Kuanguka kwa CCM - Unabii Utatimia!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,474
39,987
Kuanguka kwa CCM – Unabii Utatimia?

Iko siku ambapo Watanzania wataamka na watakuta kwamba Chama cha Mapinduzi hakishiki tena hatamu za uongozi wa nchi, na badala yake Ikulu na Bunge vimechukuliwa na chama kingine. Siku hiyo ambayo haina jina, itakuwa ni siku ambapo Chama cha Mapinduzi kitaanguka kwa kishindo kikuu na sauti ya kuanguka kwake itasikika kila kona ya Tanzania, na mwangwi wa kuporomoka kwake kurindima katika bara letu la Afrika na mabaki ya mtetemo wa kuvunjikavunjika kwake kusimuliwa kama hadithi za Alfu Leyla wa Uleyla kwa vizazi vijavyo vya Watanzania. Kuanguka kwa Chama cha Mapinduzi kutakuwa ni mwanzo wa msemo, na bila ya shaka kutatungiwa methali.

Siku hiyo ni siku ambayo kina Malecela, Msuya, Kingunge, Kikwete,Lowassa,Makamba,Karume na magwiji wengine wa Chama hicho waombee wasijeiona. Kwani itakuwa ni siku ya huzuni kwa watawala na furaha kwa watawaliwa! Itakuwa ni siku ambapo "nyota ya jaha" itaangazia Taifa letu na nuru ya "jua la haki" itachomoza na miale yake kumulika kila kona ya Taifa letu. Hiyo ni siku ambapo kama mwali atolewaye nje, kila mtu atatamani kuiona isipokuwa wale ambao huyo mwali ni ishara ya wao kukosa mke na wengine kupata!

Bila ya shaka unajiuliza iweje nianze kwa kusema maneno hayo. Nilikuwa natafakari maneno ya Mwalimu aliyoyatoa mwanzoni mwa miaka ya 90 mara baada ya vyama vingi kuruhusiwa tena nchini. Baada ya Mwalimu Nyerere kutoa maneno makali ya "Ikulu inanuka Rushwa" watu wengi walianza kujiuliza mapenzi ya Mwalimu kwa chama alichokiasisi na kama anaweza kujitoa kwenye chama hicho. Alipoulizwa kuhusu kujiondoa CCM, mwalimu alijibu "CCM siyo Mama yangu". Maneno hayo ya Mwalimu yamebakia mawazoni mwangu (na bila shaka ya wengine pia) kama unabii na kama wosia. Hii leo kuna baadhi ya viongozi wa Chama tawala ambao wanasisitiza maneno ya Mwalimu ya "Bila CCM madhubuti Tanzania Itayumba" na kusahau kabisa maneno hayo ya onyo kali kuwa hata kama mtu ana mapenzi kiasi gani na CCM, iko siku anaweza kukiacha na kujitahidi kukivunja! Ni rahisi kukiacha CCM kuliko kumuacha Mama mzazi!

Siku hiyo ambapo Chama hiki maarufu kitakapojikuta kiko katika kambi ya upinzani ndipo viongozi wake na mashabiki wake watakapotambua kuwa "CCM siyo Mama" na Tanzania itaendelea na inaweza kuwepo bila CCM kuwa madarakani! Hiyo siku iso jina, iko, yaja, na yafanya hima kufika! Kwanini basi CCM itakuja kuanguka kwa mshindo mkuu namna hiyo?

Ndugu zangu, punda mnyama wa kazi kuna mahali anafikia kikomo! Na akifikia kikomo, punda hendi hata kwa mijeredi mia. Mtu unaweza kumtwisha punda mizigo, lakini akifikia kikomo chake hata umfanye nini punda hanyanyui mguu. Kuna baadhi ya viongozi ambao wanadhani kuwa Watanzania wataendelea kuinama na kukubali kutwishwa mizigo ya kila namna kana kwamba hawasikii maumivu! Ni hawa viongozi ambao huendelea kutuingiza katika mikataba mibovu, wanaendelea kuvumilia ufujaji wa mali ya umma katika maofisi yao, wanaendelea kupuuzia rushwa hadi imezoeleka na kuonekana kama kawaida. Viongozi hawa wanaimba wimbo na pambio ya uongozi bora wakitumbuiza kwa kasida za maneno ya kizalendo. Mawazoni mwao wanaishi wakifikiri kwamba Watanzania wataendelea kuvumilia. Kama punda iko siku hugoma, iko siku Watanzania nao watasema "Sasa inatosha"!

