Akizungumza na wana habari katika ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM jijini Dar es Salaam jana jioni kuelezea kuhusu tukio hilo la Kikwete kuanguka, mkuu wa kitengo cha habari cha kampeni za CCM, Kanali mstaafu, Abdulrahman Kinana, alisema kilichosababisha hali hiyo ni upungufu wa sukari, kulikosababisha kushuka kwa shinikizo la damu.
Kwa mujibu wa madaktari wake, sababu kubwa iliyosababisha tukio la leo ni upungufu wa sukari mwilini na kushuka kwa pressure, kwa sababu alikuwa amefunga, alisema Kinana wakati akitoa maelezo yanayoshabihiana na yale ya mwaka 2005, ambayo pia yalihusisha tukio la Kikwete kuanguka kwa sababu ya mfungo.
Kinana alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wanachama, wapenzi na mashabiki wa CCM kwamba hali ya afya ya Kikwete ilikuwa njema na ataendelea na ziara yake ya kampeni leo hii mkoani Mwanza na kwingineko nchini.
Mbali ya hilo, Kinana alisema uamuzi wa Kikwete kufunga ulikuwa ni kinyume cha ushauri aliopewa na madaktari wake ambao walishauri asifunge.
Alisema tayari chama hicho na madaktari wake wameshachukua hatua zote za tahadhari ili kuhakikisha kuwa mgombea huyo wa urais anaendelea na kampeni zake za urais pasipo kukwama.
Katika hatua nyingine, mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, jana alimtumia Rais Kikwete salamu za pole kutokana na tukio la kuanguka kwake.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Dk. Slaa, alisema aliamua kumtumia salamu za pole Rais Kikwete kwa kuwa Watanzania wote ni ndugu na siasa si uadui.
Alisema kuwa anakumbuka kuwa Rais Kikwete alimtumia yeye (Slaa) salamu za pole aliposikia kuwa amevunjika mkono baada ya kuanguka bafuni mkoani Mwanza. Mheshimiwa Rais nimepokea kwa masikitiko taarifa ya hali ya afya iliyokupata Jangwani leo, nakuombea sana upate nguvu haraka hasa katika kipindi hiki kigumu, nakupa pole sana sana. Alisema Dk. Slaa katika ujumbe mfupi aliomtumia Kikwete.