CCM mapande
Mwandishi Wetu Julai 2, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
Wapinga ufisadi waundiwa mizengwe
Bungeni zazuka kambi tatu za upinzani
TUHUMA za ufisadi zilizoshika kasi ndani na nje ya Bunge zinakitafuna Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho sasa kina kambi mbili za wazi zinazopingana, Raia Mwema imebaini.
Mgawanyiko huo unatokana na mzimu wa ufisadi uliojikita kwenye tuhuma za mradi wa umeme wa dharura uliokabidhiwa kwa kampuni tata ya Richmond Development, sakata ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na tuhuma inayomkabili Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ya kuwa alifanya biashara Ikulu akiwa madarakani.
Baada ya kupigana vijembe kwenye vikao vyao vya CCM kiasi cha hata kutishana, sasa wameanza kupashana ukweli na kuumbuana ndani na nje ya Bunge linaloendelea Dodoma.
Raia Mwema ina taarifa kwamba aliyejeruhiwa kwanza kutokana na mpasuko huo ni Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro ambaye baada ya kumtuhumu Mkapa bungeni kwa kufanya biashara Ikulu, sasa 'wabaya' wanamchimba wakipenyeza habari ambazo wanaamini zitamfanya aonekane kuwa si lolote si chochote katika vita dhidi ya ufisadi.
Ghafla mbunge huyo ambaye hiki ni kipindi chake cha kwanza cha ubunge anafuatiliwa alikotoka. Inaelezwa kwamba alipata kuwa mwanachama wa chama cha NCCR Mageuzi na kwamba amejipatia katika mazingira ya kutatanisha ardhi kubwa kwa nia ya kujenga hoteli kubwa ya kitalii.
Lakini alipozungumza na Raia Mwema wiki hii Dodoma, bila kuingia katika undani wa tuhuma hizo, zilizopenyezwa kwenye gazeti moja, alikana akisema anaamini kwamba hakuna kosa lolote alilolifanya katika kupata eneo hilo ambalo kweli ana nia ya kujenga hoteli ya kitalii.
Kwa ujumla, ndani ya Bunge mambo si shwari kwani wiki iliyopita, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe aliishiwa uvumilivu aliposimama kutema cheche kuwashambulia wale wanaoonekana kufanya kazi kubwa ya kuwasafisha watu waliotajwa katika kashfa ya kampuni ya Richmond.
"Kumekuwa na michango hapa ya waheshimiwa wabunge ikijaribu kukosoa kwa ujanja ujanja maamuzi yaliyofanywa na Bunge hili kuhusu Richmond na vile vile kumekuwa na attempt ya kutaka kusafisha baadhi ya watu waliotajwa ndani ya ripoti ile," alisema Mwakyembe.
Dk. Mwakyembe ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyoichunguza Richmond alisema kwamba yeye na wanakamati wenzake watajiuzulu ikithibitika kwamba walimwonea mtu. "... badala ya kupigania kuhusu matatizo chungu mzima katika majimbo yetu tuko busy kusafishana, mnamsafisha nani?" aliuliza.
Akionekana dhahiri kukerwa kweli kweli na hali hiyo, Dk. Mwakyembe alisema: "Nchi hii siyo ya mabwege bwana, watu wanaelewa, utasafisha kitu gani?
Mwakyembe aliwataka wanaosafisha watuhumiwa waseme yote ili na wao waliokuwa katika kamati na wao waseme hata yale ambayo hawakutaka kuyasema kulinda heshima ya Serikali.
Kwamba kamati teule haikusema yote katika ripoti yake ili kulinda Serikali, ni kauli ambayo iliibua minong'ono ya hapa na pale miongoni mwa wabunge hao hao wa CCM.
Akizungumza na gazeti hili nje ya Bunge kuhususiana na suala hilo la kamati kutosema yote katika ripoti yake, Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), Kapteni John Komba alieleza kushangazwa kwake na kamati hiyo kutokuweka wazi yote ambayo ilichunguza katika kashfa hiyo.
"Kamati hiyo ilipewa hadidu za rejea, kwa nini ilichuja wakati wa kutoa ripoti yake? Ilikuwa inaficha nini katika ripoti yake? Hiyo ni kasoro kubwa," alisema Komba.
Alisema katika sakata la Richmond yeye hamtetei mtu wala hamshutumu mtu yeyote kwa sababu mpaka sasa hakuna aliyetuhumiwa kwa ushahidi usio na shaka. Alitoa mfano wa aliyekuwa Waziri Mkuu,, Edward Lowassa kwamba alilazimika kujiuzulu kwa kuwajibika. "Tusisahau vile vile kwamba kamati haikumhoji wakati inachunguza Richmond," alisema.
Mambo yanavyokwenda Dodoma yanathibitisha kuwa sasa CCM ni makundi mawili, moja likifanya kila linalowezekana kuwasafisha watuhumiwa wa kashfa mbalimbali na jingine likimwaga petroli katika moto ambao tayari unawaka. Hiyo sasa imelifanya Bunge kuwa na pande tatu za 'upinzani', mbili zisizo rasmi za CCM zinazokinzana na moja rasmi ya Upinzani.
Huhitaji kuchunguza sana kujua ya kuwa katika makundi mawili ya CCM, moja lina wabunge wanaotolea macho kashfa za kifisadi na jingine linalojaribu kupoza vita dhidi ya ufisadi.
Kundi linalotolea macho vita ya ufisadi likiongozwa na Spika Samuel Sitta, linajumuisha wabunge kama Anne Kilango Malecela (Same Mashariki), John Samwel Malecela (Mtera), Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), Victor Mwambalaswa (Lupa), Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii, Alyoce Kimaro (Vunjo) na James Lembeli wa Kahama.