Siku moja ambayo ipo, Watanzania watajiuliza iweje viongozi wetu wanunue rada Bilioni 40 wakati hospitali yetu ya kijiji yenye kugharibu shilingi milioni moja haina hata bomba la maji! Hiyo siku Watanzania watajiuliza iweje ili kupata elimu nzuri ni lazima wapeleke watoto wao kwenye shule binafsi wakati shule za serikali zilizokuwa zikisifika huko nyuma zikibakia historia? Hawa wana na mabinti wa Tanzania wataamka siku moja na kusema "Imetosha".

Chama cha Mapinduzi kitaunguka pia kwa sababu hatimaye Watanzania wataelewa ya kwamba kuendelea kukaa kwa chama hicho madarakani ni kujitakia kutokuendelea na kurudi nyuma kwa maisha yao. Wataelewa kuwa CCM haina lengo hata chembe la kutimiza na zaidi ya kutimiza ahadi zake ambazo imekuwa ikizitoa tangu uhuru. Itadhihirika kuwa CCM iko madarakani ili kuendelea kujikita katika kutawala huku wakifanya mambo machache ya manufaa kwa wananchi huku viongozi wao na watu wachache waliobarikiwa na chama hicho wakiishi katika paradiso ya Bongo.

CCM itaunguka kwa sababu hata kipofu akigonga ukuta anauzunguka! Kutokuona siyo kikwazo cha kujua kukwama. Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikifanya mambo kana kwamba Watanzania wote ni vipofu na viziwi. Miaka nenda rudi tumewapa imani kuwa labda watabadilika. Wanavutia kwa maneno matamu na nyimbo za shangwe, wanafurahisha kwa rangi nzuri za mavazi yao, na mvuto wa kupepea kwa vibendera vyao vya kijani! Lakini wamekuwa kama makaburi yaliyopakwa chokaa, lakini ndani yake ni mifupa mitupu! Siku hiyo watanzania watakuwa kama kipofu aliyeona mwezi. Watagundua kuwa CCM siyo jua bali ni mwezi mchanga na mwanga ambao watu wamekuwa wakiusifia si mwangaza wa jua, bali mmuliko wa mbalamwezi. Watagundua kuwa wanachotaka kimulike maisha yao na kuanzia maisha ya watoto wao ni chama na viongozi wenye nuru ya jua, ambao mwangaza wao hautegemei kuakisiwa na kitu kingine bali unatoka ndani yao wenyewe! Wataamua kuachana na Chama ambacho miaka nenda rudi kimekuwa kikijificha kati yao mwangaza wa jua na hivyo kuwapa kivuli cha "kupatwa jua". Watu wamekuwa wakiogopa kuwa huo mwezi ukiondoka kati yao na jua, dunia itafikia mwisho! Kumbe zote hizo ni porojo. Mwezi huzija jua, lakini hatimaye hupisha!

Chama hicho kitaanguka si kwa sababu hakina watu wenye sura nzuri, na watanashati kwani wamejaa tele, siyo kwa sababu hakina watu waliosoma na kubobea katika nyanja mbalimbali kwani wapo bwelele, bali kwa sababu wale waliodhaminiwa uongozi katika chama hicho na kwa kupitia chama hicho nchi yetu, ni viongozi wasio na maoni, waliolala hadharani, wenye kutetea maslahi ya matumbo yao na ya wanawe, wakihangaika kutwa kucha kufikiri ni jinsi gani watamegeana fedha za walipa kodi. Kwa kutumia vipaji vyao na elimu yao baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wamebuni miradi hewa ya kugereshea umma huku fedha nyingi za miradi hiyo zikiishia vibindoni mwao. Watanzania hatimaye watatambua kuwa wakati wa kuangalia onesho la mazingaombwe umepita, na watataka kitu halisi! CCM haiwezi kubadilika, imelewa ugimbi wa madaraka na kuvimbiwa na mlo wa uchu! Ndiyo! Watanzania watagundua ya kuwa kuwa na CCM au kutokuwa nayo yote ni sawa! Hawana cha kupoteza tena. Kama miaka yote hiyo CCM imeshindwa kuboresha elimu yetu, sekta ya afya na maji, matatizo ya nishati n.k itakuwaje waweze kufanya hivyo miaka arobaini ijayo wakati kizazi kinachoingia madarakani sasa ni cha wana na wajukuu wa viongozi wa chama hicho!? Watanzania watasema "CCM Asante, lakini Kwaheri"!

