Kongamano la Wanamitandao ya Jamii: Wizara ya Fedha yatoa wito Mitandao ya Kijamii itumike kuelimisha jamii umuhimu wa kodi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,813
11,991
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja amefungua Kongamano la Wanamitandao ya Kijamii na Wizara ya Fedha linalofanyika katika Ukumbi wa 88 Mkoani Morogoro, leo Jumatatu Oktoba 23, 2023 ambapo amesisitiza matumizi ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya faida ya Nchi.

Mwaipaja amesisitiza kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii yanapotumika vizuri yanaweza kuwa msaada mkubwa katika sekta ya maendeleo na pia yakitumika vibaya yanaweza kuharibu taswira zaidi ya jamii hata kama kuna mambo mazuri yanafanyika.

Benny Mwaipaja1.JPG

Benny Mwaipaja.JPG

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ,Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja akizungumza wakati akifungua Kongamano la Wanamitandao ya Kijamii na Wizara ya Fedha linalofanyika Mkoani Morogoro kwa siku mbili kuanzia Oktoba 23 hadi 24, 2023.

Amesema “Nitoe mfano, Jamii inatakiwa kutambua umuhimu wa kutoa na kuchukua risiti baada ya kufanya manunuzi, kwani kodi inayopatikana hapo inakuwa ni kielelezo kizuri kwa Serikali upata fedha kwa ajili ya kuhudumia Wananchi wake.

“Mitandao ya kijamii ni muhimu katika kufikia watu wengi, itumike vizuri kwa lengo la kusaidia Jamii na kuongeza idadi ya Walipa kodi.”

Amesema Mitandao ikitumika kutoa elimu walipa kodi wataongezeka kuliko ilivyo sasa.

Sehemu ya elimu hiyo ni kuhusu matumizi ya risiti halali ambapo Watanzania wanatakiwa kutambua umuhimu wa kuwa na risiti halali kulingana na malipo stahiki kwa kuwa bila kupata kodi ni vigumu Serikali kutekeleza maendeleo ambayo imejiwekea.

Kuhusu mikopo

Ameeleza kuwa hakuna Serikali ambayo haikopi, kwani licha ya kuingiza kipato kupitia mapato ya ndani bado kuna mikopo ya riba nafuu inafaa kwa ajili ya maendeleo ya Nchi.

“Tukikopa tukajenga Reli, tukaongeza tija kwenye miundombinu yetu, hayo ni manufaa, mfano watu wanalalamika kuhusu umeme lakini Bwawa la Mwalimu Nyerere likikamilika litapunguza changamoto ya umeme, hivyo ili kukamilisha miradi mikubwa kama hiyo lazima tukope,” amesema Mwaipaja.

Amesisitiza kuwa "Tutaendelea kutumia Mitanda ya Kijamii ili tuwafikie watu wengi ambao wanatumia mitandao hiyo."

Wizara yapongezwa
Aidha, akizungumza wakati wa ufunguzi huo Mathias Canal aliyeteuliwa na washiriki kuwa Mwenyekiti wa Kongamano ameipongeza Wizara ya Fedha kwa kuandaa kongamano hilo na kusema hiyo itakuwa fursa ya kurahisisha utendaji kazi wao kwa umma.

Canal ameishauri Wizara ya Fedha kutoa ufafanuzi kwa umma kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali na umuhimu wa mikopo ili kuondoa sintofahamu kwa jamii kuhusu mikopo ya serikali.

Amesema “Umuhimu wa kupitishwa kwa Sheria ya marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2023 ambapo amesema Masharti yaliyokuwemo yalisababisha kuwepo kwa ushiriki hafifu wa Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa utaratibu wa ubia.”

Ameongeza “Hongera sana Mkuu wa Kitengo cha Habari Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja kwa kubuni kongamano hili pia tufikishie salamu za pongezi kwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kukubali kufanyika kwa kongamano hili muhimu kwa Wanahabari.”
dbfafb07-a142-4cac-9dee-2951336781f2.jpeg
Mwenyekiti wa Kongamano la Wanamitandao ya Kijamii, Mathias Canal akizungumza wakati wa Kongamano la Wanamitandao ya Kijamii na Wizara ya Fedha linalofanyika Mkoani Morogoro.

ab9921ee-d785-4c03-9499-ab9f9138b056.jpeg

5-5-1024x682.jpg

Sehemu ya washiriki wa Kongamano.
VIKUNDI VYA KIKOBA VISAJILIWE
Akizungumza vikundi mbalimbali vya kukusanya na kuhifadhi fedha zilivyopo mitaani ikiwemo sehemu za kazi, Kamishna Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Dionesia Mjema amesema ni muhimu vikundi vikasajiliwa kwa lengo la kuhakikisha usalama wa fedha unakuwepo.

Amesema “Hakikisheni vikundi vyenu vya kuhifadhi fedha vimesajiliwa kwa kuwa kutofanya hivyo ni kujiweka hatarini kupoteza fedha katika mazingira ya kutapeliwa.”

Amesema hilo linatakiwa kuzingatiwa kwa kuwa ni kwa mujibu wa Kanuni Sheria Ndogo za Fedha (Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo) za Mwaka 2019).

Kanuni Sheria Ndogo za Fedha (Vikundi vya Kijamii vya Huduma Ndogo za Fedha) za Mwaka 2019 kama vile: VICOBA, VISLA, Kijumbe, Mary Go Round.

Kanuni za Kuwalinda Watumiaji wa Huduma za Fedha za Mwaka 2019.
Dionesia Mjema.JPG

Dionesia Mjema 2.JPG

Dionesia Mjema
Amesema kutoa Elimu ya Fedha ni suala endelevu pia uwepo wa Sheria unaonesha jinsi gani ambavyo Serikali ina nia ya kudhibiti utapeli wa masuala ya fedha, pia tunategemea kutengeneza program katika ngazi mbalimbali.

Utafiti unaonesha kuwa mara nyingi wale wanaokuwa na nafasi ya kushika fedha wanakuwa hawapendi kupata elimu kwa kuwa wanajua ikiwa hivyo wao hawatafanikiwa kufaidika.

Dionesia ameongeza kuwa "Kuna wakati watu wanaibiwa kwa kuwa kutokana na kukosa ufahamu, ndio maana tunaomba kupitia majukwa ya Mitandao ya Kijamii kufikisha ujumbe huu kwenye jamii kuwa masuala ya fedha yanahitaji umakini, kuchanga na kumpa mtu mmoja au wachache bila kuwa na usajili ni wazi kunakuwa na hatari ya kupotezea fedha hizo.

"Ukitaka kuingia kwenye huduma za kifedha ni vizuri ukatafuta mtaalam akakupa muongozo, ikitokea mtu anaingia kwenye suala la Kisheria lazima amtafute mwanasheria au ushauri wa kisheria lakini watu hawafanyi hivyo katika suala la fedha, hiyo ni changamoto.

"Wananchi wengi wakiingia katika mifumo rasmi itarahisisha hata Serikali kuwa na fedha zinazopatikana kwenye mfumo na kusaidia jamii."
 
Mimi nafikiri kabla ya kukimbilia kwenye jamii, waelimishane kwanza wao wenyewe juu ya matumizi sahihi ya hizo kodi. Siyo watu wanalipa kodi kwa mateso, halafu wakusanyaji wanatumia sehemu kubwa kwenye matumizi ya hovyo.

Kodi inatakiwa itumike zaidi kwenye shughuli za maendeleo. Na siyo kulipana mishahara mikubwa, kulipana posho nono, kununulia magari ya kifahari, na kuzipigia dili.
 
Back
Top Bottom