitu kinachoitwa "Baraza la uongozi la Mkoa" na hivyo hivyo kwenye wilaya zenye jimbo zaidi ya moja mfumo ni huo huo. Haya mabaraza ya Uongozi hayana hata mamlaka ya kusimamia kura za maoni kwenye maeneo yao.
Maana yake Uongozi wa Mkoa utapewa tu Nakala ya kujulishwa nani kachaguliwa kwenye kura za maoni kuwa Mgombea ubunge au udiwani bila ya wao kusimamia mchakato huo, lakini kamati kuu ndiyo inayotoa uamuzi wa mwisho nani awe mgombea wa chama. Na viongozi hawa wa MKoa na wilaya zenye jimbo zaidi ya moja kwenye kupiga kura za maoni za kuchagua mgombea ubunge si wapiga kura ingawa kwenye udiwani kuna mwanya wa kuwaingiza wawe wapiga kura.
Wenyeviti wa Wilaya ni wajumbe wa Baraza Kuu la chama lakini Makatibu wa MiKoa si Wajumbe wa Baraza Kuu, Mkutano Mkuu, wala hakuna kikao chochote cha kitaifa kinachowakutanisha Makatibu wa Mikoa. Maana yake Mwenyekiti wa wilaya anakwenda kwenye kikao cha kuagiza Makatibu wa Mikoa wafanye nini halafu unatarajia Katibu wa Mkoa akishapewa maagizo hayo naye amwagize Mwenyekiti wa wilaya ayasimamie!?
Sekretarieti ya chama imejaa watu wengi sana ambao lengo lao kubwa ni kugombea uongozi hasa ubunge kwenye majimbo watokayo. Athari zake kwa chama ni mgawanyo usio sawa wa rasirimali za chama. Watendaji hao wa chama hupeleka vifaa vingi kwenye majimbo watakako wakati sehemu nyingine hakuna vifaa au vilivyopo havitoshelezi.
Kutokana na watendaji hao kuwa wagombea kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 kulikuwa hakuna mtu anayeweza kujibu na kutoa maamuzi kuhusu matatizo mbalimbali yaliyojitokeza kwenye sehemu tofauti tofauti za nchi kwani karibu wote walikuwa kwenye majimbo wanayogombea au kwenye timu ya Kampeni ya Mgombea Urais na Makamu wake.
Huu ni sehemu tu ya mtizamo wangu kuhusu vikwazo vinavyoikabili CHADEMA kuelekea mwaka 2015!!