Watakishukuru chama hicho kwa kutujengea misingi ya udugu, umoja na mshikamano. Watakishukuru chama hicho kwa kutulindia utaifa wetu na kuhakikisha kuwa tunabakia kuwa huru kisiasa. Watakishukuru Chama hicho kwa kutujengea utambulisho wetu wa "watanzania" na kutufutia hisia ya ukabila na udini. Ndiyo, watakishukuru chama hicho kwa yale machache mazuri ambayo kimefanya kwa muda mrefu, barabara chache za lami, shule, mahospitali, n.k Ndiyo, Watanzania watasema "asante"!!

Lakini wana hao na mabinti hao wa Kitanzania pia watasema "Kwaheri"! Watakiambia chama hicho kwaheri kwa kushindwa kujenga misingi mizuri ya utawala wa kidemokrasia! Watakiaga chama hicho kwa mamia baada ya kugundua kuwa hakina lengo la dhati la kuwashughulikia wala rushwa wakubwa na viongozi wabadhirifu! Watakiaga chama hicho baada ya kuona kuwa Mikakati yake mingi yenye majina ya ajabu ni sehemu ya mazingaombwe hayo! Wataangalia maisha ya viongozi hao na watoto wao na kuona kuwa wenzao wananeemeka wakati wao wanaganga njaa! Ndiyo! Watakiaga chama hicho kwa sababu, hatimaye watagundua ya kuwa njia pekee ya kukifundisha somo la utawala ni kuwaweka nje ya madaraka na kuwanyima nafasi nyingine ya kura na kula! Ndiyo, CCM itaanguka! Watatambua ya kuwa CCM ni chama cha kisiasa na siyo mama yao mzazi! Watakiaga na kushukuru kwa onesho lao la mazingaombwe, lakini wakati umefika wa kuingia kazini!

Ni matumaini yangu kuwa maandamano ya wapinzani yanayofanyika jijini Dar hayatakuwa ni ishara tu ya kuchukizwa na matendo ya serikali ya CCM na ufisadi uliokithiri. Ni matumaini yangu kuwa viongozi wa vyama vya upinzani watadhamiria kushirikiana siyo katika kupiga kelele kwa kutumia vipaza sauti hapo Jangwani bali ushirikiano wa kweli utakaofanya waziunganishe nguvu zao na kuunda chama kipya cha siasa chenye itikadi inayoakisi matamanio na matarajio ya Watanzania wengi, na chenye viongozi ambao kwao utumishi wa Taifa lao ndio kitu kinachowasukuma!