Wamo pia Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Mbunge wa Sikonge, Saidi Nkumba na Mbunge wa Viti Maalumu Stela Manyanya, huku wakiungwa mkono kwa kiwango kikubwa na wabunge wengi ambao hawazungumzi waziwazi lakini wamekuwa na mchango mkubwa kwao.
Kundi hilo kutokana na mambo linalopigania linajiona wakati mwingine linaingia katika anga za hatari na wengine sasa wameanza kujiandaa kukabiliana na upinzani mkali majimboni mwao kutokana na kuwapo mikakati ya wazi ya kuwangoa.
Anne Kilango alipotema cheche kushutumu ufisadi wa EPA kwamba pesa zisiporudi serikalini 'patachimbika, patakuwa hapatoshi'', aliwataka watu wa aina yake wasiogope vitisho na kueleza yote yaliyo moyoni.
"Tusimame imara, tusiogope vitisho wala tusimwogope mtu yeyote yule, bali tusimamie Serikali yetu ya CCM. Ugomvi wangu ni wale wanaoichafua Serikali ya CCM kwa kuhodhi pesa za Watanzania isivyo halali," alisema na kupigiwa makofi huku Spika Sitta akimuunga mkono kwa kusema, "Asante sana na bahati njema huyu Spika mliye naye haogopi kitu."
Hata hivyo, kauli ya Kilango na Spika ilijibiwa na Mbunge wa Viti Maalumu Anna Abdalah, ambaye alionekana wazi kubeza wanaojadili ufisadi wa EPA na mwingineo kwa hamasa.
Nguvu kubwa ya kukabiliana na wanaoonyesha kushupalia suala la ufisadi inaonekana kuwa nyuma ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa akiwa karibu mno na Mbunge wa Igunga Rostam Aziz, wakishikamana na Waziri wa Miundombinu aliyejiuzulu Andrew Chenge na kuungwa mkono kwa staili ya aina yake na Mbunge wa Kwela, Chrisant Mzindakaya.
Lowassa anatajwa kupata nguvu zaidi kutoka kwa watu waliokuwa karibu naye alipokuwa Waziri Mkuu, wakiwamo mawaziri wa sasa kama Laurence Masha ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi na mbunge kijana kutoka Kigoma Mjini, Peter Serukamba.
Mwenendo wa mambo unaonyesha ya kuwa kundi la la kwanza linalomjumuisha Spika Sitta lina nguvu bungeni wakati lile linalojumuisha Lowassa na Rostam likiwa na nguvu kwenye vikao vya CCM na hasa NEC, hali iliyoelezwa kwamba ilichangia kukifanya kikao cha NEC kilichofanyika mwezi uliopita kupata kigugumizi kutoa azimio kuhusu kashfa mbalimbali zinazotikisa nchi hivi sasa.
Kila kundi lina watu ambao wamepangwa kusema nini iwe bungeni au kwenye vikao vya chama. Ni wachache tu miongoni mwa wabunge wa CCM ambao huwezi kuwagawa katika kambi hizo, na hao ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye alionekana kuyumba wiki iliyopita kuhusu suala la kampuni ya Meremeta na lile linalomhusu Mkapa na mradi wa mkaa wa mawe wa Kiwira
Inaaminika kwamba baada ya mchakato wa uchaguzi kupita na makambi kuvunjwa, Rais Jakaya Kikwete hakuwa upande wowote wakati makundi hayo mawili yanaanza kujipanga na kujiotea mizizi, lakini sasa taratibu inahofiwa ya kuwa anaweza ama ameanza kuegemea upande wa kundi linaloongozwa na Lowassa kwa sababu zilizo dhahiri. Kundi hilo lina nguvu ya pesa na ushawishi mkubwa NEC sasa hivi na kuelekea katika mchakato wa uchaguzi 2010.
Taarifa zinasema makundi pinzani hayo mawili yameanza kujiweka sawa kwa uchaguzi wa 2015 ambao CCM italazimika kuwa na mgombea mpya badala ya Kikwete atakayekuwa akimaliza muda wake wa miaka 10 kama akipitishwa na CCM kama ilivyo kawaida, mwaka 2010.
Taarifa pia zinasema katika makundi hayo, kundi la Sitta, linaweza kumsimamisha ama mgombea wake wa kupigiwa debe atakuwa Bernard Membe ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Majina kadhaa yanatajwa katika kundi la pili kwa ajili ya 2015 likiwamo la Masha. Lakini yote hayo yatategemea na hali halisi itakavyokuwa hadi kufikia wakati huo kwa kuwa kazi iliyoanza sasa ya kupakana matope na mikakati inaweza ikabadili upepo huo.
Hali hiyo inaweza pia kubadilishwa na jambo lisilotarajiwa kutokea kabla ama wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010. Hayo ni ikiwa CCM itagawanyika na kundi kubwa kuweka mgombea mwenye nguvu na iwapo kutatokea sababu zozote zitakazomfanya Kikwete asigombee ama kupingwa ndani ya chama chake, mambo ambayo yote katika dunia ya sasa ya mabadiliko yanawezekana.
Katika vikao vya CCM hivi karibuni, kulikuwa na taarifa za mmoja wa wakongwe ndani ya CCM kutaka kuwasilisha hoja ya kuwafukuza chamani wabunge kadhaa waliojitokeza kushupalia tuhuma za ufisadi, hoja ambayo ingeweza kusababisha kuharakishwa kuanikwa hadharani kwa mpasuko unaoendelea sasa ndani ya chama hicho.