Dkt. Mpango ahimiza ubunifu sekta ya fedha

Dalton elijah

JF-Expert Member
Jul 19, 2022
216
478
1709824530103.jpg
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amepongeza jitihada za taasisi zote za sekta ya fedha nchini kuhimili vihatarishi vyote vilivyojitokeza na kufanya sekta hiyo kuwa imara na himilivu kwa kuongeza ubunifu na uwezo wa kubadilika kuendana na mazingira yaliyopo.

Amesema hayo wakati akifungua Kongamano la 21 la Taasisi za Fedha linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha tarehe 7 Machi 2024 likiwa na mada kuu isemayo: "Kuimarisha Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha Nyakati za Changamoto za Kiuchumi".

“Hakika, mmesaidia kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi na maendeleo,” Dkt. Mpango amewaeleza viongozi wa taasisi za fedha ambao

Aidha, Makamu wa Rais amewataka watoa huduma wa mifumo ya malipo kuendelea na ubunifu ili kudumisha utengenezaji wa bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji mbalimbali ya jamii yetu kuendana na mahitaji yake yanavyobadilika.

Amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya malipo kwa njia za kidigitali, hasa katika sekta za benki, bima, mifuko ya Hifadhi ya Jamii na huduma nyingine.

“Mabadiliko haya yanapelekea uhitaji wa kuhama kutoka kwenye matumizi ya pesa taslimu kwenda kwenye njia za malipo za kielektroniki ili kupunguza hatari zinazohusiana na kutumia pesa taslimu na kuongeza urahisi wa ufanyaji malipo,” amesema.

Dkt. Mpango ameipongeza Benki Kuu na taasisi zote zilizoshiriki katika uundwaji wa Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Hapo, yaani Tanzania Instant Payment System (TIPS).

“Ninatarajia kwamba mfumo wa TIPS utasaidia kuendeleza huduma rasmi za kifedha na kupunguza gharama za miamala,” amesema Makamu wa Rais ambaye baadaye alizindua rasmi mfumo wa TIPS.

Aidha, ameipongeza Benki Kuu kwa kuanza kutumia mfumo mpya wa utekelezaji wa sera ya fedha unaotumia riba, akieleza matumaini kwamba utaimarisha ufanisi wa sera ya fedha katika mazingira ya sasa ya kiuchumi na hivyo kutoa ishara kwa riba za mikopo inazotolewa na taasisi za fedha ili kuchochea uwekezaji na ukuaji wa uchumi.

Mapema, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, alieleza kwamba pamoja na mada kuu, washiriki wa kongamano watapata fursa katika kujadili masuala kuhusu ufanisi na uhimilivu wa taasisi za fedha wakati wa majanga na Ustahimilivu wa sekta ya fedha katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi: Jukumu la sheria mbalimbali, ubunifu na usimamizi wa vihatarishi.

“Ubunifu wa teknolojia mpya unatoa fursa kwa taasisi za fedha katika kuboresha utoaji wa huduma za fedha na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza,” ameeleza Gavana Tutuba.

Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Chande amesema sekta ya fedha ya Tanzania imeonyesha uhimilivu katika kupambana na changamoto za uchumi wa dunia za hivi karibuni.

“Uimara wa sekta ya benki umesaidiwa na uwiano mzuri wa mtaji na ukwasi ambao ulikuwa juu ya mahitaji ya chini ya udhibiti,” amesema.

Tangu mwezi Mei 1980, Benki Kuu imekuwa ikiandaa mikutano ya taasisi za fedha mara kwa mara ili kujadili mada mbalimbali zinazoendana na vipindi husika kwa lengo la kuhakikisha kwamba sekta ya fedha nchini inapata mbinu mbalimbali ili iendelee kuwa tulivu na inayokua licha ya changamoto zinazojitokeza nchini na duniani.

CHANZO. Bank of Tanzania
 
Back
Top Bottom