Endapo wapinzani wataishia kuwa waandamanaji, na wapiga kelele lakini wakishindwa kuungana na kutuonesha kuwa wako makini na mafanikio ya nchi yetu, basi CCM itaendelea kupeta kila kukija uchaguzi! Wapinzani wasililie huruma ya CCM ili wabadilishe Katiba au kuwajengea mazingira mazuri ya kushindana nao! Wapinzani wachukua hatima yao mikononi mwao wao wenyewe! Wawaambie Watanzania kuwa lengo lao mwaka 2010 ni kulichukua Bunge la Tanzania kwani limeendelea kuwa kicheko na dhihaka katika utawala wetu wa Demokrasia! Bunge lenye kutoa azimio la kulaani filamu ya mapanki kabla hawajaiona, na likakaa kimya kwenye mikataba ya madini na nishati bila kutoa azimio la kulaani mikataba hiyo, wabunge wa bunge hilo waondolewe kwa kura! Bunge ambalo linatumia siku 60 kuzungumzia maneno ya watu wawili na kushindwa kutumia siku moja kuzungumzia suala la rada, Richmond, IPTL, ATC n.k hilo ni bunge uchwara!! Bunge lenye spika anayeangalia matumizi ya maneno "kukaza" na "kutia" badala ya kuangalia matumizi ya shilingi Bilioni 80 ya vitu tusivyovihitaji Bunge hilo ni karibu ya Bunge la serikali ya nchi ya Wagagagigikoko! Kama kweli wanataka kuwapa Watanzania matumaini viongozi wote wa upinzani ifikapo 2010 wagombee Ubunge wakiwa wamuengana na kuhamasisha Watanzania wawachague wanachama wao! Kama Watanzania watataka Kikwete apewe nafasi nyingine hilo lao, lakini Bunge lisiende CCM!

Wapinzani wakiweza kunyakuwa wingi katika Bunge la Muungano, basi mwanzo wa CCM kuporomoka utakuwa umefika! Wakiweza kuwashawishi Watanzania baada ya wao kuungana kuwa wanamaanisha wanachosema basi CCM itaanza kutikisika! Watakapochaguliwa Wabunge na wakaanza kusimamia na kupitisha sheria ambazo zina manufaa kwa wananchi watamlazimisha Rais azikubali au atumie uwezo wake wa turufu. Na akifanya hivyo kwenye miswada fulani mara kadhaa avunje Bunge na uchaguzi mpya utafanyika! Huo utakuwa ni mwisho wa Kikwete, huo utakuwa ni mwisho wa CCM!

Je wapinzani wako tayari kusimama na kuchukua nafasi yao ambayo historia imewatengenezea? Je wako tayari kuitwa majina na kujipanga mstari kuongoza Taifa letu? Je, ndani ya vyama hivyo wapo kweli viongozi ambao Tanzania inaweza kuwaangalia na kuwategemea kuwavusha kutoka katika jangwa la utawala wa CCM.

Kuna maneno ya Maandiko Matakatifu yanayosema "Mlivyouzunguka mlima huu vyatosha, geukeni upande wa kaskazini." (Kumb. 2:3). Ndugu zangu Watanzania, tulivyouzunguka mlima wa CCM sasa imetosha! Tulivyouimbia kwa kuuzoea na kuusifia utawala mbovu wa chama hicho sasa inatosha! Tulivyozoea mazingaombwe na mikataba iliyodumaza uchumi wetu sasa inatosha! Ndiyo CCM inaweza kuwa na watu wachache waadilifu, wamwogopao Mungu, na waipendao nchi yao! Ndiyo inawezekana kuna wale wanaojaribu kuibadilisha toka ndani ili ikidhi mahitaji ya Taifa letu, hata hivyo kuombea watu hawa wapo, inatosha! CCM imefanya mambo mengi mazuri kwa Taifa lakini yakipimwa na yale mabaya kwenye mizani ya Mama Haki, mambo mabaya yanazidi kwa uzito na wingi wake yale mazuri! Kuombea kuwa miaka mitano ijayo mambo yatabadilika inatosha! Tugeuke upande tofauti! Labda tutafika iliko NCHI YA AHADI!

Kwani kuanguka kwa chama hicho kupo, kunakuja, na kunafanya hima kutufikia. CCM siyo mama yetu! Unabii huo utatimia!!!

( nitasahihisha kesho)
 
Mwanakijiji nimeipenda hii makala, tatizo langu watakapoporomoka hao, nani atachukua nafasi yao? CUF, NCCR, CHADEMA au DP? natumaini wakati umefika ambao tusitegemee sana vyama vya siasa, bali taasisi za jumuiya mbalimbali, kama umoja wa wanafunzi na vyama vya wafanyakazi.
 
Mwana kijiji,

Hongera sana nimekipenda sana kile kipande cha makaburi yaliyopakwa chokaa nyeupe, kumbe ndani yake ni mifupa mitupu!...
 
I belive Technically CCM is dead, hata hiyo mafia au mtandao ni watu ambao wamevamia CCM, they have no grip/clout.
Hawa wazee akina JM, Msuya, Warioba, SAS the number is long, are watching things from very far, they already lost grip, but for them is difficult to come out and say any opposite because their existance for the rest of their lives depend on CCM government. If only they will be assured of their daily bread and a strongman comes up out of nowhere, will dare support him. Nobody is happy with CCM from all the corners; it is taken by dogs!
 
Maneno yako Mzee Mwanakijiji ni mazito; nimetafuta jina la kukubatiza sijalipata.

Naamini mambo manne ni muhimu ili huu utabiri wako utimie.

Kwanza, watu wapigike sana kimaisha na waweze kuhusisha kikamilifu madhira wanayoyapata na utawala wa CCM. Pili, wananchi walio wengi watakapogundua kuwa CCM ni gari lililokwisha kufa na halikarabatiki hata aje dereva awaye yule, awe Mwinyi, Mkapa, Kikwete, na yeyote yule hii gari haiendi. Tatu, wananchi walio wengi waamini kwamba wana uwezo wa kuitoa CCM madarakani kwa kutumia kura zao. Nne, wananchi wakiangalia pembeni waone chama na viongozi mbadala cha kuwapa hizo kura zao. Yaani, waione gari mpya na dereva aliye mwerevu wa kuiendesha.

Mimi nafikiri wananchi walio wengi tayari wameshapigika sana na maisha na kwamba matumaini waliyopewa na Kikwete yameshayeyuka. Ila sidhani kwamba wananchi walio wengi wameweza kuoanisha sawasawa katika kupigika huko kimaisha na utawala wa CCM. Naamini pia kuwa wananchi walio wengi pia bado wanafikiri kwamba tatizo la CCM ni dereva na sio gari. Yaani, wanafikiri ukibadilisha dereva hamna neno. Hadi pale watakapoelewa kuwa CCM ni gari lililokwisha kufa, halikarabatiki hata aje fundi na dereva wa namna gani hawezi! Naamini kuwa wananchi sasa wanaamini kwamba wanaweza kubadilisha uongozi kwa kura zao. Vinginevyo, upinzani usingepata hao wabunmge wachache waliowapata.

Kuhusu vyama na viongozi mbadala (gari jipya na dereva mwerevu)-Japokuwa mwanga umeanza kupenyeza, nafikiri hapa ndio bado kuna kazi kidogo. Tatizo moja kubwa sana lililopo ni kukosekean kwa umoja wa vyama vya siasa. Watanzania wanapenda sana umoja. Kwa hivyo kwa hili la kuwa kila chama kinajiona bora kuliko chama kingine na kijiendeshea mambo yake chenyewe, ni kikwazo kikubwa kwa vyama vya upinzani kupenyeza katika nyoyo za watanzania. Ndio maana makala yako Mzee Mwanakijiji imenikuna hasa ulipogusia muungano wa vyama vya siasa. Nakwambie siku vyama vya upinzani vikiungana, utakuwa ndio mwanzo wa mwisho wa CCM. Lakini nisisitize hapa kuwa sio muungano, bali muungano miongoni mwa vyama vilivyo makini kwani tunajua kuna vyama vingine ni matawi ya haohao CCM.

Mimi ninashawishika sasa kuliko kipindi kingine chochote juu ya nguvu ya ushawishi tulio nayo katika forum hii. Kwa hivyo, nawaombeni ndugu zangu tuanze rasmi kuwapa shinikizo viongozi wa vyama vya siasa wa upinzani waanze mazungumzo ya kuunganisha vyama vyao. Kwa kuanzia ningeomba tuanze na vyama hivi: CHADEMA, CUF, NCCR, TLP na UDP. Ninaamini vyama hivi vikiungana, itakuwa ni nguvu kubwa na itakuwa ndio mwisho wa shutuma za udini na ukabila zinazotusumbua CHADEMA na CUF.

Tunaweza kuanza kwa kuandika barua ambayo wale tunao amini katika muungano tutaisaini. Barua hiyo iwe ni barua rasmi kutoka kwa watanzania wanaoishi nje na iende kwa viongozi wakuu wote wa vyama vya siasa vya upinzani.

Naomba kuwasilisha
 
Sheria inasemaje kuhusu kuungana kwa Vyama ndugu Mwanasiasa ?
Mzee MKJJ katema nondo nzito sana na hizi ni tishio kwa wale walala uwanjani kweney shughuli nzito za Kitaifa wakiwa na maana kwamba wamechoka mno na ndiyo maana wanalala ovyo lakini bado wanatakamadaraka . Kwa kuwa vyama vya kijamii TZ havina mwelekeo na sijui kama vipo maana sivisikii watu wa nje wainge mfano wa Mzee MKJJ na hata kujenfa kitu strong na kukabiliana na uovu ambao ma West wana ushabikia kwa wao kupata chao mapema . Barua kwa Blair nk toka Mzee MKJJ ziwe nyingi na umoja uwepo wa kutetea Nchi tusahau tofauti za vyama .Vyama vije baadaye na sasa lengo ni Tanzania wote tuwe kitu kimoja .

Naomba kutoa hoja .
 
Sheria inasemaje kuhusu kuungana kwa Vyama ndugu Mwanasiasa ?


Sheria ilikuwa inazuia muungano technically maana inabidi msajili chama upya na taratibu zote zinaanza upya. Lakini nasikia msajili wa vyama "ameshinikiza" mabadiliko ya sheria ili vyama viruhusiwe kuungana bila kulazimika kusajili hicho chama upya. Alituaidi katika mkutano wa CHADEMA wa Septemba pale PTA kuwa mswada utakuwa tayari na utapelekwa katika bunge la mwezi wa pili.

Nafikiri sisi wapinzani hatujatia pressure ya kutosha kubadilisha hii sheria.
 
Mwanakijiji, sasa umekuwa mwanakijiji kweli kweli. Unastahili tano zangu kwa tamko hili. Na halina budi kusambazwa zaidi ya mtandao huu ili liwafikie wanakijiji wenzio wa ''Masasí. Kazi hiyo nitaifanya mimi, kwa heshima yako. Asante.
 
Kichwamaji huyu Mzee MKJJ ndiyo maana nimekuwa namshambulia siku zote kwa kuwa najua uwezo wake ni mkubwa .Nakuunga mkono kulisambaza kama ambayo mimi nimesha fanya hivyo tayari . Mzee MKJJ hongera tena tupo pamoja na message inasambaza mnoo.
 
Wazee tangazeni, sambazeni, fanyeni vyovyote vile! Nilitetea matendo ya CCM kidogo kwa kuangalia kuwa sijaona mbadala. Lakini sasa, mawazo yangu nataka kuyaelekeza katika kuundwa kwa nguvu thabiti ya kuiondoa CCM madarakani kuanzia kwenye Bunge 2010 na urais ifikapo 2015, tukiweza kuyafanya yote 2010 itakuwa bora zaidi!

Nitaandika kwa kifupi wiki inayokuja mikakati mathubuti ambayo wapinzani wanaweza kuitumia kuing'oa CCM (sijui kama nitapost hapa au la maana makada wa CCM nao wanasoma hapa ) na michango yenu kama kawaida ni muhimu. Wakati wa kulala umepita, wakati wa kunung'unika umepita, na wakati wa kuombea kudra za Mnyezi Mungu umepita! Mungu ameshatupa uwezo wa kuona, kufikiri, kuamua na kutenda! It is about time!!

Yoyote ninayoyaandika hapa, mtu yoyote yuko huru kuyanukuu, kuyatumia, na kuyaweka kama maneno yake (hata kwa kufanyiwa mabadiliko) ili ujumbe uwafikie wengi zaidi.

Maandishi yangu pekee ambayo nazuia kuninakili au kuchapisha bila idhini yangu ni hadithi zangu na insha ambazo nimesema wazi zisitumiwe pasipo idhini yangu. Mengine yote ni fair game!!!

Nashukuru kwa kunitia moyo!! na mimi nawatia moyo ninyi nyote wenye mapenzi na nchi yenu, ninyi ambao kila kukicha mnawaza mfanye nini ili kulinusuru Taifa letu! Ninawapa moyo ninyi nyote ambao ndani ya mioyo yenu moyo kama ule wa gesi unawaka, na kuwapa joto la kuitumikia nchi yenu!! Nawapa moyo ninyi ambao mmechoka kuona watu wachache kama vile wamepewa kibali na Mungu wakiendelea kunufaika wakati wananchi wenzao wanahangaika kila kukicha!! Msikate tamaa, msirudi nyuma, na msisalimu amri!! Songeni mbele wana na mabinti wa Tanzania, songeni mbele wazalendo!! kazi kubwa iko mbele yenu, Taifa linawangojea!!!

M. M.
 
Mwanakijiji,

Shetani gani huyo kakukamata?.... maanake sasa naona mkereketwa mkali sana utadhani Che...
Kisha ulivyokuwa mhuni umemalizia na dua moja kali ambayo hata mbingu zote zimefunguka waaa!..

Nashukuru kwa kunitia moyo!! na mimi nawatia moyo ninyi nyote wenye mapenzi na nchi yenu, ninyi ambao kila kukicha mnawaza mfanye nini ili kulinusuru Taifa letu! Ninawapa moyo ninyi nyote ambao ndani ya mioyo yenu moyo kama ule wa gesi unawaka, na kuwapa joto la kuitumikia nchi yenu!! Nawapa moyo ninyi ambao mmechoka kuona watu wachache kama vile wamepewa kibali na Mungu wakiendelea kunufaika wakati wananchi wenzao wanahangaika kila kukicha!! Msikate tamaa, msirudi nyuma, na msisalimu amri!! Songeni mbele wana na mabinti wa Tanzania, songeni mbele wazalendo!! kazi kubwa iko mbele yenu, Taifa linawangojea!!!


Na sisi tunasema AAAAMIN...
 
Mkandara, kuna mtu mmoja wa CCM amenisukuma hivi na kunikasirisha sana.. nilipoandika hayo maneno ya mwisho hadi nywele zikanisimama...I need to take a break na kupumua kidogo.
 
Kula tano kaka MKJJ

Kuanguka kwa CCM ni dhahiri sasa ni wakati muafaka kuandaa mfumo dhabiti ambao utakubaliwa na wengi ili watakao chukua uongozi baadaada ya muanguko huu wasije kutusaliti.

Kama sheria inaruhusu napendekeza yafanyike yafuatayo,

1. Itengenezwe rasimu ya katiba ambapo wanabodi na wanaanchi wengine wataruhusiwa kuchangia mawazo kwa njia ya mtandao [internet]

2. upendekezwe mfumo wa uongozi wa nchi na instititution ambazo zitaweza kuisukuma mbele nchi yetu.

Forum inavichwa ninahakika tutakuja na kitu kikali

Naomba kutoa hoja
 
CCM inaweza kuanguka hata leo hii, tatizo hakuna mtu /watu wa kuiangusha.
 
Mzee Mwanakijiji,

Heshima yako mkuu, lakini I beg kukupinga bro, maneno yako pamoja na kwamba sijayasoma yote kutokana na shughuli nyingi ninajaribu kukielewa kichwa chako cha habari, na nimesoma mstari wa kwanza kwamba eti kuna siku wananchi wataamuka na kukuta CCM hawapo na ukataja baadhi ya viongozi wa CCM na serikali wengi wao wakiwa wastaafu na ambao hawahusiki kabisa na maaamuzi ya serikali yetu ya leo,

What a joke? eti serikali iliyochaguliwa kwa njia zote za kidemokrasia na zinazokubalika duniani katika civil world, kwamba itayeyuka tu au itaondoka tuuuu kama kusadikikika, unless sikuelewi vizuri, ila kama ninakuelewa vizuri ni kwamba uliyoyasema ni ndoto ya alinacha.

Wananchi wengi haturidhishwi na serikali na matendo yake, lakini what to do about it so far imekuwa ni hadithi kichaaaa, but kuwaaambia wananchi walale usingizi tu lakini siku moja kuna utabiri somewhere ulitabiriwa either na wewe au sijui ni Shehe Yahya, kwamba nji yetu itaamuka na kukuta CCM hawapo ni underst satement of the century bro!

Taifa letu limeburuzwa for tooo long na viongozi ambao ni incompetent, I do not care woteee waliowahi kuwa viongozi, hakuna mwenye nafuuuu ndio maana tumekwama, hata kama ni Mwalimu, I mean woteee, walikuwa na uwezo kidogo lakini weaknesses nyingi mnoo kiasi kwamba ukweli ni kwamba hawakufaaa kuwa viongozi period, but Mwalimu tunampa heshima kubwa kwa sababu kuna machache kati ya mazuri yametusaidia big time, otherwise viongozi wote waliowahi kuwa na wanaotaka kuwa wote ni bureeee, labda hii generation iondoke kwanza ndio watakuja viongozi wa kweli huko mbele, ninarudia wote ni bure, wewe Mwanakijiji majuzi tui ulikuwa unalia na watu hapa kuwa CCM ni safi na srikali ni bomba leo kulikoni blaza? Yaaani katika kipindi cha miezi sita tu ndio umekuwa hata na idea ya how kuwaondoa CCM? Sasa ungekuwa kiongozi wananchi walitakiwa kukufuata nyuma, jana CCM leo kuwang'oa CCM, sounds like a sell out! sasa tofauti yako na Kaburu, Tambwe, na Lamwai ni nini?

Eti umegeuza mawazo yako over CCM kwa sababu kuna kiongozi mmoja wa CCM iliyekuudhi? that is all? Serikali ya awamu ya nne ina walakini, lakini pia nayo imeyarithi matatizo sugu ya toka tupate uhuru, na ina matatizo mengi tunyajua na tunayasema kila siku hapa ili yarekebishwe, na ni vyema kwamba awamu ya nne imeingia na kurithi matatizo makubwa, maana matatizo ndio mwalimu bora kuliko mwalimu yoyote duniani!
 
Mzee Es,
Come to think of Ur comments... U have a point!

Lakini kikubwa ulichoshindwa kuelewa hapa ni pale hukusoma maelezo yote. Hapo juu ameanza kama kiamsho na jarida la habari nzima kisha huko mbele kayasema mengi ambayo yanaashiria kuwa mapinduzi ya CCM yatakuwa ya haraka sana kiasi kwamba aliyelala anaweza kuamka na kukuta CCM haipo madarakani.

Hivi ndivyo navyafahamu mimi upeo wa maelezo ya Mzee Mwanakijiji.
 
Mzeee Bob,

Heshimayako mkuu na ninakusikia, lakini for how long wabongo tutaendelea kudanganywa na the former CCM's? Mwanakijiji ni former CCM, kilichomshinda kuwapa haya mawaidha CCM wakafanya tofauti ni nini mpaka asubiri kuudhiwa na kiongozi wa CCM, ndio atoke na kutoa ideas za kuwatoa madarakani?

CCM watatolewaje madarakani bila ya kutopigiwa kura? Wewe leo Ulaya yaaani majuuu kuna wananchi wanaoweza kwenda kwenye mkutano wa rais na uniform za CCM unaamini kuna uwezekano wa kuwatoa CCm kwa kura? Hiyo ni ndoto ya mwendawazimu ndugu yangu, CCM hawafai na upinzani hawafai pia sasa sisi wananchi tufanye nini?

Kichwa cha habari na mstari wa kwanza wa hadithi unapaswa kuwa na utamu wote wa habari, maneno ya Mwanakijiji pamoja na uzuri kwa hamasa kisiasa, I am afraid ni empty katika kuleta results, CCM hawaondoki labda kwa kura na kura za kuwaondoa hakuna, upinzani wako mjini tu, na tunajua by history kuwa wapiga kura hawapo mjini,

Mzee tunayemuamini kuleta mabadiliko ndio kwanza anaenda shule saaa hizi wakati viongozi wa CCM walishaenda shule zamani, sasa watakaaa wanamsubiri mpaka amalize shule ili wampe nji?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom